Radio Fortune Africa -Na Cantona Joseph
https://zeno.fm/radio/radio-fortune-africa
Karibu katika Matangazo yetu ya jioni moja kwa moja kutoka Communication Center. Tumekuandalia mengi ikiwa ni pamoja
Muhtasari
- Israel yashambulia maeneo ‘yanayoshukiwa’ ya silaha za kemikali nchini Syria
- Syria Hakuna ushahidi wa maeneo ya chini ya ardhi katika gereza la Saydnaya- Shirika la haki za binadamu
- Mwisho wa utawala wa Assad ‘unaleta matumaini mengi’
- Jay-Z ashtakiwa na Diddy katika kesi ya kumbaka msichana, mwenye umri wa miaka 13, mwaka 2000
- Korea Kusini yaamuru marufuku ya kusafiri iwekwe dhidi ya Rais Yoon
- Mzozo wa Syria: Wasyria wanakimbilia katika gereza maarufu la Saydnaya kutafuta jamaa
- Wasyria wanarejea nyumbani kutoka Jordan na Lebanon
- Israel yaliteka eneo la amani la Milima ya Golan baada ya wanajeshi wa Syria kuondoka katika maeneo yao
- ‘Hatukuombwa msaada na Assad’ – Iran
- Ni wachache waliomlilia Assad baada ya utawala wake kuangushwa
- Assad yuko Moscow baada ya kutoroka Syria na atapewa hifadhi, vyombo vya habari vya serikali ya Urusi vimeripoti
- Ni wachache waliomlilia Assad baada ya utawala wake kuangushwa
- Marekani haitaruhusu IS kutumia fursa ya ukosefu wa madaraka nchini Syria, asema Biden
Naam,Natumai U buheri wa afya popote pale ulipo duniani kwa mwoyo mkunjufu na mikono miwili Hujambo na karibu katika matangazo yetu Afrika Leo Jioni ya moja kwa moja ikiwa ni tarehe 09/12/2024 Jina langu ni Cantona Joseph,
Uingereza yamuwekea vikwazo Mkenya anayedaiwa kusafirisha dhahabu kwa magendo

Serikali ya Uingereza leo imetangaza kumuwekea vikwazo vya kifedha mfanyabiashara wa Kenya na anayedaiwa kusafirisha dhahabu kwa njia ya magendo, anayehusishwa na mojawapo ya kashfa kubwa zaidi za ufisadi katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki.
Maafisa wa Uingereza walisema watazuia mali ya Kamlesh Pattni na wengine wanne wanaoaminika kuwa sehemu ya mzunguko wake, akiwemo mkewe na shemeji yake.
Katika taarifa yake, Ofisi ya Mambo ya Nje, Jumuiya ya Madola na Maendeleo ya Uingereza ilisema vikwazo hivyo vinalenga kuvuruga shughuli za kibiashara za Pattni, ambaye ilimtuhumu kwa kusafirisha dhahabu iliyoibwa kutoka kusini mwa Afrika.
Taarifa hiyo ilisema: “Uingereza pia imeweka vikwazo zaidi ili kukabiliana na pesa chafu, wakati huu ikilenga biashara haramu ya dhahabu.
Dhahabu haramu ni shambulio dhidi ya biashara halali ya bidhaa yenye thamani kubwa, kuchochea ufisadi, kudhoofisha utawala wa sheria na kuingiza ukiukwaji wa haki za binadamu kama vile ajira ya watoto.
Urusi inatumia biashara haramu ya dhahabu kutakatisha fedha na kukwepa vikwazo, kwa kufanya hivyo kuimarisha juhudi za vita za Putin.
“Vikwazo vya leo vitavuruga na kuzuia biashara haramu ya dhahabu kwa kuweka vikwazo vya mali kwa watu watano, akiwemo mlanguzi wa dhahabu kutoka Uingereza na Kenya Kamlesh Pattni na wawezeshaji wake.
Pattni anasafirisha dhahabu haramu kutoka kusini mwa Afrika kwa matumizi ya ufujaji wa fedha na alihusishwa na Kashfa ya ufisadi ya Goldenberg katika miaka ya 1990.”
Pattni alitajwa kuwa mmoja wa wasanifu wakuu wa kashfa ya Goldenberg, ulaghai mkubwa wa dhahabu na sarafu katika miaka ya 1990 ambao ulihusisha viongozi wakuu wa serikali ya Kenya na inaaminika kuigharimu nchi hiyo takribani $600m.
Alikabiliwa na kesi mwaka wa 2006 kwa madai ya jukumu lake katika mpango huo lakini kesi zilisambaratika.
Tangu wakati huo amekabiliwa na madai ya kuhusika katika biashara haramu ya dhahabu nchini Zimbabwe.
Tangazo la Uingereza la vikwazo leo linakuja wakati Ofisi ya Mambo ya Nje ikithibitisha maelezo ya mpango mpya wa kusaidia kukabiliana na ufisadi duniani.
Israel yashambulia maeneo ‘yanayoshukiwa’ ya silaha za kemikali nchini Syria

Waziri wa Mambo ya Nje wa Israel Gideon Saar amethibitisha kuwa Israel ilishambulia maeneo yanayoshukiwa kuwa ya hifadhi ya silaha za kemikali na makombora nchini Syria akisema hatua hiyo ilikuwa ni kuzuia kuangukia mikononi mwa makundi yenye itikadi kali.
“Nia pekee tuliyo nayo ni usalama wa Israeli na raia wake,” aliwaambia waandishi wa habari.
Ripoti za vyombo vya habari zinaonesha kuwa kumekuwa na mashambulizi kadhaa ya anga ya Israel katika siku moja hivi iliyopita, ikiwa ni pamoja na kwenye eneo la Damascus inayosemekana kutumiwa kutengeneza roketi na wanasayansi wa Iran.
Jeshi la Israel limetoa picha zinazowaonesha wanajeshi wa Israel waliovuka eneo la milima ya Golan linalokaliwa na Israel na kuingia katika eneo lisilo na ulinzi wa kijeshi.
Saar alikariri kuwa jeshi la Israel limeingia katika eneo linaloshikiliwa na Syria kama hatua ya muda ya kujihami ili kuzuia mashambulizi ya kuvuka mpaka. Alisema “itazuia hali ya Oktoba 7 kutoka Syria”.
Hakuna ushahidi wa maeneo ya chini ya ardhi katika gereza la Saydnaya- Shirika la haki za binadamu

