Ukraine ‘italazimika kuachia’ Urusi baadhi ya maeneo yake- Meya wa Kyiv

Radio Fortune Africa -Na Cantona Joseph

https://zeno.fm/radio/radio-fortune-africa

Meya wa jiji kuu la Ukraine, Kyiv, Vitali Klitschko
Maelezo ya picha,Meya wa jiji kuu la Ukraine, Kyiv, Vitali Klitschko

Meya wa jiji kuu la Ukraine, Kyiv, Vitali Klitschko, amesema kuwa huenda Ukraine ikalazimika kutoa sehemu ya ardhi yake kama sehemu ya makubaliano ya amani na Urusi, katika kile kinachoonekana kuwa shinikizo linalozidi kuongezeka kutoka kwa Rais wa Marekani, Donald Trump, kuikubali hali hiyo.

“Moja ya uwezekano ni… kutoa ardhi. Siyo haki. Lakini kwa ajili ya amani hata kama ni ya muda huenda hilo likawa suluhisho,” alisema Klitschko katika mahojiano na BBC. Hata hivyo, bingwa huyo wa zamani wa masumbwi ambaye sasa ni mwanasiasa, alisisitiza kwamba watu wa Ukraine “hawatakubali kamwe uvamizi au udhibiti wa Urusi.”

Kauli yake ilitolewa saa chache tu baada ya shambulizi kubwa la makombora na droni kutoka Urusi mjini Kyiv lililosababisha vifo vya watu 12 na kujeruhi zaidi ya 80, likiwa ni mojawapo ya mashambulizi makubwa zaidi katika miezi ya hivi karibuni dhidi ya mji huo mkuu.

Tangu Rais Vladimir Putin kuanzisha uvamizi wa kijeshi dhidi ya Ukraine mwaka 2022, Urusi inakadiriwa kudhibiti karibu asilimia 20 ya ardhi ya Ukraine kwa sasa.

Kwa kutoa kauli hiyo, Klitschko amekuwa mmoja wa viongozi wa ngazi ya juu nchini Ukraine kuashiria hadharani uwezekano wa kukubaliana na mpango wa muda wa kutoa ardhi ili kupata amani – jambo ambalo limekuwa gumu kulikubali miongoni mwa viongozi wa taifa hilo.

Alipoulizwa kama Rais Volodymyr Zelensky amewahi kumshirikisha katika mazungumzo au mipango ya suluhisho la amani, Klitschko alijibu kwa kifupi, “Hapana.” “Rais Zelensky hufanya hayo binafsi.

Sio jukumu langu,” aliongeza. Wawili hao wanajulikana kwa tofauti zao za kisiasa. Klitschko amewahi kumtuhumu Zelensky na timu yake kwa kujaribu kudhoofisha mamlaka yake kama meya wa Kyiv.

Akitolea mfano wa mvutano wa wazi uliojitokeza kati ya Zelensky na Trump katika Ikulu ya Marekani mwezi Februari, Klitschko alisema kuwa masuala nyeti baina ya viongozi wa juu wa kisiasa yanapaswa kujadiliwa “bila uwepo wa kamera.”

Mapema wiki hii, Trump alimtuhumu Zelensky kwa kuzuia juhudi za kutafuta suluhu ya amani, baada ya rais huyo wa Ukraine kusisitiza tena kuwa hatakubali udhibiti wa Urusi katika Rasi ya Crimea eneo la kusini mwa Ukraine lililotwaliwa na Moscow mwaka 2014 kwa njia isiyo halali.

Trump alihoji kuwa Crimea “ilipotezwa miaka mingi iliyopita” na kwa sasa “si suala la kujadiliwa.”

Hata hivyo, Zelensky alikumbusha kuhusu tamko la mwaka 2018 lililotolewa na waziri wa mambo ya nje wa Marekani wa wakati huo, Mike Pompeo, ambapo Marekani ilisema wazi kuwa “inakataa jaribio la Urusi la kutwaa Crimea.”

Katika wiki za hivi karibuni, Ukraine na washirika wake wa Ulaya wameeleza wasiwasi wao kuhusu mwelekeo mpya wa Trump, ambao wengi barani Ulaya wanautafsiri kama juhudi za kurejesha uhusiano wa karibu kati yake na Rais Vladimir Putin wa Urusi.

All Rights Reserved © The Cantona Group PLC||2025


Discover more from cantonadigital

Subscribe to get the latest posts sent to your email.

Leave a comment