Radio Fortune Africa -Na Cantona Joseph
https://zeno.fm/radio/radio-fortune-africa
Mwandilishi wa Hitachi, Ltd. Najua wengi wetu tumewahi kututumia bidhaa za Hitachi katika maisha yetu, umewahi jiuliza muanzilishi alianzishaje hii kampuni hadi kufika hapa ilipo leo?

Mwanzoni mwa karne ya 20, Japani ilikuwa jamii ya kilimo inayoanza kuingia kwenye mapinduzi ya viwanda. Wakati nchi za Magharibi zilikuwa zimeendelea sana na uzalishaji wa viwandani, Japani ilikuwa nyuma, huku nyumba nyingi zikiwa hazina umeme, maji safi wala gesi. Katika hicho kipindi kuna kijana anaitwa Namihei Odaira aliyezaliwa (1874) katika kijiji cha Suwa, eneo la Fukushima, Japani. Alikulia katika familia ya kawaida lakini alionyesha hamu kubwa ya kujifunza mambo, hasa katika masuala ya sayansi na teknolojia. Baada ya kumaliza shule, alijiunga na Chuo Kikuu cha Imperial Tokyo (Sasa Chuo Kikuu cha Tokyo), ambapo alisomea uhandisi wa umeme. Baada ya kuhitimu, Odaira alianza kufanya kazi kama mhandisi katika mgodi wa Kuhara, ambao muanzilishi wake Fusanosuke Kuhara nae ndo alikuwa ameingia kwenye sekta ya uchimbaji wa shaba. Odaira alifanya kazi kwa bidii hadi mwishowe akateuliwa kuongoza kitengo cha uhandisi. Katika kazi yake, aliona changamoto nyingi za kiufundi zinazokumba sekta ya madini, hasa hitaji la vifaa vya kuaminika vya umeme. Kipindi hicho migodi na viwanda vingi nchini japani vilikuwa vinategemea sana vifaa kutoka nje, ambavyo vilikuwa ghali na vigumu kupata.

Tatizo hilo likawa lina mtatiza sana Odaira na isitoshe uzuji alikuwa nao akaona anahaja ya kusaidia kampuni. Hivyo, kwa kutumia vifaa vya ndani ya mgodi, alifanikiwa kutengeneza motor ya umeme yenye uwezo wa 7.5 horsepower mwaka 1910. Motor hii ilikuwa ya kwanza kabisa kutengenezwa nchini Japani kwa kutumia malighafi za ndani. Mafanikio ya motor hii yaliboresha uzalishaji wa mgodini, na Fusanosuke Kuhara aliona fursa na umuhimu wa uvumbuzi huu. Hivyo alimteua Odaira kuendelea kutengeneza motor hizo ili waanze kuziuza ndani ya nchi. Fusanosuke Kuhara naye haikuchukua muda mwingi; mwaka 1912 alifungua kampuni yake rasmi, akiita Kuhara Mining Company, akilenga kupanua biashara yake ya uchimbaji madini na kuendeleza sekta ya shaba nchini Japan. Kitengo hiki alichopewa Odaira akakiita Hitachi Works kama jina la heshima kwa sababu walikuwa wanafanya kazi ndani ya mji wa Hitachi (Jina Hitachi maana yake ni alfajiri au mwanzo mpya) hivyo kitengo kikanza kwa kuunda motors ndogo kwa matumizi ya viwanda vidogo. Lakini kama ilivyo kawaida kwa start-up yoyote, kwao changamoto zilianza mapema sana. Timu ya Odaira haikuwa na uzoefu wa kutosha na vifaa bora vya kushughulikia miradi mikubwa, hali ambayo ilisababisha ucheleweshaji wa oda na bidhaa zenye kasoro. Hitachi pia ilijikuta imekuwa tegemezi kwa mahitaji ya ndani ya nchi, jambo lililowafanya wapokee oda nyingi kuliko uwezo wao wa kuzalisha. Hii iliwalazimu kuanza kutengeneza bidhaa mara tu oda zilipopokelewa, bila kufanyiwa testing na maandalizi ya kutosha.