Picha za video zimekuwa zikisambazwa kuhusu wafungwa wakitoka katika gereza la Saydnaya, ambapo inakadiriwa kuwa zaidi ya wafungwa 30,000 walinyongwa au walikufa kati ya 2011 na 2018.
Kumekuwa na ripoti kuwa ndani ya gereza hilo, baadhi ya watu walinaswa au kufichwa katika maeneo ya siri ya chini, lakini kundi moja la misaada ya kibinadamu linasema kuwa halijapata ushahidi wowote wa hili hadi sasa.
“Hadi sasa, timu zetu zilizofika katika gereza la Saydnaya hazijapata mlango wowote wa siri unaozungumzwa,” taarifa imeeleza.
Ikielezea utendakazi wake, inaongeza: “Timu zinatumia uchunguzi wa sauti na vifaa vya utafutaji pamoja na timu za mbwa zilizo na mbwa waliofunzwa.”
Shirika la The White Helmets linasema kwamba timu zake pia zinaongozwa na watu “wanaojua maeneo ya kuingilia ya gereza na njia za siri” na kuongeza kuwa upekuzi utaendelea “mpaka tutambue sehemu zake zote kwa usahihi”.
Mwisho wa utawala wa Assad ‘unaleta matumaini mengi’

Kupinduliwa kwa utawala wa Assad “kunaleta matumaini makubwa”, anasema Msyria mmoja ambaye alikamatwa na kuteswa chini ya utawala wa Assad.
Qutaiba Idlbi, mjumbe mkuu katika taasisi ya kimataifa ya masuala ya kimataifa ya Baraza la Atlantiki, anaiambia BBC Newsday kwamba hatimaye “inafunga sura ya takribani miaka 13 ya vita vya wenyewe kwa wenyewe”.
Anasema ana “matumaini ya siku zijazo”. “Watu wengi wanaweka kando mawazo yoyote ya kulipiza kisasi … na kwa kweli wanatafuta kile kitakachofuata”.
Moja ya wasiwasi wake mkuu, Idlbi anaongeza, ni kama jumuiya ya kimataifa itaweza kusaidia kwa mafanikio kuleta makundi mbalimbali pamoja, na kuchukua fursa hii “mara moja katika maisha” kwa ajili ya mpito wa kisiasa nchini Syria.
Bendera ya waasi wa Syria yapandishwa juu ya ubalozi Moscow
Bendera ya makundi ya waasi wa Syria imewekwa katika ubalozi wa Moscow na wanachama wa raia wa Syria nwalio nje ya nchi.
Hatua hiyo ni ya kiishara kwani Urusi imekuwa mshirika mkubwa wa utawala wa Assad na kumuunga mkono rais wa nchi hiyo Bashar al-Assad wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa miaka 13 nchini humo.
Na, kama tulivyoripoti hivi punde, Kremlin imethibitisha kwamba Rais Putin aliamua binafsi kumpa Assad na familia yake hifadhi nchini Urusi.


Jay-Z ashtakiwa na Diddy katika kesi ya kumbaka msichana, mwenye umri wa miaka 13, mwaka 2000

Rapa wa Marekani Jay-Z amejibu kuhusu kesi inayodai kuwa yeye, pamoja na Sean “Diddy” Combs, walimnywesha dawa za kulevya na kumbaka msichana wa miaka 13 kwenye sherehe mwaka 2000.
Mtu ambaye alimshtaki ambaye jina lake halikujulikana anadai alivamiwa kwenye sherehe ya nyumbani baada ya Tuzo za Muziki za Video za MTV (VMAs) huko New York na kwamba mtu mashuhuri wa kike ambaye hakutajwa jina alikuwa kwenye chumba hicho wakati huo.
Katika taarifa yake, Jay-Z, ambaye jina lake halisi ni Shawn Carter, alipuuza hatua hiyo ya kisheria na kusema ni “jaribio la ulaghai”.
Bw Combs, ambaye yuko jela akisubiri kesi yake baada ya kushtakiwa mwezi Septemba kwa biashara ya ngono na makosa mengine, alikanusha shtaka la hivi punde.
Kesi hiyo iliwasilishwa mwezi Oktoba, na iliwasilishwa tena Jumapili ili kuorodhesha Bw Carter kama mshtakiwa.
BBC imewasiliana na wakili wa Bw Carter, Alex Spiro, na mtangazaji wake kwa maoni.
Hatua hiyo ya kisheria iliwasilishwa chini ya sheria ya ulinzi ya waathiriwa wa unyanyasaji wa kijinsia ya New York, na wakili wa Texas, Tony Buzbee.
Bw Buzbee amewasilisha kesi kadhaa katika miezi ya hivi karibuni akimtuhumu Bw Combs kwa shambulio na ubakaji. Msanii huyo wa hip-hop anatarajiwa kukabiliwa na kesi ya jinai tarehe 5 Mei.
Korea Kusini yaamuru marufuku ya kusafiri iwekwe dhidi ya Rais Yoon

