Radio Fortune Africa -Na Cantona Joseph
https://zeno.fm/radio/radio-fortune-africa

Erika Kirk awashukuru maafisa na Donald Trump baada ya mtuhumiwa wa mauaji Tyler Robinson kukamatwa Alhamisi akiwa ametafutwa kwa masaa 33.
Mjane wa Charlie Kirk, Erika, ametoa hotuba iliyotoa wengi machozi ambapo aliwashukuru waliojaribu kutoa huduma ya kwanza kuokoa maisha ya mumewe baada ya kupigwa risasi kwenye chuo kikuu cha Utah.
Katika tukio hilo lililoonyeshwa moja kwa moja, akiwa amesimama kando ya kiti cha mumewe ambacho alikuwa ameketi kabla ya kupigwa risasi lakini wakati huu kikiwa hakina mtu, alinukuu Biblia na kuzungumza kuhusu upendo wake kwa Rais Donald Trump, Makamu wa Rais JD Vance, Marekani na watoto wao wawili.
Katika maelezo yake, Bi Kirk aliahidi: “Sauti ya mume wangu itaendelea kusikika.”
Tukio hilo lililofanyika katika makao makuu ya shirika la Turning Point USA huko Arizona lililoanzishwa na mume wake, Charlie Kirk.
Tukio hilo lilianza kimya cha dakika kadhaa, huku kamera ikielekezwa kwenye kiti kisichokuwa na mtu cha Charlie Kirk.
Mkewe alipoanza kuzungumza, alitazama juu na kuomba sala kimya kimya.
Kisha akawashukuru waliojaribu kwanza kumwokoa mume wake, wafanyakazi, na Ikulu ya Marekani.
“Mheshimiwa Rais, mume wangu alikupenda. Na alijua kwamba unampenda pia,” alisema huku akitokwa na machozi, na pia kuwashukuru Vance na mkewe Usha kwa kuandamana na msafara wa jeneza hadi Arizona.
“Lakini zaidi ya yote, Charlie aliwapenda watoto wake. Na alinipenda. Kwa moyo wake wote. Na alihakikisha kuwa nilijua hilo kila siku.”
Akihutubia “watenda maovu”, Bi Kirk alisema: “Hujui ni moto kiasi gani ambao umewasha ndani yangu, kilio cha mjane huyu kitasikika kote ulimwenguni kama kilio cha vita.
“Wote wanapaswa kujua hili: ikiwa ulifikiri kwamba misheni ya mume wangu ilikuwa na nguvu, hujui ni nini umekianzisha katika nchi hii nzima na duniani.”
Ziara ya mume wake katika vyuo vikuu vya Marekani itaendelea katika msimu wa vuli, na katika miaka ijayo, alisema, bila kutoa maelezo zaidi. Podikasti yake pia itaendelea.
Bi Kirk pia alizungumza kuhusu mtoto wao wa kiume mwenye umri wa mwaka mmoja na binti wa miaka mitatu, akisema kwamba hajui jinsi ya kuelezea kifo cha ghafla cha baba yao.
“Mtoto wangu, baba yako anakupenda sana. Ameenda safari ya kikazi na Yesu” alimwambia binti yao.
Bi Kirk, 36, na watoto wao waliripotiwa kuwa kwenye hadhira wakati mumewe alipopigwa risasi.
Erika Kirk ni mfanyabiashara na mshindi wa zamani wa Miss Arizona USA, ambaye alikutana na mumewe mwaka wa 2018.
Wenzi hao walikuwa wamechumbiana kufikia 2020 na walifunga ndoa chini ya mwaka mmoja baadaye.
Mshukiwa wa mauaji ya Charlie Kirk yuko kizuizini baada ya kukiri kwa baba yake

