Jaji amzuia Trump kuifunga Sauti ya Amerika (VOA)

Radio Fortune Africa -Na Cantona Joseph

https://zeno.fm/radio/radio-fortune-africa

fc
Maelezo ya picha,Nembo ya Sauti ya Amerika huko Washington, DC.

Jaji wa mahakama ya shirikisho ya Washington ameuamuru utawala wa Trump kurejesha kazi zote na ufadhili kwa Sauti ya Amerika (VOA) na vyombo vingine vya habari vinavyofadhiliwa Marekani, na kusema juhudi za kuisambaratisha zinakiuka sheria na Katiba.

Zaidi ya wafanyakazi 1,300 wa VOA, wakiwemo wanahabari 1,000, walipewa likizo kufuatia agizo la Rais Donald Trump. Ikulu ya White House imekishutumu chombo hicho cha habari “kwa kumpinga Trump” na kuwa na misimamo mikali.”

VOA, kama huduma ya redio, ilianzishwa wakati wa Vita vya Pili vya Dunia ili kukabiliana na propaganda za Nazi, ni chombo kikubwa cha utangazaji duniani.

Uamuzi wa jaji Jaji Royce Lamberth, kutoka Washington, DC umebainisha kuwa kwa sababu ya kukata ufadhili, “VOA imeshindwa kuripoti habari kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 80.”

Jaji Lamberth amesema utawala ulichukua hatua “bila kuzingatia madhara kwa wafanyakazi, wanakandarasi, waandishi wa habari, na watumiaji wa vyombo vya habari duniani kote.”

Ameamuru utawala huo kuchukua hatua za kuwarejesha wafanyakazi katika kazi walizokuwa nazo kabla ya agizo hilo, na kufanya vivyo hivyo kwa Radio Free Asia na Mitandao ya Utangazaji ya Mashariki ya Kati.

Jaji huyo aligundua kuwa agizo la serikali linakiuka Sheria ya Kimataifa ya Utangazaji na mamlaka ya Bunge ya kutoa ufadhili.

Trump kwa muda mrefu ameikosoa VOA kama sehemu ya mashambulizi yake makubwa dhidi ya vyombo vya habari, mara kwa mara akivishutumu vyombo vikuu vya habari kwa upendeleo.

Baada ya kuchukua madaraka mwezi Januari, alimteua mshirika wa kisiasa, Kari Lake, kuendesha VOA. Lake hapo awali aliunga mkono madai ya uwongo ya Trump kwamba uchaguzi wa 2020 uliibiwa.

Jaji Lamberth ameamua kuwa utawala wa Trump hauna mamlaka ya kuifunga VOA, ambayo inafadhiliwa na Congress na ina mamlaka ya kisheria ya kutoa habari za kuaminika duniani kote.

All Rights Reserved © The Cantona Group PLC||2025


Discover more from cantonadigital

Subscribe to get the latest posts sent to your email.

Leave a comment