Mwendesha mashtaka mkuu wa ofisi ya uchunguzi wa ufisadi ya Korea Kusini ameamuru marufuku ya kusafiri iwekwe kwa Rais Yoon Suk Yeol, ambaye kwa sasa anachunguzwa kutokana na tamko lake la kushtua la sheria ya kijeshi wiki iliyopita.
Marufuku ya kusafiri pia imewekwa dhidi ya maafisa kadhaa wakuu katika utawala wa Yoon.
Maelfu ya watu walijitokeza kupinga amri hiyo ya muda mfupi ya sheria ya kijeshi, wakitaka Yoon ajiuzulu au kushtakiwa.
Lakini kura ya kumshtaki Yoon haikupigwa siku ya Jumamosi , na chama tawala cha People Power Party (PPP) kilisema badala yake kiongozi wa chama chake na waziri mkuu wangeendesha nchi hadi rais “atakapoondoka kwa utaratibu”.
Katika hotuba ya hadhara siku ya Jumapili, kiongozi wa PPP Han Dong-hoon alisema Yoon hatajihusisha tena na masuala ya kigeni na ya ndani hadi ajiuzulu na kuongeza kuwa Waziri Mkuu Han Duck-soo atasimamia masuala ya serikali wakati huo huo.
“Rais hatahusika katika masuala yoyote ya serikali ikiwa ni pamoja na ya kidiplomasia kabla ya kuondoka,” alisema kiongozi wa chama Han.
Hatahivyo, kiongozi wa ngazi ya chama cha Democratic Park Chan-dae alielezea mpango uliopendekezwa kama “uasi wa pili usio halali, kinyume na katiba na mapinduzi ya pili”.
Mwakilishi Kim Min-seok wa chama cha kidemokrasia vile vile alikosoa mpango huo, akisema “hakuna mtu aliyempa” kiongozi wa PPP Han mamlaka ya kufanya maamuzi kama hayo.
Mzozo wa Syria: Wasyria wakimbilia katika gereza maarufu la Saydnaya kutafuta jamaa

Kundi la ulinzi wa raia wa Syria linalojulikana kwa jina la White Helmets linasema kuwa linachunguza ripoti kutoka kwa manusura wa gereza maarufu la Saydnaya nchini humo kwamba watu wanazuiliwa katika seli zilizofichwa chini ya ardhi.
Saydnaya ni mojawapo ya magereza yaliyokombolewa huku waasi wakichukua udhibiti wa nchi.
Hapo awali, wapiganaji wa waasi walivamia jela hiyo na kuwaachilia baadhi ya wafungwa. Gereza hilo lilikuwa limetumika kuhifadhi maelfu ya watu, wakiwemo wafungwa wa kisiasa na raia.
Shirika linafuatilia vita vya Syria makao yake makuu nchini Uingereza, Shirika la Uangalizi wa Haki za Kibinadamu la Syria (SOHR), linaamini kuwa maelfu ya watu wamefariki katika gereza hilo kutokana na mateso, mateso na kunyongwa kwa wingi.
Juhudi zinaendelea kujaribu na kufikia “zaidi ya wafungwa 100,000 ambao wanaweza kuonekana kwenye viteo za CCTV”.
Wasyria wanarejea nyumbani kutoka Jordan na Lebanon

Picha za mapema Jumapili zilionyesha Wasyria huko Lebanon na Jordan wakiingia Syria, saa chache baada ya kuangushwa kwa Rais Bashar al-Assad.
Katika mpaka wa Lebanon na Syria, mwandishi wa shirika la habari la AFP aliyaona makumi ya magari yakiwa kwenye kivuko kikuu cha Masnaa, huku umati wa watu ukishangilia na kuimba nyimbo za kumpinga Assad.
Katika kivuko cha Jaber kutoka Jordan, mwanamume mmoja aliiambia Reuters: “Nimekuwa Jordan kwa miaka 12. Tuliposikia habari kwamba Bashar al-Assad alianguka, tulijisikia vizuri zaidi kihisia. Tunaweza kurudi nchini kwetu kwa usalama na usalama. “
Israel yaliteka eneo la amani la Milima ya Golan baada ya wanajeshi wa Syria kuondoka katika maeneo yao

Waziri Mkuu wa Israel ametangaza kuwa jeshi lake limetwaa udhibiti wa eneo lisilo na wanajeshi katika eneo la Milima ya Golan (Golan Heights), akisema makubaliano ya mwaka 1974 ya kujitenga na Syria “yaliporomoka” baada ya waasi kuiteka nchi hiyo.
Benjamin Netanyahu amesema ameliamuru jeshi la ulinzi la Israeli (IDF) kuingia eneo la lisilo na mapigano baina ya nchi hizo mbili na “kuamuru kuchukuliwa kwa udhibiti” wa eneo linalokaliwa na Israeli la Milima ya Golan.
“Hatutaruhusu nguvu yoyote ya uadui kujiimarisha kwenye mpaka wetu,” alisema.
Mchanganuzi wa vita mwenye makao yake makuu nchini Uingereza alisema kuwa wanajeshi wa Syria wameondoka katika maeneo yao katika mkoa wa Quneitra, ambao sehemu yake iko ndani ya eneo lililotengwa lisilo na mapigano, siku ya Jumamosi.
Siku ya Jumapili, IDF iliwaambia wakaazi wa vijiji vitano vya Syria ndani ya eneo hilo kubaki majumbani mwao hadi ilani nyingine itakapotolewa.
Milima ya Golan ni ukanda wa miamba likiwa na ukubwa wa takriban kilomita 60 (maili 40) kusini-magharibi mwa Damascus.
Israel ililiteka eneo la Golan kutoka Syria katika hatua za mwisho za Vita vya siku iita vya 1967 na kuchukua sehemu yake mwaka 1981. Hatua hiyo haikutambuliwa kimataifa, ingawa Marekani ilifanya hivyo kwa upande mmoja mwaka 2019.
Hatua ya Israel katika eneo hilo inakuja baada ya wapiganaji wa waasi wa Syria kuuteka mji mkuu Damascus na kuuangusha utawala wa Bashar al-Assad. Yeye na baba yake walikuwa madarakani nchini humo tangu 1971.
‘Hatukuombwa msaada na Assad’ – Iran

