‘Zaidi ya 30 wamekufa kwa Ebola nchini Congo’, – Shirika la Afya Duniani

Radio Fortune Africa -Na Cantona Joseph

https://zeno.fm/radio/radio-fortune-africa

Shirika la Afya Duniani siku ya Alhamisi lilisema maambukizi 48 ya Ebola yamethibitishwa katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo na watu 31 wamekufa.

“Imepita wiki mbili tangu serikali ya DRC itangaze mlipuko wa Ebola …Hadi sasa, maambukizi 48 yamethibitishwa…, na watu 31 wamekufa,” mkuu wa Shirika la Afya Duniani Tedros Adhanom Ghebreyesus aliwaambia waandishi wa habari kupitia video kutoka makao makuu ya WHO huko Geneva.

Mlipuko huo, wa kwanza nchini humo katika kipindi cha miaka mitatu, ulitangazwa mapema Septemba.

Shirika la Afya Duniani Jumapili lilisema limeanza kutoa chanjo kwa wafanyikazi wa afya walio mstari wa mbele na walio wasiliana na watu walioambukizwa virusi vya Ebola katika Mkoa wa Kasai nchini Congo, ambapo mlipuko umetangazwa.

WHO imesema dozi 400 za awali za chanjo ya Ervebo Ebola kutoka akiba ya dozi 2,000 nchini humo zimefikishwa Bulape, kitovu cha mlipuko huo.

Marekani yapiga kura ya 6 ya turufu kwa Umoja wa Mataifa kuhusu vita vya Gaza

.

Marekani imepiga kura ya turufu siku ya Alhamisi katika mswada wa azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambalo lingetaka usitishaji vita mara moja, usio na masharti na wa kudumu huko Gaza na kwamba Israel iondoe vikwazo vyote vya kupeleka misaada kwa wapalestina.

Mswada huo uliyoandaliwa na wajumbe 10 waliochaguliwa wa baraza la wanachama 15, pia ungetaka kuachiliwa mara moja, kwa heshima na bila masharti mateka wote wanaoshikiliwa na Hamas na makundi mengine.

Ulipata kura 14 za ndio. Ilikuwa ni mara ya sita kwa Marekani kupiga kura ya turufu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu vita vya takriban miaka miwili kati ya Israel na Hamas.

“Njaa imethibitishwa huko Gaza – haijakadiriwa, haijatangazwa, alithibitishwa,” Balozi wa Denmark wa Umoja wa Mataifa Christina Markus Lassen akiambia baraza kabla ya kupiga kura.

“Wakati huo huo, Israel imepanua operesheni yake ya kijeshi katika Mji wa Gaza, na hivyo kuzidisha mateso ya raia. Matokeo yake, ni hali hii ya janga, kushindwa kwa binadamu ambako kumetulazimisha kuchukua hatua leo,” alisema.

Mji wa Gaza na maeneo yanayozunguka yanakabiliwa rasmi na njaa, na huenda ikaenea, wafuatiliaji wa njaa duniani walibainisha mwezi uliopita.

Vikwazo vya Umoja wa Mataifa kwa Iran vitarudishwa, asema Rais Macron

.

Mataifa yenye nguvu ya Ulaya huenda yakaiwekea tena Iran vikwazo vya kimataifa ifikapo mwisho wa mwezi baada ya duru ya hivi karibuni ya mazungumzo na Iran kuzingatiwa kutochukuliwa kwa uzito unaostahili, Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron alisema siku ya Alhamisi.

Uingereza, Ufaransa na Ujerumani, zinazojulikana kama E3, zilizindua mchakato wa siku 30 mwishoni mwa Agosti kurejesha vikwazo vya Umoja wa Mataifa. Waliweka masharti kwa Iran kuyatimiza mnamo mwezi wa Septemba.

Pendekezo la E3 la kuahirisha mazungumzo hayo kwa hadi miezi sita ili kuwezesha kuwa ya kina ni masharti kwa Iran kuruhusu ufikiaji wa wakaguzi wa nyuklia wa UN – ambao pia watajaribu kuangalia kiasi cha hifadhi ya Iran ya madini ya uranium yaliorutubishwa – na kushiriki katika mazungumzo na Marekani.

Alipoulizwa katika mahojiano kwenye Idhaa ya Channel 12 ya Israel ikiwa hatua hiyo ilikuwa imekubaliwa, Macron alisema:

“Ndiyo. Nafikiri hivyo kwa sababu taarifa za hivi punde kutoka kwa Wairani hazina uzito unaostahili.”

Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas Araqchi alisema baadaye siku ya Alhamisi kwamba aliwasilisha “mpango wa busara na unaoweza kutekelezeka kwa washirika wa E3/EU ili kuepusha mgogoro usio wa lazima na unaoweza kuepukika katika siku zijazo.”

Mawaziri wa mambo ya nje wa E3, mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya na mwenzao wa Iran walipigiana simu siku ya Jumatano ambapo wanadiplomasia wa pande zote mbili walisema hakukuwa na maendeleo makubwa ingawa bado kuna fursa ya kufikia makubaliano kabla ya muda uliowekwa kufikia ukomo wake.

