Thailand yashutumu Cambodia kwa kukiuka makubaliano ya usitishaji mapigano

Radio Fortune Africa -Na Cantona Joseph

https://zeno.fm/radio/radio-fortune-africa

.

Thailand imeishutumu Cambodia kwa kukiuka makubaliano ya kusitisha mapigano kwa “makusudi” ambayo nchi hizo mbili zilikubaliana kumaliza vita vya mpaka vilivyosababisha vifo vya takriban watu 33 na maelfu ya wengine kuyahama makazi yao.

Ni mwanzo mbaya wa usitishaji mapigano, ambao unalenga kukomesha siku tano za mashambulizi ya mabomu na makombora kwenye mpaka wao wa pamoja.

Jeshi la Thailand linasema liliacha kufyatua risasi baada ya saa sita usiku, lakini liliendelea kushuhudia milio ya risasi kutoka upande wa Cambodia “katika maeneo mengi” hadi leo asubuhi.

Hata hivyo, wizara ya ulinzi ya Cambodia ililiambia shirika la habari la AFP kwamba hakujakuwa na “makabiliano ya silaha” kati ya pande hizo mbili tangu usitishaji mapigano uanze usiku wa manane.

Urusi yashambulia gereza nchini Ukraine na kuwauwa watu 17, wengine kadhaa wajeruhiwa

Zaporizhzhia ni moja ya mikoa minne ya mashariki mwa Ukraine ambayo Urusi inadai kuwa imetwaa tangu 2022

Shambulizi la anga la Urusi katika gereza moja katika eneo la mstari wa mbele kusini mashariki mwa Ukraine limeua watu 17 na kuwajeruhi wengine 42, kulingana na maafisa wa Ukraine.

Shambulio la usiku huko Zaporizhzhia pia liliharibu nyumba zilizo karibu, kiongozi wa mkoa Ivan Fedorov alisema.

Vikosi vya Urusi vilianzisha mashambulizi manane kwa kutumia mabomu ya angani yenye milipuko mikubwa, aliongeza.

Mkuu wa wafanyakazi wa rais wa Ukraine, Andriy Yermak, alilaani shambulizi hilo kama “uhalifu mwingine wa kivita” uliofanywa na Urusi.

Zaporizhzhia ni moja ya mikoa minne ya mashariki mwa Ukraine ambayo Urusi inadai kuwa imetwaa tangu 2022, ingawa eneo hilo liko chini ya udhibiti wa Ukraine.

Kamishna wa haki za binadamu wa Ukraine alisema kushambulia jela ni ukiukaji mkubwa wa sheria za kibinadamu kwani watu walio kizuizini hawakupoteza haki yao ya kuishi na kulindwa.

Rais wa Marekani Donald Trump alitoa kauli ya mwisho kwa Moscow Jumatatu, akionya kwamba Urusi ina “takriban siku 10 au 12” kukubali kusitishwa kwa mapigano au kukabiliwa na vikwazo vikubwa.

Akizungumza katika ziara yake nchini Scotland, Trump aliwaambia waandishi wa habari kwamba “atatangaza huenda usiku wa leo au kesho,” na kuongeza, “hakuna sababu ya kusubiri, ikiwa unajua jibu ni nini”.

Jeshi la DRC laapa ‘kuwafuatilia wanamgambo bila kuchoka’ baada ya shambulio katika kanisa

Wanajeshi

Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (FARDC) limeapa “kuwafuatilia bila kuchoka” wanamgambo wanaohusishwa na IS baada ya shambulio la tarehe 26 Julai ambapo takriban waumini 43 wa Kikatoliki, wakiwemo watoto tisa, waliuawa katika mji wa Komanda Kaskazini-mashariki mwa Mkoa wa Ituri, Actualite inayomilikiwa na watu binafsi liliripoti jana.

Jeshi liliwashutumu wanamgambo hao kwa kuwaua na kuwajeruhi waumini kwa mapanga ili kulipiza kisasi hasara waliyopata kutokana na operesheni ya pamoja na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Uganda (UPDF).

