Trump na Netanyahu wakubaliana mpango mpya wa amani wa Gaza

Radio Fortune Africa -Na Cantona Joseph

https://zeno.fm/radio/radio-fortune-africa

Chanzo cha Palestina kinachofahamu mazungumzo ya kusitisha mapigano kiliambia BBC kwamba maafisa wa Hamas wamepewa pendekezo lenye kugusia vipendele 20 la Ikulu ya Marekani.

Rais wa Marekani Donald Trump na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu wanasema wamekubaliana mpango mpya wa amani wa Gaza, na kuionya Hamas kuukubali.

Mpango huo unapendekeza kusitishwa mara moja kwa operesheni za kijeshi na Hamas kuwaachilia huru mateka 20 wa Israel na wengine zaidi ya 20 ambao wanaaminika kufariki dunia ndani ya saa 72, ili kubadilishana na mamia ya raia wa Gaza wanaozuiliwa.

Chanzo cha Palestina kinachofahamu mazungumzo ya kusitisha mapigano kiliambia BBC kwamba maafisa wa Hamas wamepewa pendekezo lenye kugusia vipendele 20 la Ikulu ya Marekani.

Moja wapo ya mapendekezo ni kwamba Hamas haitakuwa na jukumu lolote katika kutawala Gaza, na kufungua mlango kwa upatikanaji kamili wa taifa la Palestina.

Akizungumza katika mkutano na wanahabari kufuatia mazungumzo katika Ikulu ya White House, Trump aliutaja mpango huo kuwa “siku ya kihistoria kwa amani”.

Lakini alisema kuwa Netanyahu ataungwa mkono na Marekani “kumaliza kazi ya kuharibu tishio la Hamas” ikiwa Hamas haitakubali mpango huo.

Netanyahu kisha akasema Israel “itamaliza kazi” ikiwa Hamas itakataa mpango huo au haitaufuata.

Putin asema Urusi inashinda ‘vita vya haki’ nchini Ukraine

.

Rais wa Urusi Vladimir Putin amesema Jumatatu kwamba vikosi vya Urusi vinashinda katika kile alichosema kuwa “vita vya haki” nchini Ukraine.

“Wapiganaji wetu na makamanda wanaendelea na mashambulizi, na nchi nzima, Urusi yote, inapigana vita hivi vya haki na kufanya kazi kwa bidii,” Putin alisema katika video iliyochapishwa kwenye tovuti ya Urusi.

“Kwa pamoja tunatetea upendo kwa Nchi yetu na umoja wa hatima yetu ya kihistoria, tunapigana na tunashinda.”

Urusi ilianzisha uvamizi dhidi ya Ukraine mnamo Februari 24, 2022, na kuiita “operesheni maalum ya kijeshi”. Kyiv na washirika wake wanasema uvamizi huo ni jaribio la kibeberu la unyakuzi wa ardhi.

Vita hivyo bado havijapata ufumbuzi licha ya juhudi za kidiplomasia za Rais wa Marekani Donald Trump kumaliza mzozo huo, ikiwa ni pamoja na mikutano tofauti na Putin, Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy na viongozi wengine wa Ulaya.

Serikali ya Taliban yazima mfumo wa mawasiliano

.

Serikali ya Taliban nchini Afghanistan imezima mfumo wa mawasiliano nchi nzima, wiki kadhaa baada ya kuanza kukatika kwa miunganisho ya intaneti.

Nchi kwa sasa inakabiliwa na “kukatika kabisa kwa mtandao”, shirika la uangalizi wa mtandao la Netblocks linaripoti.

Mashirika ya habari ya kimataifa yanasema yamepoteza mawasiliano na ofisi zao katika mji mkuu Kabul. Mtandao wa rununu na TV za satelaiti pia zimetatizwa sana kote nchini Afghanistan.

Taliban bado haijatoa sababu rasmi ya kuzima intaneti lakini tangu kutwaa madaraka mwaka wa 2021, Taliban wameweka vikwazo vingi kwa mujibu wa tafsiri yao ya sheria ya Kiislamu.

Rais wa Madagascar avunja serikali baada ya maandamano ya ‘Gen Z’

.

Rais wa Madagascar amesema kuwa atavunja serikali yake, kufuatia siku kadhaa za maandamano yanayoongozwa na vijana kuhusu kukosekana kwa maji na kukatika kwa umeme kwa muda mrefu.

