Radio Fortune Africa -Na Cantona Joseph
https://zeno.fm/radio/radio-fortune-africa

Rais wa Kenya William Ruto amejibu hatua ya Marekani ya kutaka kupitia tena hadhi ya nchi yake ya mshirika mkuu asiye mwanachama wa NATO, akisema kuwa machaguo yake ya sera za masuala ya mambo ya nje yanazingatia kile ambacho kinafaa zaidi kwa Kenya.
Akizungumza na sekta za kibinafsi, Ruto alitetea ukuaji wa kibiashara na nchi kama China akisema kuwa lengo la utawala wake ni kunufaisha wazalishaji wa Wakenya na kurekebisha kile ambacho hakijakuwa sawa kwa muda mrefu.
Rais Ruto alikiri kuwa baadhi ya washirika wake wanahoji ukuaji wa kibiashara kati ya Kenya na China lakini akasisitiza kuwa maamuzi ya hatua hizo yanashinikizwa na mahitaji ya Kenya kiuchumi.
“Baadhi ya marafiki zetu wanalalamika kwamba tunafanya biashara nyingi na China. Wakati nilikutana na Rais Xi Jinping, nilimwambia Kenya inaingiza bidhaa za Sh600 bilioni kutoka China, lakini tunasafirisha tu labda 5%. Usawa huo wa kibiashara ni mbaya,” Ruto alisema.
Ruto aliongeza kuwa China imekubali kufungua soko lake kwa bidhaa za kilimo za Kenya.
“Wamekubali kufanya ya mabadiliko ya usawa wa kibiashara katika ya Kenya na China. Wamekubali kuondoa ushuru wote kwa chai yetu, kahawa, parachichi na bidhaa zote za kilimo tunazouza nje ya nchi.
“Tunaendeleza mazungumzo na India. Tuna uhusiano mzuri na Uturuki na Canada,” Ruto alisema.
Wakati huo huo, mwenyekiti wa kamati ya Bunge juu ya masuala ya ulinzi nchini Kenya Nelson Koech amemwandikia mwenzake Seneta wa Marekani Jim Risch akisema,
‘’…Namuomba mwenzangu wa Marekani Seneta Jim Risch mwenyekiti wa masuala ya mambo ya nje kufikiria upya mapendekezo ya marekebisho ya Sheria ya Uidhinishaji wa Kitaifa wa Ulinzi (NDAA) ya Mwaka 2026 kwa maslahi bora ya mataifa yetu mawili ya kirafiki.
Mapitio yaliopendekezwa na Seneta Risch ikiwa yataidhinishwa, yatajumuisha tatathmini ya sera za kigeni na za kidiplomasia za Kenya kama vile kujifungamanisha na Marekani na ushirikiano wake na China, Urusi na Iran.
Pamoja na makubaliano yanayowezekana ya Kenya, uhusiano wa kisiasa au kifedha na wanamgambo wenye silaha kama vile al-Shabaab na Rapid Support Forces (RSF) na mengineo.
Trump asema kuna ‘matarajio’ ya kukutana na Putin na Zelensky

Rais Donald Trump wa Marekani amesema kuwa “kuna fursa” ya kukutana na viongozi wa Urusi na Ukraine, kufuatia kile alichokitaja kuwa “mazungumzo yenye tija” kati ya mjumbe wake na Vladimir Putin.
Alipoulizwa katika Ikulu ya White House ikiwa viongozi hao wawili wamekubaliana kuwa na mkutano kama huo, Trump alisema kuna “matarajio makubwa”, lakini hakutoa maelezo zaidi.
Ukraine hapo awali ilitoa taarifa isiyo ya moja kwa moja kuhusu mazungumzo kati ya Putin na Steve Witkoff, huku msaidizi wa sera za kigeni akisema pande hizo mbili zimekuwa na mazungumzo “yenye tija” mjini Moscow.
Mjumbe wa Marekani amekutana na Putin siku chache kabla ya tarehe ya mwisho ya Trump kwa Urusi kukubali kusitisha mapigano nchini Ukraine, la sivyo ikakabiliwe na vikwazo vipya.
UN yashutumu waasi wa M23 kwa mauaji ya raia mashariki ya Congo

