Radio Fortune Africa -Na Cantona Joseph
https://zeno.fm/radio/radio-fortune-africa

Mtawa mwenye misimamo mikali nchini Sri Lanka ambaye ni mshirika wa karibu wa rais wa zamani aliyeondolewa madarakani Gotabaya Rajapaksa, amehukumiwa kifungo cha miezi tisa jela kwa kosa la kuutusi Uislamu na kuchochea chuki za kidini.
Galagodaatte Gnanasara, mtawa wa kibudha alihukumiwa siku ya Alhamisi kwa matamshi aliyoyatoa mwaka 2016.
Ni mara chache Sri Lanka huwahukumu watawa wa Kibudha, lakini hii si mara ya kwanza kwa Gnanasara kufungwa jela. Amekuwa akishutumiwa mara kwa mara kwa chuki na ghasia dhidi ya Waislamu.
Hukumu hiyo, iliyotolewa na Mahakama ya Colombo, inakuja baada ya msamaha wa rais aliopata mwaka 2019 kwa kifungo cha miaka sita kwa kutoa vitisho na kudharau mahakama.
Gnanasara alikamatwa mwezi Disemba kwa matamshi aliyoyatoa wakati wa mkutano na wanahabari mwaka 2016, ambapo alitoa matamshi kadhaa ya kudhalilisha Uislamu.
Siku ya Alhamisi, mahakama ilisema raia wote, bila kujali dini, wana haki ya uhuru wa imani chini ya Katiba.
Pia amepigwa faini ya rupia 1,500 za Sri Lanka ($5; £4). Kushindwa kulipa faini kunaweza kusababisha kifungo cha ziada cha mwezi mmoja.
Gnanasara amewasilisha rufaa kupinga hukumu hiyo. Mahakama ilitupilia mbali ombi la mawakili wake la kutaka aachiliwe kwa dhamana hadi uamuzi wa mwisho utakapotolewa kuhusu rufaa hiyo.
Wakati wa urais wa Rajapaksa, Gnanasara aliteuliwa kuwa mkuu wa kikosi kazi cha rais kuhusu mageuzi ya kisheria yenye lengo la kulinda maelewano ya kidini.
Baada ya kuondolewa madarakani Rajapaksa, Gnanasara alihukumiwa kwenda jela mwaka jana kwa mashtaka yanayohusiana na matamshi ya chuki dhidi ya Waislamu, ambao ni wachache nchini humo lakini alipewa dhamana wakati akikata rufaa dhidi ya kifungo chake cha miaka minne.
Mwaka 2018, alihukumiwa kifungo cha miaka sita kwa kudharau mahakama na kumtisha mke wa mchora katuni wa kisiasa ambaye inaaminika ametoweka.
Alitumikia miezi tisa tu ya kifungo hicho kwa sababu alipata msamaha wa Maithripala Sirisena ambaye alikuwa rais wa nchi wakati huo.
All Rights Reserved © Cantona Group PLC||2025
Discover more from cantonadigital
Subscribe to get the latest posts sent to your email.