Radio Fortune Africa -Na Cantona Joseph
https://zeno.fm/radio/radio-fortune-africa
Mjue Caleb D. Bradham: Mwanzilishi wa Pepsi, Kinywaji Maarufu Duniani. “Mwanzilishi aliyeunda kampuni iliyofilisika mara mbili na kujaribu kuiuza kwa Coca-Cola mara tatu, lakini walikataliwa kila wakijaribu. Leo hii, Pepsi inadunda kama moja ya brand kubwa duniani, ikiwa na thamani ya $226.02 billion.”


Caleb D. Bradham alizaliwa mwaka 1867. Caleb alikulia katika mji mdogo wa wakulima huko North Carolina, Marekani. Baba yake alikuwa mfanyabiashara mwenye kipato kikubwa, na hali hii ilimpa Caleb fursa ya kupata elimu bora. Baada ya muda, alienda kusomea udaktari katika Chuo Kikuu cha North Carolina. Lakini bahati haikuwa upande wake; baba yake alikumbana na matatizo ya kifedha na hakuwa na uwezo wa kumlipia ada. Caleb alilazimika kuacha masomo, lakini aliporudi mtaani, wakazi walimwona kama daktari kamili kwani hakukuwa na daktari yeyote wa karibu. Hivyo, aliwasaidia kwa ushauri wa afya huku akifundisha shule ili kuweza kuokoa pesa kwa ajili ya masomo. Baada ya miaka miwili, alipata fedha za kutosha kurudi chuo, lakini safari hii hakutaka tena kuwa daktari. Labda kutokana na uzoefu wa kuwasaidia wakazi wa mtaa na matatizo yao ya kiafya, aliamua kubase na dawa na kuwa mfamasia. Mwaka 1892, akiwa na miaka 25, Caleb alinunua jengo katika mji wa New Bern, North Carolina na kufungua duka lake la dawa aliloliita “Bradham Pharmacy.” Wakati huo, maduka ya dawa yalikuwa sehemu maarufu ambapo watu walikusanyika na kuzungumza. Caleb alikuwa mtu wa watu sana, na hivyo kwa muda mfupi alikuwa na marafiki wengi mtaani.
Mwaka huo huo, kampuni ya Coca-Cola ilianzishwa huko Atlanta, Georgia na walianza kuuza syrup ya kola ambayo ilikuwa maarufu kwenye maduka ya dawa. Caleb aliona haraka sana fursa iliyokuwepo kwenye kinywaji hiki, lakini alihisi tatizo moja: mwanzilishi wa Coca-Cola alikuwa ameweka kemikali za kulevya kwenye kichocheo chake, kitu ambacho Caleb hakukipenda. Aliamua kuunda syrup yake mwenyewe ya kola bila kutumia kemikali hizo, akiamini kuwa angeweza kuunda kinywaji chenye afya zaidi ambacho kingeweza kusaidia mmeng’enyo wa chakula. (Syrup ni kimiminika cha utamu kinachotengenezwa kwa kuchanganya sukari na maji na hutumika kuongeza ladha katika vinywaji au vyakula. Kola ni aina ya kinywaji chenye ladha ya kipekee inayotokana na mimea ya kola, ambacho hutengenezwa kwa mchanganyiko wa syrup na viungo vingine kama vile kafeini na rangi za vinywaji) Caleb alitengeneza formula ya syrup yake kwa kuchanganya ladha za asili kama karamel, mafuta ya mimea adimu na matunda. Hivi karibuni, alizindua kinywaji chake kwenye duka lake na kuwashawishi marafiki zake wajaribu. Wakazi wa mtaa walikifurahia sana na wakakipa jina la utani “Brad’s Drink.” Baada ya miaka mitano ya kupendwa miongoni mwa wakazi wa mtaa, Caleb alikusanya ujasiri na kubadilisha jina la kinywaji kuwa “Pepsi-Cola” mwaka 1898, jina lililotokana na neno la Kigiriki “Pepsis” (Pepsin enzyme, wazee wa kusoma najua mnanielewa) lenye maana ya mmeng’enyo.
