Radio Fortune Africa -Na Cantona Joseph
https://zeno.fm/radio/radio-fortune-africa

Msemaji wa kundi la wapiganaji la Hamas, Abu Obeida, ameuawa katika shambulizi la anga katika mji wa Gaza, Israel imesema.
Waziri wa Ulinzi wa Israel Israel Katz alipongeza Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) na shirika wa usalama wa Israel, Shin Bet, kwa “utekelezaji sahihi” wa mauaji hayo kwenye ujumbe wake katika mtandao wa X.
Hata hivyo, Hamas bado haijathibitisha kifo cha Abu Obeida. Kundi la wapiganaji wa Palestina hapo awali lilisema makumi ya raia waliuawa na kujeruhiwa katika mashambulizi ya anga ya Israeli kwenye jengo la makazi katika wilaya hiyo.
Waandishi wa habari wa eneo hilo waliripoti kuwa takriban watu saba wameuawa na wengine 20 kujeruhiwa katika mashambulizi hayo katika kitongoji chenye wakazi wengi cha al-Rimal katika mji wa Gaza, huku watoto wakiwa miongoni mwa waliojeruhiwa.
Shambulio hilo la Jumamosi limetokea huku kukiwa na mashambulizi ya anga yanayoendelea katika mji wa Gaza kabla ya mashambulizi yaliyopangwa na Israel.
Katz alionya Jumapili kwamba wengi zaidi “walioshirikiana na Obeida katika uhalifu” wangelengwa katika ” kampeni inayoendelea huko Gaza” – akirejelea mpango ulioidhinishwa hivi karibuni wa Israeli wa kutwaa udhibiti wa jiji la Gaza.
IDF na Shin Bet walitoa maelezo zaidi kuhusu shambulizi la siku ya Jumamosi ambalo lililenga msemaji wa Hamas.
Rais wa China azungumzia ‘tabia ya uonevu’ katika utaratibu wa dunia

Rais wa China Xi Jinping amepinga kile alichokiita ‘tabia ya uonevu’ katika utaratibu wa ulimwengu wakati akitoa hotuba katika mkutano muhimu wa usalama na kiuchumi kaskazini mwa China wa Shirika la Ushirikiano la Shanghai (SCO).
Katika kile kinachoonekana kama ukosoaji wa Marekani, Bwana Xi alitoa wito kwa viongozi zaidi ya ishirini wa dunia waliohudhuria mkutano huo kupinga kile alichokiita ‘fikra za Vita Baridi’.
China na Urusi ziliwahi kusema Shirika la Ushirikiano la Shanghai (SCO) ni njia mbadala ya Ushirikiano wa Jeshi la NATO.
“Hali ya sasa ya kimataifa inakuwa ya machafuko,” Xi aliwaambia viongozi.
“Majukumu ya usalama na maendeleo yenye kukabili nchi wanachama yamekuwa magumu zaidi,” aliongeza.
“Ukitazama siku zijazo, huku ulimwengu ukiwa unapitia msukomsuko na mabadiliko, lazima tuendelee kufuata ari ya SCO, kuwa makini, kufikiria mbele na kufanya maamuzi mazuri, na kushirikiana vizuri kama shirika,” Rais wa Xi Jinping alisema.
Marufuku ya kutotoka nje yawekwa katika maeneo yenye ghasia za kikabila Kenya

Mamlaka nchini Kenya imeweka marufuku ya kutotoka nje kwa siku saba kuanzia jioni hadi alfajiri katika baadhi ya sehemu za kaunti ya Nakuru baada ya kuanza kwa ghasia za kikabila.
Takriban mtu mmoja ameuawa na wengine wanane kujeruhiwa huku nyumba takriban 12 zikichomwa moto kufuatia mapigano ya kikabila huko Tipis na maeneo ya Mwisho wa Lami.
Vurugu hizo, ambazo ziliibuka Jumamosi katika mpaka wa Nakuru -Narok, zilisababisha familia kadhaa kuhama makazi yao baada ya washambuliaji kuchoma moto nyumba na mali.
Kufikia jana Jumapili 30/08/2025, hali ya wasiwasi bado ilikuwa juu wakaazi walipofunga sehemu za Barabara ya Nakuru -Narok huko Mwisho Wa Lami, wakipinga mauaji hayo na kudai serikali iingilie kati.
Kufuatia ghasia hizo, serikali imepeleka maafisa wa usalama eneo hilo kurejesha utulivu.
Waasi wa Houthi wavamia majengo ya UN nchini Yemen

