Radio Fortune Africa -Na Cantona Joseph
https://zeno.fm/radio/radio-fortune-africa

Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi ya Israel (IDF), amesema kuwa kuna “mapatano mezani” kuhusu mateka waliobaki huko Gaza, kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Israel.
Kulingana na taarifa ya Channel 13 News, Jenerali Luteni Eyal Zamir alieleza kuwa jeshi la Israel limeweka mazingira ya kufanikisha makubaliano hayo, na sasa suala hilo lipo “mikononi mwa Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu.”
Jumanne hii, baraza la usalama la Israel linatarajiwa kujadili pendekezo jipya lililotolewa na wapatanishi wa kikanda, ambalo Hamas ililikubali wiki iliyopita.
Haya yanajiri baada ya maandamano makubwa mapema mwezi huu, ambapo mamia kwa maelfu ya watu walijitokeza mjini Tel Aviv, wakitaka kumalizwa kwa vita vya Gaza na kufikiwa kwa makubaliano ya kuwaachilia mateka walioko mikononi mwa Hamas.
Jukwaa la Mateka na Familia za waliopotea limesema kuwa Zamir ametamka kile “Waisraeli wengi wanachodai,” ikiwa ni pamoja na kufikiwa kwa makubaliano ya kuwarudisha nyumbani mateka wote 50 waliobaki, ambapo takriban 20 kati yao wanadhaniwa kuwa bado hai, pamoja na kumaliza vita hivyo.
Kundi hilo linapanga maandamano mengine makubwa siku ya Jumanne.
Pendekezo la hivi karibuni, linalotoka kwa wapatanishi wa Misri na Qatar, linadaiwa kuzingatia muundo uliowasilishwa na mjumbe wa Marekani, Steve Witkoff, mwezi Juni.
Kwa mujibu wa pendekezo hilo, Hamas ingewaachilia karibu nusu ya mateka hao kwa awamu mbili katika kipindi cha siku 60 za usitishaji mapigano.
Aidha, kungekuwa na mazungumzo ya kufikia makubaliano ya kudumu ya kusitisha mapigano.
Awali, ofisi ya Netanyahu ilieleza kuwa Israel itakubali tu makubaliano yatakayohakikisha “mateka wote wanaachiwa kwa pamoja, kwa wakati mmoja.”
Jumamosi iliyopita, ndege za kivita na vifaru vya Israel vilishambulia maeneo ya Jiji la Gaza, huku Israel ikiendeleza mpango wake wa kulitwaa eneo hilo kubwa zaidi la mijini katika Ukanda wa Gaza.
Benjamin Netanyahu ameapa kuishinda Hamas, na ameendelea kupuuzia ukosoaji wa ndani na wa kimataifa kuhusu mpango wake wa kupanua vita hivyo hata kutoka kwa Jenerali Zamir mwenyewe.
Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Israel, Zamir amekuwa akipinga uvamizi wa kijeshi wa kiwango kikubwa, akihofia kuhatarisha maisha ya mateka na kuingiza jeshi la Israel, ambalo tayari limechoka, katika mzozo wa muda mrefu ndani ya Gaza.
Mashambulizi hayo yamelenga kuwahamisha kwa nguvu zaidi ya watu milioni moja kutoka Jiji la Gaza hadi kwenye kambi za muda kusini, lakini Israel haijatoa ratiba maalum ya ni lini wanajeshi wake wataingia rasmi katika jiji hilo.
Inaripotiwa kuwa Netanyahu anatamani mji mzima uwe chini ya udhibiti wa Israel kuanzia tarehe 7 Oktoba.
Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa (UN), tayari takribani watu milioni 1.9 katika Gaza sawa na karibu asilimia 90 ya wakazi wamekwisha kulazimika kuhama makazi yao.
Takriban watu wanane wauawa katika shambulizi la Israel kwenye hospitali ya Gaza, wizara ya afya yasema

Takriban watu wanane wameuawa katika shambulizi lililofanywa na Israel katika hospitali moja kusini mwa Ukanda wa Gaza, wizara ya afya inayosimamiwa na Hamas imesema.
