Kiongozi wa Korea Kaskazini asimamia jaribio jipya la kombora la ulinzi wa anga

Radio Fortune Africa -Na Cantona Joseph

https://zeno.fm/radio/radio-fortune-africa

gg

Kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong Un, amesimamia jaribio la makombora mawili mapya ya ulinzi wa anga, kwa mujibu wa taarifa ya Shirika la Habari la Korea Kaskazini (KCNA).

Taarifa hiyo ya serikali imesema kuwa silaha hizo zina “uwezo wa juu wa kivita” na zinatumia “teknolojia ya kipekee,” ingawa haikutoa maelezo ya kina kuhusu vipengele vya teknolojia hiyo.

Jaribio hilo lilitekelezwa Jumamosi na, kulingana na KCNA, “limethibitisha kuwa sifa za kiteknolojia za aina hizo mbili za makombora zinafaa sana kwa kuharibu malengo mbalimbali ya angani,” likiwemo mashambulizi kutoka kwa ndege zisizo na rubani (drones) na makombora ya mwelekeo wa chini (cruise missiles).

Hatua hiyo inajiri wakati mvutano unaongezeka katika Rasi ya Korea.

Siku chache kabla ya jaribio hilo, Korea Kusini ilifyatua risasi za onyo Jumanne dhidi ya wanajeshi wa Korea Kaskazini waliovuka kwa muda Mfereji wa Kutenganisha Kijeshi (DMZ) unaotenganisha nchi hizo mbili.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Yonhap, Kamandi ya Umoja wa Mataifa ilieleza kuwa karibu wanajeshi 30 wa Korea Kaskazini walivuka mpaka huo unaolindwa kwa ulinzi mkali kati ya pande hizo mbili.

Pyongyang ilijibu tukio hilo kwa kuishutumu Seoul kwa kile ilichokiita “uchokozi wa makusudi,” ikiongeza ukakasi katika uhusiano wa muda mrefu uliojaa misuguano.

Wakati huo huo, Korea Kusini na Marekani zimeendelea na mazoezi makubwa ya kijeshi ya pamoja katika eneo hilo tangu Jumatatu. Mazoezi hayo yanafanyika katika kipindi ambacho diplomasia kati ya Korea Kaskazini na Kusini inadorora, licha ya ahadi za kisiasa zilizotolewa wakati wa kampeni na Rais mpya wa Korea Kusini, Lee Jae Myung, ambaye aliahidi “kuboresha uhusiano wa pande mbili.”

Licha ya juhudi hizo, dada wa Kim Jong Un amezipinga vikali, akizitaja kuwa ni za hila na zisizo na dhati.

Hili limeifanya hali ya kidiplomasia kati ya nchi hizo mbili kuwa tete zaidi.

Korea Kaskazini na Korea Kusini zimegawanyika tangu kumalizika kwa Vita vya Korea mwaka 1953.

Ingawa vita hivyo vilikoma kwa kusainiwa kwa makubaliano ya kusitisha mapigano, hakuna mkataba rasmi wa amani uliowahi kutiwa saini, jambo ambalo limeacha nchi hizo mbili zikiwa bado “kihalali katika hali ya vita,” licha ya kwamba hakuna mashambulizi ya moja kwa moja yaliyotokea kwa miaka mingi.

Mashambulizi ya Ukraine huko Urusi yapandisha bei ya mafuta duniani.

gg

Bei ya mafuta imepanda kwa kushtua siku ya Jumatatu baada ya Ukraine kuongeza mashambulizi yake dhidi ya Urusi, na kuongeza wasiwasi kuwa usambazaji wa mafuta ya Urusi dunaini unaweza kukatizwa.

Wakati huo huo, matarajio ya Marekani kupunguza viwango vya riba yalikuza mtazamo chanya kwa uchumi wa dunia na ongezeko la mahitaji ya nishati.

Bei ya mafuta ghafi aina ya Brent ilipanda kwa senti 6, au 0.09%, kufikia dola $67.79 kwa pipa, huku mafuta ghafi ya West Texas Intermediate (WTI) yakiongezeka kwa senti 9, au 0.14%, hadi kufikia dola $63.75 kwa pipa.

