Umoja wa Mataifa wataka uchunguzi kuhusu mauaji karibu na eneo la usambazaji wa misaada Gaza

Radio Fortune Africa -Na Cantona Joseph

https://zeno.fm/radio/radio-fortune-africa

dc
Maelezo ya picha,Miili ilipelekwa katika hospitali ya Nasser baada ya tukio hilo

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ametaka uchunguzi huru ufanyike kuhusu mauaji ya Wapalestina karibu na kituo cha kusambaza misaada huko Gaza siku ya Jumapili, huku kukiwa na ripoti kwamba vikosi vya Israel vilifyatua risasi.

Mashahidi waliripoti kupigwa risasi wakati wakisubiri chakula katika kituo cha Rafah kinachoendeshwa na Wakfu wa Kibinadamu wa Gaza (GHF) unaoungwa mkono na Marekani na Israel.

Shirika la Msalaba Mwekundu lilisema hospitali yake ilipokea majeruhi 179, 21 kati yao wakiwa wamekufa. Shirika la Ulinzi la Raia linaloendeshwa na Hamas linasema idadi ya waliofariki ni 31.

Siku ya Jumapili, jeshi la Israeli lilikanusha kuwafyatulia risasi raia karibu au ndani ya eneo hilo na kusema ripoti kuhusu tukio hilo ni za uwongo.

GHF pia ilisema ripoti hizo ni “uzushi mtupu” na haijaona ushahidi wa shambulio katika kituo chake au karibu na kituo chake.

Israel hairuhusu mashirika ya habari ya kimataifa, ikiwa ni pamoja na BBC, kuingia Gaza, na kufanya uhakiki wa kile kinachotokea katika eneo hilo kuwa mgumu.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Guterres alisema katika taarifa yake siku ya Jumatatu: “Nimechukizwa na ripoti za Wapalestina kuuawa na kujeruhiwa wakati wakitafuta msaada huko Gaza jana. Natoa wito wa uchunguzi wa haraka na huru kuhusu matukio haya na wahusika wawajibishwe.”

Wizara ya mambo ya nje ya Israel ilijibu kwa kuyataja maoni yake kama “fedheha” katika chapisho kwenye X, na kumkosoa kwa kutoitaja Hamas.

Israel ilianzisha kampeni ya kijeshi huko Gaza kujibu shambulio la Hamas la kuvuka mpaka tarehe 7 Oktoba 2023, ambapo takriban watu 1,200 waliuawa na wengine 251 walichukuliwa mateka.

Takriban watu 54,470 wameuawa huko Gaza tangu wakati huo, wakiwemo 4,201 tangu Israel ianze tena mashambulizi yake mwezi Machi mwaka huu, kulingana na wizara ya afya ya eneo hilo inayoendeshwa na Hamas.

All Rights Reserved © The Cantona Group PLC||2025


Discover more from cantonadigital

Subscribe to get the latest posts sent to your email.

Leave a comment