Radio Fortune Africa -Na Cantona Joseph
https://zeno.fm/radio/radio-fortune-africa

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa unaosaidia Kuleta Utulivu katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (MONUSCO) umelaani vikali mashambulizi yaliyofanywa na kikundi cha waasi wa Allies Democratic (ADF) kati ya 9 na 16 Agosti 2025, katika maeneo kadhaa ya Beni na Lubero, katika mkoa wa Kivu Kaskazini.
MONUSCO imesema mashambulizi hayo yalisababisha vifo vya watu takriban 52 na huenda idadi hiyo ikaongezeka.
MONUSCO imeongeza kuwa vurugu hizo ziliambatana na matukio ya utekaji nyara, uporaji, uchomaji wa majumba na magari na uharibifu wa mali za raia ambao tayari wanakabiliana na mgogoro wa kibidamanu.
“Mashambulizi hayo yaliyolenga raia ambayo ni pamoja na mauaji yaliyotekelezwa usiku wa tarehe 26 hadi 27 Julai huko Komanda eneo la Irumu, Ituri, hayakubaliki na ni ukiukaji mkubwa wa sheria za kimataifa na haki za binadamu,’’ taarifa ya MONUSCO ilisema.
Ujumbe huo umetoa wito kwa serikali ya DR Congo kufanya uchunguzi wa kina na kuwajibisha waliohusika na mauaji ya raia.
MONUSCO imetoa hakikisho la kuendelea kuunga mkono serikali ya Congo na jamii za wenyeji kuzuia ghasia zaidi, kulinda raia pamoja na kuchangia urejeshaji wa utulivu katika maeneo yalioathirika na vita.
Bobi Wine achukua fomu ya urais kwa chama cha (NUP) Uganda

Kiongozi wa chama cha National Unity Platform (NUP) Robert Sentamu Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine, hapo jana alichukuliwa fomu ya urais ya uchaguzi mkuu utakaofanyika Januari, 2026 nchini Uganda.
Kiongozi wa upinzani bungeni Joel Ssenyonyi , Katibu Mkuu wa chama David Rubongoya na Msimamizi wa Hazina ya Kitaifa ya chama Benjamin Katana walichukua fomu kwa niaba ya Kyagulanyi kutoka makao makuu ya Tume ya Uchaguzi.
Chama cha NUP kilisema kitafanya kampeni zake chini ya kauli mbiu, ‘’Uganda Mpya Sasa’’ na kuongeza kuwa hilo litafikiwa kwa upigaji kura wa kiwango cha juu.
‘’Uganda mpya tunayozungumzia ni nchi ambayo watu wote wakuwa wanakwenda kwenye hospitali za umma na kupata matibabu mazuri, barabara zetu ziwe katika hali nzuri, mahali ambapo watoto wetu wanakwenda shule kupata elimu bora,’’ Ssenyonyi aliambia vyombo vya habari.
Hii itakuwa mara ya pili kwa Robert Kyagulanyi kugombea urais dhidi ya Rais Yoweri Museveni.
Mwaka 2021, alimaliza kinyang’anyiro hicho katika nafasi ya pili kwa kupata kura 3,475,398 sawa na asilimia 34.83 ya kura zote.
Marekani yabatilisha zaidi ya viza 6,000 za wanafunzi

Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani imebatilisha zaidi ya viza 6,000 za wanafunzi wa kimataifa kwa sababu ya ukiukaji wa sheria za Marekani na kupitisha muda wa kukaa nchini humo, idara hiyo iliambia BBC.
Wizara hiyo ilisema idadi ” kubwa” ya ukiukaji huo ni mashambulizi, kuendesha gari ukiwa umekunywa kileo, wizi na “kuunga mkono ugaidi”.
Hatua hiyo inajiri huku utawala wa Trump ukiendelea na msako mkali dhidi ya wahamiaji na wanafunzi wa kimataifa.
Ingawa wizara hiyo haikufafanua walichomaanisha na “kuunga mkono ugaidi”, utawala wa Trump umewalenga baadhi ya wanafunzi ambao wameandamana kuunga mkono Palestina, wakisema walikuwa wameonyesha tabia ya chuki.
Kanisa la miaka 113 kuhamishwa hadi katikati ya jiji la Uswidi