Wanahabari watatu ni miongoni mwa waliofariki, maafisa wa afya na shirika la habari la Reuters limesema.
Wanajumuisha mpiga picha wa Al-Jazeera na mkandarasi wa Reuters.
Shambulio hilo limefanyika katika Hospitali ya Nasser katikati ya asubuhi siku ya Jumatatu.
Jeshi la Israel na ofisi ya waziri mkuu walisema hawakuwa na maoni ya mara moja.
M23 yaituhumu serikali kwa kutumia mamluki wa kigeni katika mashambulizi yanayoendelea

Wanamgambo wa M23 wameituhumu serikali ya DR Congo kwa kutumia “mamluki wa kigeni” katika mashambulizi ya Jumapili, ambayo wanadai yalilenga maeneo yanayokaliwa na jamii ya Kadasomwa pamoja na viunga vyake, katika eneo la Kalehe, mkoani Kivu Kusini.
Hata hivyo, jeshi la serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) halijatoa tamko lolote kuhusu tuhuma hizo za M23.
Shirika la BBC liliwasiliana na msemaji wa jeshi kuhusiana na madai hayo ya matumizi ya mamluki, lakini bado hajatoa majibu.
Ripoti za mapigano kati ya pande hizo mbili ziliripotiwa siku ya Jumamosi na Jumapili katika maeneo mbalimbali ya mkoa wa Kivu Kusini, ambapo mashuhuda mbalimbali wamedokeza kuwa mapigano hayo yamesababisha wakazi wengi kukimbia makazi yao.
Katika taarifa kwa vyombo vya habari, msemaji wa kundi la AFC/M23, Lawrence Kanyuka, alisema kuwa mashambulizi ya Jumapili huko Kadasomwa “yamesababisha vifo vya watu wengi” na “kuwaacha maelfu bila makazi” kutokana na mashambulizi ya ndege zisizo na rubani.
Kanyuka aliongeza kuwa hapo awali, serikali iliwahi kutumia mamluki kutoka barani Ulaya, ambao waliruhusiwa kupitia Rwanda kurejea makwao baada ya M23 kuteka jiji la Goma.
Sasa, anadai kuwa mamluki waliotumika safari hii, ambao pia anawashutumu kwa kuhusika na mauaji, “hawatarudi kwa amani”.
Wakati huohuo, jeshi la Rwanda nalo linatuhumiwa kuisaidia M23, tuhuma ambazo serikali ya Rwanda imekanusha vikali.
Mapigano makali pia yalishuhudiwa siku ya Jumamosi katika eneo la Mwenga, mkoani Kivu Kusini, katika eneo la Efpo, na kusababisha watu wengi kukimbia makazi yao, kwa mujibu wa ripoti ya Radio RFI.
Inaripotiwa kuwa mapigano hayo pia yalipelekea kundi la M23 kuteka eneo la milimani la Lubumba, takriban kilomita 80 kutoka jiji la Uvira.
Pierre Mheshera, afisa wa serikali za mitaa katika jiji la Uvira, ameieleza BBC kuwa mapigano ya Jumamosi yamesababisha wakazi wengi “kuhama maeneo ya Lubumba na Kadjoka na kuelekea Uvira.”
Mheshera amethibitisha kuwa kwa mujibu wa taarifa walizonazo, M23 kwa sasa inalitawala eneo la Lubumba.
Taarifa hizi pia zimethibitishwa na baadhi ya vyombo vya habari vya ndani nchini DRC.
Hata hivyo, hadi sasa hakuna uthibitisho rasmi kutoka kwa serikali wala kwa kundi la M23 kuhusu madai hayo.
Mwezi uliopita, pande hizo mbili zilitia saini makubaliano ya kusitisha mapigano katika mazungumzo ya amani yaliyofanyika Doha, Qatar.
Mazungumzo hayo yalilenga kufikia mkataba wa amani ifikapo tarehe 18 mwezi huu, lakini malengo hayo hayakufikiwa.
Hata hivyo, pande zote mbili kwa sasa zimeendelea na mazungumzo mjini Doha.
