Radio Fortune Africa -Na Cantona Joseph
https://zeno.fm/radio/radio-fortune-africa

Idadi rasmi ya watu waliofariki baada ya mafuriko kukumba mji wa Mokwa nchini Nigeria siku ya Alhamisi imeongezeka na kufikia zaidi ya 200, maafisa wanasema.
Watu wengine 500 bado hawajulikani walipo katika mji ulio katikati mwa Jimbo la Niger, hata hivyo, afisa wa eneo hilo Musa Kimboku aliambia BBC kwamba juhudi za uokoaji zimesitishwa kwa sababu mamlaka haiamini tena kuwa kuna mtu yeyote ambaye bado anaweza kupatikana akiwa hai.
Mafuriko hayo, yanayosemekana kuwa mabaya zaidi katika eneo hilo kwa miaka 60, yalikumba miji ya Tiffin Maza na Anguwan Hausawa baada ya mvua kubwa kunyesha.
Katika juhudi za kuzuia magonjwa katika eneo hilo, mamlaka hivi karibuni itaanza kutafuta maiti zilizozikwa chini ya ardhi, mkuu wa wilaya ya Mokwa Muhammadu Aliyu alisema.
Wakisimulia matukio ya maafa, wakaazi wa eneo hilo waliambia BBC kwamba waliona nyumba na familia zao zikisombwa na maji.
Mwanamume mmoja, Adamu Yusuf, alipoteza mke wake na mtoto mchanga.
“Nilitazama bila msaada huku maji yakiisomba familia yangu. Nilinusurika kwa sababu niliweza kuogelea,” aliambia BBC.
Shirika la Msalaba Mwekundu la Nigeria lilitoa taarifa siku ya Ijumaa likisema mafuriko hayo yamesababisha “hasara kubwa na dhiki karibu kila sehemu”.
Huwa kunatokea mafuriko yasio ya kawaida wakati wa msimu wa mvua nchini Nigeria, ambao hudumu kutoka Aprili hadi Oktoba.
Mnamo mwaka 2024, Nigeria ilikumbwa na mafuriko kutokana na mvua kubwa ambayo ilisababisha vifo huku watu wakilazimika kuhama makazi yao.
Pia kulikuwa na mafuriko makubwa mnamo 2022, wakati zaidi ya watu 600 walikufa na milioni 1.3 walilazimika kuyahama makazi yao.
All Rights Reserved © The Cantona Group PLC||2025
Discover more from cantonadigital
Subscribe to get the latest posts sent to your email.