Mapema Jumapili, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas Araghchi aliviambia vyombo vya habari vya ndani kuwa Iran – mshirika wa Rais wa zamani Assad – haikuombwa kuingilia kati wakati waasi walipokuwa wakielekea kuiteka Damascus.
“Hatukuwahi kuombwa msaada, jukumu lilikuwa ni la jeshi la [Syria] kimsingi, hatukuona kama jukumu letu sisi wenyewe,” alisema.
“Kilichoshangaza ni kushindwa kwa jeshi la Syria kukabiliana na uvamizi huu,” aliongeza.
Assad yuko Moscow baada ya kutoroka Syria na atapewa hifadhi, vyombo vya habari vya serikali ya Urusi vimeripoti

Rais wa Syria aliyeondolewa madarakani Bashar al-Assad na familia yake wamewasili Moscow, vyombo vya habari vya serikali ya Urusi vimeripoti, vikinukuu vyanzo vya habari katika ikulu ya Kremlin.
Ripoti zinasema kuwa Assad na familia yake wamepewa hifadhi na Urusi.
BBC haijaweza kuthibitisha taarifa hizo kwa uhuru.
Ni silaha kali za Urusi zilizosaidia kumuweka Bashar al-Assad madarakani kwa miaka tisa iliyopita.
Lakini, katika siku chache, mradi wa Kremlin wa Syria haujakamilika, na Moscow, inaonekana, haina nguvu ya kufanya chochote kuhusu hilo.
Kuanguka kwa utawala wa Assad ni pigo kwa heshima ya Urusi.
Kuwatuma maelfu ya wanajeshi wake kumuunga mkono Rais Assad mwaka 2015, lilikuwa ni moja ya malengo muhimu ya Urusi ya kujitangaza kama taifa lenye nguvu duniani.
Urusi yaomba mkutano wa Jumatatu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa
Wakati huo huo, Urusi imeomba mkutano wa dharura wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ili kujadili hali nchini Syria, kwa mujibu wa mmoja wa wawakilishi wake.
Dmitry Polyanskiy, ambaye ni naibu mwakilishi wa kwanza wa kudumu wa Urusi katika Umoja wa Mataifa, ameandika wenye Telegram kwamba anatarajia mkutano huo utafanyika Jumatatu.
Shirika la habari la AFP limenukuu duru za kidiplomasia zikisema kuwa mkutano utafanyika wakati huo.
Ni wachache waliomlilia Assad baada ya utawala wake kuangushwa

Kumekuwa na hali ya ‘machozi machache’ kufuatia kuanguka kwa utawala wa Assad.
Rais Macron wa Ufaransa alisema taifa katili limesambaratika.
Kansela Scholz wa Ujerumani alisema watu wa Syria wameteseka sana na mwisho wa Assad ulikuwa habari njema. Lakini wengi wanahangaika kuhusu nini kitakachofuata.
Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa nchini Syria, Geir Pedersen, alisema ni wakati wa “matumaini ya tahadhari” tu na alisisitiza haja ya mabadiliko ya utulivu.
Nchi za Kiarabu katika Ghuba ambazo zilirekebisha uhusiano na Assad katika miaka ya hivi karibuni zinasema zinatazama kwa uoga matarajio ya Syria inayoongozwa na Waislam.
Wizara ya mambo ya nje ya Qatar ilisema ina “wasiwasi mkubwa” na kutaka umoja wa Syria ulindwe.
Mwanadiplomasia mwandamizi wa Imarati, Anwar Gargash, aliliambia gazeti la Syria Manama Dialogue Syria “haijatoka msituni” na anatumai vikundi tofauti huko vinaweza kufanya kazi pamoja.
Marekani ina vikosi vya kijeshi mashariki mwa Syria na afisa mkuu wa Pentagon alisema watasalia huko ili kupambana na kundi la Islamic State ambalo, alikiri, linaweza kutumia machafuko hayo kuongeza operesheni zake.
Uturuki inawahifadhi zaidi ya wakimbizi milioni tatu wa Syria na waziri wa mambo ya nje wa nchi hiyo, Hakan Fidan, alisema sasa wanaweza kurejea nyumbani.
Pia amesema Uturuki itaendelea kupambana na makundi ya Wakurdi nchini Syria ambayo nchi yake inayataja kuwa ni magaidi.
Kuhusu washirika wa Assad, Urusi na Iran, mkuu wa mashauri ya kigeni wa Umoja wa Ulaya, Kaja Kallas, alisema mataifa yote mawili ni dhaifu. Wizara ya mambo ya nje ya Urusi imesema vituo vyake viwili vya kijeshi nchini Syria viko katika hali ya tahadhari lakini hakuna tisho kubwa.
Rais mteule Donald Trump alisema kuanguka kwa Assad kulimaanisha kuwa Rais Putin anafaa kukubaliana na usitishaji mapigano mara moja nchini Ukraine.
Iran – ambayo imepoteza kiungo chake cha eneo na Hezbollah nchini Lebanon – ilisema, bila kejeli, watu wa Syria wanapaswa kuamua mustakabali wao “bila kuingiliwa kwa uharibifu au kulazimishwa na mataifa ya nje”.
Marekani haitaruhusu IS kutumia fursa ya ukosefu wa madaraka nchini Syria, asema Biden

Mtazamo wa Marekani kwa Syria “umebadili uwiano wa mamlaka katika Mashariki ya Kati”, Rais Biden alisema Jumapili.
Akizungumza kutoka chumba cha Roosevelt, Biden alielezea njia tatu za mgogoro – “msaada kwa washirika wetu, vikwazo na diplomasia, na kulenga nguvu za kijeshi wakati itakapohitajika”, alisema, akimaanisha kuendelea kuwepo kwa jeshi la Marekani nchini Syria.
“Macho yetu yako wazi kuhusu ukweli kwamba ISIS [kundi la Islamic State – IS] litajaribu kutumia fursa yoyote ya ukosefu wa mamlaka ili kurejesha uwezo wake na kuunda mahali pake salama. Hatutaruhusu hilo kutokea,” Biden alisema.
Siku ya Jumapili, kituo cha Marekani cha utoaji wa amri za kijeshi cha kilithibitisha kuwa walifanya operesheni iliyolenga zaidi ya malengo 75.
Maeneo yaliyolengwa yalikuwa katika jangwa la Badiyah mashariki mwa Syria, ambako wanamgambo wa IS wanaaminiwa kujikusanya upya, alisema afisa mwandamizi wa utawala wa kituo hicho.
Je, Uturuki na Urusi zinaushughulikiaje mgogoro wa Syria, na tofauti zao ni zipi?

