Utawala wa Trump waidhinisha msaada wa silaha wa Ukraine uliolipiwa na washirika, duru zinasema

Radio Fortune Africa -Na Cantona Joseph

https://zeno.fm/radio/radio-fortune-africa

Vifurushi vya kwanza vya msaada wa silaha za Marekani kwa utawala wa Trump kwa Ukraine vimeidhinishwa na vinaweza kusafirishwa hivi karibuni wakati Washington inaanza tena kutuma silaha Kyiv, Reuters inaripoti.

Wakati huu hatua hiyo inafanyika chini ya makubaliano mapya ya kifedha na washirika – vyanzo viwili vinavyofahamu hali hiyo viliiambia Reuters.

Huu ni utaratibu mpya wa Marekani na washirika wa kuipatia Ukraine silaha kutoka kwa hifadhi za Marekani kwa kutumia fedha kutoka nchi za NATO.

Ushirikiano huo mpya ambao unalenga kuimarisha Kyiv kwa silaha zenye thamani ya dola bilioni 10, unakuja wakati Rais wa Marekani Donald Trump ameelezea kuchoshwa na mashambulizi yanayoendelea ya Moscow dhidi ya jirani yake licha ya juhudi zake za kumaliza mzozo huo kwa njia ya mazungumzo.

Kufikia sasa, utawala wa Trump umeuza silaha kwa Ukraine pekee au kutuma misaada ambayo iliidhinishwa na Rais wa zamani Joe Biden, ambaye alikuwa akipendelea Ukraine.

Vyanzo hivyo vilikataa kutoa hesabu kamili ya kile ambacho kimeidhinishwa kununuliwa kwa ajili ya Ukraine, lakini vilisema ni pamoja na mifumo ya ulinzi wa anga, ambayo Ukraine inahitaji haraka kutokana na ongezeko kubwa la mashambulizi ya ndege zisizo na rubani na makombora ya Urusi.

Wabunge Uganda wataka serikali kulinda wanaofanyakazi nje ya nchi, baada ya uchunguzi wa BBC Africa Eye

.

Wabunge wa Uganda wameiomba serikali kuwalinda raia wa Uganda wanaofanya kazi nchi za nje, baada ya uchunguzi wa BBC Africa Eye, uliofichua mwanamume anayeendesha mtandao wa biashara ya ngono kutoka kwenye maeneo ya kifahari ya Dubai, akiwanyanyasa wanawake walio katika mazingira magumu.

Uchunguzi wa BBC umeonyesha jinsi Charles Mweisgwa, mzaliwa wa Uganda na dereva wa zamani wa basi la London anaendesha mtandao wa ukahaba huko Dubai ambao unawatumia vibaya wanawake wadogo wa Uganda.

Wabunge wameitaka wizara ya jinsia ya nchi hiyo kutoa taarifa kamili kuhusu unyanyasaji wa wafanyikazi wahamiaji wa Uganda.

Mheshimiwa Henry Oryem Okello, Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo ameiambia BBC kupitia simu kwamba serikali inachunguza suala hilo kwa kushirikiana na Ubalozi wake nchini UAE. Pia alisema mamlaka zinachukua hatua zaidi kumkamata mtuhumiwa. [Mweisgwa]

“Tutawaomba polisi wetu hapa pia wawasiliane na polisi katika UAE ili kujua ukweli wa suala hili. Ikiwa polisi watagundua kuwa ni kesi ya kufunguliwa mashtaka, tunataka ashtakiwe.” Aliiambia BBC.

Wakati wa kikao hicho, naibu msemaji wa nchi hiyo Thomas Tayebwa ameiambia Bunge kwamba kuna haja ya mamlaka kutatua suala la unyanyasaji wa wafanyikazi wa Uganda katika Mashariki ya Kati.

“Serikali inawajibika kwa raia wake mahali walipo, hata ikiwa wako chini ya sheria fulani katika nchi tofauti, serikali inapaswa kuingilia kati.” Alisema.

.
Maelezo ya picha,Charles Mwesigwa anayeendesha mtandao wa biashara ya ngono

Mshukiwa wa Charlie Kirk alikiri kufanya mauaji katika ujumbe aliomuandikia mwenzake

.

