Radio Fortune Africa -Na Cantona Joseph
https://zeno.fm/radio/radio-fortune-africa

Karibu katika Matangazo yetu ya jioni moja kwa moja kutoka Communication Center. Tumekuandalia mengi ikiwa ni pamoja
Muhtasari
- Urusi yatoa onyo juu ya “propaganda” baada ya ajali ya ndege ya Azerbaijan
- Morocco kuwapa wanawake haki zaidi
- Wanakijiji wauawa kwa mashambulio ya anga siku ya Krismasi Nigeria
- Ethiopia ‘yafunga mpaka na Somaliland’ huku mapigano ya kiukoo yakiendelea
- Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo ‘ladungua ndege zisizo na rubani’ za Rwanda
- Makumi wamenusurika katika ajali ya ndege ya abiria ya Kazakhstan
- Polisi hawahusika na utekaji nyara wowote – Afisa Mkuu wa polisi Kenya
- Papa ahimiza mazungumzo ya kumaliza vita vya Ukraine na Urusi
- Man City wanaweza kukosa kushiriki ligi ya mabingwa – Guardiola
- Mwili wapatikana kwenye gurudumu la ndege ya United Airlines baada ya kutua Hawaii
- Mamia watoroka jela ya Msumbiji kufuatia maandamano ya uchaguzi
- Syria yasema maafisa 14 wa usalama waliuawa kwa shambulio la ‘kuviziwa’ na wafuasi watiifu wa Assad
Naam,Natumai U buheri wa afya popote pale ulipo duniani kwa mwoyo mkunjufu na mikono miwili Hujambo na karibu katika matangazo yetu Afrika Leo Jioni ya moja kwa moja ikiwa ni tarehe 26/12/2024 Jina langu ni Cantona Joseph,karibu.
Syria yasema maafisa 14 wa usalama waliuawa kwa shambulio la ‘kuviziwa’ na wafuasi watiifu wa Assad

Mamlaka mpya inayoongozwa na waasi nchini Syria imesema maafisa 14 wa wizara ya mambo ya ndani wameuawa na wengine 10 kujeruhiwa katika shambulizi la kuvizia lililofanywa na vikosi vinavyomtii Rais aliyepinduliwa Bashar al-Assad magharibi mwa nchi hiyo.
Wanasema mapigano hayo yalifanyika karibu na bandari ya Mediterranean ya Tartous siku ya Jumanne.
Ripoti zinasema kuwa vikosi vya usalama vilivamiwa wakati vikijaribu kumkamata afisa wa zamani kuhusiana na jukumu lake katika gereza maarufu la Saydnaya, karibu na mji mkuu Damascus.
Zaidi ya wiki mbili zilizopita, urais wa Assad ulipinduliwa na vikosi vya waasi vinavyoongozwa na kundi la Kiislamu la Hayat Tahrir al-Sham (HTS).
Shirika la Haki za Kibinadamu la Syria (SOHR) lenye makao yake nchini Uingereza limesema wanamgambo watatu pia waliuawa katika mapigano hayo.
SOHR iliongeza kuwa vikosi vya usalama baadaye viliweka usalama.
Kwengineko , mamlaka ya Syria iliweka amri ya kutotoka nje usiku kucha katika mji wa kati wa Homs, vyombo vya habari vya serikali viliripoti.
Ripoti zinasema kuwa hii ilifuatia machafuko baada ya video inayodaiwa kuonyesha shambulio kwenye hekalu la Alawite.
Wizara ya mambo ya ndani ya Syria ilisema ni video ya zamani, iliyoanzia kwenye mashambulizi ya waasi huko Aleppo mwishoni mwa mwezi Novemba, na ghasia hizo zilitekelezwa na makundi yasiyojulikana.
SOHR ilisema mtu mmoja aliyekuwa akiandamana aliuawa na watano kujeruhiwa huko Homs.
Maandamano pia yaliripotiwa katika maeneo yakiwemo miji ya Tartous na Latakia, na mji alikozaliwa Assad wa Qardaha.
Alawites ni madhehebu ya wachache ambayo familia ya Assad inatoka, na ambayo wengi wa wasomi wa kisiasa na kijeshi wa utawala wa zamani walitoka.
Mashambulizi makali yaliyoongozwa na HTS ambayo yalianza kutoka kaskazini-mashariki mwa Syria na kuenea nchi nzima yalihitimisha utawala wa zaidi ya miaka 50 wa familia ya Assad.
Syria: Ujumbe wa Iraq wakutana na mamlaka mpya Damascus
Ujumbe wa Iraq umekutana siku ya Alhamisi, Desemba 26, na mamlaka mpya ya Syria mjini Damascus, amesema msemaji wa serikali ya Iraq, zaidi ya wiki mbili baada ya rais Bashar Al Assad kutimuliwa mamlakani.

