Wahouthi wazamisha meli ya pili ya mizigo Bahari ya Shamu ndani ya wiki moja

Radio Fortune Africa -Na Cantona Joseph

https://zeno.fm/radio/radio-fortune-africa

Wafanyakazi sita wameokolewa na takriban wengine watatu kufariki dunia baada ya meli ya mizigo kushambuliwa na Wahouthi wa Yemen na kuzama kwenye Bahari ya Shamu, ujumbe wa wanamaji wa Ulaya unasema.

Meli kubwa ya kubeba mizigo ya Eternity C iliyokuwa na bendera ya Liberia, inayoendeshwa na Ugiriki ilikuwa na wafanyakazi 25 ilipoharibiwa vibaya na kupoteza mwelekeo baada ya kushambuliwa na maguruneti ya kurushwa kwa roketi Jumatatu kutoka kwa boti ndogo, kulingana na shirika la Uingereza la Uendeshaji Biashara Baharini (UKMTO).

Shambulizi hilo liliendelea Jumanne na shughuli za uokoaji zilianza usiku kucha.

Wahouthi wanaoungwa mkono na Iran walisema walishambulia meli ya Eternity C kwa sababu ilikuwa ikielekea Israel, na kwamba walichukua idadi isiyojulikana ya wafanyakazi hadi “mahali salama”.

Ubalozi wa Marekani nchini Yemen ulisema Wahouthi “wamewateka nyara wafanyakazi wengi walionusurika” na kutoa wito waachiliwe mara moja.

Mamlaka nchini Ufilipino ilisema 21 kati ya wafanyakazi hao walikuwa raia wake.

Mwingine kati yao ni raia wa Urusi ambaye alijeruhiwa vibaya katika shambulizi hilo na kupoteza mguu.

Ni meli ya pili ya Wahouthi kuzama ndani ya wiki moja, baada ya kundi hilo Jumapili kurusha makombora na ndege zisizo na rubani kwenye meli nyingine ya mizigo yenye bendera ya Liberia, Magic Seas, ambayo walidai “ni ya kampuni iliyokiuka marufuku ya kuingia kwenye bandari za Palestina inayokaliwa”.

Picha za video zilizotolewa na Wahouthi siku ya Jumanne zilionyesha watu wenye silaha wakiingia kwenye chombo hicho na kuilipua maraa kadhaa kabla ya kuzama.

Mnamo mwezi Mei, Wahouthi walikubali makubaliano ya kusitisha mapigano na Marekani kufuatia wiki saba za mashambulizi makali ya Marekani dhidi ya Yemen kujibu mashambulizi dhidi ya meli za kimataifa.

Hata hivyo, walisema makubaliano hayo hayajumuishi kukomesha mashambulizi dhidi za Israel, ambayo imefanya mashambulizi mengi ya kulipiza kisasi nchini Yemen.

All Rights Reserved © The Cantona Group PLC||2025


Discover more from cantonadigital

Subscribe to get the latest posts sent to your email.

Leave a comment