Wakati mazungumzo yakiendelea, pande zote mbili zimeendelea kushutumiana kwa kuanzisha mashambulizi ya hapa na pale ambayo yameripotiwa katika mikoa ya Kivu Kusini na Kivu Kaskazini.
Vikosi vya wanamgambo vya Sudan vyaongeza mashambulizi ili kudhibiti jiji la al-Fashir

Kikundi cha wanamgambo wa Sudan kinachojulikana kama Rapid Support Forces (RSF) kimeongeza mashambulizi yake dhidi ya jiji la magharibi linaloshikiliwa na jeshi, al-Fashir, na kudhibiti “maeneo kadhaa ya makazi,” kwa mujibu wa tovuti ya habari inayoendeshwa binafsi ya Darfur24 iliyotoa taarifa jana.
“Video zilizothibitishwa na Darfur24 zinaonesha wapiganaji wa RSF wakidai kudhibiti maeneo kadhaa na sehemu muhimu ndani ya jiji hilo,” tovuti hiyo ilisema.
Jeshi limekanusha madai ya kusonga mbele kwa kikundi hicho, likisema kuwa wanajeshi wake wamekabiliana na mashambulizi yote ya RSF dhidi ya jiji hilo na kwamba “matokeo ya mapigano ya hivi karibuni hayajabadilika.”
Al-Fashir, ambayo ni makao makuu ya jimbo la Darfur Kaskazini na kitovu muhimu cha misaada ya kibinadamu, ndilo jiji kubwa zaidi katika eneo hilo ambalo bado lipo chini ya udhibiti wa jeshi.
RSF wamekuwa wakilizingira jiji hilo kwa zaidi ya mwaka mmoja.
Kikundi hicho kimeshtumiwa kwa kuua na kuwateka raia waliokuwa wakijaribu kukimbia jiji hilo pamoja na kushambulia kambi za wakimbizi wa ndani zilizoko karibu.
Wakati huohuo, makundi ya wanaharakati wa Sudan yanajiandaa kuzindua kampeni ya kutaka muda wa ujumbe wa uchunguzi wa Umoja wa Mataifa kuhusu nchi hiyo yenye vita uongezwe kwa miaka miwili, kufuatia madai ya ukiukwaji wa haki za binadamu unaoendelea na hali mbaya ya kibinadamu, kwa mujibu wa tovuti ya Sudan Tribune yenye makao yake Paris.
Umoja wa Mataifa uliunda ujumbe huo mwaka 2023 ili kuchunguza ukiukwaji wa haki unaofanywa na jeshi na RSF.
Ujumbe huo unatarajiwa kuwasilisha ripoti yake ya mwisho kwa Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa mwezi Septemba, wakati ambapo muda wake unatarajiwa kumalizika.
Isitoshe, Mtandao wa Madaktari wa Sudan unasema kuwa watu 46 wamefariki kutokana na utapiamlo katika kipindi cha miezi miwili iliyopita, huku wanawake wanaonyonyesha wapatao 19,000 wakihitaji msaada wa dharura wa lishe katika jimbo la Sudan la Kordofan Kusini.
Vifo hivyo vilitokea kati ya mwezi Julai na Agosti na waathirika wengi ni wanawake na watoto.
Mgogoro wa chakula unaoendelea Kordofan Kusini umetokana na mvutano unaoongezeka kati ya Sudan People’s Liberation Movement – North (SPLM-N) inayoongozwa na Abdelaziz al-Hilu na vikosi vya wanamgambo wa Rapid Support Forces (RSF) ambao wanapigania udhibiti wa eneo hilo lenye utajiri wa mafuta.
Mgogoro wa Sudan hadi sasa umesababisha vifo vya takriban watu 150,000 na kuwalazimu watu wengine milioni 12 kuyakimbia makazi yao.
Warundi wajitokeza kwa wingi kuchagua viongozi wa vijiji na mitaa

Zaidi ya Warundi milioni sita wamejitokeza kwa wingi kushiriki duru ya mwisho ya uchaguzi wa viongozi wa taasisi mbalimbali za kitaifa, mchakato ulioanza mwezi Juni.