6 Disemba 2024
Pamoja na mashambulizi ya hivi karibuni nchini Syria ambayo yamesababisha hasara kubwa kwa utawala wa Assad, macho yote yamegeukia tena harakati za kidiplomasia kati ya Ankara na Moscow.
Nchi hizo mbili, ambazo zilikuwa na jukumu muhimu katika kila kipindi cha vita vya wenyewe kwa wenyewe vya Syria vilivyoanza mwaka 2011, ziko katika nafasi zinazopingana katika mgogoro wa hivi karibuni na kushikilia sera za kila mmoja kuwajibika na kuongezeka kwa mvutano.
Mkutano kati ya rais wa Urusi Vladimir Putin na Rais Recep Tayyip Erdoğan tarehe 3 Disemba ulikuwa muhimu katika suala la kufunua mitazamo ya pande zote.
Putin alimtaka Erdogan kuachana na makundi ya kigaidi yanayoshambulia utawala wa Assad.
Erdogan, kwa upande mwingine, anamtarajia Putin aihimize Damascus zaidi kupata suluhu la kisiasa.
Hali ya utulivu katika vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Syria tangu mwaka 2020 ilivurugika kufuatia mashambulizi yaliyoanzishwa na makundi yanayoongozwa na Hayat Tahrir al-Sham (HTS) dhidi ya vikosi vya serikali, hatua ambayo imeanzisha enzi mpya ya vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Wakati HTS iliuteka mji wa Aleppo kwa muda mfupi, jeshi la taifa la Syria linaloungwa mkono na Uturuki (SNA) lilichukua hatua dhidi ya uwepo wa vikosi vya ulinzi wa watu (YPG) huko Tel Rifaat na Manbij.
Uhasama huo kati ya Ankara na Moscow, ambazo zina uwepo mkubwa wa kijeshi na ushawishi wa kisiasa katika eneo hilo, umewahusisha tena katika mzozo huo.

Waasi wakishambulia vikosi vya Assad viungani mwa mji wa Hama.
Mawasiliano ya kwanza kati ya nchi hizo mbili yalifanyika kati ya mawaziri wa mambo ya nje Hakan Fidan na Sergey Lavrov mnamo Novemba 30.
Mkutano wa viongozi hao ulifanyika Desemba 3.
Taarifa zilizoandikwa baada ya mkutano wa Erdoğan na Putin zilikuwa muhimu katika kufichua tathmini na matarajio tofauti ya vyama kuhusu mchakato huo.
Ankara: Serikali inapaswa kuzungumza na upinzani
Taarifa iliyotolewa na Uturuki, ilielezwa kwamba Ankara inaunga mkono uadilifu wa eneo la Syria lakini “utawala wa Syria lazima ushiriki katika mchakato wa kupata suluhisho la kisiasa” ili kuwezesha suluhu la kudumu na la haki.
Umoja wa Mataifa ulizindua mchakato wa Geneva, uliowezesha kuwaleta pamoja watawala na upinzani nchini Syria ili kupata suluhisho la kisiasa kwa mujibu wa azimio la Baraza la Usalama nambari 2254, lakini hawakuweza kupigia hatua kutokana na kizuizi cha utawala wa Damascus.
Uturuki na nchi nyingine za Magharibi zinawatuhumu washirika wa Urusi na Iran kwa kutoishinikiza serikali ya Assad au hata kutafuta suluhisho la kisiasa.
Ankara pia inaishutumu Moscow na Tehran kwa kutounga mkono juhudi za muda mrefu za Uturuki za kurejesha uhusiano na Syria.

Katika taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Rais, ilibainika kuwa Erdoğan alifikisha ujumbe kwa Putin kwamba “suala muhimu zaidi katika muktadha wa hali ya hivi karibuni nchini Syria ni kwamba raia hawadhuriwi.”
Inadhaniwa kuwa Erdogan alikuwa akizungumzia mashambulizi yaliyofanywa na Urusi na Syria katika mkoa wa Idlib katika wiki za hivi karibuni alipotoa kauli hizi.
Vyanzo vya usalama mjini Ankara vinasema kuwa HTS na makundi mengine ya upinzani yalianzisha operesheni ya sasa kujibu mashambulizi ya hivi karibuni.
Kremlin: Uvamizi wa ‘kigaidi’ lazima ukome
Kauli ya Kremlin kuhusu mkutano kati ya viongozi hao wawili ilikuwa na lugha tofauti.
Ilibainika kuwa Putin alifikisha ujumbe kwa Erdogan kwamba “uvamizi wa kigaidi” ulioanzishwa dhidi ya serikali ya Syria lazima usimame mara moja na utawala lazima uungwe mkono ili kuanzisha utaratibu wa kikatiba na utulivu nchini kote.
Taarifa hiyo ilisema Putin alielezea matarajio yake kwamba Ankara itatumia ushawishi wake katika eneo hilo kufikia malengo hayo.

