Radio Fortune Africa -Na Cantona Joseph
https://zeno.fm/radio/radio-fortune-africa

Eneo la Masisi katika jimbo la Kivu Kaskazini limekuwa na mapigano makali katika siku za hivi karibuni kati ya kundi lenye silaha la M23/AFC na jeshi la Congo, likisaidiwa na washirika wake.
Kulingana Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu, OCHA, imesema mapigano hayo yamesababisha takribani watu 102,000 kukimbia eneo hilo katika muda wa chini ya wiki moja.
“Kati ya tarehe 3 na 6 Januari, timu za Madaktari wasio na Mipaka (MSF) na Wizara ya Afya zilihudumia majeruhi 75 katika Hospitali Kuu ya Rufaa ya Masisi na Kituo cha Afya cha Rufaa cha Nyabiondo,” amesema Stephane Goetghebuer, Mkuu wa Ujumbe wa MSF huko Kivu Kaskazini.
Ameongeza kuwa mbali na kutoa huduma, “vituo hivi viwili vya afya pia vimehifadhi mamia ya raia kwa siku kadhaa, ambao walitafuta hifadhi ili kufaidika na ulinzi.”
Kufuatia mapigano haya, M23/AFC walichukua udhibiti wa jiji la Masisi na eneo jirani mwishoni mwa juma. Tangu wakati huo mapigano yameendelea kusini zaidi katika eneo hilo, kwenye mpaka na Kivu Kusini.
Kutokana na hali hiyo, timu za MSF katika Hospitali Kuu ya Rufaa ya Minova na Hospitali ya Numbi, zote za Kivu Kusini, pia zinasaidia kuwatibu majeruhi wengi.
“Mapigano yameripotiwa katika nyanda za juu za Numbi za Minova huko Kivu Kusini. Watu wamekimbia na majeruhi 84 wanatibiwa katika hospitali ya Numbi na hospitali kuu ya Minova,” amesema Julien Gircour, mkuu wa ujumbe wa MSF huko Kivu Kusini.
Timu za MSF huko Masisi, Nyabiondo, Minova na Numbi zinaendelea kutoa msaada wa matibabu kwa watu walioathirika. Mapigano haya ni ya hivi punde katika mgogoro wa miaka mitatu wa kivita kati ya M23 dhidi ya jeshi la Congo na makundi washirika mashariki mwa DRC.
Mzozo huo umesababisha maelfu ya watu kuyahama makazi yao na kusababisha hali mbaya ya kibinadamu na kiafya mashariki mwa DRC.
All Rights Reserved © Cantona Group PLC||2025
Discover more from cantonadigital
Subscribe to get the latest posts sent to your email.