Afrika Leo Jioni-Oktoba 7,2024

Radio Fortune Africa -Na Cantona Joseph

https://zeno.fm/radio/radio-fortune-africa

Muhtasari

  • Hezbollah yasema ‘ina imani’ inaweza kuzuia uvamizi wa Israel
  • Mwanamume akumbuka maisha ‘mazuri’ kabla ya vita kuua jamaa wake Gaza
  • Makumbusho yafanyika mwaka mmoja tangu kutokea kwa shambulizi la Hamas
  • ‘Mwanaume aliyetekwa nyara Oktoba 7 auawa’
  • Jeshi la Israel lashambulia maeneo ya Hamas kote Ukanda wa Gaza
  • Mwanajeshi wa Israel auawa kwenye mpaka wa Lebanon
  • Mlipuko waua Wachina wawili karibu na uwanja wa ndege wa Karachi, Pakistan
  • Mwanaharakati wa upinzani wa Urusi aliuawa akipigania Ukraine
  • ‘Binti yangu mateka wa Uingereza-Israel amesahaulika’ – mama

Israel yashambulia Gaza na Beirut huku shambulio la Oktoba 7 likikumbukwa mwaka mmoja baadaye

Mwaka mmoja baada ya mashambulizi ya Oktoba 7, Israel inasema inashambulia maeneo yanayolengwa ya Hamas katika eneo la Gaza, pamoja na Hezbollah nchini Lebanon.

IDF yawataka wakazi wa kusini mwa Gaza na Lebanon kuhama

Moshi ukitanda

Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) limewataka wakazi wa Gaza na Lebanonkuhama.

Msemaji wa IDF Avichay Adraee anasema watu wa kusini mwa Gaza, karibu na Khan Younis, wanapaswa kuelekea katika eneo la kibinadamu la Al-Mawasi, ukanda mwembamba wa ardhi karibu na Bahari ya Mediterania katika Ukanda wa Gaza.

Hapo awali, wakazi katika maeneo ya kaskazini mwa Gaza, ikiwa ni pamoja na Jabalia, Beit Hanoun na Beit Lahia walitakiwa na IDF kuhama.

Mbali na Gaza, Adraee pia alitoa onyo la dharura kwa wakazi wa vijiji zaidi ya 20 kusini mwa Lebanon, ikiwa ni pamoja na Tayr Harfa na al-Mansouri.

IDF imewaambia waliohamishwa kuondoka makwao na kuelekea “kaskazini mwa Mto Awali”. “Mtu yeyote ambaye yuko karibu na wanachama wa Hezbollah, mitambo au silaha anaweka maisha yake hatarini,” IDF inasema.

Maafisa 10 wa zimamoto wauawa kwa shambulio la Israel-Lebanon

Tunapata ripoti za shambulio la Israel kusini mwa Lebanon ambalo limewaua maafisa kadhaa wa zima moto, kulingana na wizara ya afya ya nchi hiyo.

Wizara ya afya inasema uvamizi katika jengo moja huko Baraachit umewaua maafisa 10 wa zimamoto .

Mamlaka zinasema kuwa zimetoa miili ya watu wanane kufikia sasa, shirika la habari la AFP linaripoti.

Wizara ya afya ya Lebanon imesema kuwa shambulio hilo lilifanyika kwenye jengo la manispaa huko Baraachit katika eneo la Bint Jbeil, kusini mwa Lebanon.

Wizara ya afya ya Lebanon inasema uondoaji wa vifusi kutoka kwa jengo lililoharibiwa vibaya unaendelea kwani waliouawa bado hawajatambulika.

Ukraine yashambulia bohari ya mafuta Crimea

Vazi

Jeshi la Ukraine limesema limefanya shambulio kwenye kituo kikubwa cha mafuta karibu na rasi ya Crimea inayokaliwa kwa mabavu, ikiwa ni shambulio la hivi karibuni zaidi katika wimbi la mashambulizi yaliyolenga vituo vya nishati vinavyodhibitiwa na Urusi.

Maafisa wa Kyiv walisema vikosi vya makombora vya nchi hiyo vilianzisha shambulio usiku kwenye kituo cha Feodosia, kituo kikubwa zaidi cha usindikaji wa mafuta kwenye peninsula.

Maafisa waliowekwa rasmi na Urusi huko Crimea hawajathibitisha kutokea kwa shambulizi hilo, lakini walikiri kutokea moto katika kituo hicho.

