Mjue Phil Knight:

Radio Fortune Africa -Na Cantona Joseph

https://zeno.fm/radio/radio-fortune-africa

Mwanzilishi wa Nike, Mfalme wa Vifaa vya Michezo Duniani. “Wakati wengine darasani wakiandika essay kupata alama nzuri, Phil Knight aliandika essay iliyobadilisha maisha yake na kuanzisha safari ya kuunda kampuni. Leo, Nike inathamani ya $114.47 bilioni na inaongoza kama kampuni kubwa zaidi ya vifaa vya michezo duniani.”

Phil Knight alizaliwa tarehe 24 Februari, 1938, huko Portland, Marekani, alikulia katika familia yenye misingi wa nidhamu na kazi. Baba yake, William Knight, alikuwa mchapishaji wa gazeti, mtu mwenye msimamo mkali kuhusu maadili ya kujitegemea. Hii ilimfanya Phil kukulia katika mazingira ambapo alilazimika kujifunza thamani ya bidii na uvumilivu mapema. Baba yake alikuwa mkali katika kuhakikisha Phil anasimama mwenyewe badala ya kumtegemea kwa msaada wa kifamilia. Kwa sababu hii, Phil alijitahidi kujitengenezea njia yake ya maisha tangu akiwa kijana mdogo. Wakati wa ujana wake, Phil alikuwa mpenda michezo, hasa mbio za masafa marefu. Alisoma katika Chuo Kikuu cha Oregon, ambapo alijiunga na timu ya mbio za masafa na akafundishwa na kocha maarufu, Bill Bowerman.

Bowerman hakuwa tu mkufunzi wa michezo bali mtu mwenye maono makubwa kuhusu michezo na vifaa bora vya wanariadha. Alijulikana kwa ubunifu wake hasa katika kutengeneza viatu (kienyeji) ambavyo vilikuwa nyepesi lakini vyenye ubora kwa ajili ya wanariadha wake. Phil, akiwa mmoja wa wanariadha wake, alivutiwa sana na juhudi za Bowerman, jambo lililomfanya atambue umuhimu wa vifaa vya michezo katika kuboresha utendaji wa mwanariadha. Baada ya kuhitimu kutoka Chuo Kikuu cha Oregon, Phil aliamua kuendelea na masomo ya juu katika Chuo Kikuu cha Stanford, akijiunga na programu ya Uzamili ya Biashara (MBA). Moja ya masomo aliyosoma huko Stanford lilikuwa la ujasiriamali, likifundishwa na Profesa Frank Shallenberger, ambaye alijulikana kwa kuwahamasisha wanafunzi wake kufikiria nje ya mipaka ya kawaida ya biashara. Phil, mbali na kuwa mpenzi wa riadha, masomo yake mapya yalimfanya kuwa mfuatiliaji wa mabadiliko ya soko duniani. Yakamfanya awe na uwezo wa kuona fursa mbalimbali zinazo mzunguka, akitambua jinsi soko lilivyokuwa likibadilika na jinsi alivyoweza kutumia mabadiliko haya kutafuta nafasi za kibiashara.

Image

Siku moja, akiwa darasani na Profesa Shallenberger, alitoa kazi ya kuandika insha (essay) inayohusu wazo la kibiashara. Phil alielezea jinsi alivyotambua mabadiliko ya soko na jinsi ushindani wa bidhaa za Kijapani ulivyokuwa unapata nguvu dhidi ya zile za Ulaya. Aliona jinsi kamera za bei nafuu kutoka Japani zilivyokuwa zikichukua nafasi ya zile za Ujerumani kwenye soko la Marekani, na aliamini kwamba dhana hiyo hiyo ingeweza kutumika kwenye viatu. Phil alipendekeza kwamba pengine na viatu vya Kijapani vinaweza kuwa vya bei nafuu, vyenye ubora na vinaweza kuwa mbadala wa Brand kubwa kama Puma na Adidas, ambazo zilikuwa zikidhibiti soko la viatu vya michezo Marekani. Siku baada ya siku, wazo hili likaanza kuwa serious ndani ya kichwa cha Phil, likaanza kumkaa na kumvutia zaidi. Alijua kuwa hii haikuwa tu insha ya kawaida kwa ajili ya darasa, bali ilikuwa ni sehemu ya kujiaminisha yeye mwenyewe na kwa baba ake kwamba anaweza kufanya hili sema tatizo ni likawa ni moja tu, Phil alikuwa anahisia tu, hakuwa na viatu vya michezo kutoka japani, na vile vichache alivyowahi kuona vililetwa Marekani na wanajeshi waliokuwa wamehudumu nchini Japani wakati wa Vita vya Pili vya Dunia.

