Radio Fortune Africa -Na Cantona Joseph
https://zeno.fm/radio/radio-fortune-africa

Rais wa Marekani Donald Trump amesema kuwa watu wasio na makaazi lazima “waondoke” Washington DC huku akiapa kukabiliana na uhalifu katika mji huo.
Trump alitia saini amri mwezi uliopita ili kurahisisha kuwakamata watu wasio na makazi, na wiki iliyopita aliamuru utekelezaji wa sheria katika mitaa ya Washington DC.
Kupitia ujumbe alioweka kwenye mtandao wake wa kijamii Truth Social siku ya Jumapili, Trump aliandika:
“Wasiokuwa na makazi wanapaswa kuondoka MARA MOJA.”
Aliendelea kwa kusema kuwa watu hao watapewa mahali pa kuishi, lakini mbali na mji mkuu.
Kwa upande wa wahalifu, alisema hawatabeba virago vyao bali watawekwa jela.
Trump alifuatisha ujumbe huo na picha zinazoonesha mahema na takataka mitaani.
Mpango huu mpya haujafafanuliwa kwa kina, lakini si mara ya kwanza Trump kulizungumzia suala la watu wasio na makazi.
Mwaka 2022, alieleza kuwa watu hao wanapaswa kuhamishiwa kwenye maeneo ya nje ya miji, wakipewa mahema ya kisasa pamoja na huduma muhimu kama vyoo na matibabu.
Lakini matamshi haya, japo yamepata uungwaji mkono kutoka kwa baadhi ya wafuasi wake, pia yameibua hisia mseto kwa wengine hasa wanaoona kuwa watu wasio na makazi ni raia wanaokumbwa na changamoto halisi kama ukosefu wa ajira, afya ya akili, au matatizo ya kiuchumi, si wahalifu wala hatari kwa jamii.
Katika ujumbe mwingine, alimpongeza Meya Bowser kama “mtu mwema anayejitahidi,” lakini akasisitiza kuwa licha ya juhudi zake, mji unazidi kuwa “mchafu, hatari na usiovutia.”
Hata hivyo, Meya Muriel Bowser amekosoa hatua ya baadhi ya viongozi wa Ikulu ya White House kuwa DC ni hatari zaidi kuliko Baghdad, akisema kuwa kulinganisha mji wa Marekani na nchi iliyo kwenye vita ni jambo la kupindisha ukweli.
Meya huyo akizungumza na MSNBC, alisema “Ni kweli tuliona ongezeko kubwa la uhalifu mwaka 2023, lakini tangu wakati huo tumefanya kazi kubwa kuupunguza. Kwa sasa, tuna viwango vya chini zaidi vya uhalifu wa kutumia nguvu katika kipindi cha miaka 30.
Trump anatarajiwa kufanya mkutano na wanahabari katika Ikulu, ambapo atatoa mpango wa kukabiliana na uhalifu jijini.
Pia ametangaza kuwa atagusia mabadiliko ya kimazingira na ukarabati wa sura ya mji.
Kwa mujibu wa Community Partnership, shirika linalosaidia kupunguza ukosefu wa makazi, takribani watu 3,782 hulala bila makazi katika jiji kuu la Marekani kila usiku.
Kati yao, wengi wako kwenye makazi ya muda au nyumba za dharura, lakini takriban 800 wanalala wazi mitaani.
Australia yatangaza rasmi tarehe ya kuitambua Palestina kama taifa

Serikali ya Australia imetangaza kuwa itaitambua rasmi Palestina kama taifa huru katika Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa utakaofanyika mwezi Septemba, hatua inayofuatia maamuzi sawa yaliyofikiwa na mataifa kama Uingereza, Ufaransa na Kanada.
Taarifa hiyo imetolewa na Waziri Mkuu wa Australia, Anthony Albanese.