Pepsi-Cola ikaanza kupata umaarufu kwa ladha yake nzuri, na Caleb alianza kuuza mapipa ya syrup ya Pepsi kwa maduka mengine. Kufikia mwaka 1903, Caleb aliifunga duka lake la dawa ili aelekeze nguvu zake zote kwenye Pepsi. Mwaka huo walifanikiwa kuuza galoni 8,000 za syrup, na Caleb akawekeza kwenye matangazo ya magazeti. Mauzo yakazidi kuongezeka hadi galoni 20,000 mwaka 1904, na Pepsi ikawa biashara kubwa kuliko uwezo wa duka lake. Hivyo, alifungua kiwanda kikubwa na kuingia ushirikiano na kampuni za kuwekea vinywaji kwenye chupa, jambo lililosaidia Pepsi kuwa bidhaa inayopatikana kwenye chupa. Lakini mwaka 1914, Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia ilianza, na bei ya sukari ikapaa kwa sababu ya uhaba wa bidhaa hiyo. Caleb aliamini kuwa bei ingeendelea kupanda, hivyo akawekeza fedha nyingi kwenye kununua sukari kwa wingi. Bahati mbaya, bei ya sukari ilishuka ghafla na kumfanya akose faida. Pepsi haikuweza kufidia hasara hiyo, na Caleb alilazimika kutangaza kufilisika mwaka 1920. Akiwa na miaka 53, Caleb alirudi kwenye kazi yake ya awali kama mfamasia.
Miaka kadhaa baada ya Caleb Bradham kufilisika na kuuza Pepsi, mmiliki mpya wa Pepsi alijaribu kuifufua kampuni hiyo. Lakini mnamo mwaka 1929, mdororo wa uchumi (Maarufu kama “The Great Depression”) uligonga uchumi wa Marekani, na Pepsi ilijikuta tena ikikabiliwa na changamoto kubwa za kifedha. Pepsi ilifilisika kwa mara ya pili na ikawa vigumu sana kuendesha kampuni hiyo kwa faida. Mwaka 1931, wamiliki wa wakati huo, kampuni ya The Loft Candy, walinunua Pepsi wakijaribu kuitengeneza upya. Loft Candy ilikuwa na matumaini kuwa Pepsi ingepata uhai mpya, lakini kutokana na hali ngumu ya kiuchumi, juhudi zao hazikuleta mafanikio waliyotarajiwa. Hivyo, Loft Candy walijaribu kuuza Pepsi kwa Coca-Cola mara tatu tofauti kwa kipindi hicho, wakitumaini kwamba Coca-Cola ingekuwa tayari kuinunua na kuepuka ushindani wa baadaye. Hata hivyo, Coca-Cola waliikataa ofa hizo zote tatu, wakiiona Pepsi kama kampuni isiyoweza kushindana nao na isiyokuwa na thamani ya kununuliwa. Baada ya Coca-Cola kukataa kuinunua Pepsi, Loft Candy waliamua kutafuta njia mpya ya kuokoa biashara yao hawakuweza kuacha kampuni ipotee hivi hivi . Mojawapo ya maamuzi muhimu waliyoyachukua ilikuwa kutumia chupa za bia zilizotumika kwa ajili ya kuokoa gharama za uzalishaji. Hatua hii iliwasaidia kuuza chupa ya Pepsi yenye mililita 355 (takriban gramu 355) kwa senti tano tu. Kwa bei hiyo hiyo, Coca-Cola ilikuwa inauza chupa yenye mililita 177 (takriban gramu 177), hivyo Pepsi ilimpa mteja kiasi mara mbili zaidi ya soda kwa gharama sawa.