Ujumbe huo, ukiongozwa na mkuu wa idara ya ujasusi ya Iraq, Hamid al-Shatri, “umekutana na utawala mpya wa Syria,” msemaji wa serikali Bassem al-Awadi ameviambia vyombo vya habari vya serikali, na kuongeza kuwa pande zote mbili zimejadili “maendeleo” ya hivi karibuni nchini Syria, na vile vile “mahitaji ya usalama na utulivu katika mpaka” kati ya nchi hizo mbili.
Mamia watoroka jela ya Msumbiji kufuatia maandamano ya uchaguzi

Zaidi ya wafungwa 1,500 wametoroka katika gereza moja nchini Msumbiji, wakitumia fursa ya machafuko ya kisiasa yanayoendelea yaliyochochewa na matokeo ya uchaguzi yenye utata, polisi wamesema.
Watu 33 waliuawa na 15 kujeruhiwa katika mapigano na walinzi, mkuu wa polisi Bernardino Rafael aliambia mkutano na waandishi wa habari.
Takriban watoro 150 zaidi wamekamatwa tena, aliongeza.
Maandamano yalizuka siku ya Jumatatu kujibu mahakama ya juu zaidi ya Msumbiji ikithibitisha kwamba chama tawala cha Frelimo, kilichokuwa madarakani tangu mwaka 1975, kilishinda uchaguzi wa rais wa Oktoba.
Bw Rafael alisema makundi ya waandamanaji wanaoipinga serikali yalikaribia gereza hilo katika mji mkuu Maputo siku ya Jumatano. Wafungwa walitumia machafuko hayo kuangusha ukuta na kutoroka, alisema.
Msumbiji imekumbwa na machafuko tangu uchaguzi uliozozaniwa mwezi Oktoba. Matokeo rasmi yalionyesha mgombea urais wa chama tawala cha Frelimo, Daniel Chapo, akishinda.
Maandamano mapya yalizuka siku ya Jumatatu, wakati mahakama ya kikatiba ilipoamua kuwa Chapo alishinda uchaguzi huo, huku ikirekebisha tofauti yake ya ushindi.
Matokeo ya awali ya mwezi Oktoba yalisema Daniel Chapo alipata asilimia 71 ya kura dhidi ya mpinzani wake mkuu Venâncio Mondlane aliyepata 20%. Mahakama sasa imeamua kwamba alishinda 65% dhidi ya 24% ya Mondlane.
Mwili wapatikana kwenye gurudumu la ndege ya United Airlines baada ya kutua Hawaii

Mwili umepatikana katika sehemu gurudumu, la ndege ya United Airlines baada ya kutua Hawaii usiku wa mkesha wa Krismasi, kampuni hiyo ilisema.
Ndege aina ya Flight 202 iliondoka kwenye uwanja wa ndege wa Chicago wa O’Hare Jumanne asubuhi na kutua katika uwanja wa ndege wa Kahului wa Maui alasiri.
Shirika la ndege la United Airlines lilisema bado haijafahamika ni lini mtu huyo aliingia kwenye eneo hilo, ambalo ilisema linaweza kufikiwa tu kutoka nje ya ndege ya Boeing 787-10.
Kampuni hiyo ilisema inashirikiana na mamlaka ya kutekeleza sheria katika uchunguzi.
Marehemu bado hajatambuliwa
Katika taarifa, idara ya polisi iliiambia Hawaii News Now kwamba ilikuwa ikifanya uchunguzi “kuhusu mtu aliyefariki aliyegunduliwa kwenye ndege iiliowasili kutoka bara leo mchana. Kwa wakati huu, hakuna maelezo zaidi yanayopatikana”.
Israel na Hamas washutumiana kwa kukwamisha makubaliano ya kuwaachilia mateka Gaza
Israel na Hamas zinashutumiana kwa kukwamisha kuendelea kwa mazungumzo ya usitishaji vita na kuachiliwa kwa mateka. Israel imewarejesha nyumbani wajumbe wake katika mazungumzo kwa ajili ya mashauriano. Wakati huo huo, mazungumzo huko Doha, mji mkuu wa Qatar, kwa mara nyingine tena yamesimama.

Nchini Israel, ofisi ya Waziri Mkuu leo inaishutumu Hamas kwa kusema uongo na kuweka vikwazo vipya katika mazungumzo. Kwa upande wake, Hamas inathibitisha kuwa hayo ni masharti mapya ya Israel ambayo yanaondoa zaidi uwezekano wa kupatikana makubaliano huko Gaza.
Kwa mara nyingine tena, familia za mateka, bado zina wasiwasi. Saa 48 tu zilizopita, Waziri Mkuu aliripoti maendeleo katika mazungumzo hayo, wakati juzi usiku, Israel ilitangaza kuwarejesha nyumbani timu ya wajumbe katika mazunguzmo waliokuwa Qatar kwa mashauri ya ndani. Katika hatua hii, mazungumzo yatazingatia usitishaji vita wa siku 45 hadi 60 na kuachiliwa kwa mateka 34 badala ya wafungwa 250 wa Kipalestina. Siku ya Jumatano, Desemba 25, Israel ilithibitisha nia yake ya kuendelea na juhudi za kuwarejesha nyumbani mateka wote.
Mazungumzo yamesimama
Hali ni ngumu haswa kwa familia za mateka 100, wakati 67 kati yao bado wako hai. Kwa mfululizo huu wa maendeleo na vizuizi, idadi kubwa ya familia inamtuhumu Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu kwa kuvunja mara kwa mara maendeleo katika mazungumzo. Siku chache zilizopita, aliliambia Gazeti la Wall Street Journal kwamba hakuna suala la Israeli kumaliza vita huko Gaza.
Kwa kweli, familia za mateka zinapinga utaratibu ambao unapendekezwa kwa makubaliano haya mapya, ambayo yanataka kuachiliwa kwa sehemu ya mateka ambao bado wako hai. “Ni amri kwa wengine,” wanasisitiza familia.
Syria: Wafuasi wa Assad watafutwa kwa udi na uvumba baada ya makabiliano makali
Mamlaka mpya ya Syria imeanzisha operesheni siku ya Alhamisi Desemba 26, 2024 dhidi ya “wanamgambo” watiifu kwa Bashar Al Assad magharibi mwa nchi hiyo, na kuua watu watatu kulingana na shirika moja lisilo la kiserikali, siku moja baada ya makabiliano makali na maandamano ya wachache kutoka dhehebu la Alawite.