Mwanamume anayeshutumiwa kwa kumpiga risasi Charlie Kirk amekiri kumuua mwanaharakati huyo wa mrengo wa kulia katika ujumbe aliomuandikia mwenzake, waendesha mashitaka wamedai, huku wakitangaza mashtaka saba dhidi yake.

Tyler Robinson, 22, aliacha barua chini ya baobonye ili mwenzake ajue alichofanya, alisema Wakili wa Kaunti ya Utah Jeffrey Gray akiongeza kuwa mwenzake huyo alikuwa mpenzi wa mshtakiwa.

Kulingana na Bw Gray, barua hiyo ilisema: “Nilipata fursa ya kumuondoa Charlie Kirk, na nimeitumia.”

Mwendesha mashtaka pia alituma ujumbe wa maandishi kati ya wawili hao ikiwa ni pamoja na mmoja ambao mshtakiwa alisema kuwa alimpiga risasi Kirk kwa sababu “namchukia sana”.

Mshukiwa anazuiliwa bila dhamana katika kitengo maalum cha makazi katika jela ya kaunti ya Utah. Alifikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza Jumanne, huku waendesha mashtaka wakisoma mashtaka saba dhidi yake.

Mashitaka hayo ni mauaji ya kuchochewa, kukutwa na silaha, makosa mawili ya kuzuia haki, makosa mawili ya kuharibu ushahidi, na kufanya uhalifu wa kutumia nguvu wakati watoto wapo.

Kenya yamfungulia mashtaka Feisal ya biashara za pembe za faru aliyefungwa jela 2018 kwa kusafirisha pembe za ndovu

.

Mahakama ya Kenya jana Jumanne ilimshtaki mwanamume mmoja kwa biashara ya pembe mbili za faru zenye thamani ya shilingi milioni 8.2 za Kenya (dola 63,000), miaka tisa baada ya kufungwa jela kwa kusafirisha pembe za ndovu.

Feisal Mohamed Ali na mshukiwa mwenzake Mohammed Hassan walikamatwa katika mji wa bandari wa Mombasa mwezi uliopita.

Siku ya Jumanne, wawili hao walikana shtaka la kuhusika na wanyamapori walio hatarini kutoweka.

Ali aliachiliwa baada ya kukata rufaa mwaka wa 2018, miaka miwili ndani ya kipindi cha miaka 20 alichohukumiwa kwa ulanguzi wa pembe za ndovu, kutokana na dosari za utaratibu katika kesi hiyo.

Polisi walikuwa wamemshutumu kwa kuhusika na kundi la kimataifa la uwindaji haramu lililohusishwa na kunaswa kwa meno 120 ya ndovu.

Iran yamhukumu kunyongwa mtu anayetuhumiwa kufanya ujasusi wa Israel

Iran imemhukumu kunyongwa mtu aliyetuhumiwa kufanya ujasusi kwa ajili ya Israel, kulingana na ripoti kutoka kwa vyombo vya habari vya serikali siku ya Jumatano aliyetambulishwa kama Babak Shahbazi.

Iran imetoa hukumu ya kifo kwa watu wengi inaowatuhumu kuwa na uhusiano na idara ya kijasusi ya Israel ya Mossad na kuwezesha shughuli zake nchini humo.

Visa vya hukumu ya kunyongwa kwa Wairani waliopatikana na hatia ya kufanya ujasusi kwa ajili ya Israel vimeongezeka kwa kiasi kikubwa mwaka huu, huku takriban hukumu tisa za vifo zikitekelezwa katika miezi ya hivi karibuni.

Vyombo vya habari vya serikali vilisema Shahbazi alifanya kazi na Esmaeil Fekri, mfungwa mwingine aliyenyongwa mwezi Juni kwa kufanya ujasusi wa Israel tangu mapema 2022.

Shahbazi alishtakiwa kwa kutumia wadhifa wake kama mwanakandarasi anayeweka vifaa vya kupozea ili kukusanya taarifa kutoka sehemu nyeti na vituo vinavyohusishwa na jeshi na vyombo vya usalama.

Wakili wa mshtakiwa alikuwa ameomba kukata rufaa kwa Mahakama ya Juu Zaidi, ambayo ilikataa ombi hilo.

All Rights Reserved © The Cantona Group PLC||2025


Discover more from cantonadigital

Subscribe to get the latest posts sent to your email.

Leave a comment