Estonia yaomba kushauriana na Nato baada ya ndege za Urusi kukiuka anga yake

Radio Fortune Africa -Na Cantona Joseph

https://zeno.fm/radio/radio-fortune-africa

Estonia imeomba mashauriano na wanachama wengine wa Nato baada ya ndege za kivita za Urusi kukiuka anga yake siku ya Ijumaa.

Ndege tatu za kivita za Urusi aina ya MiG-31 ziliingia katika anga ya Estonia “bila idhini kwa takriban dakika 12” kwenye Ghuba ya Finland, serikali ilisema.

Msemaji wa Nato alisema “huu ni mfano mwingine wa mwenendo wa kutojali wa Urusi na uwezo wa Nato kujibu”.

Urusi ilikanusha kukiuka anga ya Estonia. Lakini mvutano umekuwa ukiongezeka hivi karibuni, baada ya Poland na Romania – wanachama wa Nato – kusema ndege zisizo na rubani za Urusi ziliingia anga zao.

Kifungu cha 4 cha mkataba wa Nato kinaanza rasmi kutekelezwa kwa mashauriano ya dharura ndani ya muungano wa wanachama 32, ambao unajumuisha Marekani na mataifa mengi ya Ulaya kushirikiana katika ulinzi wa pamoja.

Ni mara ya pili mwezi huu kwa mwanachama wa Nato kuomba mashauriano ya Kifungu cha 4.

Poland ilifanya hivyo tarehe 10 Septemba baada ya ndege zisizo na rubani za Urusi kuingia katika anga yake.

Waziri Mkuu wa Estonia Kristen Michal alisema “Jibu la Nato kwa uchokozi wa aina yoyote lazima liwe na umoja na nguvu”.

Estonia, ambayo inapakana na Urusi upande wa mashariki, inasema hii ni mara ya tano Urusi imekiuka anga yake mwaka huu.

Heathrow miongoni mwa viwanja vya ndege vilivyokumbwa na shambulio la mtandaoni

.

Uwanja wa ndege wa kimataifa wa Heathrow ni miongoni mwa viwanja vya ndege kadhaa vya Ulaya vilivyokumbwa na shambulio la mtandao lililoathiri mfumo wa kielektroniki wa kupakia mizigo.

Uwanja huo ulitoa tangazo la kuwaonya abiria kuhusu uwezekani wa huduma hiyo kujikokota kutokana na “suala la kiufundi” linaloathiri programu iliyotolewa na Collins Aerospace kwa mashirika kadhaa ya ndege.

Uwanja wa Ndege wa Brussels ulisema shambulio la mtandaoni siku ya Ijumaa usiku lilimaanisha kuwa abiria watalazimika kukaguliwa kwa mikono, huku Uwanja wa Ndege wa Berlin wa Brandenburg pia ukisema “hitilafu ya kiufundi” imewafanya watu kusubiri kwa muda mrefu kuhudumiwa.

Kampuni ya RTX, ambayo inamiliki Collins Aerospace, ilisema “inafahamu changamoto inayokumba mfumo wake “katika viwanja vya ndege maalum” na kwamba inajitahidi kutatua suala hilo haraka iwezekanavyo.

Trump na Xi wajadili mustakabali wa TikTok nchini Marekani

Rais wa Marekani Donald Trump amesema kuwa yeye na mwenzake wa China Xi Jinping

Rais wa Marekani Donald Trump amesema kuwa yeye na mwenzake wa China Xi Jinping wamefikia makubaliano kuhusu mustakabali wa mtandao wa kijamii wa TikTok nchini Marekani walipozungumza kwa njia ya simu siku ya Ijumaa, ingawa Beijing haijathibitisha hilo.

Trump aliandika kwenye Mtandao wake wa Truth Social kwamba mazungumzo yetu yalikuwa “na tija” na kwamba “alithamini” hatua ya Xi ya kuidhinisha makubaliano hayo, ambayo yataiwezesha TikTok nchini Marekani kununuliwa na kundi la wawekezaji wa Marekani.

Shirika rasmi la habari la serikali ya China Xinhua halikuangazia kikamilifu matokeo ya mazungumzo hayo, huku Xi akinukuliwa akisema kuwa Beijing “inakaribisha mazungumzo kuhusu TikTok”.

TikTok, ambayo inaendeshwa na kampuni ya Kichina ya ByteDance, hapo awali ilishauriwa kuuza biashara yake kwa Wamarekani la sivyo itakabiliwa na tishio la kufungwa.

Ureno yathibitisha kuwa italitambua taifa la Palestina

Maandamano yamefanyika nchini Ureno kushinikiza kusitishwa kwa mapigano huko Gaza
Maelezo ya picha,Maandamano yamefanyika nchini Ureno kushinikiza kusitishwa kwa mapigano huko Gaza

Ureno inasema italitambua taifa la Palestina siku ya Jumapili, na kulifanya taifa la hivi punde zaidi la Magharibi linalojiandaa kubadili sera kwani vita katika Ukanda wa Gaza havionyeshi dalili ya kusitishwa.

Wizara ya mambo ya nje imetoa tangazo hilo kabla ya mkutano mkuu wa Umoja wa Mataifa (UNGA) utakaofanyika wiki ijayo mjini New York.

Ufaransa, Uingereza, Canada na Australia zinajiandaa kutoa matangazo sawa na hilo.

Israel imelaani hatua hiyo, huku Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu akisema “inatukuza ugaidi” kufuatia shambulio la Hamas la tarehe 7 Oktoba 2023 dhidi ya Israel.

Marekani – mshirika mkuu wa Israel – inaunga mkono hoja ya Netanyahu.

Akizungumza na Waziri Mkuu wa Uingereza Sir Keir Starmer wiki hii katika ziara ya kitaifa nchini humo, Rais wa Marekani Donald Trump, alisema hakubaliani na na hatua ya kulitambua taifa la Palestina.

Takriban robo tatu ya wanachama 193 wa Umoja wa Mataifa tayari wanalitambua taifa la Palestina, ambalo mwaka 2012 lilipewa hadhi ya kuwa nchi isiyokuwa mwanachama.

Viongozi wa dunia wakijiandaa kukusanyika katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Jumanne ijayo, vifaru vya wanajeshi wa Israel vinaendelea kuingia katika mji wa Gaza kama sehemu ya mashambulizi ya ardhini, ambayo yamewalazimu maelfu ya watu kukimbia mji huo.

Jeshi la Israel lilianzisha operesheni huko Gaza kujibu mashambulizi yaliyoongozwa na Hamas kusini mwa Israel mwaka 2023, ambapo takriban watu 1,200 waliuawa na wengine 251 watekwa nyara.

Takriban Wapalestina 65,141 wameuawa katika mashambulizi ya Israel huko Gaza tangu wakati huo, kulingana na wizara ya afya ya eneo hilo.

All Rights Reserved © The Cantona Group PLC||2025


Discover more from cantonadigital

Subscribe to get the latest posts sent to your email.

Leave a comment