Operesheni hiyo inafanyika katika mkoa wa pwani wa Tartus (magharibi), ngome ya walio wachache kutoka dhehebu la Alawite ambako rais aliyeondolewa madarakani anatokaAssad aliotimuliwa mamlakani tarehe 8 Desemba na muungano wa waasi unaoongozwa na kundi la Waislam wenye itikadi kali la Hayat Tahrir al-Sham (HTS) .
Operesheni hii imefanya iwezekane “kuangamiza idadi fulani” ya “wanamgambo” watiifu kwa Bashar Al Assad, linabainisha shirika la habari la serikali SANA. Lengo ni “kurejesha usalama, utulivu na amani ya raia” katika eneo hili la pwani, linabainisha shirika hili la habari.
Shirika la Uangalizi wa Haki za Binadamu la Syria (SOHR) limeripoti “vifo vitatu” katika operesheni hii, na kubainisha kuwa waathiriwa ni kutoka safu ya “wapiganaji watiifu kwa serikali ya zamani”.
– Watu kadhaa wakamatwa –
Shirika hili lisilo la kiserikali lenye makao yake makuu nchini Uingereza, ambalo lina mtandao mkubwa wa vyanzo nchini Syria, pia limeripoti “kukamatwa” kwa watu kadhaa kuhusiana na mapigano na maandamano ya watu kutoka dhehebu la walio wachache la Alawite siku moja kabla.
Kulingana na mashahidi na SOHR, maelfu ya Wasyria walifanya maandamano siku ya Jumatano huko Tartus, Banias, Jableh, na Latakia magharibi mwa nchi, ambapo jamii ya Alawite, tawi la Uislamu wa Kishia, iko, na pia huko Homs (katikati), baada ya kurushwa video inayoonyesha shambulio dhidi ya moja ya sehemu zao takatifu.
Maandamano haya ni ya kwanza tangu kupinduliwa kwa bwana Assad.
“Mwandamanaji mmoja ameuawa na watano wamejeruhiwa baada ya vikosi vya usalama huko Homs kufyatua risasi kuwatawanya waandamanaji,” kulingana na SOHR.
Watu kutoka jamii ya Alawite walipandwa na hasira baada ya kurushwa video kwenye mitandao ya kijamii inayoonyesha “shambulio la wapiganaji” dhidi ya sehemu takatifu ambayo ilichomwa moto huko Aleppo (kaskazini), kulingana na SOHR. Wafanyakazi watano wa sehemu hiyo katifu waliuawa, kulingana na shirika hili lisilo la kiserikali.
Huko Damascus, Wizara ya Mambo ya Ndani imehakikisha kuwa video hiyo ni “ya zamani” na ni ya tarehe ya kutekwa kwa Aleppo na waasi mnamo Desemba 1.
“Lengo la kusambaza tena picha kama hizo ni kuzusha mifarakano kati ya raia wa Syria (…),” wizara imeongeza, ikishutumu “makundi yasiyojulikana” yaliyofanya shambulio hilo.
Hata hivyo, makabiliano kati ya watu wenye silaha na vikosi vya usalama ambao walikuwa wakijaribu kumkamata afisa wa serikali iliyoondolewa katika jimbo la Tartous yalisababisha vifo vya watu 17 siku ya Jumatano, kulingana na SOHR.
Wakati wa makabiliano haya, “wajumbe kumi na wanne wa Wizara ya Mambo ya Ndani waliuawa na wengine 10 kujeruhiwa,” Waziri mpya wa Mambo ya Ndani Mohammed Abdel Rahman amesema katika taarifa.
Kulingana na SOHR, watu watatu waliokuwa na silaha pia waliuawa.
– “Hali inaweza kuwa mbaya zaidi” –
Mamlaka mpya zimeongeza ishara za uhakikisho kwa watu wote walio wachache katika nchi iliyoathiriwa na miaka 13 ya vita vikali, vilivyoanzishwa mwaka 2011 na ukandamizaji wa kikatili wa maandamano ya kuunga mkono demokrasia, na ambayo yalisababisha vifo vya zaidi ya watu 500,000.
Huko Jableh, waandamanaji waliimba “Alawite, Sunni, tunataka amani”, muandamanaji, Ali Daoud, ameliambia shirika la habari la AFP, akitaka “wauaji waadhibiwe”.
Picha zimeonyesha umati wa watu wakiandamana mjini, wakipeperusha bendera ya waasi enzi za uhuru.
“Hapana kuteketeza kwa moto mahali patakatifu na ubaguzi wa kidini, ndio kwa Syria iliyo huru,” imeandikwa kwenye moja ya mabango.
“Kwa sasa tunasikiliza wito wa utulivu (…) Lakini hali inaweza kuwa mbaya zaidi,” amehofia Ghidak Mayya, muandamanaji mwenye umri wa miaka 30, huko Latakia.
Baada ya Bashar Al Assad kukimbilia Moscow kutokana na mashambulizi ya waasi, wanachama wa wachache wa Alawite walifurahia kuanguka kwake lakini walisema wanahofia kutengwa au kulipizwa kisasi.
Kulingana na mtaalamu wa masuala ya siasa Fabrice Balanche, “Alawite walikuwa karibu sana na utawala wa Bashar”, ambao waliunda “kikosi cha walinzi wa rais”. Anakadiria idadi yao kuwa milioni 1.7 leo, au karibu 9% ya raia.
Korea Kusini: Upinzani unasema umewasilisha ombi la kumtimua rais wa mpito Han Duck-soo
Upinzani nchini Korea Kusini umetangaza siku ya Alhamisi, Desemba 26, kwamba umewasilisha ombi la kumtimua Rais wa mpito Han Duck-soo baada ya kukataa kuteua majaji wa Mahakama ya Katiba, hatua muhimu ya kushinda utaratibu wa kumng’atua mtangulizi wake Yoon Suk-yeol.