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lenye wanachama 15 litapiga kura siku ya Ijumaa kuhusu azimio litakaloondoa kabisa vikwazo vya Umoja wa Mataifa dhidi ya Iran – hatua ambayo inatakiwa kuchukuliwa baada ya E3 kuanzisha mchakato huo.

Azimio hilo huenda likashindwa kupata kiwango cha chini cha kura tisa zinazohitajika kupitisha, wanasema wanadiplomasia, na kama litapishwa huenda likapigiwa kura ya turufu na Marekani, Uingereza.

Uingereza yazindua tovuti maalum kuvutia majasusi wa Urusi

.

Shirika la Ujasusi la Uingereza la MI6 limezindua tovuti maalum kwa matumaini ya kuvutia majasusi wapya mtandaoni, haswa kutoka Urusi.

Jukwaa salama la kutuma ujumbe Silent Courier linalenga kuimarisha usalama wa taifa na kurahisishia shirika la ujasusi kuajiri, Ofisi ya Mambo ya Nje ya Uingereza ilisema.

Mawakala nchini Urusi na ulimwenguni kote watalengwa na Uingereza, tovuti hiyo inaongeza.

Tangazo hilo linatarajiwa kuthibitishwa katika hotuba mjini Istanbul na mkuu wa shirika la MI6 anayeondoka Sir Richard Moore siku ya Ijumaa asubuhi.

Kabla ya tangazo la Ijumaa kuhusu tovuti hiyo mpya, Waziri wa Mambo ya Nje Yvette Cooper alisema: “Usalama wa kitaifa ni jukumu la kwanza la serikali yoyote na msingi wa Mpango wa Mabadiliko wa Waziri Mkuu.

“Dunia inapobadilika, na vitisho vinavyotukabili vinapoongezeka, lazima tuhakikishe kwamba Uingereza daima iko hatua moja mbele ya maadui zetu.

“Mashirika yetu ya kijasusi ya kiwango cha juu duniani yanakabiliwa na changamoto hii, yakijitahidi kwa kila namna kuhakikisha Usalama wa Waingereza.

“Sasa tunaimarisha juhudi zao kwa teknolojia ya hali ya juu ili MI6 iweze kuajiri majasusi wapya wa Uingereza – nchini Urusi na duniani kote.”

Waliofurushwa Marekani waishtaki Ghana kwa kuwekwa kizuizini kinyume cha sheria

.

Watu 11 waliozuiliwa nchini Ghana baada ya kufukuzwa kutoka Marekani wameishtaki serikali ya taifa hilo la Afrika Magharibi, wakili wao ameiambia BBC.

Oliver-Barker Vormawor alisema waliofukuzwa hawakukiuka sheria yoyote ya Ghana, na kuzuiliwa kwao katika kambi ya kijeshi ni kinyume cha sheria.

Alitaka serikali iwafikishe watu hao mahakamani, na kusema kwa nini wanashikiliwa kinyume na matakwa yao, wakili huyo aliongeza.

Serikali bado haijatoa maoni yoyote kuhusu kesi hiyo, lakini hapo awali ilisema inapanga kuwapokea watu wengine 40 waliofukuzwa nchini Marekani.

Wabunge wa upinzani wanadai kusitishwa mara moja kwa mpango wa kuwapokea kuliofukuzwa hadi bunge litakapoidhinisha suala hilo, wakisema hatua hii inahitajika chini ya sheria za Ghana.

Bangili ya miaka 3,000 iliibiwa na kuyeyushwa, Misri yasema

.

Bangili ya dhahabu ya miaka 3,000 ambayo ilitoweka kwenye Jumba la Makumbusho la Misri huko Cairo iliibiwa na kuyeyushwa, wizara ya mambo ya ndani ya Misri inasema.

Mtaalamu wa uhuishaji alichukua bangili hiyo – ambayo ilianzia enzi ya Mfalme Amenemope, farao aliyetawala Misri karibu 1,000BC – kutoka kwa sefu kwenye jumba la makumbusho siku tisa zilizopita, kulingana na wizara.

Mwanamke aliyeiba bangili hiyo aliwasiliana na sonara wa vito vya fedha aliyemjua, ambaye naye pia, aliuza bangili hiyo kwa sonara wa vito vya dhahabu kwa $3,735 (£2,750), Wizara ilisema.

Kisha akaiuza kwa $4,025 kwa mfanyakazi wa kutengeneza vitu vya dhahabu, ambaye alikuwa ameiyeyusha na vito vingine, taarifa iliyotolewa iliongeza.

Wizara hiyo ilisema watu hao wanne walikiri makosa yao baada ya kukamatwa na kwamba pesa hizo zilinaswa.

All Rights Reserved © The Cantona Group PLC||2025


Discover more from cantonadigital

Subscribe to get the latest posts sent to your email.

Leave a comment