“Tunakubali na kuomba radhi kwani wanachama wa serikali hawajatekeleza majukumu waliyopewa,” Andry Rajoelina alisema katika hotuba ya kitaifa iliyotangazwa na televisheni siku ya Jumatatu.

Maandamano hayo yanayoitwa Gen-Z yameshuhudia maelfu ya waandamanaji ambao wengi wao ni vijana wakiingia mitaani katika miji kote Madagascar tangu Alhamisi, chini ya kauli mbiu: “Maisha, bila kuteseka”.

Mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa amelaani “kikosi kisicho cha lazima” kinachotumiwa na vikosi vya usalama kutuliza machafuko, akisema kuwa watu wasiopungua 22 wameuawa na wengine 100 kujeruhiwa.

Wataalamu wa UN walaani ‘kiwango kikubwa’ cha mauaji nchini Iran

.

Wataalamu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa wamesema wanashangazwa na “kuongezeka kwa kasi” kwa idadi ya watu wanaonyongwa nchini Iran, huku zaidi ya watu 1,000 wakiuawa katika kipindi cha miezi tisa ya kwanza ya 2025.

“Kiwango cha kunyongwa nchini Iran ni cha kushangaza na kinawakilisha ukiukwaji mkubwa wa haki ya kuishi,” waandishi hao watano maalum walionya katika taarifa yao ya pamoja.

Walibainisha kuwa nusu ya hukumu za kunyongwa zinazojulikana zilikuwa kwa makosa yanayohusiana na dawa za kulevya na kwamba kunyongwa kwa watu tisa kwa siku kwa wastani kumerekodiwa katika wiki za hivi karibuni.

Hakukuwa na maoni ya mara moja kutoka Iran. Lakini serikali hapo awali ilitetea utumiaji wake wa hukumu ya kifo, ikisema ni mdogo tu kwa “uhalifu mbaya zaidi”.

Hili linawadia siku hiyo hiyo ambapo Iran ilisema mtu anayetuhumiwa kufanya ujasusi wa Israel ameuawa.

Mwanamke wa China ahukumiwa kwa wizi wa pesa nyingi zaidi za “kidigitali duniani”

.

Raia wa China amepatikana na hatia kwa jukumu lake muhimu katika kile kinachoaminika kuwa uwizi mkubwa zaidi wa pesa za kidijitali duniani, wa thamani ya zaidi ya £5bn ($6.7bn).

Zhimin Qian, anayejulikana pia kama Yadi Zhang, alikiri kuwa na hatia siku ya Jumatatu katika Mahakama ya Southwark Crown, London kwa kupata na kumiliki fedha hizo kinyume cha sheria.

Kati ya 2014 na 2017, aliongoza kashfa kubwa nchini China kwa kudanganya zaidi ya waathiriwa 128,000 na kuhifadhi pesa zilizoibiwa katika mali ya bitcoin, Polisi wa jiji walisema katika taarifa.

Polisi ilisema ombi la kuwa na hatia la mwanamke huyo mwenye umri wa miaka 47 linafuatia uchunguzi wa miaka saba katika mtandao wa kimataifa wa utakatishaji fedha.

Polisi walisema uchunguzi ulianza mwaka wa 2018 baada ya kupata taarifa kuhusu uhamisho wa mali ya uhalifu.

Qian alikuwa “akikwepa mkono wa sheria” kwa miaka mitano hadi kukamatwa kwake, kuliko hitaji uchunguzi tata unaohusisha mamlaka nyingi, alisema Detective Sajenti Isabella Grotto, ambaye aliongoza uchunguzi huo.

Alitoroka China kwa kutumia hati za uwongo na kuingia Uingereza, ambapo alijaribu kutumia pesa zilizoibiwa kwa kununua mali, ilisema polisi.

Alipata usaidizi kutoka kwa raia mwingine wa China, Jian Wen. Mfanyikazi huyo wa zamani aliyefungwa jela miaka sita na miezi minane mwaka jana kwa jukumu lake katika operesheni ya uhalifu.

Polisi ilisema imekamata jumla ya sarafu za bitcoin 61,000 kutoka kwa Qian.

All Rights Reserved © The Cantona Group PLC||2025


Discover more from cantonadigital

Subscribe to get the latest posts sent to your email.

Leave a comment