Kwa mujibu wa Albanese, uamuzi huo umetanguliwa na makubaliano muhimu kati ya Australia na Mamlaka ya Palestina, yakiwemo masharti ya kupokonywa silaha kwa makundi yenye silaha, kufanyika kwa uchaguzi mkuu, na uthibitisho wa Palestina kulitambua taifa la Israel na haki yake ya kuendelea kuwepo.
“Suluhishila kutambua kuwa ni mataifa mawili tofauti ndilo tumaini la kweli kwa binadamu kuvunja mzunguko wa vurugu katika Mashariki ya Kati, na kumaliza migogoro, mateso na baa la njaa linaloikumba Gaza,” alisema Waziri Mkuu huyo siku ya Jumatatu.
Hata hivyo, Israel ambayo inaendelea kukabiliwa na shinikizo la kimataifa kusitisha vita vinavyoendelea Gaza imekosoa hatua hiyo, ikisema kuwa kutambuliwa kwa taifa la Palestina ni sawa na “kutunuku ugaidi”.
Tangu Jumamosi iliyopita, watu watano wamefariki dunia kutokana na njaa na utapiamlo huko Gaza, na kufikisha idadi ya vifo kutokana na hali hiyo kuwa 217, kwa mujibu wa taarifa ya Wizara ya Afya inayoendeshwa na Hamas.
Aidha, tangu kuanza kwa mashambulizi ya kijeshi ya Israel mwaka 2023, zaidi ya watu 61,000 wamepoteza maisha, kwa mujibu wa idadi iliyotolewa na mamlaka hiyo.
Mashambulizi hayo ya Israel yalizuka kufuatia uvamizi mkubwa ulioongozwa na kundi la Hamas mnamo tarehe 7 Oktoba mwaka huo, ambapo watu wapatao 1,200 waliuawa na wengine 251 kuchukuliwa mateka.
Kwa upande wake, Mamlaka ya Palestina ambayo inasimamia baadhi ya maeneo ya Ukingo wa Magharibi yanayokaliwa na Israel imesema kutambuliwa kwa taifa hilo ni ishara ya kuongezeka kwa uungwaji mkono wa kimataifa kwa haki ya Wapalestina ya kujitawala.
Waziri Mkuu Albanese alieleza kuwa uamuzi wa serikali yake umetokana na ahadi ya Rais wa Mamlaka ya Palestina, Mahmoud Abbas, kuwa Hamas haitakuwa na nafasi yoyote katika uongozi wa taifa la Palestina litakapoundwa.
Hatua hii pia inatajwa kuwa zao la mashauriano ya karibu kati ya Australia na viongozi wa mataifa mengine, yakiwemo Uingereza, Ufaransa, New Zealand na Japan, yaliyofanyika katika kipindi cha wiki mbili zilizopita.
“Tunaamini kuwa huu ni wakati wa fursa ya kihistoria, na Australia iko tayari kushirikiana na jumuiya ya kimataifa kuitumia ipasavyo,” alisema Albanese katika mkutano na waandishi wa habari.
Jumapili iliyopita, maelfu ya waandamanaji waliounga mkono taifa la Palestina walishiriki maandamano makubwa yaliyovuka Daraja la Bandari la Sydney, siku moja baada ya mahakama kuidhinisha maandamano hayo kufanyika.
Wakati huo huo, Israel imeendelea kukosolewa vikali na wajumbe wa Umoja wa Mataifa kufuatia mpango wake wa kuikalia Gaza, hatua ambayo Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu anaitetea kuwa “njia bora ya kukomesha vita.”
Mwaka uliopita, mataifa ya Hispania, Ireland na Norway yalitangaza kutambua rasmi Palestina kama taifa huru, kwa matumaini kwamba hatua hiyo itachochea kusitishwa kwa mapigano kati ya Israel na Hamas.
Hadi sasa, taifa la Palestina limetambuliwa rasmi na nchi 147 kati ya wanachama 193 wa Umoja wa Mataifa.