Katika hali nyingine, malalamiko kutoka kwa wateja hayakuwa nadra. Odaira alikabiliwa na lawama na malalamiko mengi kiasi kwamba alivyokuwa na miaka 42 alifikiria kujiuzulu. Hata hivyo, aliamua kusimama imara, akisisitiza umuhimu wa kujifunza kutokana na changamoto na kuboresha bidhaa kwa lengo la kuimarisha teknolojia ya ndani. Odaira alikataa dhana ya kutegemea vifaa kutoka nje na kuendeleza maono yake ya kuona Japani ikijitegemea kiteknolojia kwa kutumia malighafi za nyumbani. Badala ya kukata tamaa, Odaira alitumia changamoto hizi kama fursa ya kujifunza. Aliboresha mifumo ya uzalishaji kwa kuanzisha kikundi maalum cha majaribio, ambacho kilihakikisha kila kifaa kipya kilipimwa kikamilifu kabla ya kupelekwa kwa wateja. Njia hii ilisaidia kuboresha ubora wa bidhaa na kujenga uaminifu wa wateja, ambao mwanzoni walikuwa na shaka na uwezo wa kampuni. Nikukumbushe kwamba haya yote yaliendelea wakati Vita vya Kwanza vya Dunia vilivyokuwa vimeshaanza mwaka 1914, hali iliyofanya utegemezi nchini Japani kuongezeka zaidi kwa bidhaa za ndani kama zile zilizotengenezwa na Hitachi. Hii ni kwa sababu nchi nyingine zilihamia katika utengenezaji wa vifaa vya kijeshi, na hivyo Japan, ambayo ilikuwa tegemezi kwa bidhaa nyingi za Magharibi, ilikumbwa na uhaba mkubwa wa bidhaa za viwandani.
Hali ya uhaba wa bidhaa kutoka nje ililazimisha Hitachi kuzalisha kwa bidii, na juhudi hizi zilianza kuzaa matunda. Bidhaa za Hitachi zilipata umaarufu kutokana na ubora wake, na hili likasaidia kampuni hiyo kujitanua. Hadi kufikia mwishoni mwa Vita vya Kwanza vya Dunia mwaka 1918, Hitachi ilikuwa imeimarisha nafasi yake kama mmoja wa wazalishaji muhimu wa vifaa vya viwandani nchini Japani. Mazingira haya ya kiuchumi, yaliyosababishwa na vita, yalitoa msingi mzuri kwa ukuaji wa kitengo hicho hivyo wakaamua kujitegemea kutoka kwa Kuhara Mining Company na kuanzisha Kampuni rasmi la Hitachi mwaka 1920. Baada ya kuanzisha rasmi Kampuni ya Hitachi, kampuni hiyo ilianza kupanua uzalishaji wake kutoka kwa motors za umeme hadi vifaa vingine vya viwanda kama transfoma, injini za mvuke, na genereta za umeme. Hitachi ililenga kufanikisha uzalishaji wa vifaa vya hali ya juu ambavyo vilihitajika sana katika kipindi cha ukuaji wa viwanda nchini Japani. Mafanikio yao yalitokana na umakini wa kuhakikisha bidhaa bora na juhudi za kuboresha teknolojia kupitia tafiti za ndani. Katika kipindi hiki, Hitachi ilishirikiana kwa karibu na sekta ya reli ya Japani, ikitengeneza motors za umeme na vifaa vya transfoma kwa treni za umeme, hatua iliyoweka msingi wa maendeleo ya miundombinu ya usafiri wa kisasa nchini. Kupitia ushirikiano huu, kampuni ilionyesha uwezo wake wa kubuni na kutengeneza vifaa vinavyokidhi mahitaji maalum ya wateja. Sambamba na hili, Hitachi ilianza kutengeneza turbines za mvuke kwa ajili ya viwanda vya uzalishaji wa nishati na vifaa vya uzalishaji wa chuma, hatua iliyosaidia kujenga uchumi wa ndani na kupunguza utegemezi wa teknolojia za kigeni.
