Ndege ya Japan yatua kwa dharura baada ya mtu mmoja kujaribu kufungua mlango

Radio Fortune Africa -Na Cantona Joseph

https://zeno.fm/radio/radio-fortune-africa

Polisi walisema mtu huyo alizuiliwa na abiria wengine na wafanyakazi wa ndege

Ndege ya Japan iliyokuwa ikitoka Tokyo kuelekea Texas ililazimika kutua kwa dharura baada ya abiria kujaribu kufungua moja ya milango yake wakati wa safari hiyo.

Ndege nambari 114 ya Nippon Airways (ANA) ilielekezwa Seattle saa chache baada ya kupaa siku ya Jumamosi “kutokana na abiria mkorofi”, shirika hilo la ndege lilisema.

Polisi wa Seattle waliambia vyombo vya habari kuwa walikuwa wamearifiwa kuhusu mtu ambaye “alijaribu kufungua milango ya kutokea wakati wa safari ya ndege”.

Mwanaume huyo, ambaye hakutambuliwa, alikuwa “na shida ya kiafya” na ilibidi azuiliwe na abiria wengine na wafanyakazi wa ndege, polisi walisema.

Baadaye alipelekwa hospitali. Haijabainika iwapo atakabiliwa na mashtaka yoyote.

“Usalama wa abiria na wafanyakazi wetu ndio kipaumbele chetu kikuu na tunapongeza juhudi za watekelezaji sheria wa eneo hilo kwa msaada wao,” ANA ilisema katika taarifa.

Wakati ndege ilikuwa ikingoja kwenye lami ya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Seattle-Tacoma, mtu wa pili aliondolewa kwenye ndege kwa “tabia mbaya”, mamlaka ilisema.

Data ya safari ya ndege inaonesha kwamba ndege hiyo ilifika mahali ilipo, George Bush Intercontinental Airport huko Houston, Jumamosi mwendo wa 12:40 saa za ndani (17:40 GMT), saa nne baada ya muda wake uliopangwa kuwasili.

Hili ni tukio la hivi karibuni zaidi katika msururu wa matukio kama haya.

Mnamo Aprili, ndege ya Jetstar kutoka Bali, Indonesia ililazimika kugeuka wakati wa safari yake kuelekea Melbourne, Australia, baada ya abiria vilevile kujaribu kufungua mlango wa ndege angani.

Novemba mwaka jana, mwanaume aliyejaribu kufungua mlango wa ndege wakati wa safari ya ndege ya American Airlines alizuiliwa na kufungwa na abiria wenzake kwa mkanda.

Na mnamo Novemba 2023, abiria tisa wa ndege ya Asiana Airlines walipelekwa hospitalini wakiwa na matatizo ya kupumua baada ya mtu kufanikiwa kufungua mlango wa dharura wa ndege kabla ya kutua kwenye uwanja wa ndege wa Korea Kusini.

All Rights Reserved © The Cantona Group PLC||2025


Discover more from cantonadigital

Subscribe to get the latest posts sent to your email.

Leave a comment