Radio Fortune Africa -Na Cantona Joseph
https://zeno.fm/radio/radio-fortune-africa
Mjue William Colgate: Mwanzilishi wa Dawa ya Meno Maarufu Leo Hii, Colgate Wakati wengi walikuwa wanatafuta njia za kufanikiwa kwa kuuza bidhaa zao, William Colgate aliona fursa kwenye biashara ya usafi wa kinywa. Alikumbukwa sana kwa kauli yake maarufu inayosema: “The most successful enterprises are the ones that meet real needs.” Na hii ndiyo hadithi yake…

Mnamo mwaka 1806, kijana William Colgate kutoka Uingereza alihamia New York, Marekani akiwa na miaka 23, akiwa na ndoto moja ya kuusaka utajiri. Kipindi hicho, watu wengi duniani walikuwa na msemo wa “The American Dream”, kwa maana kwamba Marekani ilikuwa inajulikana kama nchi ya fursa ambapo mtu yeyote, bila kujali asili yake, anaweza kufanikiwa kwa bidii na juhudi. Kijana William Colgate hakuwa na mtaji mkubwa wala jina maarufu, lakini alikuwa na ndoto za kuwa mfanyabiashara. Baada ya kuizoea Marekani, alianza kutengeneza na kuuza sabuni, ujuzi ambao alitoka nao kwao Uingereza. Kijana alijikuta akiingia kwenye ushindani wa kibiashara kwani watu maarufu miaka hiyo walikuwa tayari wakiuza bidhaa kama yake, hii ikampelekea kukosa wateja na baadaye kijana alikata tamaa akambidi atafute tena kazi kwa mara ya pili kukimudu na hali ya maisha.

Kijana alipokuwa kazini alipata wazo la kutengeneza bidhaa za kusafisha meno ambazo zingekubalika kwa watu kwani wakati huo usafi wa kinywa ulikuwa changamoto kubwa kwa watu wengi, huku bidhaa za kusafisha mdomo zikiwa adimu na ghali. Watu wakati huo walikuwa wakitumia mchanganyiko wa chaki na baking soda. Colgate akawa na shauku sana ya kutengeneza sabuni maalum ya kusafisha meno, hii ikamfanya kushindwa kabisa kutulia kazini. Alipata tu kiasi alichokuwa anakihitaji, akaanza kutengeneza dawa ya meno kwenye chumba chake, dawa ambayo walikuwa wakitumia kwao Uingereza lakini bado akaona kuna vitu vinapungua. Kijana ikambidi kukodi wataalamu wa kemia ili kuhakikisha kuwa awamu hii anaingia vizuri sokoni na bidhaa yake inakuwa salama na yenye ufanisi, na hapo ndipo Dr. Pomroy na Dr. Sheffield wanaingia kwenye story ya maisha yake.

Watu hawa watatu wakawa na chemistry nzuri sana na pia wakawa na maono makubwa zaidi sio tu kutengeneza mchanganyiko mzuri wa dawa hiyo bali kubadilisha kabisa dawa ya meno kutoka kuwa ya poda na kuwa jelly kama hii tunazotumia leo. Lengo lao kuu lilikuwa ni kutengeneza dawa ambayo ni salama, bora, na nyepesi kutumika. Baada ya utafiti na majaribio kadhaa kufeli, hatimaye vijana walipata mchanganyiko ambao aliamini kwao ilikuwa ndio final product, mchanganyiko huo ulikuwa baking soda, chaki, makaa ya mawe, mharadufu (peppermint), sodium bicarbonate, fluoride na calcium carbonate. Ndipo bidhaa yake akaaiita Colgate Toothpaste. (Hivi ndivyo viungo ambavyo vilichangia sana mabadiliko uwanja wa dawa za meno ingawa, kwa sasa vitu vingine vimeongezwa na kupunguzwa)

Colgate alianzisha kampuni yake rasmi akaaiita William Colgate & Company lakini haikumchukua muda akajikuta kwenye tatizo lile lile “Ushindani wa Kibiashara”. Awamu hii kulikuwa na washindani kama Pearl Dental Cream na Sheffield’s Creme Dentifrice. Lakini Colgate alitumia mbinu tofauti na ya kipekee ya kuweka ubora na bei nafuu kwenye bidhaa zake, akishawishi wateja wake kupitia matangazo ya nyumba kwa nyumba akidhamiria kujenga imani na wateja. William Colgate & Company ikaanza kupata jina, watu wakaanza kuipenda dawa hii mpya ya meno kwani ilikuwa inapatikana kwa bei nafuu ambayo kila mtu kipindi hicho alikuwa anauwezo wa kununua.

Colgate aliingiza faida sana kwani biashara yake ilipanuka sio tu Marekani bali ilifika hadi nyumbani kwao Uingereza na aliiendesha kampuni yake vizuri sana hadi umauti ulivyomkuta mwaka 1857 akiwa na miaka 74. (William Colgate, ukiacha na biashara yake, dunia inamkumbuka kama mtoaji mkubwa wa misaada (philanthropist). Alijitolea sana kwa jamii, akichangia fedha katika miradi ya kibinadamu, elimu, na misaada mingine. Alikuwa na moyo wa kusaidia kuboresha maisha ya watu wengi, na michango yake ililenga kusaidia hospitali, shule, na taasisi zinazosaidia wanyonge na wasiojiweza). William Colgate aliacha watoto sita, na mtoto wake wa mwisho, James Boorman Colgate, alichukua jukumu la kuendeleza biashara ya baba yake. Huku akibeba mzigo wa urithi mkubwa, James alijua kuwa ili kampuni iendelee kukua, ilihitajika mabadiliko ya kimkakati.

Baada ya kifo cha baba yake, James alianzisha juhudi za kupanua kampuni kwa kuongeza bidhaa mpya. Alianza kuzalisha sabuni za kuogea, mafuta ya ngozi, na mafuta ya nywele, akiongeza aina mpya za bidhaa zilizozidi kufahamika sokoni. Bidhaa hizi zilisaidia kuongeza umaarufu wa kampuni na kuifanya kuwa maarufu zaidi katika soko la usafi wa mwili. Lakini James alijua kuwa ushindani katika sekta ya bidhaa za usafi ulikuwa mkali, hivyo aliona umuhimu wa kuungana na kampuni nyingine ili kupanua soko na kuongeza nguvu. Mnamo mwaka 1928, Colgate & Company ilijiunga na Palmolive-Peet Company, mzalishaji maarufu wa sabuni za mafuta ya michikichi na mizeituni. Muungano huu ulileta faida kubwa kwa kampuni, kwani bidhaa za Colgate za usafi wa mdomo na sabuni za Palmolive ziliuzwa pamoja na kuongeza umaarufu wa Colgate-Palmolive kimataifa.

Leo, Colgate-Palmolive ni mojawapo ya kampuni kubwa zaidi za bidhaa za usafi wa mwili na nyumbani duniani. Kwa mwaka 2024, kampuni hii inakadiriwa kuwa na thamani ya zaidi ya dola bilioni 68. Thamani hii inajumuisha mtaji wa soko na mapato kutoka kwa mauzo ya bidhaa zinazotegemewa duniani kote, kama vile dawa za meno za Colgate, sabuni za Palmolive, na bidhaa zingine za usafi na utunzaji wa ngozi na nywele.
All Rights Reserved © Cantona Group PLC||2025
Discover more from cantonadigital
Subscribe to get the latest posts sent to your email.