Radio Fortune Africa -Na Cantona Joseph
https://zeno.fm/radio/radio-fortune-africa

Hisa za kampuni za Marekani na dola ya nchi hiyo vyashuka thamani tena huku Rais Donald Trump akizidisha mashambulizi kwa bosi wa benki kuu ya Marekani kwa kutopunguza viwango vya riba.
Katika chapisho kupitia mtandao wa kijamii, Trump ametoa wito kwa mwenyekiti wa Hifadhi ya Shirikisho, Jerome Powell kupunguza viwango vya riba ili kusaidia kukuza uchumi.
“Uchumi unaweza kudorora, isipokuwa Bwana Mcheleweshaji, mpotofu mkuu, apunguze viwango vya riba sasa” aliandika.
Ukosoaji wa Trump juu ya jinsi Powell anavyoshughulikia uchumi wa Marekani unakuja wakati mipango yake mwenyewe ya ushuru imesababisha kushuka thamani kwa soko la hisa na kuibua hofu ya kuzorota kwa uchumi.
Mzozo wa rais huyo na Powell umeongeza msukosuko wa soko.
S&P 500, ambayo unafuatilia kampuni 500 kubwa zaidi za Marekani, ilishuka kwa takriban 2.4% siku ya Jumatatu. Imepoteza takriban 12% ya thamani yake tangu kuanza kwa mwaka.
Kampuni ya Dow Jones Industrial Average imeshuka kwa 2.5% na imeshuka karibu 10% hadi sasa mwaka huu, huku Nasdaq imeshuka zaidi ya 2.5% na iko chini ya 18% tangu Januari.
Fahirisi ya dola – ambayo hupima nguvu ya dola dhidi ya sarafu nyingine kama Euro – Jumatatu ilishuka hadi kiwango cha chini kabisa tangu 2022.
Viwango vya riba kwa deni la serikali ya Marekani pia vimepanda.
Wakati huo huo, bei ya dhahabu imepanda huku wawekezaji wakitafuta mali salama. Jiwe hilo la thamani hutazamwa kama mali salama ya kuweka pesa wakati wa mvurugiko wa kiuchumi.
Ukosoaji wa Trump kwa Powell ulianzia muhula wake wa kwanza madarakani, iliripotiwa kwamba Trump alijadili juu ya kumfukuza kazi. Tangu kushinda uchaguzi huo, Powell amemtaka kupunguza gharama za kukopa.
Ukosoaji wa hivi punde unafuatia maonyo ya Powell kwamba ushuru wa Trump unaweza kupandisha bei ya bidhaa na kupunguza ukuaji wa uchumi.
Powell mwaka jana aliwaambia waandishi wa habari kuwa haamini kuwa rais ana mamlaka ya kisheria ya kumwondoa madarakani.
All Rights Reserved © The Cantona Group PLC||2025
Discover more from cantonadigital
Subscribe to get the latest posts sent to your email.