“Wakifuatiliwa bila kuchoka na FARDC na UPDF katika maeneo ya Irumu na Mambasa, magaidi hawa wamechagua kulipiza kisasi kwa watu walio na amani na wasio na ulinzi ili kueneza ugaidi na kugeuza operesheni ya pamoja kutoka kwenye malengo yake,” jeshi lilisema.

limetoa wito kwa wakazi kusitisha “ushirikiano wote na adui”, likisema wanamgambo wa Allied Democratic Forces (ADF) walijipenyeza katika mji huo kwa msaada wa washirika.

China yatoa motisha ya $1,500 kwa wazazi ili kuongeza watoto

Mama na mwana

Wazazi nchini China wanapewa yuan 3,600 (£375; $500) kwa mwaka kwa kila mtoto wao aliye chini ya umri wa miaka mitatu katika ruzuku ya kwanza ya serikali nchini kote inayolenga kuongeza viwango vya uzazi.

Kiwango cha uzazi nchini humo kimekuwa kikishuka, hata baada ya Chama tawala cha Kikomunisti kukomesha sera yake tata ya mtoto mmoja karibu miaka kumi iliyopita.

Msaada huo utasaidia karibu familia milioni 20 kwa gharama ya kulea watoto, kulingana na vyombo vya habari vya serikali.

Mikoa kadhaa kote China imefanya majaribio ya aina fulani ya malipo ili kuhimiza watu kuwa na watoto zaidi huku taifa hilo la pili kwa uchumi mkubwa duniani likikabiliwa na mzozo wa idadi ya watu.

Mpango huo uliotangazwa Jumatatu, utawapa wazazi jumla ya hadi yuan 10,800 kwa kila mtoto.

Sera hiyo itatumika mara kwa mara kuanzia mwanzoni mwa mwaka huu, shirika la utangazaji la serikali ya Beijing CCTV lilisema.

Familia zilizo na watoto waliozaliwa kati ya 2022 na 2024 pia zinaweza kutuma maombi ya ruzuku kiasi.

Hatua hiyo inafuatia juhudi za serikali za mitaa kuongeza viwango vya uzazi nchini China.

Mashirika ya kutetea haki yaishutumu Israel kwa mauaji ya kimbari huko Gaza

Ni hospitali 18 tu kati ya 36 za Gaza ambazo bado zinafanya kazi kwa kiasi, kulingana na UN

Mashirika mawili makuu ya kutetea haki nchini Israel yamesema mwenendo wa Israel katika vita huko Gaza ni mauaji ya halaiki dhidi ya Wapalestina.

B’Tselem na Madaktari wa Haki za Kibinadamu-Israel walitoa ripoti tofauti siku ya Jumatatu kulingana na tafiti za miezi 21 iliyopita ya migogoro.

Mashirika hayo, ambayo yamekuwa yakifanya kazi nchini Israel kwa miongo kadhaa, yalisema katika taarifa ya pamoja kwamba “katika nyakati hizi za giza ni muhimu sana kutaja vitu kwa majina yao”, huku “ikitoa wito kwa uhalifu huu kukomeshwa mara moja”.

Msemaji wa serikali ya Israel amesema inakanusha vikali shutuma za mauaji ya halaiki ambayo ni ya kwanza kutolewa na mashirika ya kutetea haki za binadamu yenye makao yake nchini Israel.

“Vikosi vyetu vya ulinzi vinalenga magaidi na kamwe si raia. Hamas inahusika na mateso huko Gaza,” David Mencer alisema.

Israel ilianzisha vita vyake huko Gaza kulipiza kisasi shambulio la Hamas la tarehe 7 Oktoba 2023, ambalo liliua takriban watu 1,200 na wengine 251 kuchukuliwa mateka.

Mashambulizi ya Israel tangu wakati huo yameua zaidi ya watu 59,900 huko Gaza, kulingana na wizara ya afya inayosimamiwa na Hamas.

Takwimu za wizara hiyo zimenukuliwa na UN na wengine kama chanzo cha kuaminika zaidi cha takwimu zinazopatikana za majeruhi.

Islamic State yadai kuhusika na shambulizi dhidi ya raia DRC

ISIS

Wanamgambo wa Islamic State wamedai kuhusika na shambulizi dhidi ya raia nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Takribani watu 45 wakiwemo waumini wa kanisa waliuawa katika shambulio hilo linalodaiwa kufanywa na Alliance Democratic Forces (ADF), kundi lenye uhusiano na IS.

