Radio Fortune Africa -Na Cantona Joseph
https://zeno.fm/radio/radio-fortune-africa

Georges Abdallah, mwalimu wa Lebanon mwenye umri wa miaka 74 ambaye alipendelea Palestina, ataachiliwa na Ufaransa siku ya Ijumaa baada ya miaka 41 jela.
Akizungumziwa na wakili wake kama “mtu ambaye amekaa gerezani muda mrefu zaidi kwa matukio yanayohusiana na mzozo wa Israel na Palestina,” Abdallah anatarajiwa kupandishwa kwenye ndege moja kwa moja hadi Beirut.
Alihukumiwa mwaka 1987 kwa kuhusika katika mauaji nchini Ufaransa ya wanadiplomasia wawili – Mmarekani na Muisraeli – kwa kiasi kikubwa Abdallah amesahaulika na umma.
Abdallah alikamatwa mjini Lyon mwaka wa 1984. Akiwa amefuatiliwa na maafisa wa kijasusi wa Ufaransa, alifikiri alikuwa akifuatiliwa na wauaji wa Israel na kujisalimisha katika kituo cha polisi. Mara ya kwanza alishtakiwa kwa kuwa na hati za kusafiria za uwongo na kushiriki katika uhalifu.
Muda mfupi baadaye raia wa Ufaransa alitekwa nyara kaskazini mwa Lebanon, na huduma ya siri ya Ufaransa iliingia kwenye mazungumzo kupitia Algeria ili kufikia mabadilishano ya wafungwa.
Raia huyo wa Ufaransa aliachiliwa, lakini muda mfupi kabla ya Abdallah kuachiliwa, polisi mjini Paris walipata silaha kwenye nyumba yake, ikiwa ni pamoja na bunduki iliyotumiwa kuwaua wanadiplomasia. Hii ilifanya asiweze kuachiliwa.
Miaka miwili baadaye, Paris ilikumbwa na msururu wa mashambulizi ya kigaidi yaliyoua watu 13. Wanasiasa na vyombo vya habari walilaumu washirika wa Abdallah kwa kujaribu kushinikiza Ufaransa kumwachilia huru.
Baadaye ilithibitishwa kwamba ilikuwa kazi ya kundi la Washia wa Lebanon la Hezbollah, chini ya maelekezo kutoka Iran.
Katika kesi hiyo, Abdallah alikanusha kuhusika na mauaji hayo lakini akahukumiwa kifungo cha maisha.
Mshawishi wa Marekani adai kuwa mke wa rais wa Ufaransa alizaliwa akiwa mwanaume

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron na mkewe Brigitte wamewasilisha kesi ya kuchafuliwa jina dhidi ya mshawishi wa mrengo wa kulia Candace Owens, ambaye anadai kuwa mke wa rais wa Ufaransa alizaliwa akiwa mwanaume.
Kesi iliyowasilishwa siku ya Jumatano katika jimbo la Delaware nchini Marekani, ilisema Owens amekuwa akieneza “hadithi zisizo za kawaida na kuwaharibia jina”.
Owens amerudia mara kwa mara madai hayo kwenye podcast yake maarufu na chaneli za mitandao ya kijamii, na mnamo mwezi Machi 2024 alisema kwamba angeweka hatarini “sifa yake kitaalam” kwa imani kwamba Bi Macron “ni mwanaume”.
Katika kipindi cha podikasti yake iliyotolewa Jumatano, Owens aliendeleza madai yake na kuzungumza juu ya kesi hiyo akisema: “Huu ni upuuzi”
Owens alimdhihaki mke wa rais wa Ufaransa na kuelezea kushitakiwa naye kama “mkakati wa wazi na wa kukata tamaa…”.
Dhana ambayo imesambaa kwa miaka mingi kwenye mitandao ya kijamii inadai kuwa Bi Macron alizaliwa akiwa mwanaume kwa jina la Jean-Michel Trogneux, ambaye ni kaka yake.
Owens ameeneza dhana hiyo kwa watazamaji wake, ikiwa ni pamoja na karibu wafuasi 7m kwenye mtandao wa X. Mapema mwaka huu alitoa mfululizo wa video unaoitwa ‘Becoming Brigitte’.
Upande wa Macron ulisema katika taarifa iliyotolewa na mawakili wao kwamba walimwomba Owens mara kwa mara kufuta madai hayo, lakini “hatimaye waliamua kupeleka suala hilo mahakamani kwa sababu ndiyo njia pekee iliyosalia kupata suluhu”.
“Kampeni ya Bi Owens ya kumharibia sifa ilibuniwa kutunyanyasa na kusababisha maumivu kwetu na familia zetu na kuvutia nadhari na sifa mbaya,” ilisema taarifa hiyo.
Macron kulitambua taifa la Palestina