“Tumewasilisha hoja kabla ya kikao cha mashauriano,” Mbunge Park Sung-joon amewaambia waandishi wa habari katika Bunge la taifa. “Tutapiga kura kesho,” ameongeza.
Upinzani unamkosoa Bw. Han kwa kukataa kujaza viti vitatu vilivyoachwa wazi katika Mahakama ya Katiba, ambayo inapaswa ndani ya miezi sita ithibitishe au kubatilisha kufutwa kazi kwa rais wa kihafidhina Yoon Suk Yeol, hatu iliyopigiwa kura na wabunge mnamo Desemba 14, kwa jaribio lake ambalo halifanikiwa la kuweka sheria ya kijeshi na kulifunga Bunge mdomo kwa kulipelekea jeshi siku kumi na moja mapema.
Han Duck-soo, Waziri Mkuu, anakaimu nafasi ya rais, na Bw. Yoon alisimamishwa kazi kusubiri uamuzi wa Mahakama ya Katiba. Hii inapaswa kutawala kwa wingi wa theluthi mbili. Hata hivyo, viti vyake vitatu kati ya tisa viko wazi kutokana na kustaafu kwa majaji msimu uliopita.
Majaji hao watatu wapya kimsingi walipaswa kuteuliwa na rais siku ya Alhamisi kutoka miongoni mwa wagombea waliochaguliwa na Bunge lataifa, linalodhibitiwa na upinzani.
Lakini Bw. Han, mtumishi wa serikali mwenye umri wa miaka 75, anashikilia kuwa hadhi yake kama rais wa mpito haimpi mamlaka ya kufanya uteuzi mkubwa, na anadai kwamba uchaguzi wa majaji uwe wa kwanza kuchunguzwa upya na chama cha People’s Power Party (PPP, kilicho madarakani) na vyama vya upinzani.
Rais wa mpito anapaswa “kujiepusha kutumia mamlaka muhimu ya kipekee ya urais, ikiwa ni pamoja na uteuzi wa taasisi za kikatiba”, amesema Bw. Han. “Makubaliano kati ya chama tawala na upinzani katika Bunge la taifa, ambalo linawakilisha wananchi, lazima kwanza yafikiwe,” ameongeza.
Mahakama ya Katiba imepanga kusikiliza kesi ya kwanza kuhusu kuondolewa kwa Bw. Yoon siku ya Ijumaa.
Iwapo viti vitatu vilivyoachwa wazi havitajazwa kabla ya kukamilika kwa utaratibu huo, majaji sita waliosalia watalazimika kutoa uamuzi kwa kauli moja ili kumwondoa kabisa Bw. Yoon mamlakani. Kura moja dhidi ya kung’atuliwa mamlakani ingemaanisha kurejeshwa kwake moja kwa moja katika ofisi.
Kukataa kwa Bw. Han kuteua majaji wapya kunathibitisha “kwamba hana nia wala ujuzi wa kuheshimu Katiba”, amelalamika kiongozi wa wabunge wa Chama cha Kidemokrasia katika Bunge hilo, Park Chan dae.
Iwapo hoja iliyowasilishwa na upinzani itapitishwa, itakuwa ni mara ya kwanza kutimuliwa kwa rais wa mpito baada ya kutimuliwa kwa rais aliyetangulia mwenye cheo katika historia ya Korea Kusini. Waziri wa Fedha Choi Sang-mok atakuwa rais mpya wa muda.
Katiba ya Korea Kusini inasema kuwa Bunge linaweza kumuondoa rais kwa thuluthi mbili ya kura, na waziri mkuu na wajumbe wengine wa serikali kwa kura nyingi tu.
Upinzani, ambao una viti 192 kati ya 300 katika Bunge, unasema unahitaji tu wingi wa kura ili kumuondoa Bw Han, kwa vile yeye ni waziri mkuu pekee. Lakini PPP badala yake inahoji kuwa kura ya thuluthi mbili ni muhimu, kwa vile Bw. Han ni kaimu rais.
Yoon Suk Yeol, 64, pia anachunguzwa kwa “uasi”, uhalifu unaoadhibiwa kwa kifo.
Ofisi ya Uchunguzi wa Ufisadi, ambayo inajikita na uchunguzi, tayari imemwita rais aliyeondolewa madarakani mara mbili ili kumhoji kuhusu matukio ya usiku wa Desemba 3 kuamkia 4, ambayo yaliishangaza nchi. Lakini Bw. Yoon hajaripoti .
Wachunguzi lazima waamue katika siku zijazo kama watoe shauri la tatu, au iwapo wataomba mahakama kibali cha kumfikisha Bw. Yoon mahakamani kwa nguvu.
Sudani Kusini: Wimbi la wakimbizi wa Sudan lazidisha janga la kipindupindu, yaonya MSF
Shirika la Umoja wa Mataifa linalohudumia Wakimbizi (UNHCR) lilionya tarehe 20 Desemba kuhusu wimbi la wakimbizi nchini Sudani Kusini, kutoka Sudani katika wiki za hivi karibuni.