Hakuna majeruhi walioripotiwa. Hali ya dharura katika ngazi ya manispaa imetangazwa, huku watu 300 wakihamishwa kutoka Feodosia kutokana na moto huo, shirika la habari la serikali la Tass liliripoti.

Hezbollah yasema ‘ina imani’ inaweza kuzuia uvamizi wa Israel

Katika taarifa mpya ya kuadhimisha mwaka mmoja tangu mashambulizi ya Oktoba 7 ya Hamas, Hezbollah inasema ina “ujasiri” katika uwezo wake wa “kuzuia uvamizi wa [Israel]”, na imeapa kuendelea kupigana.

Kundi hilo lenye makao yake makuu Lebanon linashirikiana na Hamas, na yote yanaungwa mkono na kufadhiliwa na Iran.

Hezbollah inayaelezea matukio ya tarehe 7 Oktoba kama “ya kishujaa”, ikisema yatakuwa na athari za “kihistoria” katika eneo hilo.

“Hakuna mahali” kwa Israel huko, inasema, na “lazima iondolewe, haijalishi itachukua muda gani”.

Hezbollah pia inalaumu “Marekani na washirika wake” kwa ghasia huko Gaza na Lebanon iliyofuata shambulio la Hamas la Oktoba 7, wakisema “wanawajibika kikamilifu”.

Mwanamume anakumbuka maisha ‘mazuri’ kabla ya vita kuwaua mwanawe, mama, na dada yake Gaza

.
Maelezo ya picha,Ahmed Younis alipoteza watu watatu wa familia yake katika shambulizi huko Gaza mwezi uliopita

Maisha katika eneo la Gaza iliyozingirwa kabla ya vita hayakuwa rahisi kabisa, lakini anapokumbuka siku za nyuma huku akiwa ameshika picha za watoto wake wanne wakitabasamu, Ahmed Younis anayakumbuka maisha kuwa “mazuri”.

“Nilikuwa nalenga kujiimarisha. Nilinunua nyumba na nilikuwa na uthabiti wa kifedha,” anasema. “Nilikuwa nikipanga maisha bora ya baadaye kwa watoto wangu. Niliwapeleka kwa shule bora za chekechea.”

Familia hiyo iliondoka nyumbani kwao Nuseirat katikati mwa Gaza wakati wanajeshi wa Israel waliposonga mbele, lakini walikuwa wamejisikia salama vya kutosha na kurejea. Kisha, mwezi mmoja uliopita, nyumba yao ilishambuliwa na mashambulizi ya anga ya Israel.

“Ndani ya sekunde chache tulikuwa tumezungukwa na moto na kunaswa kwenye vifusi,” Ahmed anasimulia akiwa kwenye kitanda chake hospitalini.

Mwanawe mwenye umri wa miaka sita, Hossam – mvulana mchangamfu ambaye alipenda kuendesha baiskeli yake na kumfanya baba yake kuwa na kazi za hapa na pale kwa ajili yake – aliuawa. Jamaa mmoja alibeba maiti yake kwenye shuka nyeupe huku Ahmed akitiririkwa na machozi.

Mama na dadake Ahmed pia waliuawa. Yeye na mkewe na watoto wao watatu waliosalia waliungua vibaya na binti mmoja kupoteza miguu yake.

“Nataka kujua ni kwa nini,” Ahmed anamwambia mpigapicha wetu wa BBC. “Sisi ni raia, na hatuna tishio lolote.”

Sasa, hamu kuu ya Ahmed ni kuondoka Gaza kutafuta matibabu bora kwa familia yake.

“Kama ningeweza, ningeondoka, na kuwapeleka kutibiwa nje ya nchi kabla ya kitu kingine chochote,” anatuambia. “Natumai kutoka kwa Mungu kwamba [vita] hivi vitakoma leo, kabla ya kesho.”

Makumbusho yafanyika mwaka mmoja tangu kutokea kwa shambulizi la Hamas

,

Asubuhi ya leo, watu wamerejea kwenye eneo kulikofanyika shambulio wakati tamasha lilikuwa likiendelea la Supernova huko Re’im, kusini mwa Israel, ambapo zaidi ya watu 350 waliuawa na Hamas mwaka mmoja uliopita leo.

Wakati huohuo, jamaa walishikilia picha za wapendwa wao waliokuwa kwenye tamasha hilo.

Wengi katika sherehe hiyo wamevalia fulana zenye picha za wapendwa wao

.
Maelezo ya picha,Rais wa Israel, Isaac Herzog, pia amehudhuria na kutoa taarifa akisema dunia “lazima iunge mkono Israel” ikiwa inataka kuleta amani na “mustakbali mwema” katika eneo hilo.