Msemaji wa wizara ya mambo ya Nje ya Urusi Maria Zakharova pia alisema katika mkutano na waandishi wa habari mnamo tarehe 4 Disemba kwamba Urusi inaunga mkono kwa nguvu zote vita vya uongozi wa Syria dhidi ya “makundi ya kigaidi.”
Zakharova alidai kuwa makundi ya upinzani yalipokea ndege zisizo na rubani na msaada wa mafunzo kutoka kwa mataifa ya kigeni.
Licha ya tathmini tofauti, msisitizo wa kawaida wa Ankara na Moscow ulikuwa kuendelea na uratibu na diplomasia kati ya washirika wa mchakato wa Astana na ushiriki wa Tehran.
Mawaziri wa mambo ya nje wa nchi hizo tatu wanatarajiwa kukutana pembezoni mwa mkutano wa Doha nchini Qatar tarehe 7 na 8 Disemba, lakini mkutano huo bado haujathibitishwa.
Ni majanga gani yaliyotokea katika siku za nyuma?
Uturuki na Urusi wameendeleza uhusiano wa kiuchumi na nishati tangu mwanzoni mwa miaka ya 2000.
Hatahivyo, katika miaka 10 iliyopita, wameingia katika mgogoro mara nyingi kutokana na matatizo ya kijiografia, hasa yale yanayotokana na Syria.
Uturuki imeyaunga mkono makundi ya upinzani dhidi ya utawala wa Assad katika vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Syria.
Urusi, kwa upande mwingine, imeelekeza uzito wake wa kijeshi kwenye eneo la Syria tangu mwaka 2015 na kuzuia kupinduliwa kwa serikali ya Damascus.
Tarehe 24 Novemba , 2015, Uturuki ilidungua ndege ya kivita ya Urusi kwa misingi kwamba ilikiuka anga ya Uturuki jambo lililosababisha mgogoro usio wa kawaida kati ya Ankara na Moscow.
Mgogoro huo ulisitishwa mnamo mwezi Juni 2016 kutokana na mazungumzo ya siri ya diplomasia kati ya vyama.
Hata hivyo, mauaji ya balozi wa Urusi nchini Uturuki Andrey Karlov mjini Ankara katika siku za mwisho za mwaka huo huo yalirudisha umakini kwa nchi hizo mbili.
Mchakato wa Astana ulianzaje?
Uturuki na Urusi wameshiriki katika ushirikiano mkubwa ili kupunguza ghasia na vifo vya raia nchini Syria baada ya kipindi cha mvutano.
Walichukua hatua ya kwanza katika mchakato huu mwishoni mwa mwaka 2016, wakati wa kuzingirwa kwa serikali ya Aleppo, wakati wa mchakato wa kuanzisha ukanda salama kwa ajili ya kuwahamisha wapinzani na raia kutoka mji huo.
Mchakato huu baadaye ulibadilishwa jina na kuwa mchakato wa Astana mwaka 2017, ukishirikisha Iran.
Ulinzi wa pamoja wa doria kati ya Uturuki na Urusi iliyofanyika Idlib mwaka 2020.
Mbali na mikutano iliyofanyika katika mji mkuu wa Kazakhistan wa Astana, viongozi wa nchi hizo tatu waliandaa mikutano ya kupokezana na walitaka kuratibu maendeleo ya kisiasa na kijeshi kuhusu Syria.
Hatahivyo, jaribio la Urusi la kuivamia Ukraine mnamo mwezi Februari, 2022 lilisababisha Syria kunaswa zaidi katika ajenda ya Moscow.
Makubaliano ya Idlib
Hali nyingine iliyoileta Uturuki na Urusi katika mgogoro mkubwa ile iliyoukumba mkoa wa Idlib kaskazini magharibi mwa Syria.
Kutokana na makubaliano yaliyofikiwa mwaka 2016, maeneo manne ya kupunguza mapigano yalitangazwa nchini Syria, lakini kutokana na mashambulizi ya Urusi na Syria, mikoa mitatu ilitekwa na makundi ya upinzani katika maeneo hayo yalielekezwa Idlib.
Miongoni mwa makundi hayo ni mashirika kama vile HTS na Al Nusra, ambayo yalitangaza kuwa yamejitenga na al-Qaeda.
Ingawa Uturuki na Urusi walikubaliana kuanzisha eneo salama lisilo na silaha huko Idlib mwaka 2018, mashambulizi ya utawala wa Damascus katika eneo hili hayakutoa matokeo yaliyohitajika.
Kifo cha wanajeshi 34 wa Uturuki kilichotokana na shambulio la anga yaliyofanywa na jeshi la anga la Urusi katika eneo hilo mwezi Februari 2020, ambayo yaliupiga msafara wa kijeshi wa Uturuki, lilisababisha mvutano mpya katika eneo hilo.
Kufuatia mvutano huu, Erdogan na Putin walikutana tena na kutangaza makubaliano mapya halali kuanzia Machi 6, 2020.
Hali ya kutokuwa na mzozo, ambayo ilifikiwa na makubaliano kwamba vikosi vya Uturuki na Urusi vitaanzisha doria za pamoja katika njia salama ambazo wangeanzisha, iliendelea hadi tarehe 27, Novemba 2024.
Raila atakavyoamua mshindi wa urais 2027