Bahati ilimfuata Phil. Onitsuka alivutiwa na ujasiri wake pamoja na shauku kubwa aliyoonyesha juu ya bidhaa yake. Walianza mazungumzo rasmi, ambapo Phil alielezea jinsi soko la Marekani lilivyokuwa na nafasi kubwa kwa bidhaa bora na nafuu kama viatu vyao. Onitsuka alikubali kumpa nafasi ya majaribio na round ya kwanza, Onitsuka walimtumia pair 12 za viatu kwa gharama ya jumla ya $3.44 kwa kila pair. Phil alipanga kuuza viatu hivyo kwa takriban $6.00 kila pair akipata faida kidogo baada ya gharama za usafiri lakini muhimu kwa kusaidia biashara yake mpya. Phil hakuwa na duka wala jina kubwa la biashara, hivyo ilibidi atafute njia mbadala ya kuuza viatu vyake. Akatumia gari lake kama duka akienda kwenye viwanja vya michezo, maeneo ambako wanariadha na watu wenye mapenzi ya viatu vya michezo wanakusanyika. Alipofika, anafungua buti ya gari lake, kuweka viatu kwa mpangilio, na kuanza kuwaeleza watu kuhusu ubora wa viatu vyake. Kwa viatu 12 Phil alianza kukumbana na changamoto, kuwashawishi watu kununua bidhaa kutoka kwa kampuni isiyojulikana ilikuwa ni kazi ngumu kwake. Watu wengi walikuwa na mashaka kuhusu ubora wa viatu hivyo, wakilinganisha na brand zilizokuwa maarufu sokoni. Ilimlazimu Phil kutumia muda mwingi kueleza historia ya viatu hivyo, malighafi zake, na kwa nini vilikuwa bora kwa wanamichezo. Wengine walionekana kuvutiwa, lakini wengi walihitaji kusukumwa sana kabla ya kufanya maamuzi ya ununuzi. Zaidi ya hayo, kuzunguka na gari kulimgharimu pesa nyingi kwa mafuta, jambo ambalo lilipunguza faida yake..

Hata hivyo, viatu hivyo 12 vilinunuliwa vyote. Lakini Phil hakuridhika na mbinu ya biashara aliyotumia. Aliona wazi kuwa hakuwa na uwezo wa kuendelea kuzunguka huku na huko, akipoteza muda mwingi na gharama kubwa. Round ya pili, Phil aliamua kuagiza pair 50 za viatu kwa gharama ya jumla ya $175, kiasi ambacho kilitumia sehemu kubwa ya akiba yake. Lakini awamu hii alimkumbuka kocha wake wa zamani, Bill Bowerman, aliyekuwa na ushawishi mkubwa kwa wanamichezo. kama nilivyosema hapo awali, bowerman alikuwa mtu aliyependwa sana na wanariadha, na Phil aliamini kwamba kupitia yeye, angeweza kuuza viatu haraka. Bila kupoteza muda, Phil alimtembelea Bowerman akiwa na viatu hivyo mkononi. Alipofika, Phil alimweleza Bowerman kuhusu biashara yake mpya na dhamira yake ya kuleta mabadiliko kwa wanamichezo kupitia viatu bora lakini vya bei nafuu. Bowerman alivutiwa na viatu hivyo alionekana kupendezwa zaidi na ubora wake na jinsi vilivyotengenezwa kwa kuzingatia mahitaji ya wanamichezo. Aliunga mkono wazo la Phil kwa kuwashawishi wanariadha wake kununua viatu hivyo na ndani ya muda mfupi, pair zote 50 zikaisha. Bowerman alitambua dhamira ya Phil na kuona fursa kubwa katika ndoto zake. Kwa kuonyesha imani yake, alimwekezea $500, huku Phil naye akiweka $500 nyingine, sehemu kutoka kwa faida ya awali na nyingine kutoka mfukoni mwake. Kwa mtaji huu wa jumla wa $1,000, waliagiza mzigo wa viatu 300 kutoka Japani, kila pair ikiwa na gharama ya $3.33.

