Radio Fortune Africa -Na Cantona Joseph
https://zeno.fm/radio/radio-fortune-africa

Huduma ya habari ya Kremlin imeripoti kwamba Vladimir Putin alifanya mazungumzo ya simu na Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan, ambapo alijadili “maendeleo ya hivi punde kuhusu hali ya Ukraine.”
Miongoni mwa mambo mengine, Putin alizungumza juu ya msaada wa Uturuki “katika kufanya mazungumzo kati ya wawakilishi wa Urusi na Ukraine huko Istanbul.” “Rais wa Urusi alielezea tathmini yake ya mkutano wa Urusi na Marekani uliofanyika Anchorage,”ilisema huduma habari ya Kremlin ilisema.
Erdogan ameelezea mara kwa mara nia yake ya upatanishi katika kuleta suluhu ya amani ya vita kati ya Urusi na Ukraine.
Wajumbe wa Urusi na Ukraine wamefanya mazungumzo huko Istanbul mara kadhaa, lakini matokeo yao pekee yalikuwa kubadilishana kumbukumbu na makubaliano juu ya kukabidhiana kwa wafungwa wa vita na miili ya wafu.
Putin hivi karibuni alifanya mazungumzo na Rais wa Marekani Donald Trump huko Alaska; Trump pia alimkaribisha Volodymyr Zelensky na viongozi wa Ulaya katika Ikulu ya White House mapema wiki hii.
Baada ya mikutano hiyo, maafisa wa Marekani walisema Ukraine na Urusi zinaweza kupanga mkutano kati ya Putin na Zelensky, lakini Moscow haijathibitisha taarifa hiyo.
Israel yasajili askari wa akiba 60,000 kabla ya mashambulizi yaliyopangwa Gaza

Jeshi la Israel linasema kuwa linawasajili askari wa akiba wapatao 60,000 kabla ya mpango wa mashambulizi ya ardhini ili kuuteka mji wote wa Gaza.
Afisa wa kijeshi alisema askari wa akiba wataripoti kazini mnamo Septemba na kwamba wanajeshi wengi waliokusanywa kwa ajili ya shambulio hilo watakuwa wanafanya kazi. Waliongeza kuwa wanajeshi tayari wanahudumu katika maeneo ya Zeitoun na Jabalia kama sehemu ya maandalizi ya mpango huo, ambao Waziri wa Ulinzi Israel Katz aliupitisha siku ya Jumanne na utawekwa kwenye baraza la mawaziri la usalama baadaye wiki hii.
Mamia kwa maelfu ya Wapalestina katika mji wa Gaza wanatarajiwa kuamrishwa kuhama na kuelekea kwenye makazi kusini mwa Gaza.
Washirika wengi wa Israel wamelaani mpango huo, huku Umoja wa Mataifa na mashirika mengine yasiyo ya kiserikali yameonya kwamba mashambulizi mengine na uhamisho wa watu wengi zaidi utakuwa na “athari za kutisha za kibinadamu” baada ya miezi 22 ya vita.
Serikali ya Israel ilitangaza nia yake ya kuliteka eneo lote la Ukanda wa Gaza baada ya mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja na Hamas juu ya kusitisha mapigano na kuachiliwa huru kwa mateka kuvunjika mwezi uliopita.
Wapatanishi wa kikanda wanajaribu kupata makubaliano kabla ya mashambulizi kuanza na wamewasilisha pendekezo jipya la kusitisha mapigano kwa siku 60 na kuachiliwa kwa karibu nusu ya mateka 50 ambao bado wanashikiliwa huko Gaza, ambayo Hamas ilisema imekubali Jumatatu.
Israel bado haijawasilisha jibu rasmi, lakini maafisa wa Israel walisisitiza siku ya Jumanne kwamba hawatakubali tena makubaliano ya sehemu na kudai yale ya kina ambayo yatawafanya mateka wote waachiliwe. Ni mateka 20 pekee wanaoaminika kuwa hai.
Netanyahu amshutumu Waziri Mkuu wa Australia kwa ‘kuisaliti’ Israel