Katika miaka ya 1930, wakati wa mdororo wa uchumi duniani, Hitachi ilikabili changamoto za upatikanaji wa malighafi na kushuka kwa mahitaji ya kimataifa. Hata hivyo, mazingira haya yalikuwa kichocheo cha kampuni kuwekeza zaidi katika uzalishaji wa bidhaa kwa soko la ndani. Ilizalisha genereta kubwa kwa mitambo ya umeme na vifaa vya mawasiliano kama redio na simu, ambavyo vilisaidia kuboresha miundombinu ya mawasiliano nchini Japani. Hitachi ilishirikiana na serikali ya Japani katika mpango wa kitaifa wa kuimarisha uzalishaji wa viwanda, hatua iliyowezesha kampuni hiyo kupanua uwezo wake wa kiteknolojia na hadi kufikia mwishoni mwa miaka ya 1930, Hitachi ilikuwa imejijengea sifa kama mmoja wa viongozi wa teknolojia za viwanda nchini Japani, ikihudumia mahitaji ya ndani kwa ufanisi mkubwa. Hata hivyo, hali ya kisiasa na changamoto za kimataifa zilizokuwa zikikaribia, Hitachi kwa shinikizo la Serikali ililazimika kuelekeza rasilimali zake zaidi katika uzalishaji wa vifaa vya kijeshi, hatua iliyokuwa muhimu kwa maandalizi ya Japani kuelekea vita. Vita vya Pili vya Dunia vilipoanza mwaka 1939, serikali ya Japani ilihamasisha sekta ya viwanda kushirikiana na juhudi za kivita. Hitachi, kama kampuni kubwa ya teknolojia, ilibadilisha vipaumbele vyake tena ili kutimiza mahitaji ya kijeshi. Ilianza kuzalisha vifaa muhimu vya kivita, vikiwemo injini za meli, injini za ndege, na vifaa vya mawasiliano kwa jeshi la Japani. Ushirikiano wake na serikali uliongezeka kwa kasi, na Hitachi ikapewa jukumu muhimu la kuendeleza teknolojia za kijeshi za hali ya juu.
Licha ya mafanikio haya ya kiteknolojia, vita vilileta changamoto kubwa kwa Hitachi. Viwanda vingi vililenga uzalishaji wa vifaa vya kijeshi, na hii ilipunguza uzalishaji wa bidhaa za kiraia. Aidha, miundombinu ya kampuni ililengwa na mashambulizi ya anga yaliyofanywa na majeshi ya washirika mwishoni mwa vita. Mashambulizi haya yaliharibu viwanda kadhaa vya Hitachi, na kampuni hiyo ilikumbana na changamoto kubwa za uzalishaji na kifedha. Baada ya Vita vya Pili vya Dunia kumalizika mwaka 1945, Japani ilikabiliwa na mabadiliko makubwa ya kiuchumi na kijamii, huku serikali mpya ya washirika ikizuia kampuni nyingi za Japani, zikiwemo Hitachi, kushiriki katika uzalishaji wa vifaa vya llkijeshi. Hali hii ililazimisha Hitachi kubadilisha mwelekeo wake na kuangazia upya uzalishaji wa bidhaa za kiraia. Hata hivyo, kipindi cha baada ya vita kilikuwa kigumu kwa Hitachi. Kampuni hiyo ilipata hasara kubwa kutokana na uharibifu wa miundombinu na mtaji uliopotea wakati wa vita. Aidha, kutokana na ukosefu wa rasilimali na upinzani wa washirika, Hitachi ililazimika kupunguza shughuli zake. Viwanda vingi vilihitaji kujengwa upya, na teknolojia mpya ilihitajika ili kuendana na mahitaji ya soko baada ya vita.

Hali hii ya baada ya vita ilileta changamoto kubwa kwa Hitachi, lakini pia ilifungua fursa ya kujifunza na kuimarisha mikakati yao ya muda mrefu. Wakianza kwa tahadhari, walirejea kwenye msingi wao wa teknolojia za viwandani, wakilenga mahitaji muhimu ya kijamii kama utengenezaji wa motor za umeme, transformata, jenereta za nishati, mashine za kufua nguo, compressor za viwandani, na redio za kiviwanda. Vifaa hivi vilihitajika sana katika juhudi za ukarabati wa miundombinu ya Japan iliyoharibiwa vibaya na vita, huku pia vikichangia kuboresha maisha ya kiraia. Hata hivyo, changamoto kubwa ilikuja kwa Namihei Odaira binafsi. Mnamo mwaka 1947, alilazimika kujiuzulu kama Rais wa Hitachi kutokana na shinikizo kutoka kwa Allied Occupation Forces (Vikosi vya Kiamri vya Muungano chini ya Mamlaka ya utawala wa Marekani na vikosi vya kijeshi vilivyokuwa chini ya usimamizi wa mataifa ya Muungano baada ya kumalizika kwa Vita vya Pili vya Dunia. Mataifa haya yalikuwa Marekani, Uingereza, Ufaransa, na Umoja wa Kisovieti, na walichukua udhibiti wa Japan kwa lengo la kubadilisha mfumo wa kisiasa na kiuchumi wa nchi hiyo baada ya kushindwa vita. Hali hii ilimlazimisha Odaira kuachana na nafasi yake ya uongozi, licha ya kwamba alikuwa bado na mchango mkubwa katika mwelekeo wa kampuni.
