Mpango mpya wa kusitisha mapigano kati ya Israel na Gaza wapendekezwa

Radio Fortune Africa -Na Cantona Joseph

https://zeno.fm/radio/radio-fortune-africa

f
Maelezo ya picha,Usitishaji vita wa mwisho ulimalizika pale Israel ilipoanza tena kupiga mabomu mwezi uliopita

Afisa mkuu wa Palestina anayefahamu mazungumzo ya kusitisha mapigano kati ya Israel na Hamas ameiambia BBC, wapatanishi wa Qatar na Misri wamependekeza mfumo mpya wa kumaliza vita huko Gaza.

Kulingana na afisa huyo, mpango huo ni wa amani ya kudumu ya kati ya miaka mitano hadi saba, kuachiliwa kwa mateka wote wa Israel na wafungwa wa Kipalestina wanaoshikiliwa katika jela za Israel, kusitisha rasmi vita, na Israel kujiondoa kabisa Gaza.

Ujumbe wa Hamas unategemewa kuwasili Cairo kwa mashauriano.

Usitishaji vita wa mwisho ulisambaratika mwezi mmoja uliopita, Israel ilipoanza tena kuishambulia Gaza, huku pande zote mbili zikilaumiana.

Israel haijatoa kauli yoyote kuhusu mpango huu mpya.

Hamas itawakilishwa katika majadiliano mjini Cairo na mkuu wa baraza lake la kisiasa, Mohammed Darwish, na mpatanishi wake mkuu Khalil al-Hayya.

Inakuja siku chache baada ya Hamas kukataa pendekezo la hivi punde la Israel, ambalo lilijumuisha matakwa ya kupokonywa silaha Hamas ili kuwepo na usitishwaji mapigano kwa wiki sita.

Siku ya Jumamosi, Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu alisema hatamaliza vita kabla ya Hamas kuangamizwa na mateka wote kurejea. Hamas imeitaka Israel kumaliza vita kabla ya mateka kuachiliwa.

Afisa wa Palestina anayefahamu mazungumzo hayo aliiambia BBC, Hamas imeonyesha utayari wake wa kukabidhi utawala wa Gaza kwa taasisi yoyote ya Palestina iliyokubaliwa “katika ngazi ya kitaifa na kikanda.”

Afisa huyo alisema hii inaweza kuwa Mamlaka ya Palestina yenye makao yake Ukingo wa Magharibi (PA) au chombo kipya cha kiutawala.

Netanyahu amefutilia mbali jukumu lolote la PA katika utawala wa baadaye wa Gaza, ambayo imekuwa ikitawaliwa na Hamas tangu 2007.

Ingawa bado ni mapema sana kutathmini uwezekano wa kufaulu, chanzo kilielezea juhudi za sasa za upatanishi kuwa kubwa na kusema Hamas imeonyesha kubadili baadhi ya msimamo.

Hamas ilishambulia Israel tarehe 7 Oktoba 2023, na kuua takribani watu 1,200 – wengi wao wakiwa raia – na kuchukua mateka 251 huko Gaza.

Israel ilianzisha mashambulizi makubwa ya kijeshi kujibu, ambayo yamesababisha vifo vya Wapalestina 51,240 – hasa raia – kulingana na wizara ya afya ya Gaza inayoendeshwa na Hamas.

All Rights Reserved © The Cantona Group PLC||2025


Discover more from cantonadigital

Subscribe to get the latest posts sent to your email.

Leave a comment