Kijana wa miaka 22 kutoka Utah amekamatwa kwa mauaji ya mwanaharakati wa mrengo wa kulia Charlie Kirk, ambaye alipigwa risasi akiwa jukwaani kwenye hafla ya chuo kikuu mapema wiki hii.
Tyler Robinson aliwekwa kizuizini siku ya Alhamisi usiku, baada ya msako wa saa 33 ambao ulikamilika babake aliposaidia kumshawishi ajisalimishe kwa polisi.
Kukamatwa kwake kulitangazwa kwa mara ya kwanza na Rais wa Marekani Donald Trump, ambaye alimtaka mshukiwa huyo kukabiliwa na hukumu ya kifo.
Mauaji ya Kirk, ambaye alipigwa risasi alipokuwa akijadiliana na wanafunzi siku ya Jumatano, yamewashtua Wamarekani na kuweka wazi migawanyiko mikali juu ya vyama nchini humo.
Wachunguzi walisema katika kikao na wanahabari siku ya Ijumaa kwamba mshukiwa alikiri kwa baba yake na kusema afadhali ajiue badala ya kujisalimisha. Kisha baba huyo alimwita mchungaji kijana ambaye ni rafiki wa familia.
Wote wawili walijaribu kumtuliza mshukiwa, polisi walisema. Mchungaji huyo, ambaye pia anahudumu kama afisa wa usalama wa mahakama, baadaye aliwapigia simu wanajeshi wa Marekani, ambao walimshika mshukiwa mwendo wa saa 22:00 kwa saa za eneo siku ya Alhamisi.
Gavana wa Utah Spencer Cox alisema kuwa picha za uchunguzi zilionyesha Bw Robinson akiwasili katika chuo kikuu cha Utah Valley takriban saa nne kabla ya tukio la mlio wa risasi kushuhudiwa, na kumuua Kirk huku wanafunzi kukikimbia kujificha.
Cox aliwaambia waandishi wa habari kwamba wakati Bw Robinson aliwekwa kizuizini, alikuwa amevalia mavazi sawa na yale yaliyoonekana kwenye kamera za CCTV katika eneo la ufyatuaji risasi.
Gavana huyo aliongeza kuwa wachunguzi walimhoji mwanafamilia, ambaye alisema mshukiwa huyo amekuwa wa siasa kali katika miaka ya hivi majuzi.
Cox alisema mwanafamilia huyo alizungumza kuhusu tukio la hivi majuzi wakati Bw Robinson alipotaja kwamba Kirk alikuwa anakuja Utah na kwamba “alikuwa amejaa chuki na kueneza chuki”.
Cox alisema wachunguzi pia walikuwa wamezungumza na mshukiwa aliyeishi naye chumba kimoja ambaye aliwaonyesha ujumbe waliobadilishana naye kwenye akaunti inayoitwa “Tyler” kwenye programu ya ujumbe ya Discord.
Jumbe hizo zilirejelea hitaji la kupata bunduki kutoka “sehemu moja” na bunduki hiyo kuachwa kwenye kichaka, ikiwa imefungwa kwa taulo.
FBI walisema siku ya Alhamisi kwamba walipata silaha inayoshukiwa kuwa – bunduki aina ya Mauser .30-06 bolt action – ikiwa imefungwa kwa taulo katika eneo lenye miti karibu na chuo kikuu.
Quad yatoa wito wa usitishaji mapigano huko Sudan

Marekani, Misri, Saudi Arabia na UAE kwa pamoja wametoa wito wa kusitishwa mapigano kwa miezi tatu huko Sudan hatua ambayo itakuwa mwanzo wa usitishaji mapigano wa kudumu na kukaribisha kipindi cha mpito cha miezi 9 hadi kupatikana kwa serikali ya raia.
Mawaziri wa Mambo ya nje kutoka Kikundi cha Mataifa kinachojulikana kama Quad walikutana huko Washington na kukubaliana kutumia ushawishi wao kusaidia kutafuta makubaliano ya usitishaji mapigano na pande husika – vikosi vya jeshi la Sudan na Rapid Support Forces.
Mawaziri hao hata hivyo walisema hakuna upande wowote unaozozana utakaosimamia kipindi cha mpito hadi kupatikana kwa serikali ya kiraia.
Quad pia ilisisitiza hitaji la Sudan kusalia na umoja na kuwa msaada wa jeshi kutoka nchi za nje ukomeshwe kwa pande zote mbili.
UAE, mwanachama wa Quad, ameshtumiwa kwa kuunga mkono RSF, shutuma ambazo imekanusha mara kwa mara.
Jeshi la Sudan na RSF wameanzisha serikali mbadala zenye mawaziri wakuu na makatibu katika wiki za hivi karibuni.
Kundi hilo la mawaziri lilisema kwamba hali ilivyo sasa hivi “inasababisha mateso yasiyokubalika” na kuongeza kuwa uingiliaji wa kijeshi hakuwezi kuleta suluhu.
Vita huko Sudan viliibuka mnamo Aprili 2023 kati ya jeshi la nchi hiyo na kikosi cha wanajeshi wanaotembea kwa miguu cha RSF.
Mzozo huo umesababisha matatizo makubwa ya kibinadamu ulimwenguni, makumi ya maelfu wakiuawa huku mamilioni wakilazimika kuhama makazi yao.
Watu wafa maji baada ya boti kuzama DR Congo