Mwanaume aliyetekwa nyara Oktoba 7 auawa – Jukwaa la Familia Zilizotoweka limesema

,

Idan Shtivi, mmoja wa mateka waliochukuliwa na Hamas kutoka tamasha la muziki la Supernova tarehe 7 Oktoba mwaka jana, ameuawa, Jukwaa la Mateka na Familia Zilizotoweka linasema.

Kundi hilo ambalo linalenga kuwarejesha waliotekwa nyara nchini Israel, linasema kijana huyo mwenye umri wa miaka 28 “alijulikana kwa kujitolea kwa ajili ya wale walio karibu naye”.

Jukwaa hilo limeongeza kuwa wakati shambulio hilo lilipoanza, Shtivi aliamua “kujitolea” kusaidia watu wawili wasiojulikana kutoroka kutoka kwa eneo la tukio, lakini gari lao lilishambuliwa njiani.

Miili ya watu hao wawili ilipatikana.

Hamas iliteka nyara watu 251 wakati wa mashambulizi ya Oktoba 7, kulingana na takwimu za Israel.

Kabla ya kifo cha Shtivi kutangazwa, 117 kati ya wale waliochukuliwa mateka walikuwa wameachiliwa, 37 walithibitishwa kufariki, na 97 hawajulikani waliko.

Jeshi la Israel lashambulia maeneo ya Hamas kote Ukanda wa Gaza – msemaji wa jeshi la Israel

.

Msemaji wa jeshi la Israel amesema (IDF) sasa inashambulia maeneo ya Hamas katika Ukanda wa Gaza.

.

Makombora manne yamerushwa kuelekea Israel kutoka kusini mwa Ukanda wa Gaza muda mfupi uliopita, jeshi la Israel linasema.

Makombora matatu kati ya hayo yalinaswa na jeshi la anga la Israel huku moja likitua katika eneo la wazi, jeshi linaongeza.

Hilo linawadia wakati Israel inaanza kumbukumbu za mashambulizi ya Oktoba 7 wakati watu wenye silaha wa Hamas walipovamia mpaka wa Gaza na kuingia Israel – takriban watu 1,200 waliuawa na wengine 251 walichukuliwa mateka.

Israel ilianza mashambulizi ya anga kwenye maeneo yaliyolenga Gaza kujibu shambulizi hilo, na baadaye kutuma wanajeshi katika eneo hilo.

Watu kumi wamejeruhiwa katika mashambulizi ya Hezbollah kaskazini mwa Israel

Watu kumi wamejeruhiwa na makombora yaliyorushwa kutoka Lebanon katika miji ya kaskazini mwa Israel ya Haifa na Tiberias usiku kucha, kulingana na huduma ya ambulensi ya Israel.

Majeruhi kadhaa walipata majeraha kutokana na vipande vya makombora, vioo na madirisha, huduma ya ambulensi inaongeza.

Makombora hayo yalishambulia mgahawa, nyumba na barabara kuu, jeshi la Israel linasema, na kuongeza kuwa linachunguza jinsi makombora ya Hezbollah yalivyoweza kupenya katika mifumo ya ulinzi ya anga ya Israel.

Hezbollah inasema ilikuwa ikilenga vituo vya kijeshi.

Mwanajeshi wa Israel auawa kwenye mpaka wa Lebanon

,
Maelezo ya picha,Wanachama wa Brigadi ya Golan ya Jeshi la Israel

Jeshi la Israel linasema mwanajeshi mmoja ameuawa katika mapigano kwenye mpaka wa Lebanon na Israel, huku wanajeshi wawili wakijeruhiwa vibaya.

Jeshi la Israel lilianza uvamizi wake wa ardhini dhidi ya kundi linaloungwa mkono na Iran la Hezbollah nchini Lebanon Jumatatu iliyopita, kwa mapigano ya mara kwa mara ya kuvuka mpaka tangu wakati huo.

IDF yashambulia hospitali ya Gaza ambako inasema kuna wanachama wa Hamas

Wakati huo huo, Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) linasema limefanya shambulizi dhidi ya kundi la Hamas waliokuwa wakiendeleza shughuli zao ndani ya hospitali ya al-Aqsa huko Deir al-Balah katikati mwa Ukanda wa Gaza.

IDF inasema vituo hivi vya kamandi vilitumiwa na Hamas kupanga mashambulizi dhidi ya wanajeshi wa IDF nchini Israel.