Hata Shirika la Madaktari Wasio na Mipaka (MSF) lilipaza sauti siku Jumatatu Desemba 23, ambapo lilibainisha kuwa zaidi ya watu 5,000 walivuka mpaka kati ya nchi hizo mbili kila siku mwezi Desemba. Matokeo: kambi mbili za muda huko Renk, kwa upande wa Sudani Kusini, zimezidiwa kabisa na janga la kipindupindu lililotangazwa mwezi Oktoba “linaongezeka kwa kutisha na kwa kasi”, kulingana na shirika hili lisilo la kiserikali.
Kambi mbili za muda huko Renk, Sudani Kusini, hivi sasa zina zaidi ya watu 17,000 waliokimbia makazi yao, ingawa zilitengenezwa kupokea idadi ya watu 8,000. Shirika la Umoja wa Mataifa linalohudumia Wakimbi (UNHCR) lilikadiria, mwishoni mwa wiki iliyopita, kwamba zaidi ya watu 80,000, hasa wanawake na watoto, walivuka mpaka chini ya wiki tatu. Hii ni baada ya kuongezeka kwa mapigano nchini Sudani katika majimbo ya White Nile, Sennar na Blue Nile, linasema shirika hili la Umoja wa Mataifa.
Kulingana na Shirika la Madaktari Wasio na Mipaka (MSF), maelfu ya wakimbizi wa Sudani sasa wanalazimika kulala nje, huku wakiwa na upungufu wa kupata chakula, maji na huduma za afya. Kambi nyingi zimezidiwa. Taka zinarundikana kila mahali, vyoo vinatapakaa… Matokeo yake: janga la kipindupindu ambalo lilizuka mwishoni mwa Oktoba linazidi kushika kasi.
MSF inabainisha ongezeko “la kutisha na la haraka” la wagonjwa wanaooshukiwa kuaùbukizwa Kipindupindu katika kambi katika majimbo ya Unity na Ikweta ya Kati hasa. Watu 92 walifariki katika Jimbo la Unity, 25 katika kambi karibu na Juba.
“Maji ya kunywa yamechafuliwa na wagonjwa wanafika katika vituo vyetu wakiwa katika hali mbaya, wengi wako kwenye hali mbaya,” anasema Mamman Mustapha. Kwa mujibu wa mkuu huyu wa misheni katika MSF, ni kuchukua “hatua za haraka”, vinginevyo “wagonjwa wa kipindupindu wataongezeka kwa kasi katika siku na wiki zijazo”, anaonya.
Guinea: Upinzani hawatatambua tena mamlaka ya Mpito kuanzia tarehe 31 Desemba
Nchini Guinea, jukwaa linaleta pamoja vyama vya upinzani na mashirika ya kiraia yanayokosoa mamlaka ya Mpito, linatangaza kwamba halitatambua tena mamlaka ya mpito kuanzia tarehe 31 Desemba. Kwa sababu tarehe hii ndiyo ilikuwa kikomo kilichowekwa kwa ajili ya kurejeshwa kwa utaratibu wa kikatiba.

Desemba 31 ni tarehe ya mwisho iliyoahidiwa ya kurejea kwa utaratibu wa kikatiba nchini Guinea, ambayo pia ilikuwa mada ya makubaliano na ECOWAS. Hatimaye, wiki mbili zilizopita, msemaji wa serikali alibainisha kwamba tarehe hiyo haitazingatiwa, akimaanisha awamu ya pili, “uundaji upya wa Serikali”, bila kutoa maelezo zaidi.
Katika taarifa yao kwa vyombo vya habari, jukwaa linaleta pamoja vyama vya upinzani na mashirika ya kiraia yanayokosoa mamlaka ya Mpito wameomba kuanzishwa kwa mpito wa kiraia.
“Tunazungumzia kuhusu hali ya kusherehekea kwa sababu agizo hili – ambalo tunaliita kalenda ya wakati wa Mpito – ambayo mamlaka ya Mpito walikubali wenyewe na, ilikubaliwa na raia wa Guinea na jumuiya ya kimataifa, inafikia mwisho. Bila ya kuwa na wajibu wowote katika masuala ya kiufundi, kiutawala na kijamii na kisiasa kusema ni ukweli gani uliochangia kutofuatwa kwa ahadi hizi”, anabainisha Abdoul Sacko, mratibu wa jukwaa la vikosi vya kijamii vya Guinea, moja ya mashirika yaliyotia saini.
“Hakuna mbinu mwafaka, inayoonekana na kamilifu ya kurejea kwa utaratibu wa kikatiba. Uwajibikaji utatuhitaji kujitolea kufanya kazi, kuwafahamisha na kuwahamasisha watu kuelekea kwenye mpito wa kiraia, kuheshimu na kutilia maanani ahadi hii. Kwa hivyo, kwa mara nyingine tena, tunakabiliwa na hali ambapo tumechoshwa katika ngazi zote,” anaongeza.
DRC: Watoto elfu tatu washerehekea Krismasi katika eneo la mashariki lililokumbwa na mapigano
Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, takriban watoto elfu tatu waliotoroka makazi yao, ambao wlikimbia mapigano kati ya Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (FARDC) na waasi wa M23 kwa zaidi ya miaka mitatu, wamesherehekea Krismasi siku ya Jumatano katika kambi ya Kanyaruchinya, kaskazini mwa mji wa Goma.