wezi Januari 1964, Phil Knight na Bill Bowerman walisajili rasmi kampuni yao na kuiita Blue Ribbon Sports (BRS), jina ambalo Phil alilitunga alipokuwa Japani. Mzigo wao wa kwanza ulifika Marekani mwezi Aprili mwaka huo, na kupitia mahusiano mazuri ya Bowerman na wanariadha wa vyuo vikuu, mzigo wote wa viatu uliuzwa ifikapo Julai 1964. Mafanikio ya mwaka wao wa kwanza yalikuwa ya kuvutia. Blue Ribbon Sports iliuza viatu vyenye thamani ya $8,000, ishara kwamba walikuwa kwenye njia sahihi. Phil alitumia mapato hayo kuajiri wauzaji wa kusaidia kusambaza bidhaa kwa wateja wengi zaidi. Kufikia mwaka 1965, mapato yao yaliongezeka hadi $20,000, na kwa mafanikio hayo, walifungua duka lao la kwanza mjini Santa Monica, California. Wakati Phil alikuwa akishughulikia upande wa biashara, ambapo aliwajibika na masuala ya kifedha, uuzaji, na usambazaji, uvumbuzi halisi ulitoka kwa Bill Bowerman. Mwaka 1966, aliandika kitabu kuhusu umuhimu wa jogging, kitabu kilichofanya vizuri sana nakala milioni moja ziliuzwa na kufanya kampuni yake kuwa miongoni mwa Kampuni za kwanza kutangaza viatu vya Tiger kwa ajili ya jogging.

Bowerman kila alipokuwa akipokea mzigo mpya kutoka kwa Onitsuka, alikata baadhi ya viatu ili kuona jinsi vilivyotengenezwa, kisha alijitahidi kuboresha miundo yake na kutuma maoni yake kwa Onitsuka, akiiomba kampuni hiyo kufanya mabadiliko kadhaa.  Moja ya design ya Bill iliyofanya Blue Ribbon Sports (BRS) kuvuma kwenye sokoni ni design viatu vyao walivyo viita Cortez. Viatu hivi vilikuwa maarufu sana, na mwaka 1968, Cortez ilijulikana kama moja ya viatu maarufu zaidi nchini Marekani, hasa kutokana na umaarufu wa michezo ya Olimpiki iliyofanyika Mexico. Kwa msaada wa Cortez, BRS iliweza kuuza viatu vyenye thamani ya $300,000 mwaka 1969. Lakini licha ya mafanikio yao, changamoto hazikuwaacha mbali. Cortez ilizidi kuwa maarufu kwa haraka hali iliyofanya mahitaji kuwa makubwa kuliko uagizaji wao. Kila mzigo mpya walioupokea ulizidi kutoka kwa haraka zaidi kuliko ule uliopita na Onitsuka waliendelea kuwatumia viatu kwa kasi ya polepole. Onitsuka walikuwa wakitimiza mahitaji yao ya ndani nchini Japan kwanza, kisha wakituma kilichobaki kwenda Marekani.