Waasi wa Yemen wanaoungwa mkono na Iran wa Houthi walivamia ofisi za Umoja wa Mataifa katika mji mkuu wa Yemen Sanaa siku ya Jumapili na kuwaweka kizuizini takriban wafanyakazi 11 wa Umoja huo, shirika hilo lilisema.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alisema Wahouthi waliingia kwa nguvu katika majengo ya Mpango wa Chakula Duniani (WFP), wakateka mali ya Umoja wa Mataifa na kujaribu kuingia katika ofisi nyingine za Umoja huo katika mji mkuu.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alisema Wahouthi waliingia kwa nguvu katika majengo ya Mpango wa Chakula Duniani (WFP), wakachukua mali ya Umoja wa Mataifa na kujaribu kuingia katika ofisi nyingine za Umoja huo katika mji mkuu.
Mjumbe Maalumu wa Umoja wa Mataifa kwa Yemen Hans Grundberg alisema katika taarifa tofauti kwamba wafanyakazi hao 11 walizuiliwa huko Sanaa na mji wa bandari wa Hodeidah.
Grundberg alisema kuzuiliwa kwao ni pamoja na wafanyikazi wengine 23 wa UN waliowekwa kizuizini hapo awali, wengine tangu 2021, na mmoja ambaye alikufa kizuizini mwaka huu.
Wawekezaji wa kashfa kubwa zaidi ya vito Uingereza walalamikia ukosefu wa uchunguzi rasmi

Wawekezaji ambao walipoteza zaidi ya dola milioni mia moja na thelathini katika kashfa kubwa zaidi ya vito nchini Uingereza wameiambia BBC hawaelewa ni kwanini hakukuwa na uchunguzi rasmi.
Vashi Dominguez, mtu mashuhuri wa Uhispania anadaiwa kudanganya watu kwa akaunti za uwongo na madai ya kuwa na hifadhi kubwa ya almasi.
Alitoweka wakati kampuni yake ilipofilisika kwa madeni ya zaidi ya dola milioni mia mbili. Bwana Dominguez aliripotiwa kwa mamlaka lakini polisi wanasema kesi hiyo bado haijawasilishwa kwao na wasimamizi wa fedha.
Mmoja wa wale waliopoteza pesa, Michael Moszynski amesema kushindwa kuchunguza udanganyifu mkubwa kama huo kunaweza kuwazuia wengine kuwekeza nchini Uingereza.
Umati wamuua mwanamke mmoja kwa madai ya kukufuru nchini Nigeria

Mwanamke mmoja ameshambuliwa na kuchomwa moto na kuuawa na umati wa watu katikati mwa Nigeria kwa madai ya kukufuru dhidi ya Mtume Muhammad.
Mauaji hayo yamesababisha hasira mpya juu ya haki ya umati nchini humo.
Kulingana na polisi wa Nigeria, mwanamke huyo – aliyetambuliwa kama muuzaji wa chakula anayeitwa Amaye – alishambuliwa na umati wa watu katika jamii ya Kasuwan -Garba Jumamosi jioni.
Ripoti za vyombo vya habari vya ndani zinaonyesha tukio hilo lilianza wakati mteja alipendekeza ndoa kwa utani kwa mwanamke huyo, akitoa mfano wa mila ya Kiisilamu.
Jibu lake lilidaiwa kukufuru. Umati wenye hasira ulimshambulia na kumuua huku viongozi wakishindwa kumlinda.
Mauaji ya umati ni kawaida kaskazini mwa Nigeria, ambapo kukufuru huonekana kama kosa la jinai chini ya sheria ya Kiislamu.

