JPM: Kutoka maumivu, uhai, hadi uchumi Tanzania

Radio Fortune Africa -Na Cantona Joseph

https://zeno.fm/radio/radio-fortune-africa

Aliposimama katika mwalo wa Kigongo akiwa Mkemia katika Chama cha Ushirika cha Nyanza, John Pombe Magufuli alikumbwa na hofu isiyosahaulika. “Nikasogea pale kwenye mwalo, waliniambia ingia na pikipiki yako ingiza… moyo ukakataa,” alisema akitoka Busisi kutoa posa kwa Janeth Magufuli na alikuwa akirejea Mwanza mjini, alipokuwa anaishi na kufanya kazi.

“Nilipofika Mwanza ule mtumbwi ukawa umezama na ukaua watu 11…”

Tukio hilo, alilolieleza kwa uchungu mnamo Desemba 28, 2020, kuhusu ajali ambayo mtumbwi aliokua apande pamoja na pikipiki yake aina ya Honda XL125, MCF124, ili avuke kutoka upande mmoja wa Ziwa Victoria, Busisi ili kwenda upande mwingine wa pili, Kigongo, na kufika Mwanza mjini, ulikua umezama na kuua watu.

Ajali hii ilimfanya kutoa ahadi isiyo ya kawaida: “Nikipewa nafasi serikalini, nitajenga daraja hapa.”

Magufuli akapata nafasi akianza katika nafasi ya uwaziri mpaka akaja kuwa Rais wa Tanzania, mwaka 2015. Akatimiza ahadi yake aliyoitoa wakati wa kampeni ya kuwania urais mwaka 2015.

“Nilipokuwa kwenye kampeni (za uchaguzi), watu hawakuamini, walisema haiwezekani, anaota, hizi ni kampeni tu”, anasimulia Magufuli.

Miezi mitatu baada ya kutoa simulizi hii, Magufuli alifariki dunia. Hakuwa hai kushuhudia kukamilika kwa ndoto yake, lakini alikwishapanda mbegu ya matumaini. Aliliacha daraja hilo likiwa limekamilika kwa asilimia 25 tu. Juni 19, 2025, Rais wa sasa wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan alizindua rasmi daraja hilo la JPM maarufu kama daraja la Kigongo – Busisi, ambalo sasa ni moja ya alama kubwa za miundombinu barani Afrika, akikamilisha 75% zilizobaki kwa pesa za ndani.

Kwa urefu wa kilomita 3.0, daraja hilo limeiweka Tanzania kwenye ramani ya bara kwa kuwa daraja refu zaidi Afrika Mashariki na kati, na la sita kwa urefu katika bara lote la Afrika. Lakini kwa maana ya kimkakati, kiuchumi, kijamii, na kijiografia, daraja hili lina uzito wa kipekee unaolihusisha mataifa zaidi ya sita.

Daraja la maumivu lililozaliwa kwa kilio cha msiba

MV
Maelezo ya picha,Kivuko cha MV. SENGEREMA kilikuwa usafiri tegemeo kati ya Kigongo – Busisi, kikiwa na uwezo wa kubeba abiria 490 na magari 24 tu sawa na tani 170

Kwa miaka mingi, eneo la kivuko kutoka Kigongo – Busisi kuunganisha Wilaya za Misungwi na Sengerema mkoani Mwanza, kilikuwa mwokozi na wakati mwingine mwiba kwa wasafiri wa Ziwa Victoria.

Hali hii haikuwa tu tatizo la usafiri, bali kiini cha vifo, kucheleweshwa kwa huduma za afya, kushuka kwa uzalishaji, na kuzorota kwa biashara.

Kivuko maarufu cha MV SENGEREMA na mitumbwi kadhaa imekuwa ikihudumia watu zaidi ya watu milioni 1.5 kwa mwaka. Kivuko cha MV. SENGEREMA kilikuwa na uwezo wa kubeba abiria 490 na magari 24 sawa na tani 170, kutokana na urefu wake wa mita 55, upana wa mita 10.5 na kina cha kuelea mita 1.4.

Kwa mujibu wa takwimu za Mamlaka ya usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) mwaka 2020, kivuko hicho kilikuwa kinavusha magari kati ya 500 hadi 600 kwa siku, kwa safari za mpaka saa 2 wakati mwingine kutokana na foleni, ucheleweshaji wa kivuko, au hali ya hewa mbaya.

Hayati Magufuli akiwa mwananchi tu wa kawaida, alipokutana na tukio la ajali ya mtumbwi iliyoua watu 11, aliweka ahadi, alipoingia wizarani kama naibu waziri na baadaye waziri alikumbuka ahadi yake na alipoutwaa urais mwaka 2015 dhamira yake ilikolea zaidi na kutimiza ahadi.