Image

Phil na Bill walijua kuwa ili kupanua biashara yao, walihitaji kuachana na kuwa waagizaji wa bidhaa pekee, hivyo walipanga mara baada ya mkataba wao na Onitsuka uliokuwa unaisha mwaka 1972, kuanza kutengeneza viatu vyao wenyewe. Hii ilikuwa ni hatua muhimu kwa ajili ya uhuru wa kudhibiti ubora wa bidhaa na kuongeza mapato yao. Wakiwa na uzoefu wa miaka kadhaa katika kuuza viatu vya Onitsuka, walijua vizuri mahitaji ya soko na walikuwa na imani kuwa kwa kubuni viatu vyao wenyewe, wangeweza kuvunja soko kwa namna ya kipekee. Mwaka 1971, Phil Knight alianza kazi ya kuunda brand ya kampuni yake mpya. Mfanyakazi wake wa kwanza alipendekeza waiite kampuni lao jipya Nike, jina la mungu wa Kigiriki wa ushindi. Phil alikubaliana mara na pendekezo hilo akiamini kwamba jina hilo lilionyesha azma na maono ya kampuni yao. Hata hivyo, bado kulikuwa na jambo muhimu lililokosekana, logo ya kutambulisha Kampuni yao. Ili kutatua hili, Phil aliamua kutafuta msaada wa kitaalamu wa kubuni nembo. Alienda kwenye Chuo Kikuu cha Portland State, kilichokuwa karibu, akiwa na lengo moja: kumpata mwanafunzi wa graphic design ambaye angeweza kubuni nembo kwa gharama nafuu. Huko alikutana na Carolyn Davidson, mwanafunzi mwenye kipaji aliyekubali kazi hiyo. Kwa malipo ya $35 tu, Carolyn alibuni nembo ya Swoosh kutoka kwenye idea ya bawa la muungu Nike. Nembo hiyo, rahisi lakini yenye nguvu, ilionyesha kasi na mwendo, ikiendana kikamilifu na maono ya Nike kama chapa ya ushindi na maendeleo.

Mnamo Mei 1971, Blue Ribbon Sports walivunja mkataba wao na kujitoa rasmi kutoka kwa Onitsuka, hatua iliyokuwa imepangwa kwa muda mrefu na kwa msaada wa mtandao wa wazalishaji wa Japani walioujenga kwa siri kabla ya hatua hii. Phil Knight na Bill Bowerman waliweza kuanzisha uzalishaji wa viatu vyao kwa wakati mzuri. Viatu vya kwanza vya Nike vilianza kutengenezwa kwa mujibu wa miundo na maelekezo ya Bowerman, ambaye aliendelea kuboresha viatu kwa kutumia teknolojia nyepesi na nyenzo bora zaidi. Mbinu zao za kupiga hatua mbele zilijumuisha kuimarisha utambulisho wa chapa yao, na kujikita zaidi katika mikakati ya masoko ili kuvutia wateja. Walitumia mbinu za uuzaji kama vile “Just Do It,” ambayo ilivutia mamilioni ya wapenzi wa michezo na kuweka Nike kama chapa ya kushinda na kuhamasisha ufanisi. Mbinu hii ilianza mwaka 1988 na ikawa moja ya kampeni bora zaidi za masoko duniani, ikilenga si tu wachezaji wa michezo bali pia wapenzi wa michezo na watu wa kila rika. Nike pia ilianza kuingia mikataba na wachezaji maarufu wa michezo, kama Michael Jordan na Tiger Woods, ambao walisaidia kuongeza umaarufu wa chapa hiyo kimataifa. Mikataba hii iliwezesha Nike kujenga uhusiano wa kudumu na wachezaji na kuleta athari kubwa kwenye sekta ya vifaa vya michezo. Michael Jordan, kwa mfano, alileta umaarufu mkubwa kwa kupitia viatu vya Air Jordan, ambavyo vilivuma sio tu kwa umahiri wake, bali pia kwa ubunifu wa kipekee.