Kiongozi wa ODM Raila Odinga anayewania kiti cha AUC. Picha|Maktaba
KIONGOZI wa chama cha Orange Democratic Movement (ODM) Raila Odinga huenda akatekeleza wajibu wa kuamua mshindi wa urais katika uchaguzi mkuu wa 2027, mmoja wa maafisa wakuu wa chama hicho amedokeza.
Naibu Kiongozi wa ODM Godfrey Osotsi, kwenye mahojiano ya kipekee na Taifa Leo, amefichua kuwa azma ya Odinga ya uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC) haitabadili hadhi yake kama kiongozi wa ODM na hata mwaniaji wake wa urais.
Lakini Bw Osotsi, ambaye ni Seneta wa Vihiga aliongeza kuwa Bw Odinga anaweza kuketi “kando ya uwanja na kutekeleza wajibu wa kocha” katika uchaguzi mkuu wa 2027.
Anaeleza kuwa Waziri huyo Mkuu wa zamani anaweza kurejelea nafasi yake ya mnamo 2002, alipotamka “Kibaki Tosha” na kumwezesha Hayati Mwai Kibaki kuibuka mshindi. Ushindi huo ulitamatisha utawala wa miaka 40 ya chama cha Kenya African National Union (Kanu).
“Wafaa kujua kuwa Raila akiwa kocha yeye ni hatari zaidi kuliko wakati ambapo yeye ni mchezaji. Uliona 2002 aliposema Kibaki Tosha na kujitwika wajibu wa kocha na ukaona jinsi alishinda uchaguzi kwa kishindo.
“Kwa hivyo nataka kuwaambia wanachama wetu kote nchini kwamba kiongozi wetu wa chama akiwa mwenyekiti wa AUC atakuwa na manufaa makubwa kwa chama kuliko vile watu wengine wanasema kwani atakuwa ataitumia nafasi hiyo kuifaidi ODM hata zaidi,” Bw Osotsi akasema.
Wandani wa Bw Odinga wanaoshikilia nyadhifa za uwaziri katika serikali ya Rais Ruto wamejitokeza katika watetezi sugu wa serikali ya Rais Ruto. Baadhi yao hata wamedokeza kuwa wataunga mkono juhudi zake za kutaka kuhifadhi kiti chake katika uchaguzi mkuu wa 2027.
Na wiki jana, kaimu kiongozi wa ODM Profesa Anyang Nyong’o alisema kuwa ingawa chama hicho hakitaki kuonekana kuwa duni au kuendeleza masilahi ya vyama vingine vya kisiasa anaelewa hitaji la chama hicho kubuni ushirikiano wa “kimkakati” na vyama vingine.
Profesa Nyong’o ambaye ni Gavana wa Kisumu alionekana kuashiria uwezekano wa ODM kuweka mkataba wa ushirikiano na chama cha United Democratic Alliance (UDA) chake Rais William Ruto.
“Kama chama cha kisiasa, tunaeleza manufaa ya kuingia katika ushirikiano na vyama vingine. Nyakati fulani tunaweza kuamua kubuni miungano na vyama vingine au makundi yenye malengo na maono sawa nasi kuhusu namna ya kuendesha Kenya,”
Profesa Nyong’o akaongeza hivi: “Miungano au ushirikiano aina hii sio vitendo vya kutumikia vyama vingine lakini juhudi za kimakusudi za kufikia lengo letu la kimsingi wa kutwaa mamlaka ya kisiasa ili kubadilisha maisha ya Wakenya.
Kauli ya kaimu huyo wa kiongozi wa ODM inaonekana kuhimili kaunti za Bw Osotsi.
Knut yaitaka TSC iajiri washauri kuzuia visa vya walimu kujitia kitanzi

Mwanamume aliyezongwa na mawazo anayewazia kujitia kitanzi. Picha|Hisani
CHAMA cha walimu (KNUT) kinataka Tume ya Kuajiri Walimu (TSC) iajiri washauri nasaha kushughulikia visa vya kujitia kitanzi na matumizi mabaya dawa za kulevya kwa walimu.
TSC inasema walimu wengi wanahangaishwa na magonjwa ya akili, hali ambayo imeathiri utendakazi wao na kusambaratisha familia zao.
Mwakilishi wa Kike wa Kwanza wa Kitaifa Mercy Ndung’u amesema maelfu ya walimu wanaumia lakini wao huwa wananyamaza tu.
“Walimu wanahitaji huduma za ushauri popote walimu nchini. Ni huduma ya lazima ambayo inafaa kutolewa na wizara na mwaajiri ili kuokoa maisha,” Bi Ndung’u akasema katika hafla ya kuadhimisha siku 16 ya kukabili dhuluma za kijinsia mjini Bomet mwisho wa juma.
“Baadhi ya changamoto za walimu huwasababisha kujihusisha na utumizi mbaya wa dawa za kulevya ili waepuke hali halisi ya maisha. Ni suala ambalo linafaa kuangaziwa na washikadau wote wa elimu nchini,” akaongeza.
Kauli yake ilikaririwa na mwanachama wa Baraza Kuu la Utendaji (NEC) Alice Bor, Katibu Mtendaji wa KNUT tawi la Bomet Desmond Langat, naibu wake Jeff Bett na mwakilishi mwanamke wa KNUT tawi la Bomet Betty Langat.
“Baadhi ya walimu wamejiua sababu ya msongo wa mawazo, wengine wametelekeza wajibu huku baadhi wakianza uraibu wa pombe baada ya kukosa msaada wa kisaikolojia,” akasisitiza Bw Langat.
Naye Bw Bett akasema: “Walimu wanahitaji msaada kutoka kwa washikadau wote katika jamii. Hatufai kupuuza changamoto ambazo zinawakabili walimu nchini.”
Walisema walimu wamekuwa wakipelekwa katika vituo vya kurekekebisha tabia nchini na wakarejea wakiwa wameimarika huku wengine wakiishia kusumbuka tena.
Bi Langat alidokeza kuwa walimu wengine wanaishi bila waume ama wake sababu ya kifo ama utengano; suala ambalo anasema halifai kupuuzwa.
TSC imekuwa ikikabili suala la ulevi na mafadhaiko miongoni mwa walimu kwa miaka kwa kuwa limeathiri utendakazi katika shule za umma.
Tukio la hivi karibuni zaidi cha kujitia kitanzi cha mwalimu wa shule ya upili ya Kenya High jijini Nairobi.
Mwili wake ulipatikana ukining’inia katika ngazi ya tenki ya maji shuleni humo mnamo Oktoba 2, 2024.
Mwalimu mwingine wa shule ya upili huko Nyamira alijitia kitanzi Juni 6, 2024 baada ya kupoteza pesa katika mchezo wa kamari.
Kabla ya hapo, mwalimu wa shule ya upili ya Senior Chief Musa Nyandusi – Kegati, Evans Onchari alijiua mnamo Februari 13, 2023.
Katika barua aliyoacha, alisema hali mbaya ya afya ilimsukuma kusitisha maisha yake.
Handisheki ya Uhuru na Ruto yanukia