Karibu watu 200 wamekufa maji huku wengine wakiwa hawajulikani walipo kufuatia ajali mbili tofauti za mashua katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kaskazini Magharibi mwa Congo.
Kikundi cha asasi za kiraia kimelaumu serikali na kudai idadi ya walioaga dunia ni kubwa.
Timu za uokoaji bado zinatafuta manusura kufuatia ajali mbaya katika mkoa wa equateur wiki hii.
Karibu watu 150 bado hawajapatikana kufuatia moto kwenye mashua Alhamisi usiku kabla ya kuzama kwenye mto wa Congo.
Siku iliyopita ajali tofauti iliua abiria zaidi ya 80, haswa wanafunzi. Ripoti zinasema chombo hicho kilikuwa kimebeba abiria wengi kupita kiasi.
Mahakama ya Colombia yasema Meta alikosea kwa kufunga akaunti ya Instagram ya nyota wa ponografia

Mahakama ya juu zaidi nchini Colombia imetoa uamuzi na kusema kuwa Meta ilikiuka haki ya uhuru wa kujieleza wa nyota wa ponografia ilipofuta akaunti yake ya Instagram.
Mahakama ya Kikatiba ya taifa la Amerika Kusini ilisema Ijumaa kwamba Meta iliondoa akaunti ya Esperanza Gómez “bila sababu ya msingi” na bila kufanya kama hivyo kwa akaunti zingine zenye maudhui sawa na yake.
Mwanamke huyo mwenye umri wa miaka 45, ambaye akaunti yake ilikuwa na wafuasi zaidi ya milioni tano, ni mmoja wa waigizaji maarufu wa maudhui ya watu wazima nchini Colombia.
Meta alisema katika kesi hiyo kwamba alikuwa amekiuka sheria zake kuhusu uchi. Kampuni hiyo, ambayo pia inamiliki Facebook na WhatsApp, haikujibu mara moja uamuzi huo.
Rubani wa Nigeria athibitishwa amekunywa kileo baada ya ndege kuacha njia

Rubani na rubani mwenza wamepimwa na kuthibitishwa kuwa wamekunya pombe baada ya ndege waliyokuwa wakiendesha kuacha njia ilipokuwa ikitua nchini Nigeria.
Ofisi ya Uchunguzi wa Usalama wa Nigeria (NSIB) iliwachunguza wawili hao baada ya kutokea kwa ajali mwezi Julai, katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Port Harcourt. Vile vile, mfanyakazi wa ndege hiyo alipimwa na kukutwa ametumia bangi.
Watu wote 103 waliokuwa kwenye ndege hiyo aina ya Boeing 737 wakati kisa hicho kinatokea hawakudhurika.
Kampuni ya Air Peace, iliyoendesha ndege hiyo, ilisema rubani huyo mwenye umri wa miaka 64 amefutwa kazi kwa kushindwa kuzingatia kanuni za usalama, wakati rubani msaidizi amerejea kwenye jukumu lake.
All Rights Reserved © The Cantona Group PLC||2025
Discover more from cantonadigital
Subscribe to get the latest posts sent to your email.