Licha ya mafanikio hayo, changamoto zilikuwepo. Wakati viatu vya Nike vilizidi kuwa maarufu, kampuni ilikumbana na changamoto za uzalishaji na usambazaji. Ili kushinda hili, Nike ilianzisha viwanda vyake nchini Marekani na baadaye kuhamia maeneo mengine kama China na Vietnam, ili kuweza kuzalisha kwa wingi na kwa gharama nafuu. Hii ilileta faida kubwa, kwani iliwasaidia kupanua uzalishaji na kugusa masoko mapya duniani kote. Nike ilianza kufanya branchi za ofisi zake katika maeneo mbalimbali duniani, huku ikipanua usambazaji wake na kujenga uwepo wa kimataifa. Kampuni ilianza kufungua maduka rasmi na ofisi katika miji mikubwa duniani, kama Tokyo, London, na Sydney, ambapo walikua na timu ya mauzo na usambazaji ya kimataifa. Kampuni iliendelea kuimarika kwa haraka na kujenga msingi imara katika tasnia ya michezo, na kufikia 1989, Nike ilijivunia kuwa kampuni ya vifaa vya michezo kubwa zaidi Marekani. Leo, Nike inakadiriwa kuwa na utajiri wa zaidi ya dola bilioni 114.47, na inamiliki kampuni nyingi kama vile Converse na Jordan Brand, ambayo imejulikana kwa viatu vya Air Jordan. Nike pia ina ushawishi mkubwa katika sekta ya mavazi ya michezo na teknolojia, ikiwa na bidhaa kama Nike Training Club na Nike+, ambazo zinashirikiana na teknolojia ya kisasa kusaidia wateja kufuatilia na kuboresha mazoezi yao.

Nike sasa inajiita kama mfalme wa soko la vifaa vya michezo, ikiongoza si tu kwa ubora wa bidhaa, bali pia kwa mafanikio yake katika masoko ya kimataifa na mikataba ya wachezaji maarufu. Kuwepo kwake ni ushahidi wa mafanikio ya mbinu za uuzaji, ubunifu wa bidhaa, na ushawishi mkubwa katika jamii ya michezo duniani kote. Katika hatua nyingine, Phil Knight aliendelea kuwa mfano wa uongozi na mafanikio. Hata baada ya kujiuzulu kama Mkurugenzi Mtendaji wa Nike mwaka 2004, alibaki kuwa Chairman Emeritus hadi leo. Kwa sasa, Phil Knight anatajwa kama mmoja wa watu matajiri zaidi duniani, akiwa na utajiri unaokadiriwa kufikia $35.2 bilioni mnamo mwaka 2024. Lakini mwenzie Bill Bowerman, alifariki December 24,1999. Nike inamkumbuka na kuthamini michango ya Bill Bowerman kwa kumheshimu kama mwasisi na mbunifu, na jina lake liliachwa kama kumbukumbu kwenye kampuni hiyo, ikiwemo kupitia Bowerman Track & Field Complex iliyoko kwenye Chuo Kikuu cha Oregon, kilichokuwa na uhusiano mkubwa na maisha yake. Phil Knight pia alikumbuka mchango wa Carolyn Davidson, msichana aliyeunda nembo ya Swoosh kwa malipo ya $35 tu. Kwa kumshukuru kwa kazi yake kubwa, Phil Knight alimpa zawadi ya hisa 500 za Nike pamoja na pete ya dhahabu yenye nembo ya Swoosh. Nike leo ni kampuni kubwa inayomiliki mamilioni ya wateja duniani kote, ikitoa vifaa vya michezo, mavazi, na teknolojia ya kisasa kwa wapenzi wa michezo na wanariadha wa kitaifa na kimataifa ingawa bado inakabiliwa na changamoto katika soko, ikiwa ni pamoja na kushuka kwa mauzo na ushindani mkali kutoka kwa makampuni mengine.

All Rights Reserved © Cantona Group PLC||2025


Discover more from cantonadigital

Subscribe to get the latest posts sent to your email.

Leave a comment