Baada ya kustaafu rasmi kutoka nafasi yake, Namihei Odaira alionekana kama mtu aliyejawa na huzuni ya kuona kampuni yake ikikumbwa na changamoto kubwa za baada ya vita. Hata hivyo, alikubali jukumu la kutoa ushauri wa kiufundi na usimamizi kwa Hitachi, akijitahidi kusaidia kampuni kujipanga upya katika mazingira magumu ya wakati huo. Alijitahidi kutafuta suluhisho la ubunifu kwa matatizo yaliyoikumba kampuni yake, lakini mzigo wa kihembe wa kuona Hitachi ikikumbwa na changamoto nyingi, pamoja na umri wake mkubwa, ulileta athari kubwa kwa afya yake. Ingawa alirejea Hitachi kama mwenyekiti wa heshima mwaka 1951, na kuendelea kuwa sehemu muhimu ya historia ya kampuni, Namihei Odaira alifariki dunia katika Oktoba ya mwaka huo akiwa na miaka 77. Kifo chake kilileta majonzi makubwa, hasa kwa familia yake na wafanyakazi wa Hitachi, ambao walimwona kama baba wa kampuni. Hata hivyo, ingawa alikufa kabla ya kuona ukuaji mkubwa wa Hitachi katika miaka ya baadaye, maono yake ya kuunda kampuni inayotumia teknolojia kwa manufaa ya jamii yamekuwa msingi wa mafanikio makubwa ya Hitachi duniani kote. Mbali na kazi yake ya uongozi na uvumbuzi, Odaira pia alikua philanthropist mwenye moyo wa kujitolea kwa jamii. Alijitolea sana katika sekta ya elimu, akisaidia kuanzisha miradi ya kusaidia vijana kupata elimu bora na mafunzo ya kitaalamu. Aliunga mkono taasisi za elimu na alifanya michango mbalimbali kwa maendeleo ya jamii, hasa katika maeneo ya afya na maendeleo ya kijamii. Jitihada zake hizi zilimfanya kuwa mmoja wa watu waliokumbukwa kwa michango yake kwa taifa, na ameacha legacy kubwa ya kujitolea kwa vizazi vijavyo.

So baada ya kifo cha Namihei Odaira, Hitachi ilikumbwa na mabadiliko makubwa, ambayo yalimlazimu kuangalia mwelekeo mpya. Kampuni, iliyojengwa kwa maono ya kiongozi huyo, ilikosa mwelekeo wazi kwa muda, lakini uongozi wa Tetsuro Higashi, aliyekuwa makamu wa rais wa Hitachi, ulileta matumaini mapya. Higgashi, ambaye alikua na ujuzi mkubwa katika uendeshaji wa kampuni, alichukua jukumu la kuhakikisha kwamba kampuni hiyo inaendelea kufanikiwa licha ya changamoto kubwa za kiuchumi na kisiasa zilizokumba Japan baada ya vita. Katika kipindi cha mpito, Hitachi ilijua kuwa ili iendelee kufanikiwa, ilikuwa lazima ibadilike na kuchukua hatua kubwa katika utafiti na maendeleo. Higgashi aliona kuwa mabadiliko ya teknolojia yanahitajika ili kuweka kampuni katika nafasi ya kushindana kimataifa. Hitachi ilianza kuwekeza katika utafiti na maendeleo ya kompyuta, ikifanya mabadiliko makubwa kwa kuhakikisha kuwa kompyuta za kampuni hiyo zilikuwa na ubora wa juu na zinakidhi mahitaji ya soko la kimataifa. Mwaka 1957, kampuni ilizindua HITAC 301, kompyuta ya kielektroniki ya kwanza ya kibiashara inayotumika kwa ajili ya biashara. Kompyuta hii ilikuwa na uwezo mkubwa kwa wakati wake, na ilileta mapinduzi katika tasnia ya ujasiriamali wa kielektroniki. Huu ulikuwa ni mwanzo wa safari ya Hitachi kuingia katika ulimwengu wa teknolojia ya habari na mawasiliano.