Inasema ilichukua hatua za kuwalinda raia kabla ya shambulizi, ikiwa ni pamoja na matumizi ya “sahihi ya silaha, uchunguzi wa angani, na taarifa za ziada za kijasusi”.

IDF inaongeza kuwa huu ni “mfano zaidi” wa Hamas wa “utumiaji mbaya wa miundombinu ya kiraia kinyume na sheria za kimataifa”.

Mlipuko waua Wachina wawili karibu na uwanja wa ndege wa Karachi, Pakistan

,

Raia wawili wa China wameuawa na takriban watu kumi kujeruhiwa baada ya mlipuko kutokea karibu na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jinnah mjini Karachi, Pakistan.

Ubalozi wa China nchini Pakistan ulisema kulikuwa na “baadhi ya majeruhi wa eneo hilo” katika kile ulichokitaja kama “shambulio la kigaidi”, ingawa jumla ya vifo bado haijulikani wazi.

Ubalozi umeongeza kuwa mlipuko huo ulilenga msafara wa wahandisi wa China wanaofanya kazi katika mradi wa umeme katika mkoa wa Sindh nchini humo.

Katika taarifa iliyotolewa Jumatatu, kundi hilo la wanamgambo lilisema “lililenga msafara wa ngazi ya juu wa wahandisi na wawekezaji wa China” unaowasili kutoka uwanja wa ndege wa Karachi.

Shambulio hilo lilitekelezwa kwa kutumia “kifaa cha vilipuzi kinachobebwa kwenye gari”, Reuters ilinukuu BLA ikisema.

Mlipuko ulitokea mwendo wa 23:00 saa za eneo. Ubalozi wa China ulisema kuwa wahandisi hao walikuwa sehemu ya kampuni inayofadhiliwa na China ya Port Qasim Power Generation Co Ltd, ambayo inalenga kujenga mitambo miwili ya kuzalisha umeme wa makaa ya mawe huko Port Qasim, karibu na Karachi.

Kiwanda hicho ni sehemu ya ukanda wa uchumi wa China na Pakistan, ambao pia unafadhili miradi kadhaa ya miundombinu na nishati katika jimbo la Balochistan nchini Pakistan, ambalo lina utajiri mkubwa wa maliasili, ikiwa ni pamoja na gesi na madini.

Jeshi la Balochistan (BLA), ambalo katika miaka ya hivi karibuni limefanya mashambulizi dhidi ya raia wa China wanaohusika na miradi, limedai kuhusika na shambulio hilo.

Mara kwa mara kundi hilo limekuwa likilenga raia wa China katika eneo hilo, likidai wakaazi wa kabila la Baloch hawakuwa wakipata mgao wao wa mali inayotokana na wawekezaji wa kigeni.

Mwanaharakati wa upinzani wa Urusi aliuawa akipigania Ukraine

.

Ildar Dadin, mwanaharakati mashuhuri wa upinzani wa Urusi ambaye alikuwa akipigana nchini Ukraine upande wa Kyiv, ameuawa akiwa vitani kwa mujibu wa kundi lililomsajili.

Msemaji wa kundi hilo, Baraza la Kiraia, aliiambia BBC kwamba Dadin alifariki, na kuongeza kwamba “alikuwa, na anasalia kuwa shujaa”.

Mwanaharakati huyo aliyegeuka kuwa mpiganaji aliuawa wakati wanajeshi wa kikosi chake cha kujitolea, The Freedom of Russia Legion, walipokabiliwa na shambulio la mizinga ya Urusi katika eneo la Kharkiv kaskazini-mashariki mwa Ukraine.

Kwa sasa, hakuna maelezo zaidi na Legion yenyewe haitatoa maoni wakati inasema operesheni ya kijeshi bado inaendelea.

Lakini Ilia Ponamarev, mwanasiasa wa upinzani wa Urusi aliye uhamishoni na ambaye hapo awali alikuwa na uhusiano na Legion, ameiambia BBC kwamba “ana hakika” kwamba Dadin amefariki.

Chanzo kingine kilifafanua kwamba hii “ilithibitishwa na wale waliokuwa pamoja naye vitani”.

Ujumbe wa hivi punde ambao nimetuma kwenye simu yake bado unaonyesha kuwa “haujasomwa”.

Ildar Dadin alijulikana nchini Urusi muongo mmoja uliopita kwa kuendelea kwake kufanya maandamano ya amani huku ukandamizaji wa kisiasa ukiongezeka.

