Radio Fortune Africa -Na Cantona Joseph
https://zeno.fm/radio/radio-fortune-africa

Marekani imefikia makubaliano na Honduras na Uganda kuwapeleka wahamiaji katika nchi hizo kama sehemu ya kukabilia na wahamiaji haramu, kulingana na nyaraka zilizopatikana na mshirika wa BBC wa Marekani CBS.
Uganda imekubali kuchukua idadi isiyojulikana ya wahamiaji wa Kiafrika na Asia ambao walikuwa wameomba hifadhi kwenye mpaka wa Marekani na Mexico, wakati Honduras itapokea mamia ya watu waliofukuzwa wa nchi zinazozungumza Kihispania, CBS inaripoti.
Hatua hiyo ni sehemu ya jaribio la utawala wa Donald Trump kutaka nchi nyingi zaidi zikubali wahamiaji waliofukuzwa nchini humo ambao si raia wao.
Wanaharakati wa haki za binadamu wamelaani sera hiyo, wakisema wahamiaji wanakabiliwa na hatari ya kutumwa katika nchi ambako wanaweza kudhurika.
Chini ya makubaliano hayo, Uganda imekubali kuwapokea wahamiaji waliofukuzwa Marekani almuradi wasiwe na historia ya uhalifu, lakini haijulikani nchi hiyo hatimaye itachukua wangapi, kulingana na CBS.
Honduras ilikubali kupokea wahamiaji wa zaidi ya miaka miwili, ikiwa ni pamoja na familia zinazosafiri na watoto, lakini nyaraka zinaonyesha inaweza kuamua kukubali zaidi.
Mikataba yote miwili ni sehemu ya shinikizo kubwa la utawala wa Trump wa kupanga mipango ya kufurushwa kwa wahamiaji na kupelekwa katika nchi mbalimbali kwenye mabara kadhaa – ikiwa ni pamoja na yale yenye rekodi tata za haki za binadamu.
Kufikia sasa, mataifa kadhaa yamekubali kuwapokea wahamiaji waliofukuzwa kutoka mataifa mengine.
Mwanamke wa Peru aficha dawa za kulevya kwenye kifaa cha kujifurahisha kingono

Mwanamke mmoja wa Peru ameshtakiwa kwa kujaribu kusafirisha dawa za kulevya aina ya Cocaine za thamani ya $70,000 (£52,000) hadi Bali, zikiwa zimefichwa kwenye nguo yake ya ndani na kifaa cha kujifurahisha kingono.
Mwanamke huyo, ambaye alitambuliwa tu na herufi za kwanza za NS, alizuiliwa na maafisa wa forodha ambao walihisi kuwa ana wasiwasi, polisi walisema.
“Mihadarati hiyo ilifichwa kwenye vifurushi sita vya plastiki vilivyofungwa kwa mkanda mweusi ndani ya sidiria ya rangi ya kijani, vifurushi vitatu kama hivyo vilipatikana kwenye chupi nyeusi na kifaa cha kujifurahisha kingono ambacho kiliingizwa mwilini mwake,” Radiant, mkurugenzi wa kitengo cha mihadarati katika polisi wa Bali, aliwaambia waandishi wa habari.
Mwanamke huyo mwenye umri wa miaka 42 ameshtakiwa chini ya sheria za dawa za kulevya nchini Indonesia, na iwapo atapatikana na hatia anaweza kukabiliwa na hukumu ya kifo.
Qatar yasema DRC, M23 bado ‘wanashiriki’ katika mchakato wa amani

Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo na waasi wa M23 hawajajiondoa katika mchakato wa amani licha ya kukosa kufikia makubaliano siku ya mwisho iliyopangwa, mpatanishi wa Qatar alisema Jumanne.
“Pande zote mbili zinashirikiana vizuri. Tunashirikiana nao pia… na tumejitolea katika mchakato huo,” msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Qatar Majed al-Ansari aliambia mkutano wa kawaida wa habari.
Serikali ya Congo na waasi wa M23 walitia saini makubaliano ya kusitisha mapigano mwezi Julai yenye lengo la kukomesha kabisa mapigano ambayo yamesababisha vurugu mashariki mwa DRC.
Chini ya masharti ya makubaliano hayo yaliyofuatia mazungumzo ya Qatar, pande hizo mbili zilipaswa kuanza mazungumzo ya amani Agosti 8 na kukamilisha makubaliano ifikapo tarehe 18 Agosti.
Licha ya muda uliopangwa kufikia kikomo, Ansari alisema bado kuna nia ya kuendelea na mchakato huo.
Siku ya Jumapili, afisa wa Qatar aliiambia AFP kwa sharti la kutotajwa jina kwamba rasimu ya mpango wa amani imetolewa na DRC na waasi wa M23 kabla ya duru nyingine ya mazungumzo inayotarajiwa kufanyika Doha katika siku zijazo.
All Rights Reserved © The Cantona Group PLC||2025
Discover more from cantonadigital
Subscribe to get the latest posts sent to your email.