Kwa kuwa mdororo wa uchumi ulikuwa bado unaathiri watu wengi wakati huo, wananchi walikuwa wakitafuta njia za kupunguza gharama. Kununua Pepsi badala ya Coca-Cola kulionekana kama chaguo la wazi kwa wengi kwa sababu walikuwa wanapata kiasi kikubwa zaidi cha soda kwa bei ile ile. Hili lilisaidia Pepsi kuanza kuvutia wateja na kuongeza mauzo. Basi Pepsi wakaanza kupata confidence, wakaanza kuwekeza kwa kiasi kikubwa kwenye kampeni za matangazo huku wakitumia njia mpya za kuvutia watu, kama vile matangazo makubwa barabarani, matangazo yaliyopitishwa na ndege angani, na hata katuni maalum ya Pepsi iliyochapishwa kwenye magazeti. Pia walitengeneza wimbo mfupi wa Pepsi uliochezwa redioni, ambao uliwafikia watu wengi kwa gharama nafuu. Wimbo huo ulikuwa na urefu wa sekunde 15 tu, hivyo kufanya matangazo ya Pepsi kuwa rahisi zaidi ukilinganisha na matangazo ya kawaida ya sekunde 60. Hii iliwapa nafasi ya kurudia matangazo yao mara nyingi zaidi, na hatimaye, watu wengi walijikuta wakiimba wimbo wa Pepsi kichwani mwao. Coca-Cola haikufurahia mafanikio haya ya ghafla ya Pepsi. Mnamo mwaka 1938, Coca-Cola iliishtaki Pepsi kwa madai ya kukiuka haki miliki kwa kutumia neno “Cola.” Coca-Cola ilikuwa imemtambua Pepsi kama tishio sokoni na walitaka kuzima ushindani mapema. Katika kesi hiyo, Coca-Cola ilidai kuwa Pepsi ilikuwa inatumia jina lao ili kuvutia wateja. Hata hivyo, Pepsi ilijitetea kwa kusema kuwa Coca-Cola ilikuwa inajaribu kuunda ukiritimba (Umimi/ Monopoly) katika tasnia ya vinywaji vya “Cola.” Mwisho wa kesi hiyo, Pepsi iliruhusiwa kuendelea kutumia jina “Pepsi-Cola,” ingawa baadaye waliamua kulifupisha jina kuwa “Pepsi” tu. Kesi hii ilimalizika huku Pepsi ikiendelea kushika nafasi yake kwenye soko, na ushindani kati ya kampuni hizi mbili ulizidi kukua.
Lakini Pepsi hakuishia hapo, mnamo mwaka 1965, kampuni ya Pepsi-Cola ilifanya muungano mkubwa na kampuni ya vitafunio ya Frito-Lay, na hivyo kuanzisha kampuni mpya iliyoitwa PepsiCo. Muungano huu ulikuwa na lengo la kupanua aina za bidhaa zinazotolewa, na kuwawezesha kufikia masoko mapya. Kuanzia wakati huo, PepsiCo haikuwakilisha tu vinywaji, bali pia bidhaa maarufu za vitafunio kama Lay’s, Doritos, na Cheetos. Muungano huu ulileta nguvu mpya kwa PepsiCo na kuipa uwezo wa kushindana kwa nguvu zaidi kwenye sekta ya vyakula na vinywaji. Mnamo mwaka 1939, Vita vya Pili vya Dunia vilianza. Wakati wa Vita vya Kwanza vya Dunia, uhaba wa sukari ulikuwa na madhara makubwa kwa Pepsi, lakini safari hii walikuwa na mpango wa kujinusuru

. PepsiCo walibadilisha rangi ya chapa yao kuwa nyekundu, nyeupe, na bluu kuonyesha uzalendo wao, hatua iliyowaunganisha na wateja wao kwa njia yenye hisia kali za kitaifa. Hivyo walizindua kampeni inayojulikana kama “Your Man in Service,” ambapo walifunga vibanda maalum vya kurekodi ujumbe kote Marekani ili wanajeshi waweze kurekodi salamu kwa familia zao bila gharama yoyote. Hatua hii iliwapa PepsiCo umaarufu mkubwa kwa uzalendo na kuungwa mkono na wananchi. Lakini pia miaka ya 1940, PepsiCo ilifanya uamuzi wa kimkakati wa kujitangaza kwa jamii ya Wamarekani wenye asili ya Kiafrika, wakiajiri timu ya mauzo na masoko yenye watu wenye asili ya Kiafrika, hatua iliyokuwa na umuhimu mkubwa kwani wapinzani wao hawakujihusisha na jamii hiyo, hivyo hii ilipelekea brand yao kupanuka zaidi na kupendwa na watu weusi. kupitia Technic hizi PepsiCo ilifanikiwa kuvuka changamoto za Vita vya Pili vya Dunia ikiwa imara zaidi.