Ukraine ilizindua shambulio la ndege isiyo na rubani dhidi ya Urusi siku ya Jumapili, ambalo lilisababisha kupungua kwa uwezo wa moja ya mitambo mikubwa ya nyuklia ya Urusi na kuchochea moto mkubwa katika kituo cha kusafirisha mafuta cha Ust-Luga, maafisa wa Urusi walisema.

Zaidi ya hapo, moto katika kiwanda cha kusafisha mafuta cha Novoshakhtinsk nchini Urusi, uliosababishwa na shambulio la ndege isiyo na rubani kutoka Ukraine, ulikuwa ukiwaka kwa siku ya nne mfululizo Jumapili, kwa mujibu wa kaimu gavana wa eneo hilo.

Kiwanda hicho kinauza mafuta hasa kwa ajili ya kuuza nje na kina uwezo wa kusafisha jumla ya tani milioni 5 za mafuta kwa mwaka, sawa na takribani mapipa 100,000 kwa siku.

“Mashambulizi ya Ukraine yanapofanikiwa kulenga miundombinu ya mafuta ya Urusi… hatari kwa bei ya mafuta ghafi sasa zinapanda,” alisema mchambuzi wa soko la IG, Tony Sycamore.

Wakati huohuo, Makamu wa Rais wa Marekani, JD Vance, alisema Jumapili kuwa Urusi imepiga hatua kwenye “makubaliano makubwa” kuelekea kufikiwa kwa suluhu ya mazungumzo katika vita vyake na Ukraine.

Kadi ya kumbukumbu ya Michael Jordan na Kobe Bryant yauzwa kwa rekodi ya dunia

gg

Kadi ya kipekee ya mpira wa kikapu iliyosainiwa na magwiji wa NBA, Michael Jordan na Kobe Bryant, imeuzwa kwa dola milioni 12.9 (takriban shilingi bilioni 33) katika mnada, na kuwa kadi ya kumbukumbu ya michezo yenye thamani kubwa zaidi kuwahi kuuzwa katika historia.

Kadi hiyo, inayojulikana kama Upper Deck Exquisite Collection ya msimu wa 2007–08, ina nembo mbili tofauti za NBA na iliuzwa na kampuni ya mnada ya Heritage Auctions huko Marekani.

Kabla ya kuuzwa, kadi hiyo ilikuwa mikononi mwa mmiliki wake wa awali kwa zaidi ya miaka kumi.

Ilipowekwa mnadani, ilikadiriwa kuwa na thamani ya karibu dola milioni 6.

Hata hivyo, jumla ya zabuni 82 ziliwasilishwa, na bei ya mwisho ikazidi mara mbili ya makadirio hayo.

Uuzwaji huu umevunja rekodi iliyowekwa na kadi ya mwaka 1952 ya mchezaji wa baseball Mickey Mantle, ambayo iliuza kwa dola milioni 12.6 mnamo Agosti 2022.

Kwa sasa, kadi ya Jordan-Bryant inashika nafasi ya pili katika bidhaa za kumbukumbu za michezo zenye thamani kubwa zaidi duniani.

Nafasi ya kwanza inashikiliwa na jezi ya Babe Ruth aliyovaa wakati wa Fainali ya Dunia ya mwaka 1932, ambayo iliuza kwa takriban dola milioni 24 mnamo Agosti 2024.

Michael Jordan anachukuliwa kuwa mchezaji bora zaidi katika historia ya NBA, akiwa na mataji sita ya ubingwa aliyoyapata na timu ya Chicago Bulls kati ya mwaka 1991 na 1998.

Kobe Bryant, ambaye alifariki dunia katika ajali ya helikopta mwaka 2020, alikuwa miongoni mwa wachezaji walioheshimika zaidi katika mchezo wa vikapu wa NBA.

Alishinda mataji matano akiwa na Los Angeles Lakers kati ya mwaka 1996 hadi 2016.

All Rights Reserved © The Cantona Group PLC||2025


Discover more from cantonadigital

Subscribe to get the latest posts sent to your email.

Leave a comment