Radio Fortune Africa -Na Cantona Joseph
https://zeno.fm/radio/radio-fortune-africa

Zaidi ya marais 100 wa vyuo vikuu na mashirika ya elimu wamechapisha taarifa ya pamoja siku ya Jumanne kupinga sera za utawala wa Trump kwa taasisi za elimu ya juu, baada ya Chuo Kikuu cha Harvard kusema utawala huo unatishia uhuru wake.
Taarifa hiyo, iliyotiwa saini na marais kutoka taasisi kama vile Princeton, Brown, Chuo Kikuu cha Hawaii na Chuo Kikuu cha Connecticut State Community, imekosoa kile ilichoelezea kama “unyanyasaji wa serikali na uingiliaji wa kisiasa ambao sasa unahatarisha elimu ya juu ya Marekani.”
“Tuko tayari kufanya mageuzi yenye kujenga na hatupingi usimamizi halali wa serikali,” ilisema taarifa hiyo. “Hata hivyo, ni lazima tupinge uingiliaji usiofaa wa serikali katika maisha ya wale wanaojifunza, wanaoishi na kufanya kazi kwenye vyuo vyetu.”
Taarifa ya pamoja ya Jumanne ni ya hivi punde ya upinzani kutoka viongozi wa elimu ya juu kwa serikali ya Trump ambayo inatumia shinikizo la kutaka ufadhili wa kifedha ili kurekebisha mifumo ya kielimu.
Aprili 14 Chuo Kikuu cha Harvard kilikataa matakwa mengi kutoka utawala wa Trump, likiwemo la utawala huo kutaka kusimamia serikali ya wanafunzi ya Harvard, vitivo na mitaala ili kuzuia itikadi za kiliberali.
Muda mfupi baadaye, utawala wa Trump ulitangaza kuzuia dola bilioni 2.3 za ufadhili wa serikali kwa chuo hicho.
Kulingana na taarifa ya msemaji wa Ikulu ya White House, Harrison Fields wakati huo, Trump anataka kuhakikisha dola za walipa kodi haziungi mkono ubaguzi wa rangi au ghasia zinazochochewa na ubaguzi wa rangi.
Utawala huo pia umetishia kuipokonya Harvard hadhi yake ya kutotozwa kodi na kuondoa uwezo wake wa kusajili wanafunzi wa kigeni.
Siku ya Jumatatu Harvard umeushitaki utawala wa Trump ili uondoe agizo la kuzuia fedha na kuondoa matakwa ambayo imetoa. Chuo hicho pia kimeituhumu serikali ya shirikisho kwa kujaribu “kubadilisha utawala wa Harvard, kudhibiti uajiri katika vitivo vya Harvard na kudhibiti unfundishaji kwa sababu za kiitikadi.”
Tangu kuapishwa kwake Januari, Rais wa chama cha Republican Donald Trump amevutana na vyuo vikuu vya juu vya Marekani, akisema vilishindwa kushughulikia maandamano ya mwaka jana ya kuunga mkono Gaza na kuruhusu chuki katika vyuo vikuu.
Aprili 15 zaidi ya marais 60 wa zamani na wa sasa wa vyuo vikuu walitia saini barua ya wazi wakisema “wanaunga mkono kwa dhati” kukataa kwa Rais wa Harvard, Alan Garber matakwa ya serikali.
All Rights Reserved © The Cantona Group PLC||2025
Discover more from cantonadigital
Subscribe to get the latest posts sent to your email.