Magufuli alikuwa na wazo moja tu la kuokoa maisha, na si vinginevyo: “Nilipokuwa Wizara ya Ujenzi, mawazo yangu yalikuwa ni kuokoa maisha ya watu hawa…”, alisema Magufuli akisimulia chimbuko la wazo la ujenzi wa daraja hili.

Daraja refu na fursa ndefu za kikanda

Boti mpya
Maelezo ya picha,Sekta ya uvuvi inazalisha ajira zaidi ya milioni 4.5 Tanzania, kwa boti za kisasa kama hizi, daraja la JPM litarahisisha usafirishaji wa tani za samaki zinazovuliwa na kukuza uchumi wa bluu

Daraja hili si la Mwanza pekee ni la kanda ya ziwa na zaidi. Linaunganisha mikoa ya Mwanza, Geita, Mara, Shinyanga, na Simiyu. Zaidi ya Watanzania milioni 15 watanufaika nalo moja kwa moja. Kwa mujibu wa Shirika la takwimu la Tanzania (NBS) kanda ya Ziwa, ambayo inachangia zaidi ya 20% ya pato la taifa, sasa ina nafasi mpya ya kuongeza thamani ya bidhaa zake kupitia viwanda vya usindikaji vilivyopo na shughuli zingine za uchumi, zikiwemo biashara, uvuvi, na kilimo.

Kilimo cha mazao ya biashara (pamba, kahawa, mahindi), uvuvi (hasa sangara), na biashara ya samaki baridi ndizo nguzo kuu, kama anavyosisitiza aliyekuwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega:

“Sekta ya uvuvi ni miongoni mwa sekta yenye mchango mkubwa wa ukuzaji uchumi wa nchi, sekta hii imezalisha zaidi ya ajira milioni 4.5 zinazojumisha wavuvi wa asili na wakuzaji na wakulima wa mwani na kusaidia kwa kiasi kikubwa kwenye usalama wa chakula”.

Kwa mantiki ya kijiografia na kiuchumi, daraja linafungua lango la biashara kuelekea mataifa ya Uganda, Kenya, Rwanda, Burundi, DRC na hata Sudan Kusini kupitia barabara kuu ya Central Corridor.

Hii ina maana biashara za kimataifa kupitia bandari ya Mwanza zitaongezeka kwa kiwango kikubwa. Kwa mujibu wa ESRF Economic Outlook 2023, takribani 40% ya mizigo ya kibiashara ya Uganda hupitia Ziwa Victoria, sehemu kubwa ikielekezwa Mwanza.

Biashara kati ya Uganda na Tanzania ilikua kwa kasi na kufikia takribani dola za kimarekani bilioni 2.23 mwaka 2024. Kukamilika kwa daraja hili kunatarajiwa kuongeza idadi ya mizigo ya transit kupitia Mwanza kwa kiwango cha hadi 60% kufikia mwaka 2027 na kuendelea kukuza biashara kati ya nchi hizi na nyingine jirani.

SAMIA
Maelezo ya picha,Rais Samia akiwa na viongozi wengine kwenye uzinduzi wa daraja la JPM (Kigongo-Busisi), Juni 19, 2025

Uganda ni mfano tu, lakini Kenya, Rwanda, Burundi, DRC na hata Sudan Kusini wanafanya daraja hili kuwa daraja muhimu la kuchochea fursa za kiuchumi.

“Dar es Salaam, tunapoteza bilioni 4 kwa siku (takriban dola za Kimarekani milioni 1.5), kama trilioni 1.3 mpaka 1.4 kwa mwaka (takriban dola za Kimarekani milioni 490 mpaka 530) kwa sababu ya foleni, ” anasema mchambuzi Gabriel Mwang’onda akirejea kuhudu muda mfupi wa kuvuka unavyoweza kuleta mapinduzi makubwa.

Daraja JPM (Kigongo-Busisi) limesitisha matatizo mengi ikiwemo muda wa kuvuka kutoka dakika 30 mpaka 60 mpaka ndani ya dakika 4 tu kwa gari, na dakika 15 kwa miguu. Tena kwa usalama, uhakika na kwa kiwango cha barabara ya kisasa.

Hapo awali, upotevu wa mazao kutokana na ucheleweshaji ulifikia hadi 30%, na samaki waliochemka kabla ya kufika sokoni, kwa mujibu wa ripoti rasmi. Daraja hili linakwenda kupunguza hili.

Serikali kupitia Wakala wa Ufundi na Umeme nchini (TEMESA) ilikarabati vivuko viwili vinavyotoa huduma Mkoani Mwanza , kikiwemo MV SENGEREMA, kilichokuwa tegemeo kwa huduma ya usafiri kati ya Kigongo wilayani Misungwi na Busisi Wilayani Sengerema kwa gharama ya shilingi bilioni 2.9.