Kanisa la kihistoria ambalo limekuwepo kwa miaka 113 lililo hatarini kuzama kutokana na mtikiso wa chini ya ardhi linakaribia kuhamishwa lote jinsi lilivyo- kwa mwendo wa kilomita 5 (maili 3) kando ya barabara kaskazini mwa Uswidi.
Kanisa hilo lenye muundo wa mbao nyekundu huko Kiruna tangu 1912 umeinuliwa kwenye majukwaa makubwa kabla ya kuhamishwa katikati mwa jiji.
Litasafirishwa kwa kasi ya 500m kwa saa, na safari hiyo inatarajiwa kuchukua siku mbili.
Kijiji cha kale kulipo kanisa hilo, kiko hatarini kutokana na ufa uliojitokeza ardhini baada ya zaidi ya karne ya uchimbaji wa madini ya chuma.
Hatua ya kuhamisha kanisa hilo ni moja ya matukio ya kuvutia zaidi na kipekee ya uhamishaji wa majengo makubwa huko Kiruna, ambayo iko kilomita 145 kaskazini mwa Mzingo wa Aktiki.
“Tumefanya matayarisho kabambe,” asema mtu anayesimamia uhamishaji huo, meneja wa mradi Stefan Holmblad Johansson.
“Ni tukio la kihistoria, operesheni kubwa sana na tata na hakuna sababu ya kutokea kwa makosa na kila kitu kiko chini ya udhibiti.”
Kufikia katikati ya miaka ya 2010, majengo mengine huko Kiruna tayari yalikuwa yakihamishwa hadi kwenye ardhi salama.
Mengi yalikuwa yamebomolewa na kujengwa upya, lakini baadhi ya majengo ya kihistoria yalihamishwa kama yalivyo.
Hamas yakubali pendekezo la kusitisha mapigano Gaza – chanzo chasema

Hamas imekubali pendekezo la hivi karibuni kutoka kwa wapatanishi wa eneo la makubaliano ya kusitisha mapigano Gaza na kuachiliwa kwa mateka na Israel, chanzo kimoja katika kundi linalojihami la Palestina kimeiambia BBC.
Pendekezo hilo kutoka Misri na Qatar linasemekana kuegemea kwenye mfumo uliowekwa na mjumbe wa Marekani Steve Witkoff mwezi Juni.
Linajumuisha Hamas kuwaachilia huru karibu nusu ya mateka 50 waliosalia wa Israel – 20 kati yao wanaaminika kuwa hai – katika makundi mawili wakati wa usitishaji mapigano wa siku 60 wa awali. Pia kutakuwa na mazungumzo ya kusitisha mapigano ya kudumu.
Haijulikani jibu la Israel litakuwa nini kwani ofisi ya Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu ilisema wiki iliyopita kwamba itakubali tu makubaliano ikiwa “mateka wote wataachiliwa kwa wakati mmoja”.
Katika video iliyotolewa baada ya ripoti za idhini ya Hamas kuibuka, Netanyahu hakutoa maoni moja kwa moja lakini alisema kwamba “kutoka kwao unaweza kupata hisia moja – Hamas iko chini ya shinikizo kubwa.”
Mkuu wa majeshi ya Israel, Lt Jenerali Eyal Zamir, wakati huo huo alisema ilikuwa katika hatua ya mabadiliko katika vita vilivyodumu kwa miezi 22, “ikilenga kuimarisha mashambulizi dhidi ya Hamas katika mji wa Gaza”.
Zelensky asema yuko tayari kwa mazungumzo ya Putin huku Ulaya ikifurahishwa na hakikisho la usalama wa Trump

Rais Volodymyr Zelensky amesema yuko tayari kwa mazungumzo ya Putin huku Ulaya ikifurahishwa na hakikisho la usalama wa Trump.
Zelensky amesema kuwa hakuna tarehe iliyothibitishwa kwa mazungumzo yoyote yajayo kati yake na Putin na kuwa “wamethibitisha tu baada ya mkutano huu wenye tija na rais,” kwamba mazungumzo yataendelea kati ya Ukraine na Urusi.
Zelensky alisema “imethibitishwa kwamba wako tayari kwa mkutano wa pande tatu,” lakini akaongeza kuwa “ikiwa Urusi ilipendekeza kwa rais wa Marekani mkutano wa kidiplomasia kati ya pande zinazowakilisha nchi mbili, pia tutaona matokeo yake”.
“Ukraine haitakuwa kikwazo cha kufikia amani,” alisema.
Hayo yanajiri baada ya Trump kumpigia simu Putin wakati wa mkutano wa White House ukiendelea.
“Wakati wa kuhitimisha mikutano hiyo, nilimpigia simu Rais Putin, na kuanza maandalizi ya mkutano katika eneo litakaloamuliwa kati ya marais Putin na Zelenskyy,” aliandika.
“Baada ya mkutano huo kufanyika, tutakuwa na mkutano wa pande tatu, ambao utakuwa Marais wawili, pamoja na mimi mwenyewe.”
Trump pia alisema dhamana ya usalama kwa Ukraine ilijadiliwa wakati wa mazungumzo ya leo, ambayo alisema “itatolewa na Nchi mbalimbali za Ulaya, kwa uratibu na Marekani”.
All Rights Reserved © The Cantona Group PLC||2025
Discover more from cantonadigital
Subscribe to get the latest posts sent to your email.