Katikati ya uwanja wenye mchanga, chini ya mvua inayonyesha, mamia ya watoto wanapanga foleni kwa matumaini ya kupokea chakula.
Nyuso za Japhet na Soleil ni zenye tabasamu wanapopokea chakula. Wakiwa na umri wa miaka 7 na 10, wanafurahi kuweza kusherehekea Krismasi kama watoto wengine. “Tulipokea mchele, nyama, viazi, juisi, maharage. Najisikia vizuri, kwa sababu nyumbani, hatukuhitaji kusherehekea Krismasi,” anaeleza Japhet. Soleil anaongeza: “Nimepata chakula. Kama mkimbizi, kwa kawaida singeweza kusheherekea Krismasi na kupata chakula hiki. “
Chakula hutolewa kwa kadi
Katika kambi hii ya watu waliotoroka makazi yao, kunahitajika kadi ili kupokea chakula. Usambazaji huu wa chakula cha Krismasi kwa watoto ni wa kipekee. Ange Jibu alikuja kuchukua chakula kwa ajili ya watoto wake watatu: “Watoto wangu wangelifanya siku moja bila kula. Msaada huu unatufariji, kabla tulipokuwa bado tunaishi nyumbani, tuliweza kusherehekea Krismasi, lakini hali haituruhusu kwa sasa. “
Depaul Bakulu ni mwanachama wa shirika la Goma Actif, ambalo lilianzisha zoezi hili la utoaji wa chakula cha Kirismasi. Anasihi vita visitishwe mashariki mwa Kongo: “Ni wito kwa wapiganaji wote kusitisha mapigano, kusitisha vita. Tunatoa wito kwa Ubinadamu kwa watoto hawa warudi nyumbani, na tunaiomba jamii iongeze nguvu na kufanya kila linalowezekana ili kuwe na makubaliano ya amani kati ya wapiganaji wote. “
Wakati huo huo mapigano yaliendelea siku ya Jumatano kati ya FARDC na M23 katika maeneo kadhaa ya Kivu Kaskazini, kilomita chache kutoka kambi hiyo ya wakimbizi wa ndani.
Papa ahimiza mazungumzo ya kumaliza vita vya Ukraine na Urusi

Papa Francis ametoa wito wa kufanyika kwa mazungumzo kati ya Ukraine na Urusi ili kumaliza vita vilivyochochewa na uvamizi wa Urusi nchini Ukraine mwaka 2022.
Katika hotuba yake Siku ya Krismasi, Papa alisema “ujasiri [ulihitajika} kufungua mlango” wa mazungumzo “ili kufikia amani ya haki na ya kudumu” kati ya pande hizo mbili.
Ombi lake linafuatia shambulio kubwa la Urusi siku ya Krismasi kwenye vituo vya kawi vya Ukraine, ambalo Ukraine ilisema lilihusisha angalau makombora 184 na ndege zisizo na rubani.
Mapema mwaka huu, Ukraine ilikataa vikali wito wa papa wa kufanya mazungumzo ya kusitisha vita na kuwa na “ujasiri wa kuinua bendera nyeupe”.
Ujumbe wake wa Urbi et Orbi (kwa jiji na ulimwengu) pia uligusa migogoro mingine.
Akizungumza na maelfu ya watu waliokusanyika katika uwanja wa St Peter’s Square, Papa huyo mwenye umri wa miaka 88 alitangaza: “Milio ya risasi inyamaze katika Ukraine iliyokumbwa na vita,” na kwingineko.
“Ninamwalika kila mtu binafsi, na watu wote wa mataifa yote… kuwa mahujaji wa matumaini, kunyamazisha sauti za risasi na kuondokana na migawanyiko,” alisema.
Polisi hawahusika na utekaji nyara wowote – Afisa Mkuu wa polisi Kenya

