Vikosi vya SADC kuondoka DRC kupitia Rwanda hadi Tanzania

Radio Fortune Africa -Na Cantona Joseph

https://zeno.fm/radio/radio-fortune-africa

gg

Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) sasa itawaondoa wanajeshi wake nchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC ) kupitia Rwanda.

Hii ni baada ya Rwanda kukubali vikosi vya SADC vilivyokuwa vikipambana na waasi mashariki mwa Congo kuondoka kupitia ardhi yake hadi Tanzania, ripoti zasema.

Jumuiya ya SADC iliiomba Rwanda kuruhusu vikosi vyake kupitia Kigali baada ya uwanja wa ndege wa Goma kufungwa.

Vikosi vya SADC kwa ushirikiano na kundi la FRDC vimetuhuwa kuwashambulia wapiganaji wa M23.

Katikati ya mwezi Machi, Jumuiya ya SADC yenye wanachama 16 ilitangaza kuwa imehitimisha rasmi mamlaka ya kikosi chake cha kijeshi kinachojulikana kama SAMIDRC, na kwamba itaendelea na mchakato wa kuondoa wanajeshi wake kutoka Congo kwa awamu.

Kwa mujibu wa mabalozi wawili ambao ni viungo muhimu kwa mazungumzo yanayoendelea walibainisha kuwa wamearifiwa kuwa silaha za kikosi hicho zitafungwa kwa usalama, lakini zitasafirishwa pamoja na wanajeshi hao wakati wa kuondoka nchini Rwanda.

Mpaka sasa wasemaji wa SADC na serikali za Congo na Rwanda hazijatoa kauli yoyote kujusiana na taarifa hii.

Haya yanajiri baada ya Mjumbe Maalum wa Marekani barani Afrika Massad Boulos, kuitaka serikali ya Rwanda kusitisha misaada yake yote kwa waasi wa M23 na kuwaondoa wanajeshi wake nchini Congo.

Kwenye kikao na waandishi wa habari, mitandaoni, Boulus pia alisisitiza kuwa waasi hao wa M23 ni sharti wasitishe mapigano, akisema kuwa mzozo huo unaokumba eneo la Mashariki mwa Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo unaweza kutatuliwa kwa njia ya mazungumzo pekee.

Waasi wa M23 wamekuwa wakidhibiti miji ya Goma na Bukavu tangu mwanzo wa mwaka huu na wametishia kuteka maeneo zaidi.

Mapigano ya hivi karibuni kati ya M23 na wanajeshi wa DRC, FRDC na washirika wao Wazalendo, yamesababisha vifo vya maelfu ya watu huku mamia ya maelfu ya wengine wakilazimika kukimbilia nchi jirani.

Kwa zaidi ya miaka thelathini iliyopita, jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo, ambayo ina utajiri mkubwa wa madini, imekumbwa na mapigano ya wenyewe kwa wenyewe yanayohusisha makundi kadhaa ya waasi ambayo yanapambana kuthibiti utajiri huo wa madini.

Aidha nchi jirani pia zimeshutumiwa kwa kufadhili uasi nchini DRC ili kupora madini yake.

Boulus amesema mzozo huo wa DRC umedumu kwa muda mrefu na sasa unapaswa kumalizwa kabisa ili wanainchi waishi kwa amani na kunufaika na rasilimali za taifa lao.

Lakini serikali ya Rwanda imekanusha mara kadhaa kuwa halitoi msaada wowote kwa waasi hao wa M23, lakini wataalamu wa Umoja wa Mataifa wamedai kuwa Rwanda ina zaidi ya wanajeshi elfu nne nchini DRC wanaowasaidia waasi hao wa M23.

Utawala wa Kigali hata hivyo umesema uwepo wa waasi wa FDLR nchini DRC ni tishio kubwa kwa usalama wake.

Kundi hilo la FDLR ambalo linajumuisha wapiganaji wengi kutoka kwa jamii ya Wahutu, wanatuhumiwa kuhusika na mauaji ya Kimbari yaliyotokea nchini Rwanda mwaka wa 1994, dhidi ya watu wa jamii ya Watutsi.

Bolous amedokeza kuwa alifanya mazungumzo na Rais wa Rwanda Paul Kagame kuhusiana na suala hilo la waasi wa FDLR.

Juhudi za kimataifa za kujaribu kumaliza mzozo huo hazijafua dafu, hasa baada ya Rais wa Angola ambaye alikuwa mpatanishi mkuu wa mzozo huo kujiondoa.

Umoja wa Afrika sasa umemteua Rais wa Burkina faso kuongoza mchakato huo.

Mwezi uliopita Qatar ilifanikisha mkutano wa kujadili usitishwaji wa uhasama na mapigano mashariki mwa Congo, kati ya rais Paul Kagame na mwenzake wa DRC Felix Tshisekedi Lakini siku moja tu baada ya mkutano huo waasi wa M23 waliuteka mji wa muhimu na wa kimkakati wa Walikale ambao una utajiri mkubwa wa madini ya dhahabu.

All Rights Reserved © The Cantona Group PLC||2025


Discover more from cantonadigital

Subscribe to get the latest posts sent to your email.

Leave a comment