Rais Emmanuel Macron amesema Ufaransa italitambua rasmi taifa la Palestina mwezi Septemba jambo ambalo litalifanya kuwa taifa la kwanza la G7 kufanya hivyo.
Katika chapisho kwenye mtandao wa X, Macron alisema tangazo hilo rasmi litatolewa katika kikao cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa huko New York.
“Lenye uhitaji mkubwa hii leo ni kukomeshwa kwa vita huko Gaza na raia waokolewe. Amani inawezekana kufikiwa. Tunahitaji usitishaji mapigano mara moja, kuachiliwa kwa mateka wote, na msaada mkubwa wa kibinadamu kwa watu wa Gaza,” aliandika.
Maafisa wa Palestina walifurahishwa na uamuzi wa Macron, huku Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu akisema hatua hiyo “inaunga mkono ugaidi” kufuatia shambulio la Hamas la tarehe 7 Oktoba 2023 nchini Israel.
Katika chapisho lake kwenye ntandai wa X siku ya Alhamisi, Macron aliandika: “Mkweli kwa ahadi yake ya kihistoria kwa haki na amani ya kudumu katika Mashariki ya Kati, nimeamua kuwa Ufaransa itatambua Jimbo la Palestina.
“Lazima pia tuhakikishe kuondolewa kwa Hamas, na kulinda na kuijenga upya Gaza.
“Mwishowe, ni lazima tujenge Taifa la Palestina, tuhakikishe uwepo wake, na pia kuhakikisha kwa kukubali kuondolewa kwa jeshi na kuitambua kikamilifu Israel, kunachangia usalama wa wote Mashariki ya Kati. Hakuna njia mbadala.”
Macron pia aliambatanisha barua kwa Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina Mahmoud Abbas kuthibitisha uamuzi wake huo.
Amnesty International: Iran ilitumia mabomu hatari ya kutapakaa dhidi ya Israel

Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International linasema Iran ilirusha mabomu hatari ya kutapakaa “mabomu ya vishada” katika maeneo ya makazi yenye watu wengi wakati wa vita vyake vya siku 12 na Israel, kitendo kilichochukuliwa kuwa ni ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa za kibinadamu.
Amnesty International ilituma maswali kwa mamlaka ya Iran kuhusu matumizi ya mabomu ya vishada tarehe 15 Julai lakini haikuwa imepokea jibu lolote kufikia wakati wa kuchapishwa kwa ripoti hii
Katika ripoti iliyotolewa Alhamisi (Julai 24), shirika hilo lilisema kuwa katika vita na Israel, Iran ilirusha makombora ya balestiki. Makombora haya yalishambulia maeneo ya makazi yenye watu wengi nchini Israel, na kuhatarisha maisha ya raia.
Amnesty International imepitia picha na video ambazo ripoti za vyombo vya habari zilisema zilitua katika eneo la Ghoshdan nje ya Tel Aviv mnamo Juni 19. Mapitio hayo yanaonyesha matumizi ya mabomu ya vishada.
All Rights Reserved © The Cantona Group PLC||2025
Discover more from cantonadigital
Subscribe to get the latest posts sent to your email.