Radio Fortune Africa -Na Cantona Joseph
https://zeno.fm/radio/radio-fortune-africa

Chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania Chadema kimetoa taarifa inayodai kuwa Mwenyekiti wa chama hicho Tundu Lissu ametolewa mahabusu hii leo na kupelekwa mahali kusikojulikana.
Lissu amekuwa akishikiliwa mahabusu katika gereza la Keko lililopo jijini Dar Es Salaam toka alipofunguliwa mashtaka ya uhaini juma lililopita.
“Naibu Katibu mkuu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo Chadema Zanzibar, Wakili Ali Ibrahim Juma, mawakili, familia na wanachama kwa nyakati tofauti wamefika katika gereza za Keko jijini Dar es Salaam ambako Mwenyekiti wa Chama hicho anashikiliwa. Hata hivyo juhudi zao za kumuona Lissu hazikufanikiwa baada ya kuelezwa kuwa hayuko katika gereza hilo,” inaeleza sehemu ya taarifa hiyo ilisainiwa na msemaji wa Chadema, Brenda Rupia.
Taarifa imeeleza kuwa watu hao hawakupewa maelezo yoyote rasmi kuhusu mahali alipopelekwa.
Chadema imelitaka jeshi la Magereza, mamlaka husika na vyombo vya dola kutoa taarifa wazi na haraka kwa umma kuhusu mahali alipopelekwa Tundu Lissu.
Mamlaka hizo mpaka sasa hazijatoa taarifa yoyote na BBC inaendelea na jitihada za kuwatafuta.
Wakati huo huo, Jeshi la Polisi Kanda Maalumu Dar es Salaam limetoa onyo kali dhidi ya mpango wa Chadema kuhamasisha watu kukusanyika katika Mahakama ya Kisutu April 24 ili kumuunga mkono Lissu atakapofikishwa Mahakamani.
Onyo hilo limekuja baada ya Makamu Mwenyekiti wa Chadema John Heche kusisitiza watu kujitokeza kwa wingi siku hiyo.
Lissu alifunguliwa kesi kwa shutuma za uhaini baada ya kukamatwa mkoani Ruvuma alipokuwa kwenye kampeni ya kushinikiza mageuzi kwenye mifumo ya uchaguzi nchini humo kabla ya uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika baadae mwezi Oktoba mwaka huu.
All Rights Reserved © The Cantona Group PLC||2025
Discover more from cantonadigital
Subscribe to get the latest posts sent to your email.