Fedha hizi sasa zinaweza kutumika kwingine, kwa sababu hakutakua na aina hii ya ukarabati wa kugharimu fedha nyingi kiasi hiki, kutokana na uwepo wa daraja la JPM.

Kwa sasa, zaidi ya magari 20,000 yanaweza kupita darajani kila siku likilinganishwa na magari kati ya 500 na 1,600 yaliyokuwa yanabebwa na kivuko. Hii ni ongezeko la zaidi ya mara 40, linaloongeza ufanisi, mapato ya serikali kupitia tozo, ukuaji wa sekta ya usafirishaji, ukuaji wa uchumi wa nchi na mtu mmoja mmoja.

Wazo la Magufuli kuhusu daraja hili lilibeba matumaini ya kuokoa uhai na kumaliza maumivu, lakini linakwenda mbali zaidi kwenye kujenga uchumi wa Tanzania na nchi jirani.

Sifa za JPM kwenye koti la daraja la JPM

Magufuli
Maelezo ya picha,Rais Magufuli (mwenye kofia), akikagua daraja la JPM Disemba 28, 2020). Ilikuwa mara ya mwisho kulikanyaga kwenye hadhira, kabla ya kufariki dunia Machi 17, 2021

Daraja la JPM (Kigongo – Busisi), lililopewa jina la Rais John Pombe Magufuli (JPM) kwa heshima ya mchango wake mkubwa katika miundombinu, si tu ujenzi wa chuma na zege, ni ishara ya matumaini na kichocheo cha uchumi kwa Tanzania na Afrika Mashariki.

JPM alikuwa na mkono mrefu wa miradi mikubwa ya miundombinu nchini, ikiwemo Reli ya Kisasa (SGR), Bwawa la Umeme la Mwalimu Julius Nyerere (JNHPP), Daraja la Mfugale (TAZARA), na upanuzi wa barabara na madaraja kama lile la juu la Kijazi (Ubungo).

Daraja hili la JPM, ambalo ujenzi wake ulisimamiwa na kampuni ya China Civil Engineering Construction Corporation (CCECC), umegharimu shilingi bilioni 716, zote zikitoka katika mifuko ya Serikali ya Tanzania. Linatumia teknolojia ya kisasa ya ‘Extra Dosed Bridge’, ambayo ni ya kwanza kutumika nchini, ikiwezesha ujenzi wa daraja refu kwa kutumia nguzo chache, na hivyo kupunguza gharama na muda wa ujenzi.

Vipimo na Sifa Muhimu:

Daraja hili lina urefu wa kilomita 3.0 na upana wa mita 28.45 likiwa namba 1 Afrika Mashariki na kati na la 6 kwa urefu Afrika. Limezidiwa urefu na daraja la 6th October- Misri (20.5 km), Third Mainland, Nigeria (11.8 km), Suez Canal Bridge, Misri (3.9 km), Dona Ana -Msumbiji (3.67 km) na El Hachef Viaduct, Morocco (3.46 km).

6th Oct
Maelezo ya picha,Daraja refu kuliko yote Afrika ni 6th October, liko Misri likiwa na urefu karibu mara ya 7 ya daraja la JPM (20.5km)

Linajumuisha njia nne za magari na njia mbili za waenda kwa miguu, kila moja ikiwa na upana wa mita 2.5. Lina jumla ya nguzo 804, ambapo nguzo kuu ni 67. Umbali wa mita 120 kati ya nguzo kuu unaruhusu meli kubwa kupita bila kikwazo. Daraja hili lina uwezo wa kubeba mzigo wa hadi tani 160 na linatarajiwa kudumu kwa zaidi ya miaka 100.

Ujenzi wa daraja hili ulianza Februari 25, 2020, na nguzo ya kwanza kusimikwa na kuzinduliwa rasmi Juni 19, 2025. Hii inamaanisha takriban siku 1941 zimetumika kukamilisha mradi huu muhimu, ikiwa ni takriban 5.31% tu ya muda wa miaka 100 ambalo daraja hili linatarajiwa kuhudumia taifa na nchi jirani.

Katika taifa lililojikita katika uchumi wa viwanda na biashara ya kikanda, daraja la JPM (Kigongo-Busisi) ni zaidi ya miundombinu; ni lango la fursa, likisogeza Tanzania karibu na malengo yake ya kimaendeleo. Magufuli alianzisha, Rais Samia akamalizia kwa zaidi ya robo tatu ya juhudi na sasa fursa anuwai zitokanazo na urefu na uwepo wake zinasubiri kuonekana zikinufaisha Tanzania na majirani zake.

All Rights Reserved © The Cantona Group PLC||2025


Discover more from cantonadigital

Subscribe to get the latest posts sent to your email.

Leave a comment