Radio Fortune Africa -Na Cantona Joseph
https://zeno.fm/radio/radio-fortune-africa

Waziri wa ulinzi wa Israel amesema wanajeshi watasalia katika kile kinachoitwa maeneo salama waliyoyaanzisha kwa kuyateka maeneo makubwa ya Gaza hata baada ya kumalizika kwa vita.
Israel Katz alisema maeneo hayo yatakuwa kwa ajili ya “usalama” kulinda jamii za Israel “katika muda wowote ama kwa kipindi fulani au wa kudumu”, na kwamba wamenyakua “asilimia” kadhaa ya ardhi ya Palestina tangu mashambulizi ya Israeli kuanza tena wiki tatu zilizopita.
Israel itaendeleza wiki ya sita ya kuzuia misaada ya kibinadamu ili kuishinikiza Hamas kuwaachilia mateka, alisema, licha ya onyo la Umoja wa Mataifa la athari “mbaya”.
Siku ya Jumatano Shirika la Madaktari Wasio na Mipaka (MSF) lilikua la hivi punde la kimataifa kupaza sauti kutokana na athari za kampeni ya Israel, likisema kwamba Gaza “imegeuzwa kuwa kaburi la umati la Wapalestina na wale wanaokuja kuwasaidia”.
“Tunashuhudia kwa wakati halisi uharibifu na kulazimishwa kuhama kwa wakazi wote huko Gaza,” Amande Bazerolle, mratibu wa dharura wa shirika la misaada huko Gaza, alisema.
Wizara ya afya ya Gaza inayoendeshwa na Hamas imesema zaidi ya watu 1,650 wameuawa tangu vita kuanza tena tarehe 18 Machi.
Maafisa wa hospitali walisema takriban Wapalestina 24 waliuawa katika mashambulizi ya Israel kote Gaza siku ya Jumatano.
Wengi wa walioripotiwa kuuawa walikuwa katika mji wa Gaza, kaskazini mwa nchi hiyo.
Walijumuisha watu 10 wa familia ya Hassouna, wengi wao wakiwa watoto na wanawake. Mmoja wao alikuwa Fatema Hassouna – mwandishi anayeibukia na mpiga picha.
All Rights Reserved © The Cantona Group PLC||2025
Discover more from cantonadigital
Subscribe to get the latest posts sent to your email.