Radio Fortune Africa -Na Cantona Joseph
https://zeno.fm/radio/radio-fortune-africa

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amekutana na kufanya mazungumzo na Mmiliki wa Klabu ya Manchester United ya Uingereza, Sir Jim Ratcliffe, Ikulu jijini Dar es Salaam tarehe 11 Aprili, 2025, ambapo amemkaribisha rasmi kuwekeza katika sekta za michezo na utalii nchini.
Mazungumzo hayo yalijikita katika fursa za ushirikiano baina ya Tanzania na Manchester United, klabu yenye mashabiki mamilioni duniani, wakiwemo wengi kutoka barani Afrika.
Sir Jim ameonesha nia ya kuitumia klabu hiyo kama jukwaa la kuitangaza Tanzania kimataifa, hususan kupitia kampeni za utalii.
Aidha, Rais Samia alipokea zawadi ya jezi ya Manchester United iliyosainiwa na wachezaji wa timu hiyo, kama ishara ya heshima na urafiki kutoka kwa mmiliki huyo wa klabu.
Rais Samia alitumia fursa hiyo kumualika Sir Jim kuangalia uwezekano wa kuanzisha vituo vya mafunzo ya michezo (Sports Academies) nchini, ili kuwawezesha vijana wa Kitanzania kukuza vipaji vyao na kushiriki kwenye mashindano ya kitaifa na kimataifa, lakini pia patika eneo la utalii.
Samia amemshukuru Sir Jim Ratcliffe kupitia Taasisi yake ya Six Rivers ambayo ina shughulika na masuala ya Uhifadhi, kwa namna inavyofanya vizuri katika kudhibiti muingiliano wa wanyamapori na binadamu kwa kushirikiana na Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) pamoja na Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (TAWIRI).
Kupitia Taasisi yake ya Six Rivers, Sir Jim Ratcliffe amebainisha kuwa Taasisi hiyo imedhamiria kurejesha hadhi ya Hifadhi ya Taifa ya Selous na kuwa na Wanyama wakubwa katika Hifadhi hiyo.
Manchester United tayari imekuwa ikifanya kazi na mashirika na mataifa mbalimbali barani Afrika, ikiwemo miradi ya kijamii kupitia Manchester United Foundation, lakini hii ni mara ya kwanza kwa mmiliki wa klabu hiyo kuonesha nia ya uwekezaji wa moja kwa moja katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Ziara ya Sir Jim Ratcliffe nchini Tanzania ni hatua muhimu inayoweza kufungua milango kwa ushirikiano wa kimkakati kati ya sekta ya michezo na maendeleo ya kijamii na kiuchumi kupitia diplomasia ya michezo.
All Rights Reserved © The Cantona Group PLC||2025
Discover more from cantonadigital
Subscribe to get the latest posts sent to your email.