Radio Fortune Africa -Na Cantona Joseph
https://zeno.fm/radio/radio-fortune-africa

Takribani watu 22 wameuawa baada ya watu wenye silaha kulifyatulia risasi kundi la watalii wa ndani waliokuwa wakitembelea sehemu maarufu ya kuvutia huko Kashmir, jimbo linalotawaliwa na India.
Serikali ya India imesema, shambulio hilo limefanyika katika mji wa kuvutia wa Pahalgam, huko Himalaya ambao mara huitwa “Switzerland ya India.”
Waziri mkuu wa eneo hilo, Omar Abdullah, amesema shambulio hilo “ni kubwa zaidi kuliko shambulio lolote ambalo tumewahi kuliona dhidi ya raia katika miaka ya hivi karibuni.”
Ripoti zinaonyesha kuna idadi kubwa ya waliojeruhiwa, huku baadhi wakiwa katika hali mahututi.
Rais wa Marekani Donald Trump, Rais wa Urusi Vladimir Putin na mkuu wa Umoja wa Ulaya Ursula Von der Leyen ni miongoni mwa viongozi wa dunia waliolaani mashambulizi hayo.
Waziri Mkuu wa India Narendra Modi – ambaye alikatisha safari yake ya Saudi Arabia kufuatia shambulio hilo – amesema wahusika “watafikishwa mahakamani.”
Shambulio la Jumanne si la kawaida, katika miongo mitatu na nusu ya vita, kwani si mara nyingi watalii kulengwa – haswa kwa kiwango kama hicho.
Luteni Gavana wa mkoa huo, Manoj Sinha, amesema jeshi na polisi wametumwa kwenye eneo la tukio.
Hakuna kundi lililodai kuhusika na shambulio hilo.
Kumekuwa na uasi wa muda mrefu katika eneo hilo lenye Waislamu wengi tangu 1989, ingawa ghasia zimepungua katika miaka ya hivi karibuni.
Shambulio hilo limetokea Baisaran, eneo la juu la mlima maili tatu (5km) kutoka Pahalgam.
Magari hayawezi kufika eneo ambalo ufyatuaji risasi ulitokea, amesema Inspekta Jenerali wa Jammu na Kashmir, Vidi Kumar Birdi.
Kanda ya video iliyosambazwa na vyombo vya habari vya India inawaonyesha wanajeshi wa India wakikimbia kuelekea eneo la shambulizi, huku video nyingine waathiriwa wakisikika wakisema watu hao wenye silaha waliwatenga kando watu wasio Waislamu.
Polisi walisema watalii wengi wamepelekwa hospitalini wakiwa na majeraha ya risasi. Eneo hilo limezingirwa na askari wanasimamisha magari kwenye vituo vya ukaguzi. Operesheni ya pamoja ya msako wa jeshi la India na polisi wa Jammu na Kashmir inaendelea.
Maandamano kadhaa yameandaliwa siku ya Jumatano, kulingana na vyombo vya habari vya India.
Tangu miaka ya 1990, waasi wenye silaha wanaotaka kujitenga dhidi ya utawala wa India katika eneo hilo wamepoteza maisha ya maelfu ya watu, yakiwemo ya raia na vikosi vya usalama.
Eneo la Himalaya liligawanywa kufuatia uhuru wa India kutoka kwa Uingereza, mgawanyo huo ulipelekea kuundwa taifa la Pakistan 1947.
Mataifa hayo mawili yenye silaha za nyuklia yote yanadai eneo hilo ni lao na yamepigana vita viwili na kuzuka mizozo mingine midogo.
Wanajeshi 500,000 wa India wametumwa katika eneo hilo tangu wakati huo.
Shambulio kubwa la mwisho dhidi ya raia lilitokea Juni 2024, watu tisa waliuawa na 33 kujeruhiwa baada ya wanamgambo kulifyatulia risasi basi lililokuwa limebeba mahujaji wa Kihindu.
All Rights Reserved © The Cantona Group PLC||2025
Discover more from cantonadigital
Subscribe to get the latest posts sent to your email.