Radio Fortune Africa -Na Cantona Joseph
https://zeno.fm/radio/radio-fortune-africa

Jeshi la Israel limesema “makosa ya kiweledi” yalisababisha kuuawa kwa wafanyakazi 15 wa huduma za dharura huko Gaza mwezi uliopita.
Uchunguzi wa tukio hilo uliofanywa na Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) uligundua makosa kadhaa, ikiwa ni pamoja na “kutoelewana” na “ukiukaji wa maagizo.”
Naibu kamanda wa kitengo kilichohusika amefukuzwa kazi “kwa kutoa ripoti isiyo kamili na isiyo sahihi” hapo awali.
Msemaji wa Jumuiya ya Hilali Nyekundu ya Palestina (PRCS) alisema ripoti hiyo “si sahihi” kwani “inahalalisha na kuelekeza lawama kwa makosa binafsi wakati ukweli ni tofauti kabisa.”
Wafanyakazi 14 wa huduma za dharura na mfanyakazi wa Umoja wa Mataifa waliuawa tarehe 23 Machi baada ya msafara wa magari ya wagonjwa ya PRCS, gari la Umoja wa Mataifa na lori la zima moto kushambuliwa kwa risasi na jeshi la Israel.
Katika taarifa hiyo, IDF inasema wanajeshi wake walifyatua risasi wakiamini walikuwa wakikabiliwa na tishio kutoka vikosi vya maadui.
IDF inasema uchunguzi wake umegundua sita kati yao walikuwa wanachama wa Hamas, na kukataa madai kuwa imefanya mauaji kiholela.
Katika taarifa ya Meja Jenerali Yoav Har-Even – ambaye alichunguza tukio hilo – aliwaambia waandishi wa habari, jeshi la Israeli linasema wafanyakazi sita wa dharura walikuwa ni wafuasi wa Hamas na watatajwa majina yao baadaye.
Ripoti hiyo inasema tukio hilo lilitokea katika kile ilichokiita “eneo la mapigano na hatari,” na kamanda aliyekuwa eneo hilo aliona tishio la mara moja na dhahiri baada ya magari kwaendea kwa kasi.
IDF inalaumu “uoni hafifu wakati wa usiku,” na ikimaanisha kuwa kamanda hakutambua magari hayo kama ambulensi.
Afisa mkuu mwingine “atapewa karipio” kwa “kuhusika katika tukio hilo,” ripoti hiyo iliongeza.
Hapo awali Israel ilidai kuwa wanajeshi walifyatua risasi kwa sababu msafara huo ulikuwa ukitembea gizani bila taa za mbele au taa dharura. Na ilidai msafara huo haukuwa umeratibiwa.
Lakini baadaye ilisema madai hayo yana makosa baada ya video iliyopatikana kwenye simu ya mtoa huduma aliyeuawa kuonyesha magari hayo yakiwa na taa za mbele na taa za dharura zikiwa zinawaka.
Video inaonyesha magari yakisimama barabarani wakati upigaji risasi unaanza. Video hiyo inaendelea kwa zaidi ya dakika tano, huku mhudumu wa afya akisali sala yake ya mwisho kabla ya sauti za wanajeshi wa Israel kusikika zikikaribia magari hayo.
Inaonyesha pia magari yalikuwa na alama za wazi na wahudumu hao wakiwa wamevalia sare ya kuakisi mwanga.
Miili ya wafanyikazi 15 waliouawa ilizikwa kwenye mchanga. Miili hiyo haikupatikana hadi wiki moja baada ya tukio hilo kwa sababu mashirika ya kimataifa, ikiwa ni pamoja na UN, hayakuweza kufika eneo hilo.
Israel ilianzisha mashambulizi ya kuiangamiza Hamas kujibu shambulio la kuvuka mpaka la tarehe 7 Oktoba 2023, ambapo watu 1,200 waliuawa na wengine 251 walichukuliwa mateka.
Takriban watu 51,201 wameuawa huko Gaza tangu wakati huo, kulingana na wizara ya afya ya eneo hilo inayoendeshwa na Hamas.
All Rights Reserved © The Cantona Group PLC||2025
Discover more from cantonadigital
Subscribe to get the latest posts sent to your email.