Radio Fortune Africa -Na Cantona Joseph
https://zeno.fm/radio/radio-fortune-africa

Silaha nusu milioni zilizopatikana na Taliban nchini Afghanistan zimepotea, kuuzwa au kusafirishwa kwa makundi ya wapiganaji, duru zimeiambia BBC – huku Umoja wa Mataifa ukiamini kuwa baadhi zimeangukia mikononi mwa washirika wa al-Qaeda.
Kundi la Taliban lilichukua udhibiti wa takriban silaha milioni moja na vifaa vya kijeshi – ambavyo vingi vilifadhiliwa na Marekani – wakati walipotwaa tena udhibiti wa Afghanistan mwaka 2021, kulingana na afisa wa zamani wa Afghanistan ambaye alizungumza na BBC lakini hakutaka kujulikana.
Wakati kundi la Taliban liliposonga mbele kupitia Afghanistan mwaka 2021, wanajeshi wengi wa Afghanistan walijisalimisha au kukimbia, na kuacha silaha na magari yao. Vifaa vingine viliachwa nyuma na vikosi vya Marekani.
Hifadhi hiyo ilijumuisha bunduki zilizotengenezwa Marekani, kama vile bunduki za M4 na M16, pamoja na silaha nyingine kuu kuu zilizokuwa mikononi mwa serikali ya Afghanistan ambazo zilikuwa zimeachwa nyuma kutokana na miongo kadhaa ya vita.
Vyanzo vya habari vimeiambia BBC kwamba, katika Kamati ya Vikwazo ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa huko Doha mwishoni mwa mwaka jana, Taliban walikiri kwamba angalau nusu ya vifaa hivi sasa “haijulikani” viliko.
Mtu kutoka katika kamati hiyo alisema wamethibitisha na vyanzo vingine kuwa vitu nusu milioni havijulikani vilipo.
Katika ripoti ya mwezi Februari , Umoja wa Mataifa ulisema kwamba washirika wa al-Qaeda, ikiwa ni pamoja na Tehreek-e-Taliban Pakistan, Vuguvugu la Kiislamu la Uzbekistan, Vuguvugu la Kiislamu la Turkestan Mashariki, na Vuguvugu la Ansarullah la Yemen, walikuwa wakipata silaha zilizotekwa na Taliban au kuzinunua kupitia soko haramu.
BBC ilimweleza haya Hamdullah Fitrat, naibu msemaji wa serikali ya Taliban, ambaye aliiambia BBC kuwa ilichukulia suala la kuhifadhi silaha kwa uzito mkubwa.
“Silaha zote nyepesi na nzito zimehifadhiwa kwa usalama. Tunakataa vikali madai ya uuzaji silaha kimagendo au kupotea,” alisema.
Ripoti ya Umoja wa Mataifa ya mwaka 2023 ilisema Taliban iliwaruhusu makamanda wa ndani kubakisha 20% ya silaha za Marekani zilizokamatwa, na kwamba soko la biashara haramu ya silaha lilikuwa likistawi kutokana na hilo.
Makamanda hawa ni washirika wa Taliban lakini mara nyingi wana kiwango cha uhuru wa kujitawala katika maeneo yao.
Umoja wa Mataifa ulibainisha kuwa “kupeana zawadi ya silaha kunatekelezwa sana kati ya makamanda wa ndani na wapiganaji ili kuimarisha mamlaka. Soko la biashara haramu linasalia kuwa chanzo kikubwa cha silaha kwa Taliban”.
All Rights Reserved © The Cantona Group PLC||2025
Discover more from cantonadigital
Subscribe to get the latest posts sent to your email.