Radio Fortune Africa -Na Cantona Joseph
https://zeno.fm/radio/radio-fortune-africa
Waasi wa Houthi nchini Yemen wamedai kuhusika na mashambulizi ya makombora na ndege zisizo na rubani dhidi ya Israel, siku moja baada ya mashambulizi mabaya ya Israel kwenye maeneo yanayodhibitiwa na waasi hao, ukiwemo uwanja wa ndege wa Sanaa alikokuwa mkuu wa shirika moja la Umoja wa Mataifa.

Katika taarifa yao, Wahouthi wamesema wamerusha kombora kuelekea uwanja wa ndege wa Tel Aviv (katikati ya Israel), wakarusha ndege zisizo na rubani kuelekea mji wa Tel Aviv na kushambulia meli katika Bahari ya Arabia.
“Uchokozi wa Israel utaongeza tu dhamira ya watu wa Yemen kuendelea kuunga mkono watu wa Palestina,” waasi wa Houthi wameongeza.
Nchini Israel, jeshi limedai kuwa kombora lililorushwa kutoka Yemen lilinaswa kabla ya kuvuka ardhi ya Israel. Ving’ora vya tahadhari vilipigwa katikati mwa Israeli kutokana na uwezekano wa kuanguka kwa mabaki ya kombora hilo.
Mashambulizi ya Houthi yanakuja baada ya Israel kushambulia siku ya Alhamisi kwenye maeneo yanayodhibitiwa na waasi, ikiwa ni pamoja na uwanja wa ndege wa Sanaa, vituo, mitambo ya kuzalisha umeme na bandari kwingineko nchini Yemen, kulingana na waasi hao ambao wamelaani “uhalifu”.
Watu sita wamefariki nchini Yemen kulingana na Houthi. Wanne kati yao waliuawa katika uwanja wa ndege wa Sanaa na karibu wasafiri 20 na wafanyakazi walijeruhiwa, kulingana na naibu waziri wa uchukuzi katika utawala wa waasi, Yahya al-Sayani.
Mkurugenzi mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Tedros Adhanom Ghebreyesus, alikuwa katika uwanja wa ndege wa Sanaa wakati wa shambulio la bomu na amesema kwenye mtandao wa kijamii wa X kwamba yuko “salama salimini.” Hata hivyo, mmoja wa wafanyakazi wa ndege yake alijeruhiwa.
Katika mkutano na waandishi wa habari, Bw. Sayani amesema kuwa safari za ndege zimeanza tena Ijumaa saa 4:00 asubuhi kwa saa za Yemen katika uwanja wa ndege wa Sanaa.
Kulingana na Bw. Sayani, shambulizi katika uwanja huo wa ndege lilitokea wakati abiria wengi walipokuwa wakijiandaa kupanda ndege kutoka Sanaa na ndege nyingine ilikuwa ikijiandaa kutua. “Abiria waliondolewa kwa mujibu wa mpango wa dharura.”
All Rights Reserved © Cantona Group PLC||2024
Discover more from cantonadigital
Subscribe to get the latest posts sent to your email.