Radio Fortune Africa -Na Cantona Joseph
https://zeno.fm/radio/radio-fortune-africa

Mahakama kuu ya Ulaya imetoa uamuzi wake na kusema kuwa haki ya Caster Semenya, mwanariadha wa Afrika kusini, ya kusikilizwa bila ubaguzi ilikiukwa na Mahakama ya Juu Zaidi ya Uswizi alipopoteza rufaa ya mwaka 2020 dhidi ya kanuni za Riadha za Dunia kulikomzuia kushiriki mashindano.
Semenya, bingwa wa Olimpiki wa mita 800 alipata ushindi kiasi fulani katika Mahakama ya Ulaya ya Kutetea Haki za Kibinadamu kwenye kesi hii ambayo imekuwa ikiendelea kwa muda mrefu juu ya sheria za ustahiki wa jinsia katika kushiriki kwenye riadha.
Semenya, 34, alizaliwa na utofauti wa kijinsia na ameshindwa kushiriki katika mbio za mita 800 za wanariadha wa kike tangu Shirikisho la Dunia la Riadha lilipoanzisha sheria mwaka 2019 inayozuia viwango kuanzia kiasi fulani vya testosteroni kwa wanaoshiriki riadha kuanzia mita 400 hadi maili.
Mwanariadha huyo wa mbio za kati wa Afrika Kusini anaamini Shirikisho la la Dunia la Riadha limeonyesha ubaguzi dhidi ya wanariadha waliozaliwa wakiwa na tofauti ya jinsia kwa kusisitiza kuwa wapunguze viwango vya testosteroni ili waweze kustahiki.
Akizungumza na BBC Sport baada ya kutolewa kwa uamuzi huo, Semenya alisema: “Hii ni hatua kubwa kuliko nilivyofikiria. Sidhani kama hii inahusu mashindano, inahusu haki za binadamu. Inahusu ulinzi wa wanariadha.
“Jukumu langu ni kuwa sauti kwa wale ambao hawawezi kuzungumza.”
Bodi inayosimamia riadha inasisitiza kuwa sheria, ambazo mwaka wa 2023 zilipanuliwa ili kuangazia mbio zote za wanawake, zinahitajika ili kuhakikisha ushindani wa haki na kulinda jamii ya wanawake.
Semenya alikuwa bingwa wa Olimpiki wa mbio za mita 800 mnamo 2012 na 2016.
Mnamo mwaka 2019, aliwasilisha pinganizi dhidi ya Shirikisho la Dunia la Riadha bila mafanikio katika Mahakama ya Usuluhishi ya Michezo (Cas) yenye makao yake Uswizi.
Mnamo Julai 2023 Mahakama ya Ulaya ya Kutetea Haki za Kibinadamu ilitoa uamuzi uliompendelea Semenya katika kesi iliyohusiana na viwango vya testosteroni kwa wanariadha wa kike.
All Rights Reserved © The Cantona Group PLC||2025
Discover more from cantonadigital
Subscribe to get the latest posts sent to your email.