Katika taasisi hiyo ya kimataifa, Palestina ina hadhi ya “taifa la mwangalizi wa kudumu”, inayoruhusu ushiriki katika vikao lakini bila haki ya kupiga kura.
Waasi wa M23 wakana madai ya kuwauwa raia katika jimbo la Kivu Kusini DRC

Waasi wa M23 waliodhibiti maeneo ya mashariki mwa DRC wamekana madai ya kuwauwa raia katika jimbo la Kivu Kusini pamoja na madai ya kuajiri askari watoto.
Msemaji wa M23 , Willy Ngoma ameiambia BBC kuwa sio lengo lao kuwalenga raia.
“Hatuui raia … Tunawezaje kuua raia ambao tunapaswa kuwalinda? Hatuwezi hata kuua kuku wao… tunaheshimu raia,” anasema Ngoma.
Jeshi katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo hivi karibuni lilishutumu kundi la M23 kwa mauaji hayo baada ya ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa kusema imepokea ushahidi wa moja kwa moja za kwamba zaidi ya raia 300 waliuawa mwezi uliopita na waasi hao wanaoungwa mkono na Rwanda.
Ngoma anasema kuwa Umoja wa Mataifa huko kuona hali halisi katika maeneo ambayo M23 inadhibiti na kwamba wamekuwa wakipokea maoni na taarifa zenye msimamo mkali kutoka kwa serikali ya DRC.
Wachambuzi wa kisiasa wanasema kwamba hata kwa juhudi za hivi karibuni za upatanishi na Marekani na Qatar, makubaliano ya amani ya kudumu yanaonekana kuwa vigumu kufikiwa.
Waandishi 5 wa Aljazeera wauawa katika shambulio la Israel Gaza

Kituo cha habari cha Al Jazeera kimethibitisha kwamba waandishi wake watano wameuawa katika shambulio la anga la Israel lililotokea karibu na lango kuu la Hospitali ya Al-Shifa, mjini Gaza.
Kwa mujibu wa taarifa ya kituo hicho, waandishi wa habari Anas al-Sharif na Mohammed Qreiqeh, pamoja na wapiga picha Ibrahim Zaher, Mohammed Noufal na Moamen Aliwa, walikuwa ndani ya hema maalum la waandishi wa habari lililokuwa limewekwa katika hospitali hiyo, wakati walipolengwa moja kwa moja na shambulio hilo la Jumapili.
Al Jazeera imelitaja tukio hilo kama “mashambuli mengine ya wazi na ya kupangwa dhidi ya uhuru wa vyombo vya habari.”
Hata hivyo Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) lilithibitisha baadaye kuwa lilimlenga Anas al-Sharif, likidai kupitia chapisho la Telegram kwamba alikuwa kiongozi wa kikosi cha wapiganaji wa Hamas.
IDF haikuwataja wala kueleza lolote kuhusu waandishi wengine waliouawa.
Jumla ya watu saba waliuawa katika shambulio hilo, kwa mujibu wa ripoti ya Al Jazeera
Kituo hicho awali kilitangaza kuwa wafanyakazi wake wanne wamepoteza maisha, lakini baadaye kilisasisha idadi hiyo na kuthibitisha kuwa ni watano.
Mhariri mkuu wa Al Jazeera, Mohamed Moawad, aliiambia BBC kuwa Anas al-Sharif alikuwa mwandishi aliyeidhinishwa rasmi, na ndiye aliyekuwa “sauti pekee inayoeleza ulimwengu kinachoendelea ndani ya Ukanda wa Gaza.”
Kwa kuwa waandishi wa kimataifa hawajaruhusiwa na Israel kuingia Gaza kuripoti kwa uhuru tangu kuanza kwa vita, vyombo vingi vya habari duniani vimekuwa vikiwategemea waandishi wa eneo hilo kupata taarifa kutoka ndani ya Gaza.
“Walilengwa wakiwa kwenye hema lao, hawakuwa mstari wa mbele wa mapigano,” alisema Moawad.