Umoja wa Mataifa imeshutumu waasi wa M23 wanaoungwa mkono na Rwanda kwa mauaji ya raia zaidi ya mia tatu mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.
Ofisi yake ya haki za binadamu imesema waathiriwa ni pamoja na wanawake arobaini na nane na watoto kumi na tisa.
Pia ililaani shambulizi dhidi ya raia lililotekelezwa na makundi mengine yenye silaha katika eneo hilo.
Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa UN, Volker Turk, amesema ameshutuka kwamba licha ya mpango wa kusitisha mapigano hivi karibuni uliosainiwa huko Qatar, vurugu upande wa mashariki ya Congo zimeongezeka.
Kulingana na UN, ofisi yake imepokea taarifa za moja kwa moja kuhusu wapiganaji wa M23 kuwauwa raia mia tatu na kumi na tisa kwa kipindi cha wiki mbili mwezi uliopita.
Waathiriwa wengi walikuwa wakulima wanaojishulisha na upanzi wakati huu wa msimu wa upandaji.
Hata hivyo, afisa mwandamizi wa M23 ametupilia mbali ripoti hiyo akisema ni propaganda.
Kulikuwa na matumaini ya kupungua kwa ghasia katika eneo hilo baada ya mpango wa hivi karibuni wa amani ulioongozwa na Marekani kati ya Rwanda na Congo lakini UN inasema raia wanaendelea kukabiliwa na athari mbaya za mgogoro huo.
Uingereza yaweka sheria kudhibiti upasuaji wa kubadili maumbile

Serikali ya Uingereza imetangaza mipango ya kukabiliana na biashara ya upasuaji kwa ajili ya kuboresha muenekano ikiwemo kuongeza makalio, kuongeza ukubwa wa viungo kama midomo na kuondoa makunyazi usoni.
Hatua hizo zinadhamiria kuwalinda watu walioko chini ya umri wa miaka 18 na kuhakikisha kuwa ni maafisa wa afya waliofuzu tu kuhudumu Uingereza watakaoruhusiwa kutoa huduma hizo za kunakshi urembo.
Kumekuwa na wasiwasi kuwa watu wanafanyiwa upasuaji na kupewa dawa katika mazingira yasiyo salama ikiwemo majumbani, kwenye mahoteli na kiliniki za muda na hivyo kuhatarisha maisha yao.
Sudan yadai imeshambulia ndege ya UAE na kuua mamluki wa Colombia

Jeshi la Sudan limetangaza kuwa limeshambulia ndege ya Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) iliyobeba takriban mamluki 40 wa Colombia kwenye uwanja wa ndege wa Nyala huko Darfur Kusini hapo jana.
Kwa mujibu wa tovuti ya Sudan Tribune iliyoko Paris, shambulio hilo liliwaua wote waliokuwa ndani ya ndege na kuharibu silaha zilizotakiwa kupelekwa kwa vikosi vya Rapid Support Forces (RSF).
Televisheni inayoendeshwa na serikali ya Sudan pia ilitoa ripoti hiyo, lakini UAE na RSF hawajasema chochote.
Serikali inayoongozwa na jeshi ya Sudan kwa muda mrefu imeshutumu UAE kwa kuchukua silaha na kuzisafirisha kwa wapiganaji wa RSF.
Mvutano uliongezeka wiki hii kufuatia ripoti ya gazeti la La Silla Vacía iliyohusisha UAE kuleta mamluki wa Colombia nchini Sudan.
Ikijibu, UAE ilisitisha safari zote za ndege kwenda na kutoka Sudan mnamo 6 Agosti.
Siku moja kabla, wizara ya mambo ya nje ya Sudan ilirejelea tena madai kuwa UAE inawapa silaha wapiganaji wa RSF .
UAE imekanusha kuhusika na mzozo huo.
zilizopitaGhana yaanza maombolezo kufuatia kifo cha mawaziri katika ajali ya helikopta

