Radio Fortune Africa -Na Cantona Joseph
https://zeno.fm/radio/radio-fortune-africa
Botswana hivi karibuni itajiunga na Ubelgiji kama kituo cha uthibitishaji na cheti cha mauzo ya almasi katika nchi za G7, kundi la mataifa saba tajiri duniani, ofisi ya rais imetangaza siku ya Alhamisi.

Baada ya G7 kupiga marufuku almasi za Urusi mnamo Januari, Anvers iliteuliwa mnamo mwezi Machi kama eneo pekee lililoidhinishwa kuthibitisha asili ya almasi ghafi na kutoa vyeti vya G7. Botswana, mzalishaji mkubwa wa almasi barani Afrika na ya pili duniani baada ya Urusi, imesema siku ya Alhamisi inatarajiwa kuwa kituo cha pili cha uidhinishaji ifikapo mapema mwaka 2025.
Uamuzi huu umechukuliwa baada ya “maandamano makali” ya nchi hiyo dhidi ya mfumo wa kituo kimoja, yaliyoonekana kuwa “isiyo ya haki, vikwazo, gharama kubwa na hivyo kuharibu uchumi”, wa Botswana, kulingana na taarifa ya ofisi ya rais kwa vyombo vya habari. Timu ya kiufundi ya G7 kuhusu almasi, chini ya uenyekiti wa Umoja wa Ulaya, imebaini kwamba iko pia “katika majadiliano na nchi nyingine za Afrika zinazozalisha alimasi kama vile Namibia na Angola kuanzisha vituo vya ziada vya uthibitisho”.
Kujumuishwa kwa Botswana katika siku za usoni “kutachukua nafasi ya nchi kama kigezo cha kimataifa katika uzalishaji wa almasi,” msemaji wa serikali Montlenyane Baaitse amesema katika taarifa. Tangazo hili linafuatia ushiriki wa Rais wa Botswana aliyechaguliwa hivi karibuni Duma Boko katika mkutano wa almasi wa FACETS 2024 nchini Ubelgiji.
Katika hotuba yake wakati wa hafla hiyo, Duma Boko aliangazia umuhimu wa almasi kiuchumi na kijamii kwa nchi yake wakati akijadili juhudi za kuimarisha uwazi na uwajibikaji katika tasnia hii. “Botswana imejitolea kuwa kinara katika ufuatiliaji na uwajibikaji wa uchimbaji madini, kuhakikisha kwamba almasi zetu zinang’aa sio tu katika urembo bali pia katika maadili,” alisema.
Mapato na biashara zinazohusiana na almasi zimeshuka katika nchi kama Botswana, ambapo ukuaji ulishuka kutoka 5.5% mwaka 2022 hadi 2.7% mwaka 2023, kulingana na Shirika la Fedha la Kimataifa. Mawe ya vito ndiyo chanzo kikuu cha mapato ya Botswana, yakichukua takriban 30% ya Pato la Taifa na 80% ya mauzo yake ya nje.
Duma Boko aliingia madarakani katika uchaguzi wa Oktoba 30 uliyokiondoa chama kilichokuwa madarakani kwa takriban miaka sitini, huku kukiwa na wasiwasi kuhusu kudorora kwa uchumi. Katika hotuba yake ya kwanza ya taifa, rais huyo mpya alitangaza nia yake ya kuleta mseto wa uchumi, unaotegemea pia almasi, kwa kuingia katika soko la bangi inayotumika kwa matibabu.
All Rights Reserved © Cantona Group PLC||2024
Discover more from cantonadigital
Subscribe to get the latest posts sent to your email.