Serikali yakiri kushindwa kumudu ufadhili wa elimu ya bure Kenya

Radio Fortune Africa -Na Cantona Joseph

https://zeno.fm/radio/radio-fortune-africa

.

Serikali nchini Kenya imetangaza kwamba haiwezi kumudu tena kufadhili elimu ya bure katika shule za msingi na za sekondari.

Akizungumza mbele ya kamati ya bunge la kitaifa Julai 24, 2025, Waziri wa Fedha John Mbadi alisema ufadhili wa masomo ya bure umekuwa mzigo mkubwa kwa serikali na kulazimika kupunguza fedha zilizotengewa sekta ya elimu kwa madai kuwa idadi ya wanafunzi shuleni imeongezeka mno.

Kulingana na serikali sasa ufadhili wa shule ya upili utapungua hadi shilingi 16,900 kwa mwanafunzi mmoja, kutoka shilingi 22,244.

“Kwa sasa, wanafunzi wanapewa ufadhili wa ada ya masomo na gharama za uendeshaji kwa kiwango cha Ksh1,420 kwa elimu ya msingi. Kwa shule ya sekondari ya chini, ni Ksh15,042 kwa kila mtoto, na katika shule ya sekondari ya juu, ni Ksh22,244 kwa kila mtoto”, Waziri Mbadi alisema.

“Hata hivyo, kwa sababu ya ukosefu wa fedha na vipaumbele vingine vinavyoibuka ndani ya sekta ya elimu, kuongezwa kwa viwango hivi kunaweza kusiwezekane lakini serikali itafikiria kuvipitia tena ikiwa upatikanaji wa mapato utaimarika.”

Akiunga mkono madai hayo, Waziri wa Elimu, Julius Ogamba, ambaye pia anaamini kuwa ongezeko la idadi ya wanafunzi limechangia hatua hii alisema “idadi hii kwa miaka minne au mitano iliyopita haijawahi kushuhudiwa katika bajeti ya fedha inayotengwa kwa ajili ya wizara ya elimu, na hiyo ni kwa sababu idadi ya wanafunzi imekuwa ikiongezeka, lakini kiwango cha fedha kilichotengwa kimesalia kuwa kile kile”, Ogamba alisema.

Hatua hii inamaana kwamba wazazi watalazimika kuchangia zaidi ili kuwezesha watoto kupata elimu.

All Rights Reserved © The Cantona Group PLC||2025


Discover more from cantonadigital

Subscribe to get the latest posts sent to your email.

Leave a comment