“Ni wazi kuwa serikali ya Israel inalenga kunyamazisha sauti yoyote inayoripoti kutoka ndani ya Gaza,” aliongeza katika mahojiano na kipindi cha The Newsroom.
“Hili ni jambo ambalo sijawahi kulishuhudia katika historia ya kisasa ya uandishi wa habari,” alisisitiza.
Anas al-Sharif, mwenye umri wa miaka 28, alionekana kuchapisha ujumbe kwenye mtandao wa X dakika chache kabla ya kuuawa, akiandika kuhusu mashambulizi makali ya mabomu yaliyoendelea mjini Gaza.
Chapisho lililofuata, ambalo linaaminika kuwa liliandaliwa mapema, lilichapishwa na rafiki yake baada ya taarifa za kifo chake.
Katika video mbili za kusikitisha zilizosambaa mitandaoni na kuthibitishwa na idara ya uhakiki ya BBC (BBC Verify), wanaume walionekana wakibeba miili ya waliouawa.
Wengine walionekana wakilitaja jina la Qreiqeh kwa uchungu, huku mtu mmoja aliyevalia fulana iliyona chapa ya “vyombo vya habari” akisema kuwa mmoja wa marehemu ni Anas al-Sharif.
Katika taarifa yake, IDF ilimshutumu al-Sharif kwa kujifanya mwandishi wa habari, ikidai kuwa alikuwa “mhusika mkuu katika kupanga mashambulizi ya roketi dhidi ya raia wa Israel na wanajeshi wa IDF.”
Jeshi hilo lilidai kuwa tayari lilikuwa limesambaza taarifa za kijasusi zinazoonesha ushiriki wa al-Sharif katika mafunzo ya kijeshi.
Mwezi mmoja kabla ya kuuawa kwake, Mtandao wa Al Jazeera, Umoja wa Mataifa na Kamati ya Kuwalinda Waandishi wa Habari (CPJ) walitoa taarifa tofauti wakionya kuwa maisha ya al-Sharif yalikuwa hatarini na kutoa wito wa kulindwa kwake.
Mkurugenzi Mtendaji wa CPJ, Bi Jodie Ginsberg, aliliambia BBC kuwa mamlaka za Israel zimeshindwa kuwasilisha ushahidi wa kuthibitisha madai yao kuwa waandishi waliouawa walikuwa magaidi.
“Huu ni mwenendo ambao tumeushuhudia kutoka Israel si katika vita vya sasa pekee, bali kwa miongo kadhaa iliyopita ambapo mara kwa mara mwandishi huuawa na baadaye Israel hudai kuwa alikuwa gaidi, lakini bila kutoa ushahidi wa kutosha kuunga mkono madai hayo,” alisema.
Hili si tukio la kwanza ambapo waandishi wa Al Jazeera wamelengwa na kuuawa na Jeshi la Israel kwa madai ya kuhusika na Hamas.
Mnamo Agosti mwaka jana, Ismael Al-Ghoul aliuawa katika shambulio la anga akiwa ndani ya gari lake.
Video ya kutisha iliyosambaa mitandaoni ilimuonesha akiwa amekatwa kichwa.
Mpiga picha Rami al-Rifi na mvulana mmoja aliyekuwa akipita kwa baiskeli pia waliuawa katika tukio hilo.
Katika kisa hicho, IDF ilidai kuwa Al-Ghoul alihusika katika mashambulizi ya Hamas dhidi ya Israel yaliyofanyika tarehe 7 Oktoba 2023 madai ambayo Al Jazeera ilikanusha vikali.
Kwa mujibu wa CPJ, waandishi wa habari 186 wamethibitishwa kuuawa tangu kuanza kwa mashambulizi ya kijeshi ya Israel dhidi ya Gaza mnamo Oktoba 2023.
All Rights Reserved © The Cantona Group PLC||2025
Discover more from cantonadigital
Subscribe to get the latest posts sent to your email.