Jumatatu ya tarehe 25 Agosti, wananchi wanapiga kura kuwachagua viongozi 3,044 wa vijiji na mitaa kutoka maeneo yote ya nchi, ambao watatumikia kwa kipindi cha miaka mitano.
Awamu za awali za uchaguzi zilifanyika mwezi Juni kwa wabunge na madiwani, na Julai kwa wagombea wa vyama vya upinzani.
Katika chaguzi hizo, chama tawala cha CNDD-FDD, ambacho kimeiongoza Burundi kwa zaidi ya miaka 20, kilitangazwa mshindi kwa asilimia 100 ya kura katika nafasi nyingi isipokuwa kwenye nafasi za madiwani wa halmashauri, ambako kilikabiliwa na ushindani mkali na kupoteza kwa chini ya asilimia 2.
Hii ni mara ya kwanza kwa chama hicho kushinda kwa kiwango hicho kikubwa tangu kipate madaraka, licha ya ushindani kutoka kwa zaidi ya vyama 20 vya siasa vilivyoshiriki uchaguzi.
Idadi ya vifo yaongezeka Sanaa baada ya mashambulizi ya anga ya Israel

Televisheni ya Al Masirah yenye uhusiano na Houthi imeinukuu Wizara ya Afya ya Yemen ikisema kuwa, idadi ya waliofariki kutokana na mashambulizi ya anga ya Israel dhidi ya Sanaa imeongezeka na kufikia sita, huku wengine 86 wakijeruhiwa.
Wizara hiyo imesema, “Raia sita waliuawa na wengine 86 walijeruhiwa kutokana na hujuma ya Wazayuni kwenye kituo cha umeme cha Haziz na kampuni ya mafuta kwenye barabara ya 60.” Idadi iliyotangazwa hapo awali ya vifo ilikuwa niwatu wanne waliokufa na majeruhi 67 .
Alisema kuwa “Vikundi vya Ulinzi wa Raia na uokoaji bado vinatafuta na kutambua watu waliopotea.”
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu alisema kuwa mashambulizi ya anga ya Israel dhidi ya Sanaa yaliharibu ikulu ya rais mjini Sanaa, pamoja na kituo cha umeme cha mji huo. Alisisitiza kuwa kundi linaloungwa mkono na Iran “linalipa gharama kubwa kwa mashambulizi yake dhidi ya Israel.”
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu alisema kuwa mashambulizi ya anga ya Israel dhidi ya Sanaa yaliharibu ikulu ya rais mjini Sanaa, pamoja na kituo cha umeme cha mji huo. Alisisitiza kuwa kundi linaloungwa mkono na Iran “linalipa gharama kubwa kwa mashambulizi yake dhidi ya Israel.”
Wakati huo huo, kanali yenye uhusiano na Houthi ilitangaza kwamba mashambulizi ya anga ya Israel yalilenga mji mkuu wa Yemen, Sanaa, siku ya Jumapili. Imewanukuu wakazi wa mji mkuu huo wakisema kuwa mashambulizi hayo ya anga yalilenga maeneo karibu na kambi ya rais, vituo vya makombora, na vinu vya mafuta na nishati.
Hamas yaishutumu srael kwa “kuchelewesha na kukwepa mambo ,” huku idadi ya vifo karibu na vituo vya misaada ikizidi 2,000

Mjumbe wa Ofisi ya Kisiasa ya Hamas, Bassem Naim, ameishutumu serikali ya Israel kwa “kuahirisha na kukwepa hali kwa kuanzisha kwa mara nyingine tena vita kwenye Ukanda wa Gaza.”
Naim alisema kupitia Telegram kwamba “vuguvugu limejifunza kuhusu uvujaji wa taarifa za vyombo vya habari unaoonyesha kwamba Israel inakataa makubaliano ya sehemu ambayo vuguvugu hilo lilikubali, na k inapendelea kuelekea kwenye makubaliano ya kina, kwa msaada wa utawala wa Marekani.”