Shambulizi hilo lilitokea katika mji wa Komanda, katika jimbo la mashariki la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo la Ituri, mwishoni mwa juma.

Padre Dieudonné Beringa, Kasisi wa Parokia ya Bienheureuse Anuarite, ambako mauaji yalitokea aliIambia BBC, “Tuliamshwa na milio ya risasi na nyumba zikiteketezwa kutoka saa 1 asubuhi hadi saa 4 asubuhi, jana.

Ni baada ya shambulio hilo tu tulipogundua mauaji hayo katika eneo la kanisa hilo.” “Watu wenye silaha na mapanga waliwaua wanawake na wanaume waliokuwa wamekusanyika wakati wa maombi ya mkesha”, aliongeza.

Kulingana na Wizara ya mambo ya nje ya Mareakani, ISIS iliitambua hadharani ADF kama mshirika mwishoni mwa 2018 na imekuwa ikidai kuwajibika kwa mashambulio ya ADF kuanzia Aprili 2019.

Tangu mwisho wa 2021, Operesheni Shujaa ni hatua ya kijeshi ya pamoja ambapo Vikosi vya Wanajeshi vya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Uganda wamekuwa wakifanya doria katika jimbo la Ituri kutafuta kambi za ADF msituni.

Ingawa ADF imekuwa ikilaumiwa kwa mashambulizi ya mabomu nchini Uganda, ambako ndiko yalikotokea, mauaji yake mengi yamefanywa mashariki mwa DRC, ambako wanachama wake wamehama na kufanya kazi, tangu mwanzoni mwa miaka ya 2000.

Gaza inakabiliwa na ‘njaa kali’, Trump asema

Mkazi akiwa amebeba chakula

Kuna “njaa kali” huko Gaza, Donald Trump amesema, baada ya Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu kusisitiza kuwa hakuna kitu kama hicho.

Alipoulizwa iwapo anakubaliana na Netanyahu kwamba ni “uongo” kusema Israel inachochea njaa huko Gaza, rais wa Marekani alijibu: “Sijui… watoto hao wanaonekana kuwa na njaa sana… hayo ni mambo ya njaa kweli.”

Akizungumza wakati wa mkutano na Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer huko Scotland, Trump alisema: “Hakuna mtu aliyefanya jambo kubwa huko. Eneo lote ni fujo… Niliiambia Israel labda wanapaswa kufanya hivyo kwa njia tofauti.”

Maoni yake yalikuja baada ya mkuu wa Umoja wa Mataifa wa masuala ya kibinadamu kusema “kiasi kikubwa” cha chakula kilihitajika ili kukabiliana na njaa.

Siku ya Jumapili Netanyahu alitupilia mbali madai kwamba Israel iliwaua kwa makusudi raia wa Gaza, jambo ambalo lingekuwa uhalifu wa kivita.

“Ni uongo ulioje. Hakuna sera ya njaa huko Gaza, na hakuna njaa huko Gaza.” Alisema.

“Tunawezesha misaada ya kibinadamu katika muda wote wa vita kuingia Gaza. Vinginevyo, kusingekuwa na Wagaza. Na kilichozuia usambazaji wa misaada ya kibinadamu ni Hamas,” aliongeza.

Netanyahu alisema kusitisha kwa misaada ya kibinadamu kwa jeshi la Israel kunamaanisha Umoja wa Mataifa “hauna visingizio” vya kutokusanya na kusambaza misaada yote kutoka kwenye vivuko.

“Acha uongo. Acha kutafuta visingizio. Fanya unachopaswa kufanya.”

Siku ya Jumatatu usiku, ofisi ya Netanyahu ilisema Israel itafanya kazi na makundi ya misaada, Marekani na mataifa ya Ulaya ili kuhakikisha “kiasi kikubwa cha misaada ya kibinadamu kinatiririka” hadi Gaza.

All Rights Reserved © The Cantona Group PLC||2025


Discover more from cantonadigital

Subscribe to get the latest posts sent to your email.

Leave a comment