Inspekta Jenerali wa polisi nchini Kenya Douglas Kanja amekanusha madai yoyote yanayohusisha polisi katika visa vya utekaji nyara vinavyoendelea nchini.
Katika taarifa yake siku ya Alhamisi, Kanja alisema kuwa hakuna kituo cha polisi nchini ambacho kwa sasa kinawashikilia watu walioripotiwa kutekwa nyara.
“Ili kuepusha shaka, Huduma ya Kitaifa ya Polisi haihusiki na utekaji nyara wowote, na hakuna kituo cha polisi nchini ambacho kinawashikilia watu walioripotiwa kutekwa,” alisema.
IG aliongeza kuwa Mamlaka Huru ya Kusimamia Polisi (IPOA) itachunguza utekaji nyara huo, kwani alitoa wito kwa umma wenye taarifa zozote muhimu kuhusu watu waliopotea kuripoti katika vituo vya polisi vilivyo karibu.
“Suala linalozungumziwa linapaswa kuchunguzwa na Mamlaka Huru ya Kusimamia Polisi na chombo kingine chochote kilicho huru. Tunatoa wito kwa mtu yeyote aliye na taarifa muhimu kuhusu mtu yeyote aliyepotea kuripoti katika kituo cha polisi kilicho karibu nawe.”
Kauli ya Inspekta Jenerali inafuatia kilio cha umma kuhusu visa vya utekaji nyara vinavyoongezeka, haswa miongoni mwa vijana Kenya, siku chache zilizopita.
Makumi wamenusurika katika ajali ya ndege ya abiria ya Kazakhstan

Makumi ya watu wamenusurika katika ajali iliyohusisha ndege iliyobeba watu 67 huko Kazakhstan, maafisa wa eneo hilo wanasema.
Mamlaka ya Kazakh ilisema watu 38 waliuawa katika ajali hiyo.
Ndege hiyo ilikuwa ikielekea Grozny nchini Urusi lakini ikaelekezwa kwengineko kwa sababu ya ukungu, shirika hilo la ndege liliambia BBC.
Ndege ya shirika la ndege la Azerbaijan J2-8243 ilishika moto ilipokuwa ikijaribu kutua kwa dharura karibu na mji wa Kazakh wa Aktau.
Picha zinaonyesha ndege ilikuwa kwa mwendo wa kasi huku gia yake ya kutua ikiwa chini, kabla ya kuwaka moto ilipokuwa ikitua.
Shirika hilo la ndege lilisema kuwa ndege hiyo “ilitua kwa dharura” yapata kilomita 3 kutoka Aktau.
Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo ‘ladungua ndege zisizo na rubani’ za Rwanda

Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo ‘limedungua’ ndege sita zisizo na rubani za Kamikaze za jeshi la Rwanda katika mji wa Mambasa eneo la Lubero katika Mkoa wa Nord Kivu, tovuti ya Radio Okapi inayofadhiliwa na Umoja wa Mataifa iliripoti jana.
Msemaji wa jeshi Lt Kanali Mak Hazukay alisema waasi wa M23 walikuwa wakiwatumia vijana waliovalia sare za kijeshi za Rwanda kama “wale wa ziada” katika maeneo ya vita.
“Jeshi linatoa wito kwa raia wanaotumiwa kama ngao kusalimisha silaha zao, na linawataka wakazi wa maeneo yanayokaliwa kuondoka kwenye kwa usalama wao,” Hazukay alisema.
Lubero imekuwa kitovu cha mapigano mapya kati ya waasi na vikosi vya usalama baada ya mazungumzo kati ya DR Congo na Rwanda hivi karibuni kushindikana.
Jeshi la Congo na waasi wa M23 wanaodaiwa kuungwa mkono na Rwanda wamekuwa wakishambulizi mara kwa mara lakini Rwanda imekuwa ikikanusha kuunga mkono waasi wa M23 na kuishtumu serikali ya Congo kushirikiana na waasi wa Rwanda wa FDLR shutuma ambazo pia Congo inakanusha.

Ethiopia ‘yafunga mpaka na Somaliland’ huku mapigano ya kiukoo yakiendelea

Ethiopia imeripotiwa kufunga mpaka wake na Jamhuri iliyojitangaza ya Somaliland jana baada ya siku kadhaa za mapigano yaliyoigharimu pakubwa katika maeneo ya mpakani ambayo yamezua mvutano na Hargeisa.
Mapigano hayo yamekuwa yakitokea ndani na karibu na kijiji cha Dawa’ley katika Wilaya ya Harshin nchini Ethiopia na yameripotiwa kuua zaidi ya watu 100 kulingana na ripoti za vyombo vya habari nchini humo.
Awali ilihusisha koo zinazohasimiana kutoka Ethiopia na Somaliland, lakini uingiliaji kati wa moja kwa moja wa Polisi wa Liyu – kitengo maalum cha polisi katika Mkoa wa Somalia wa Ethiopia – umeibua hisia na kukasirisha serikali ya Somaliland.
Wizara ya usalama wa ndani ya Somaliland jana ilitoa taarifa ikiwashutumu Polisi wa Liyu kwa kufanya “mauaji” dhidi ya raia na kufichua kuwa Somaliland iliwasilisha malalamishi kwa serikali ya Ethiopia.
Haya yanajiri huku kukiwa na ripoti kwamba mapigano mapya yaliyodumu kwa saa moja yalizuka tena katika eneo hilo hapo jana.
Mzozo huo unatishia kuharibu uhusiano wa karibu kati ya Ethiopia na Somaliland wakati ambapo hatima ya makubaliano muhimu ya baharini ambayo pande hizo mbili zilitia saini Januari 2024 iko mashakani.
Wanakijiji wauawa kwa mashambulio ya anga siku ya Krismasi Nigeria
Mamlaka katika jimbo la Sokoto Kaskazini-Magharibi mwa Nigeria wanasema wanachunguza shambulio la mabomu katika vijiji viwili yaliyoua takriban watu kumi siku ya Krismasi.
Ndege ya kivita iliyoripotiwa kulenga kundi jipya la wanamgambo wa Kiislamu – Lakurawa, ilisababisha moto katika jamii hizo mbili kwenye eneo la Serikali ya Mtaa ya Silame jimboni humo.
Takriban watu sita ambao walijeruhiwa vibaya bado wamelazwa hospitalini.
Wakaazi wa Gidan Sama na Rumtuwa, waliamka kwa hofu ya mashambulizi ya mabomu kutoka kwa vikosi vya ardhini na anga mnamo tarehe 25 Disemba.
Baadhi ya wanakijiji wanasema waliona jamaa zao wakiteketea kwa moto lakini hawakuwa na uwezo wa kutoa msaada wowote. Jamii zote ziko karibu na Msitu wa Surame, maficho yanayojulikana ya vikundi vya kigaidi na majambazi.
Pia Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Silame, Abubakar Muhammad aliambia BBC Hausa kuwa yeye na gavana ni miongoni mwa waliozika watu waliopoteza maisha wakati wa shambulio hilo.
“Nilipigiwa simu na kuambiwa kuna tukio la bomu kulipuka. Nilifuatilia na kuthibitisha kuwa ni kweli limefanyika. Ndege mbili zilionekana zikirusha mabomu kwenye vijiji hivyo,” alisema.
Wakati huo huo, taarifa iliyotolewa na Jeshi la Nigeria ilisema kwamba maeneo yaliyolengwa ya Gidan Sama na Rumtuwa yametambuliwa kuhusishwa na kundi la wanamgambo wa Lakurawa.
Morocco kuwapa wanawake haki zaidi

