Diddy alitumia umaarufu wake kuwadhulumu na kunyanyasa wanawake – waendesha mashtaka

Radio Fortune Africa -Na Cantona Joseph

https://zeno.fm/radio/radio-fortune-africa

.
Maelezo ya picha,Bw Combs na Cassandra Ventura pichani mnamo 2017

Sean “Diddy” Combs alitumia umaarufu na vurugu kuwanyanyasa kingono wanawake, waendesha mashtaka wamesema katika ufunguzi wa taarifa ya kesi ya mwanamuziki huyo, huku mawakili wake wakitetea maisha yake ya kujihusisha na “ngono za ovyoovyo”.

“Diddy” Combs mwenye umri wa miaka 55 amekanusha mashtaka yakiwemo ya ulaghai, ulanguzi wa ngono na usafirishaji ili kujihusisha na ukahaba.

Mahakama pia ilisikiza kutoka kwa mashahidi wa kwanza wa waendesha mashtaka, akiwemo mlinzi wa hoteli ambapo Bw Combs anaonekana kwenye video ambayo sasa ipo mtandaoni akimpiga mpenzi wake wa zamani mwaka wa 2016.

Ushahidi wake ulifuatiwa na mwanamume aliyesema Bw Combs alimdhulumu mpenzi wake wa zamani wakati wa kufanya ngono za kulipwa na wanandoa hao.

Onyo: Taarifa hii ina maelezo ambayo baadhi ya wasomaji wanaweza kuona ni ya kuhuzunisha.

Baada ya kuketi kwa jopo la majaji 12 na wengine sita waliokuwa mbadala siku ya Jumatatu asubuhi, serikali na mawakili wa Bw Combs walielezea kesi zao.

Mwendesha mashtaka Emily Johnson alimshutumu Bw Combs kwa kutumia hadhi yake ya mtu mashuhuri na mzunguko wa wandani wa wafanyikazi “waaminifu” kuwanyanyasa wanawake kingono na kuendesha biashara ya uhalifu.

Alilenga waathiriwa wawili katika kesi hiyo – mpenzi wa zamani wa Bw Combs, Cassandra Ventura, na mpenzi mwingine wa zamani ambaye jina halikutajwa.

Waendesha mashitaka waliambia mahakama kwamba Bw Combs alitumia vurugu na kutishia taaluma ya muziki ya Bi Ventura ili kumlazimisha kufanya ngono zisizo za ridhaa na kufanya vitendo vya ngono na wanaume wengine wakati wa kile kinachojulikana kama “freak-offs” iliyorekodiwa na Bw Combs.

Mshtakiwa “alikuwa na uwezo wa kuharibu maisha yake [Bi Ventura],” Bi Johnson alisema.

Kiini cha kesi hiyo ni video inayoonyesha Bw Combs akimpiga Bi Ventura na pia kumburuta nywele katika barabara ya ukumbi wa hoteli ya Los Angeles mnamo 2016.

Wanasheria wa Bw Combs walisema kuwa video hiyo ilikuwa ushahidi wa tabia ya Bw Combs “yenye kasoro”, lakini si ya biashara kubwa ya uhalifu. “Unyanyasaji wa majumbani sio biashara ya ngono,” alisema Teny Geragos, wakili wa Bw Combs.

Miongoni mwa waliotoa ushahidi ni pamoja na Daniel Phillip, meneja wa zamani wa watumbuizaji wa kiume wakiwa uchi, ambaye alisema alikutana na Bw Combs na Bi Ventura baada ya mkuu wake kumtaka awe kama mtumbuizaji mwenye kusherehesha wengine katika tafrija ya bachelorette.

Lakini, Bw Phillip alisema, badala yake alipokelewa katika hoteli na Bi Ventura, ambaye alimwambia ilikuwa siku yake ya kuzaliwa na mumewe alitaka kumpa zawadi.

Bw Phillip aliiambia mahakama kwamba aliendelea kufanya mapenzi na Bi Ventura mara kadhaa – kwa takriban muda wa saa 10, wakati mwingine chini ya ushawishi wa dawa za kulevya – huku Bw Combs akitazama na kurekodi tukio hilo.

Alidai kuwa alishuhudia Bw Combs akimshambulia Bi Ventura angalau mara mbili, ikiwa ni pamoja na wakati mmoja alipomvuta nywele huku akiwa anapiga mayowe akisema “Samahani”.

Bwana Combs kisha akarudi chumbani pamoja na Bi Ventura na kuwataka wawili hao wafanye ngono tena mbele yake, Bw Phillip alisema.

“Nilishtuka,” alisema. “… Niliogopa sana.”

Bw Phillip alidai kwamba hakuripoti tukio hilo polisi kwa kuhofia kuwa Bw Combs ni “mtu mwenye uwezo mkubwa” na kwamba anaweza “kukuua”.

Kesi hiyo imeratibiwa kuendelea Jumanne wakati Bi Ventura anatarajiwa kutoa ushahidi wake.

All Rights Reserved © Cantona Group PLC||2025


Discover more from cantonadigital

Subscribe to get the latest posts sent to your email.

Leave a comment