Mnamo mwaka wa 1950, PepsiCo ilimteua Alfred Steele, aliyekuwa makamu wa rais wa Coca-Cola, kuwa Mkurugenzi Mtendaji. Steele alileta mabadiliko makubwa kwenye chapa ya Pepsi kwa kuendesha kampeni kubwa za matangazo na kuanzisha nembo na chupa mpya yenye muundo wa kipekee. Pia alitumia umaarufu wa mke wake, mwigizaji maarufu Joan Crawford, kama sura ya Pepsi, jambo lililoongeza mauzo kwa kasi. Kampeni za Alfred zilisaidia Pepsi kujiondoa kwenye taswira ya kuwa soda ya gharama nafuu na kufikia mauzo ya dola milioni 11.5 mwaka wa 1958 kutoka dola milioni 1.6 mnamo 1950. Baada ya kifo cha Alfred mwaka 1959, uongozi wa Pepsi ulihamishiwa kwa Don Kendall, ambaye alikuja na mawazo tofauti kabisa

, Jamaa alianza kwa kupanua Pepsi kwenye soko la Umoja wa Kisovyeti (USSR) eneo ambalo Coca-Cola hajawahi kanyaga. Mnamo 1959, wakati wa maonyesho ya Taifa ya Marekani yaliyofanyika Moscow, Pepsi ilipata nafasi ya kujitangaza moja kwa moja kwa raia wa Soviet. Lakini changamoto kubwa ilikuwa mfumo wa fedha wa ruble wa Soviet ulikuwa hauruhusu kufanya biashara za kimataifa, ili kutatua tatizo hilo, PepsiCo ilikubaliana na Umoja wa Kisovyeti kubadilishana bidhaa badala ya fedha, kwaiho Pepsi ikawa ikiuzwa Soviet huku wakilipwa vodka aina ya Stolichnaya, ambayo waliuza Marekani na kupata dola. Hata hivyo, mwishoni mwa miaka ya 1970, Pepsi ilishindwa kuuza vodka ya kutosha na wakaamua kutafuta njia mpya ya malipo kutoka kwa Soviet. Kunao uvumi kwamba mwaka 1989, Pepsi ililipwa na Soviet meli zilizostaafu (manowari na kivita), lakini hakuna taarifa za kuaminika zinazothibitisha hayo hivyo tuyaache kama lilivyo.
So PepsiCo baadae ikaanza kupokea meli za biashara za usafirishaji kutoka kwa Soviet, lakini mpango huo pia ulishindikana na anguko la Umoja wa Kisovyeti mwaka 1991. Pamoja na kuvunjika kwa mpango huo, Pepsi bado iliendelea kuwepo katika nchi za Ulaya Mashariki, huku ikipata umaarufu mkubwa nchini Urusi. Mwaka 2008, PepsiCo ilinunua kampuni kubwa ya juisi nchini Urusi, hataivyo mwaka 2022 ilisitisha uzalishaji wake nchini humo kutokana na mgogoro wa Urusi na Ukraine. Hivyo, uhusiano wa kipekee kati ya PepsiCo na Russia, ulioanza miaka mingi iliyopita, ulikamilika rasmi. Kwa kuwa hadithi yetu ni ndefu sana, nadhani ni bora tuishie hapa kwa sasa. Katika sehemu ya pili, tutamalizia safari ya PepsiCo na kugusia kwa undani ushindani mkali baina ya PepsiCo na Coca-Cola. Ikiwa hujasoma historia ya Coca-Cola bado, naomba uipitie ili sehemu ya pili tuwe pamoja kwa undani zaidi. Pia, usisahau kunionyesha upendo wako kwa kunifollow ili uendelee kupata content za aina hii siku zijazo. Lengo letu ni kutengeneza jamii ya watu wanaopenda kujifunza kutoka kwa wenzetu walivyopitia changamoto na mafanikio. Tukianza kuanzisha startups zetu, tutakuwa na mwanga na msingi wa kujua hatua walizopitia wale waliotutangulia.
All Rights Reserved © Cantona Group PLC||2025
Discover more from cantonadigital
Subscribe to get the latest posts sent to your email.