Morocco inalenga kuwapa wanawake haki zaidi ya malezi pamoja na kupinga ndoa za wake wengi, katika mapitio ya kwanza ya kanuni za familia katika kipindi cha miaka 20, mawaziri wa haki na masuala ya Kiislamu walisema Jumanne.
Wanaharakati wa kutetea haki za wanawake wamekuwa wakishinikiza kupitiwa tena kanuni zinazosimamia haki za wanawake na watoto ndani ya familia nchini Morocco, ambako Uislamu ni dini ya serikali.
Rasimu ya kanuni inapendekeza zaidi ya marekebisho 100, hasa kuruhusu wanawake kupinga ndoa za wake wengi, waziri wa sheria Abdellatif Ouahbi aliwaambia waandishi wa habari.
Pia inalenga kurahisisha taratibu za talaka, inazingatia ulezi wa mtoto kuwa ni haki ya pamoja kati ya wanandoa na inampa kila mwanandoa haki ya kuhifadhi nyumba ya ndoa endapo mwenzake atafariki, alisema.
Wanawake walioachwa wataruhusiwa uendelea kutunza mtoto baada ya kuolewa tena.
Urusi yatoa onyo juu ya “propaganda” baada ya ajali ya ndege ya Azerbaijan

Serikali ya Urusi imeonya dhidi ya kuanzisha propaganda kuhusu sababu ya ajali ya ndege ya abiria iliyokuwa ikienda Urusi na kuua watu 38 nchini Kazakhstan Jumatano.
Picha za ndege iliyoharibika zilionyesha vipande vya chuma vya ndege, na baadhi ya wataalamu wa anga walidokeza kuwa ndege ya Azerbaijan Airlines inaweza kuwa imeshambuliwa na mifumo ya ulinzi wa anga juu ya Jamhuri ya Chechnya ya Urusi.
Ndege hiyo ilielekezwa kuelekea bahari ya Caspian kutoka Chechnya hadi Kazakhstan magharibi kabla ya kudondoka karibu na jiji la Aktau nchini Kazakhstan.
Abiria 29 kati ya 67 walinusurika, na Azerbaijan ilitangaza siku ya maombolezo kwa waathiriwa wa ajali hiyo.
Rais Ilham Aliyev alisema, “Hili ni janga kubwa ambalo limesababisha huzuni kubwa kwa watu wa Azerbaijan.”
Msemaji wa Kremlin Dmitry Peskov alisisitiza, “Itakuwa makosa kueneza propaganda kabla ya hitimisho la uchunguzi. Hatutafanya hivyo, na hakuna mtu anayeweza kufanya hivyo. Tunahitaji kusubiri uchunguzi ukamilike.”
Ndege ya Embraer 190 iliondoka kutoka Baku asubuhi ya Jumatano ikielekea Grozny, lakini ilielekezwa kwa sababu ya ukungu mzito.
Abiria mmoja aliyepona alisema rubani alijaribu kutua mara mbili kabla ya mlipuko kutokea.
Ndege ilielekezwa uwanja wa ndege wa Aktau, kilomita 450 mashariki, na video inaonyesha ndege ikianguka kwa kasi kabla ya kulipuka.
Mamlaka ya Kazakhstan zimepata rekodi za data za ndege na uchunguzi unaendelea. Awali, baadhi ya ripoti zilieleza kuwa ajali ilitokana na mgongano na kundi la ndege, lakini wataalamu walieleza kuwa hili halingeweza kusababisha ndege kutoka nje ya njia.
All Rights Reserved © Cantona Group PLC||2024
Discover more from cantonadigital
Subscribe to get the latest posts sent to your email.