Naim alithibitisha kwamba vuguvugu hilo “bado halijapokea jibu rasmi kwa kuhusiana na mapendekezo ya hivi punde, wala halijawasilishwa na mapendekezo yoyote mapya ya kuhusu mpango wa kina.”
Alidokeza kwamba “Israeli imeshindwa kufikia malengo yake yoyote aliyotangazwa, isipokuwa kutekeleza mauaji na uharibifu,” kulingana naye.
Haya yanajiri wakati Waziri wa Ulinzi wa Israel Yisrael Katz akiwa tayari amekwishaapa kuuangamiza mji wa Gaza kama Hamas haitakubali kusitisha vita kulingana na masharti ya Israel na kuwaachilia mateka wote ambao bado inawashikilia.
Wanajeshi wa kikosi cha taifa Marekani kubeba silaha Washington kuzuia uhalifu

Wanajeshi wa Kikosi cha Taifa cha Marekani (National Guard) walioko mitaani jijini Washington D.C., kama sehemu ya kampeni ya Rais Donald Trump ya kupambana na uhalifu, wataanza kubeba silaha kuanzia leo, kwa mujibu wa maafisa wawili.
Idadi kamili ya wanajeshi watakaobeba silaha bado haijathibitishwa, lakini maafisa hao walisema kuwa wanajeshi hao watabeba bastola aina ya M17 au bunduki aina ya M4.
Maafisa hao walizungumza kwa masharti ya kutotajwa majina kwa kuwa hawakuruhusiwa kuzungumza rasmi kuhusu suala hilo, haya ni kwa mujibu wa shirika la Reuters.
Kwa wiki mbili zilizopita, mamia ya wanajeshi wa Kikosi cha Taifa waliokuwa hawana silaha wamekuwa wakilinda mitaa ya Washington, kufuatia tangazo la Trump la hali ya dharura ya kiuhalifu katika jiji hilo.
Wiki iliyopita, Waziri wa Ulinzi Pete Hegseth alitoa idhini kwa wanajeshi hao kubeba silaha.
Kwa upande wake, Kikosi Kazi cha Pamoja cha Kikosi cha Taifa–DC kilitoa taarifa siku ya Jumapili kikisema kuwa askari wake watatumia nguvu “ikiwa tu hakuna njia nyingine, na kwa kujibu tishio la haraka la kifo au madhara makubwa ya mwili.”
Wakati huo huo, Rais Trump, ambaye ni wa chama cha Republican, ametangaza kuwa ana mpango wa kupanua oparesheni yake ya kupambana na uhalifu hadi jiji la Chicago, ambalo linaongozwa na chama cha Democratic.
Aidha, siku ya Jumapili, alieleza kuwa anaweza kupeleka wanajeshi katika jiji la Baltimore, Maryland, linaloongozwa pia na chama cha Democratic.
Kiongozi wa wachache katika Baraza la Wawakilishi la Marekani, Hakeem Jeffries (Democrat), alisema Jumapili kuwa Rais Trump hana mamlaka ya kupeleka wanajeshi wa Kikosi cha Taifa huko Chicago, wakati Pentagon ikiendelea na mipango ya awali kuhusu uwezekano wa kupelekwa kwao.
Iwapo Trump atatumia kifungu cha sheria cha kipengee 12406 kupeleka wanajeshi wa Kikosi cha Taifa kutoka majimbo yanayoongozwa na Republican hadi maeneo yanayoongozwa na Democratic, kuna uwezekano mkubwa wa kukabiliwa na changamoto za kisheria.
Tangu Trump kuingia madarakani, wanajeshi wametumika huko Los Angeles kuzima maandamano ya kupinga maafisa wanaokamata wahamiaji.
Mara ya mwisho kwa wanajesh kutumwa Washington DC ni wakati wa uvamizi wa Januari 6, 2021, pale wafuasi wa Trump walipovamia majengo ya Bunge la Marekani.
All Rights Reserved © The Cantona Group PLC||2025
Discover more from cantonadigital
Subscribe to get the latest posts sent to your email.