Hata hivyo, sio mara ya kwanza tukio kama hilo kutokea. Mnamo 2022, mwanafunzi Deborah Samweli alipigwa na kuchomwa moto huko Sokoto baada ya kutuhumiwa kutoa maoni ya kukufuru.
Na mwaka jana tu, muuzaji nyama Usman Buda, alipigwa mawe hadi kufa katika jimbo moja katika hali kama hiyo.
Nyumba za zama chini ya vifusi katika tetemeko la ardhi Afghanistan

Vyanzo vingi vya habari kutoka kwa serikali ya Taliban vimeiambia BBC kwamba “Nyumba kadhaa ziko chini ya vifusi” na sasa inahofiwa kuwa mamia ya watu wanaweza kuwa wameuawa na kujeruhiwa katika tetemeko la ardhi lililotekea mashariki mwa Afghanistan. Hili bado halijathibitishwa rasmi.
Inaaminika kuwa nyumba nyingi zimeharibiwa katika bonde la Mazar, wilaya ya Norgal ya jimbo la Kunar ambalo lipo katika mpaka na Pakistan.
Bonde hilo liko katika eneo la milimani.
Hadi kufikia sasa watu 20 wamethibitishwa kuuawa katika tetemeko hilo.
Mshukiwa wa mauaji ya mwanasiasa mwandamizi wa Ukraine akamatwa

Mshukiwa wa mauaji ya mwanasiasa mashuhuri wa Ukraine Andriy Parubiy amekamatwa, Rais wa nchi hiyo Volodymyr Zelensky amesema.
Mbunge huyo mwenye umri wa miaka 54 aliuawa na mshambuliaji aliyejifanya mjumbe katika mji wa magharibi wa Lviv siku ya Jumamosi, na kusababisha msako mkali.
Waziri wa mambo ya ndani wa Ukraine Igor Klymenko alisema katika taarifa yake aliyoitoa alfajiri ya Jumatatu kwamba mshukiwa amezuiliwa katika eneo la Khmelnytskyi magharibi.
Parubiy alipata umaarufu wakati wa maandamano makubwa ya Ukraine ya Euromaidan, ambayo yalitetea uhusiano wa karibu na EU na kumwangusha Rais wa zamani wa Urusi Viktor Yanukovych mnamo 2014.
Klymenko alisema uchunguzi wa awali umegundua mauaji hayo “yalipangwa kwa makini” na kuzingatia ratiba ya safari ya Parubiy na njia ikapangwa pamoja na mpango wa kutoroka.
Aliongeza kuwa jeshi la polisi la taifa la Ukraine litatoa maelezo zaidi baadaye.
Katika ujumbe kwenye mtandao wa kijamii, Zelensky alisema alikuwa amezungumza na mwendesha mashtaka mkuu Ruslan Kravchenko ambaye alisema kwamba mshukiwa ametoa ushahidi wa awali.
Mamia wahofiwa kufariki baada ya tetemeko la ardhi mashariki mwa Afghanistan

Zaidi ya watu 20 wamefariki dunia baada ya tetemeko la ardhi la kipimo cha 6.0 kupiga mashariki mwa Afghanistan, karibu na mpaka wake na Pakistan, maafisa wa eneo hilo wamethibitisha kwa BBC.
Zaidi ya watu 115 waliojeruhiwa wamepelekwa hospitali katika majimbo ya Nangarhar na Kunar, maafisa walisema.
Tetemeko hilo la kina kirefu cha kilomita 8 (maili 5), lilitokea saa 23:47 saa za eneo (19:17 GMT) siku ya Jumapili, kulingana na Utafiti wa Jiolojia wa Marekani. Tangu wakati huo, kumetokea takriban mitetemeko mitatu baadaye – yenye ukubwa wa kuanzia 4.5 na 5.2.
Kwa sekunde kadhaa tetemeko hilo lilitikisa katika mji mkuu wa Afghanistan Kabul, karibu kilomita 200 na mji mkuu wa Pakistan Islamabad karibu kilomita 400, AFP iliripoti.
Kitovu cha tetemeko la ardhi kilikuwa umbali wa kilomita 27 kutoka Jalalabad, mji mkuu wa mkoa wa Nangarhar na mji wa tano kwa ukubwa nchini Afghanistan.
Tetemeko hilo limetokea baada ya jimbo la Nangarhar kukumbwa na mafuriko kati ya Ijumaa na Jumamosi, ambayo yaliharibu mali na kuua watu watano, kulingana na mamlaka.
Matetemeko ya ardhi ni kawaida nchini Afghanistan, ambayo iko kwenye nyufa za dunia ambapo mabamba ya Hindi na Eurasia hukutana.
All Rights Reserved © The Cantona Group PLC||2025
Discover more from cantonadigital
Subscribe to get the latest posts sent to your email.