Rais John Mahama ametangaza kipindi cha siku tatu cha maombolezo ya kitaifa kufuatia kifo cha mawaziri wawili na watu wengine sita wa ngazi ya juu serikalini katika ajali ya helikopta iliyotokea jana Jumatano.
Bendera zote zitapeperushwa nusu mlingoti wakati nchi inaanza rasmi kipindi cha kuomboleza siku ya Alhamisi huku Rais Mahama akisimamisha shughuli zake zilizopangwa kwa wiki hii.
Miili ya waliofariki imepelekwa katika mji mkuu kutoka eneo la ajali hiyo ikiwa kwenye masanduku yaliyofunikwa na bendera ya Ghana, na kukafanyika hafla ya heshima katika Kambi ya Jeshi la Anga ili kuwapokea.
Mipango ya kuwazika Waislamu miongoni mwa waliokufa leo imeahirishwa hadi utambulisho kamili wa miili.
Serikali bado haijatangaza mipango ya mazishi.
Waathirika wa ajali hiyo ni pamoja na Waziri wa Ulinzi wa Ghana, Dk. Omane Boamah, Waziri wa Mazingira, Dkt. Murtala Mohammed, ambaye pia alikuwa mbunge, Alhaji Muniru Mohammed, Kaimu Naibu Mratibu wa Usalama wa Taifa, Dk. Samuel Sarpong, Makamu Mwenyekiti wa chama tawala cha National Democratic Congress na Samuel Aboagye, mgombea wa zamani wa bunge.
Pia kati ya waliokufa ni wafanyakazi wa ndege watatu.
Walikuwa njiani kwenda kwenye hafla ya kitaifa huko Obuasi iliolenga kupambana na madini haramu wakati helikopta ilipoanguka katika eneo lenye msitu mnene.
Jeshi la Ghana lilikuwa limeripoti kupoteza mawasiliano na helikopta ya Z-9 na baadaye likathibitisha kwamba imeanguka, na kusababisha vifo vya watu wote wanane waliokuwa kwenye ndege hiyo.
Mamlaka imeanzisha uchunguzi ili kubaini sababu za ajali hiyo.
Mwanajeshi wa Marekani awafyatulia risasi wenzake kambini

Wanajeshi watano wa Marekani walijeruhiwa baada ya sajenti wa Jeshi la Marekani kufyatua risasi kwenye kambi moja huko Georgia.
Kwa mujibu wa maafisa wa kijeshi, baada ya sajenti kwa jina Cornelius Radford kuwafyatulia risasi askari wenzake katika kambi ya Fort Stewart, askari waliokuwa eneo la tukio walimvamia na kumnyang’anya silaha.
Tukio hilo lilitokea Jumatano asubuhi. Kwa mujibu wa msemaji wa Ikulu ya Marekani Carolyn Leavitt, Rais wa Marekani Donald Trump amefahamishwa kuhusu tukio hilo Kwa mujibu wa maafisa wa kijeshi, silaha iliyotumika katika shambulio hilo si ya jeshi la Marekani na uchunguzi unaendelea kubaini jinsi iliingia kwenye kambi hiyo.
Jenerali John Lubas, kamanda wa Kitengo cha 3 cha Wanajeshi wa Jeshi la Marekani, ametangaza hali za wanajeshi waliojeruhiwa kuwa nzuri.
Kulingana na Jenerali Lubas, mshambuliaji huyo alikuwa mwanajeshi kutoka katika ngome hii na hakuwa na historia ya kuwa katika maeneo ya vita. Pia aliwapongeza askari waliompokonya silaha mara moja mshambuliaji huyo na kumkabidhi kwa polisi.
Kwa mujibu wa Jenerali Lubas, shabaha ya shambulizi hilo haijajulikana na mshambuliaji anahojiwa. Fort Stewart iko katika mji wa pwani wa Hinesville, kilomita 386 kutoka Atlanta.Mshirikishe mwenzako, Mwanajeshi wa Marekani awafyatulia risasi wenzake kambini
All Rights Reserved © The Cantona Group PLC||2025
Discover more from cantonadigital
Subscribe to get the latest posts sent to your email.