Waziri mkuu wa Israel amemshutumu mwenzake wa Australia kwa “kuisaliti Israeli” na “kutelekeza” jamii ya Wayahudi wa Australia, baada ya siku za mzozo unaoongezeka kati ya nchi hizo mbili.
Benjamin Netanyahu alisema Jumanne kwamba historia itamkumbuka Anthony Albanese “kwa kile alichosema: mwanasiasa dhaifu”.
Australia ilimzuia mwanachama wa siasa kali za mrengo wa kulia wa muungano unaotawala wa Netanyahu kuingia nchini humo siku ya Jumatatu, na Israel nayo ikabatilisha viza za wawakilishi wa Australia kwa Mamlaka ya Palestina.
Waziri wa Uhamiaji wa Australia Tony Burke alisema Netanyahu “ameikosoa” Canberra hivi karibuni akitangaza kuwa itaungana na Uingereza, Ufaransa na Canada katika kutambua taifa la Palestina.
“Nguvu hazipimwi kwa ni watu wangapi unaoweza kulipua au ni watu wangapi unaweza kuwaacha wakiwa na njaa,” Burke aliambia Shirika la Utangazaji la Australia Jumatano.
Albanese baadaye aliwaambia waandishi wa habari kwamba “hachukulii vitu hivi kibinafsi”. “Ninawaheshimu viongozi wa nchi nyingine, nashirikiana nao kwa njia ya kidiplomasia,” alisema.
Kiongozi wa upinzani wa Israel alikosoa matamshi ya Netanyahu, na kuyataja kuwa ni “zawadi” kwa kiongozi huyo wa Australia. Yair Lapid aliandika kwenye X: “Jambo ambalo linaimarisha zaidi kiongozi katika ulimwengu wa kidemokrasia leo ni makabiliano na Netanyahu, kiongozi mwenye sumu zaidi ya kisiasa katika ulimwengu wa Magharibi.
Waziri wa Afrika Kusini akosolewa vikali kuhusu chuki za ubaguzi wa rangi

Waziri wa Michezo, Sanaa na Utamaduni wa Afrika Kusini Gayton McKenzie amekuwa mwepesi wa kuwatangaza na kuwalaumu watu wengine kwa ubaguzi wa rangi lakini yeye mwenyewe sasa ametajwa kuwa mbaguzi wa rangi – mashtaka ambayo anayakanusha.
Mara nyingi anaonekana kama mtu wa kukatisha tamaa kwa jumuiya ya machotara chini humo, wanaotambuliwa kama watu wenye asili mchanganyiko wanarejelewa kulingana na sensa ya watu Afrika Kusini .
Lakini maoni ya zamani aliyotoa McKenzie kwenye mitandao ya kijamii, akitumia neno la kukera sana akimaanisha watu weusi, yamezua dhoruba ya kisiasa.
Ana hadi mwisho wa Jumatano kujibu kwa Tume ya Haki za Kibinadamu ya Afrika Kusini (SAHRC), ambayo inamtaka waziri kufuta jumbe hizo zinazokera na kuomba radhi kwa umma, miongoni mwa matakwa mengine.
“Mchotara” ilikuwa ni uainishaji uliotolewa kwa watu wa urithi mchanganyiko chini ya ubaguzi wa rangi. Mfumo huu uliunda utawala wa kikabila uliotekelezwa kisheria ambao uliweka matabaka na uliwaona watu weupe juu na watu weusi chini, na Wahindi na watu weusi akatika tabaka la katikati.
Licha ya ubaguzi wa rangi kukomeshwa miongo mitatu iliyopita , urithi wake mchungu unaendelea katika uchumi na siasa za nchi hiyo.
Muungano wa Patriotic wa McKenzie (PA) umevutia uungwaji mkono miongoni mwa watu weusi, na kushinda uwakilishi bungeni katika uchaguzi mwaka jana.
“Kwa mara ya kwanza kuna watu weusi pia wanaenda bungeni kupitia Muungano wa Patriotic Alliance,” McKenzie alisema, baada ya matokeo kutangazwa.
Rais Cyril Ramaphosa alijumuisha muungano wa PA katika serikali yake ya muungano wa vyama vingi baada ya chama chake cha African National Congress (ANC) kupoteza wingi wake wa wabunge kwa mara ya kwanza.
Raia 140 waliuawa na waasi DRC licha ya mchakato wa amani – Ripoti