Rais William Ruto na Rais (Mstaafu) Uhuru Kenyatta wakisalimiana wakati wa kutawazwa kwa Askofu Peter Kimani Ndung’u, katika Kaunti ya Embu. Picha|PCS
RAIS William Ruto na mtangulizi wake Uhuru Kenyatta wanasemekana kuanzisha mazungumzo katika kile kinachoonekana kama jaribio la kiongozi wa taifa kupunguza uasi dhidi yake, haswa katika eneo la Mlima Kenya.
Duru zimeambia Radio Fortune Africa, Rais Ruto pia anajaribu kuridhiana na wandani wake wa zamani ili kuongeza uthabiti katika serikali ya Kenya Kwanza.
Ushawishi wa Rais Ruto umeshuka zaidi katika Mlima Kenya kwa sababu wakazi wamekasirishwa na hatua yake ya kufanikisha kutimuliwa kwa aliyekuwa naibu rais, Bw Rigathi Gachagua.
Wakazi wa eneo hilo lililompa Rais kura nyingi katika Uchaguzi Mkuu wa 2022, pia wameelezea kutoridhishwa kwao na kutotimizwa kwa ahadi alizowapa kuelekea uchaguzi huo na uamuzi wa Dkt Ruto kufanya kazi na kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga.
Mnamo Julai mwaka huu, Rais Ruto aliwateua viongozi watano wa ODM katika baraza lake la mawaziri, hatua ambayo iliwakasirisha zaidi wakazi wa Mlima Kenya.
Kwa kuwaleta Bw Kenyatta na Bw Odinga, wanasiasa wenye uzoefu mkubwa upande wake, Rais Ruto analenga kupata uungwaji mkono kutoka kwa wafuasi wao.
Baada ya kumteua Profesa Kithure Kindiki kuwa kama naibu wake, ili amsaidie katika masuala ya uongozi, duru zinasema anamfikia Bw Kenyatta ili amfaidi kisiasa haswa katika eneo la Mlima Kenya.
Dkt Ruto, Bw Kenyatta, Prof Kindiki na Bw Gachagua walishiriki jukwaa moja, katika Chuo Kikuu cha Embu wakati wa hafla ya kutazwa kwa Kasisi Peter Kimani kuwa Askofu wa Nne wa Kanisa Katoliki jimbo la Embu.
Huku Dkt Ruto, Bw Kenyatta na Prof Kindiki wakiketi pamoja na kuonyesha urafiki, Bw Gachagua alitengwa kabisa na hata kunyimwa nafasi ya kuhutubia umati.
Licha ya kwamba kambi za Dkt Ruto na Bw Kenyatta hazijatoa taarifa rasmi kuhusu mazungumzo yanayoendelea, wandani wake wanasema yapo na yanalenga kutuliza mazingira ya kisiasa.
Umoja
“Viongozi hao wawili wanazungumza chini kwa chini na hii ikaakisi wito wa Ruto kuhimiza umoja wa kitaifa katika serikali hii ya kushirikisha wote,” duru za Ikulu zikaambia Radio Fortune Africa.
Afisa mmoja ambaye aliomba tulibane jina lake, aliongeza kuwa viongozi hao wawili walianza kuzungumza Desemba mwaka jana walipokutana Dubai.
“Mazungumzo hayo sasa yameanzishwa upya,” akaeleza.
Kando na hayo, inasemekana kuwa Rais Ruto anapanga kuwateua serikalini baadhi ya wandani wa Bw Kenyatta.
Majina ya wandani wawili wa rais huyo mstaafu yanayotajwa ni aliyekuwa Waziri wa Afya Mutahi Kagwe na aliyekuwa Gavana wa Laikipia Ndiritu Muriithi.
“Mazungumzo kati ya rais wa nne na rais wa tano (Uhuru na Ruto) bila shaka yatakuwa ya nipe nikupe. Huku vyama vya United Democratic Alliance (UDA) haswa eneo la Mlima Kenya na chama cha Jubilee kinachoongozwa na Bw Kenyatta vinatarajiwa kupata nguvu mpya,” akasema mwandani mmoja wa Bw Kenyatta.
Akaongeza: “Haja kubwa ya Uhuru si uteuzi wa wandani wake serikalini bali ni kubuni mazingira bora kwa biashara kunawiri. Haja yake kubwa ni uchumi kuliko nyadhifa serikalini.”
Katibu Mkuu wa Jubilee, Bw Jeremiah Kioni aliambia “Radio Fortune Africa” kwamba japo hana habari kuhusu mazungumzo halisi kati ya Bw Kenyatta na Rais Ruto, alisema kuwa anaongea na viongozi wengi akisaka uungwaji mkono.
“Hilo ni jambo la kawaida katika siasa; unawatafuta watu ambao unaamini wanaweza kukusaidia,” akasema Mbunge huyo wa zamani wa Ndaragua.

Baraza la Sheria nchini Uganda limenyima Martha Karua leseni ya kutoa huduma za kisheria nchini humo.
Karua, ambaye pia ni mwanasiasa aliomba kibali cha kumtetea mahakamani mwanasiasa wa upinzani wa Uganda Kiiza Besigye ambaye alikamatawa nchini jijini Nairobi nchini Kenya, akiwa na mwenzake Hajj Obeid Lutale mnamo Novemba 16, 2024.
Wawili hao walikuwa nchini Kenya kuhudhuria uzinduzi wa kitabu cha Karua.
Tanzania inaposherehekea miaka 63 ya Uhuru, imekua na jumla ya marais 6.
Je, unawakumba vipi viongozi waliotangulia wa taifa hilo la Afrika Mashariki?



All Rights Reserved © Cantona Group PLC||2024
Discover more from cantonadigital
Subscribe to get the latest posts sent to your email.