Uingereza yaandaa mazungumzo ya kuleta amani Sudan

Radio Fortune Africa -Na Cantona Joseph

https://zeno.fm/radio/radio-fortune-africa

Makumi ya maelfu ya watu wamelazimika kukimbia kambi huko Darfur kutokana na mashambulizi ya hivi karibuni
Maelezo ya picha,Makumi ya maelfu ya watu wamelazimika kukimbia kambi huko Darfur kutokana na mashambulizi ya hivi karibuni

Mkutano wa kimataifa wa ngazi ya juu umeanza jijini London, Uingereza kwa lengo la kutafuta suluhisho la kudumu la mzozo wa Sudan.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza, David Lammy, ameashiria mazungumzo hayo kuwa “njia kuelekea amani.”

Vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyoikumba Sudan miaka miwili iliyopita vimesababisha kile mashirika ya misaada yanaeleza kuwa ni janga kubwa zaidi la kibinadamu duniani kwa sasa.

Uingereza, kupitia mkutano huu, imeahidi msaada wa ziada wa pauni milioni 120 (takriban dola milioni 159) kwa ajili ya chakula na huduma za afya.

Mashirika ya misaada yameripoti kuwa watu wapatao milioni 30 wanahitaji msaada wa haraka, huku mamilioni wakikumbwa na njaa kali kufuatia athari za vita.

“Watu wengi wamekata tamaa kuhusu Sudan – jambo hili ni kosa kimaadili. Hatuwezi kuendelea kufumbia macho mateso haya ya raia wasiokuwa na hatia; vichwa vya raia vinakatwa, watoto wachanga wanabakwa, na watu wengi zaidi wanakabiliwa na njaa kuliko sehemu nyingine yoyote duniani,” alisema David Lammy wakati wa ufunguzi wa mkutano huo siku ya Jumanne.

Tangu kuanza kwa vita hivyo mnamo Aprili 15, 2023, zaidi ya watu milioni 12 wamelazimika kuyakimbia makazi yao, huku makumi ya maelfu wakiripotiwa kuuawa.

Ripoti za ukatili wa kingono zimesambaa kote nchini, na mauaji ya kimbari kuripotiwa katika eneo la Darfur.

Mkutano huo wa mawaziri unaongozwa kwa pamoja na Uingereza, Umoja wa Ulaya (EU), na Umoja wa Afrika (AU), ukiwa na lengo la kuimarisha mshikamano wa kimataifa katika kutoa msaada wa kibinadamu na kuanzisha mchakato wa kisiasa utakaoleta suluhu ya kudumu.

Hata hivyo, pande zinazohasimiana – Jeshi la Sudan (SAF) na Wanamgambo wa RSF– hazijaalikwa moja kwa moja.

Badala yake, zinawakilishwa na washirika wao wa kikanda, baadhi yao wakituhumiwa na wanadiplomasia kuwa wanachochea mzozo huo.

Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), kwa mfano, unadaiwa kulisaidia kundi la RSF kwa silaha, madai ambayo yamekanushwa vikali.

Serikali ya Kenya pia inashiriki mkutano huu licha ya kuandamwa na shutuma kuwa inaunga mkono RSF.

Rais William Ruto aliwakaribisha viongozi wa RSF mapema mwaka huu jijini Nairobi, ambapo walitangaza mpango wa kuunda serikali mbadala ya Sudan.

Hata hivyo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya, Musalia Mudavadi, amesema mkutano huo ulikuwa wa mazungumzo ya ndani na si uundwaji wa serikali mbadala.

“Kenya haijawahi kushiriki katika juhudi za kuunda serikali sambamba au mbadala katika nchi yoyote. Kenya inaunga mkono Sudan moja,” alisisitiza.

Mudavadi aliongeza kuwa Kenya ni kitovu cha upatanishi na kwamba haijachukua upande wowote katika mgogoro huo.

Alieleza pia kuwa Kenya imewahi kumkaribisha Jenerali Abdel Fattah al-Burhan, kiongozi wa kijeshi wa Sudan, kama sehemu ya juhudi zake za upatanishi.

Mgogoro huu ulianza kama mvutano wa madaraka kati ya viongozi wa SAF na RSF kuhusu mustakabali wa kisiasa wa taifa hilo.

Mjumbe wa Umoja wa Afrika, Bankole Adeoye, akizungumza mjini London, alisisitiza kuwa, “Hakuna suluhisho la kijeshi linalowezekana Sudan. Kinachohitajika sasa ni kusitishwa kwa mapigano mara moja bila masharti, ikifuatiwa na mazungumzo jumuishi ya kitaifa.” “Raia wa Sudan ndiyo wanaobeba mzigo wa vita hivi visivyo na maana.

Umoja wa Afrika unatoa wito kwa pande zote kusitisha mapigano,” aliongeza.

“AU haitakubali kugawanywa kwa taifa la Sudan.”

All Rights Reserved © The Cantona Group PLC||2025


Discover more from cantonadigital

Subscribe to get the latest posts sent to your email.

Leave a comment