Waasi wa M23 waliwaua takriban watu 140 mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo mwezi uliopita katika moja ya vitendo vya ukatili mbaya zaidi wa kundi hilo lililojihami tangu kuibuka tena mwishoni mwa 2021, Human Rights Watch imesema katika ripoti yake.
Waasi hao hapo awali walikanusha vikali kuhusika na mauaji haya, wakitaja mashtaka hayo kuwa “upotoshaji wa wazi”.
Haikujibu ombi la kutoa maoni juu ya ripoti hiyo, shirika la haki za binadamu lilisema.
Hii ni licha ya mchakato wa amani, uliosimamiwa na Marekani na Qatar, kumaliza mzozo katika eneo hilo.
Mashuhuda waliambia kikundi cha utetezi kwamba waasi wanaoungwa mkono na Rwanda “waliwaua” wakazi wa eneo hilo, wakiwemo wanawake na watoto, wengi wao kutoka kabila la Wahutu katika eneo la Rutshuru, karibu na Mbuga ya Kitaifa ya Virunga.
Mauaji hayo yanayodaiwa kutekelezwa yanaonekana kutokea wakati wa kampeni ya M23 dhidi ya kundi la Wahutu wenye silaha, FDLR, lililoundwa na wahusika wa mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 katika nchi jirani ya Rwanda.
HRW ilisema jumla ya mauaji mwezi Julai yanaweza kuzidi 300, na kuthibitisha matokeo kama hayo ya Umoja wa Mataifa mapema mwezi huu.
Mapigano kati ya wanajeshi wa serikali na waasi wa M23 yaliongezeka mwezi Januari, wakati waasi hao walipoteka sehemu kubwa ya mashariki yenye utajiri wa madini, ukiwemo mji mkuu wa eneo la Goma.
Maelfu ya watu wameuawa na mamia kwa maelfu ya raia kulazimishwa kuyaacha makazi yao katika vita vinavyoendelea, Umoja wa Mataifa unasema.
Mchina afungwa Marekani kwa kupeleka silaha Korea Kaskazini

Korea Kaskazini imepigwa marufuku kufanya biashara ya silaha na zana za kijeshi chini ya vikwazo vya Umoja wa Mataifa
Raia wa China amehukumiwa kifungo cha miaka minane jela kwa kosa la kusafirisha silaha na vifaa vingine vya kijeshi kwenda Korea Kaskazini, wizara ya sheria ya Marekani imesema.
Shenghua Wen, 42, alipokea takriban $2m (£1.5m) kutoka kwa maafisa wa Korea Kaskazini ili kusafirisha bidhaa hizo kutoka California, kulingana na taarifa kutoka kwa shirika hilo siku ya Jumatatu.
Mkazi wa Ontario, California, Wen amezuiliwa tangu Desemba 2024. Alikiri hatia mnamo Juni kwa kula njama ya kukiuka Sheria ya Kimataifa ya Uwezo wa Kiuchumi wa Dharura na kuwa wakala haramu wa serikali ya kigeni.
Kesi ya Wen inaonyesha mbinu mbalimbali ambazo Korea Kaskazini inazitumia vikwazo vya kimataifa kwa biashara yake ya silaha.
Ikimtaja Wen kama “mgeni haramu”, wizara ya sheria ilisema aliingia Marekani kwa viza ya wanafunzi mwaka wa 2012 na kusalia nchini baada ya viza yake kuisha Desemba 2013.
“Kabla ya kuingia Marekani, Wen alikutana na maafisa wa serikali ya Korea Kaskazini katika ubalozi wa Korea Kaskazini nchini China,” shirika hilo lilisema. “Maafisa hawa wa serikali walimuelekeza Wen jinsi ya kununua bidhaa kwa niaba ya Korea Kaskazini.”
Maafisa wawili wa Korea Kaskazini waliwasiliana na Wen kupitia jukwaa la ujumbe mtandaoni mwaka wa 2022 na kumwambia apitishe silaha na bidhaa nyingine kutoka Marekani hadi Korea Kaskazini, kulingana nawizara ya sheria.
All Rights Reserved © The Cantona Group PLC||2025
Discover more from cantonadigital
Subscribe to get the latest posts sent to your email.