IMF kuipa Tanzania dola Milioni 441 kusaidia Uchumi wake

Radio Fortune Africa -Na Cantona Joseph

https://zeno.fm/radio/radio-fortune-africa

.

Shirika la Fedha Duniani (IMF) limetangaza kuwa limefikia makubaliano ya awali na serikali ya Tanzania ambayo yakipitishwa rasmi, yataiwezesha nchi hiyo kupata takriban dola milioni 441 kwa ajili ya kusaidia uchumi wake.

Fedha hizi ni sehemu ya mapitio ya tano ya mpango wa mikopo ya muda mrefu (ECF) na mapitio ya pili ya mpango wa Uhimilivu na Ustahimilivu (RSF).

Makubaliano haya yamefikiwa baada ya timu ya IMF ikiongozwa na Nicolas Blancher, kufanya mazungumzo na viongozi wa Tanzania kati ya Aprili 2 hadi 17, 2025. Ujumbe wa Tanzania uliwakilishwa na Waziri wa Fedha, Dk. Mwigulu Nchemba, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Bw. Emmanuel Tutuba, viongozi wengine wakuu, washirika wa maendeleo, wawakilishi wa sekta binafsi na mashirika ya kiraia.

Kwa ujumla, IMF imesema kuwa hali ya uchumi wa Tanzania ni nzuri, na ukuaji wa pato la taifa (GDP) ulikuwa asilimia 5.5 mwaka 2024 na unatarajiwa kufikia asilimia 6 mwaka 2025.

Mfumuko wa bei umedhibitiwa, ukiwa asilimia 3.3 mwezi Machi – chini ya lengo la asilimia 5 lililowekwa na Benki Kuu. Hata hivyo, IMF imeonya kuwa kuna changamoto zinazoweza kuathiri uchumi, ikiwemo hali ya sintofahamu kimataifa, mizozo katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, na uchaguzi mkuu unaotarajiwa nchini ambao unaweza kuongeza matumizi au kuchelewesha utekelezaji wa mageuzi ya kiuchumi.

IMF pia imepongeza juhudi za Tanzania katika kuongeza mapato ya ndani na kuboresha matumizi ya fedha za umma, hasa katika elimu, afya na kulipa madeni ya ndani.

Benki Kuu ya Tanzania pia imepongezwa kwa kuruhusu kubadilika kwa thamani ya shilingi na kuimarisha soko la fedha za kigeni. Makubaliano haya yanatarajiwa kuidhinishwa na bodi ya IMF katika wiki zijazo, ambapo fedha hizo zitapatikana rasmi kwa Tanzania.

All Rights Reserved © The Cantona Group PLC||2025


Discover more from cantonadigital

Subscribe to get the latest posts sent to your email.

Leave a comment