Kwa upande mwingine ilikuwa ikitafiti na kutengeneza vifaa vya kupozea hewa (Air Conditioners), Televisheni na Excavators ambazo zilikuja kuwa mojawapo ya bidhaa muhimu ambazo Hitachi ilizalisha kwa wingi. Katika miaka ya 1960, Hitachi ilianza kutengeneza televisheni za rangi ambazo zilikuwa maarufu sana katika soko la Japan na baadaye, dunia nzima. Televisheni hizi zilikuwa na teknolojia ya kisasa na ubora wa juu, jambo lililofanya Hitachi kuwa mmoja wa watengenezaji wakubwa wa vifaa vya kielektroniki duniani. Hitachi ilijivunia kuwa miongoni mwa waasisi wa televisheni za rangi, na mafanikio haya yaliimarisha jina la kampuni hiyo katika soko la kimataifa. Kwa haraka, Hitachi ilijenga jina lake kama kiongozi katika teknolojia ya umeme na vifaa vya kielektroniki, na kuendelea kuingia katika soko la kimataifa. Kampuni ilifungua matawi ya biashara katika Marekani, Ulaya, na Hong Kong, ambapo ilianza kutoa bidhaa zake kwa masoko ya nje. Huu ulikuwa mwanzo wa upanuzi mkubwa wa kampuni hiyo, kwani ilijivunia kuwa na bidhaa zinazoendana na mahitaji ya ulimwengu wa kisasa. Kwa miaka michache tu, Hitachi ilifanikiwa kuwa moja ya makampuni makubwa ya kiteknolojia duniani. Ilikuwa na bidhaa bora katika sekta za kompyuta, televisheni, vifaa vya mawasiliano, na vifaa vya umeme, na haikubaki kuwa kiongozi wa soko tu, bali pia iliendelea kutoa mchango mkubwa kwa maendeleo ya jamii. Uongozi wa kampuni uliona kuwa uvumbuzi wa kiteknolojia, kama kompyuta na televisheni, ulikuwa ni muhimu si tu kwa faida ya kampuni, bali pia kwa kuboresha maisha ya watu.

Hitachi ilijivunia mafanikio haya, lakini pia ilijua kuwa ili iendelee kukua, ilikuwa lazima ishirikiane na makampuni mengine na kujenga mtandao mkubwa wa biashara duniani kote. Kila hatua ya upanuzi wa kampuni hiyo ilikuwa inajenga msingi wa kukua kwa kasi katika soko la kimataifa, na Hitachi ilikua kuwa moja ya makampuni makubwa na yenye ushawishi mkubwa katika ulimwengu wa teknolojia…… Kwa kuwa hadithi yetu ni ndefu sana, ningependa tuishie hapa kwa sasa. Hata hivyo, muendelezo wa hadithi hii tutazungumzia kilele cha mafanikio ya Hitachi na pia kuporomoka kwake, huku tukichambua changamoto za kiuchumi, kisiasa, na mabadiliko ya soko yaliyosababisha kampuni hii kukutana na vikwazo vikubwa. Huu utakuwa ni mchakato wa kuelewa jinsi kampuni yenye mafanikio makubwa ilivyoweza kupambana na matatizo yaliyojitokeza na kupunguza mafanikio yake, na pia ni njia ya kujifunza kutokana na makosa na mafanikio ya zamani. Lakini kwa sasa, unaweza kuchagua mojawapo ya hadithi zilizokwisha kuandikwa hapo chini. Hii itatusaidia kufahamu zaidi jinsi Hitachi ilivyoweza kufika kileleni na pia kuelewa vidonda na changamoto ambazo zilileta mabadiliko makubwa. Naamini tutapata mengi ya kujifunza kutoka kwa hadithi hii.

All Rights Reserved © Cantona Group PLC||2025
Discover more from cantonadigital
Subscribe to get the latest posts sent to your email.