Alikuwa mtu wa kwanza kushtakiwa chini ya Kifungu kipya cha 212.1 – kilichopewa jina Sheria ya Dadin – ambayo mwaka wa 2014 ilifanya kuwa kosa la jinai kufanya ukiukaji wa kurudia wa sheria za Urusi zinazozidi kuwawekea vikwazo kwenye maandamano.

Katika kesi yake, ilisemekana alisimama kwenye mitaa ya Moscow akiwa na mabango.

Akiwa amehukumiwa miaka miwili na nusu, Dadin aliwekwa kwenye seli ya adhabu na mara moja akagoma kula. Walinzi wake wa gereza kisha wakamtesa ili kusitisha mgomo huo.

‘Binti yangu aliyetekwa na Hamas amesahaulika’ – Mama

.

Mama wa mateka pekee raia wa Uingereza na Israel ambaye bado anashikiliwa na Hamas huko Gaza ameuliza kwa nini Uingereza “haipiganii kwa kila namna kuhakikisha kuachiliwa kwake”.

Emily Damari, 28, alipigwa risasi na kuchukuliwa kutoka eneo la kibbutz la Israel na kuvukishwa mpaka hadi Gaza mnamo 7 Oktoba.

Akizungumza katika hafla ya kumbukumbu ya London kuashiria mashambulizi mwaka mmoja uliopita, mama yake Mandy Damari alisema “shida ya bintiye inaonekana kuwa imesahauliwa”.

Waziri Mkuu Sir Keir Starmer alisema katika taarifa kwamba Uingereza “bila shaka ni lazima isimame na jumuiya ya Wayahudi”.

Binti huyo mwenye uraia mara mbili ni miongoni mwa mateka 97 ambao bado hawajulikani waliko.

Akiongea kwenye hafla ya ukumbusho ya Hyde Park, mama yake alisema: “[Emily] ni binti wa nchi zote mbili, lakini hakuna mtu anayetaja ukweli kwamba bado kuna mateka wa kike wa Uingereza anayeshikiliwa na Hamas kwa mwaka mmoja sasa. Na mimi wakati mwingine hushangaa kama watu wanajua kuna mwanamke wa Uingereza huko Gaza.

“Fikiria, kama Emily angekuwa binti yako. Jaribu kuwazia anachopitia.

“Tangu tarehe 7 Oktoba mwaka jana, amekuwa akishikiliwa na magaidi wa Hamas katika mahandaki ya Gaza, mita 20 au zaidi chini ya ardhi akiwa amefungiwa, kuteswa, kutengwa, kutoweza kula, kuzungumza au hata kusonga bila ruhusa ya mtu mwingine.”

Pigo tena kwa Gachagua mahakama ikikataa kutoa amri kesi zikifika 19

Naibu Rais Rigathi Gachagua ambaye kesi 19 za kupinga kutimuliwa kwake zimekosa kumfaa kortini.

JUHUDI mpya za kuzuia kung’olewa mamlakani kwa Naibu Rais Rigathi Gachagua Jumatatu zilipata pigo katika Mahakama Kuu.

Jaji Bahati Mwamuye aliamrisha kuwa kesi ambayo iliwasilishwa na aliyekuwa Katibu Mkuu wa UDA Cleophas Malala ipelekwe kwa Jaji Eric Ogola. Ni Jaji Ogola atasikiza kesi zote zilizowasilishwa na watu mbalimbali wakipinga kutimuliwa kwa Naibu Rais.

Kupitia wakili Mwenda Njagi, Bw Malala aliwasilisha kesi hiyo ambayo haitakuwa na mashiko ikizingatiwa hoja ya kumtimua Naibu Rais itawasilishwa bungeni mnamo Jumanne.

Wakili huyo jana alisema kesi hiyo haitakuwa na maana iwapo amri ambayo waliitaka itolewe haingetolewa kwa kuwa hoja itakuwa ishajadiliwa na uamuzi kutolewa.

“Mahakama hii imetambua kuwa kuna kesi kadhaa kuhusiana na kuondolewa mamlakani kwa Naibu Rais na inaona heri kesi hizo ziunganishwe. Naomba kesi hii ipelekwe kwa Jaji Ogola iunganishwe na nyingine na mahakama inakataa kutoa amri za muda,” akasema jaji huyo.

Kupitia wakili Paul Nyamodi, Bunge  jana lilifichua kuwa kuna kesi 19 ambazo zimewasilishwa mahakamani kupinga kutimuliwa kwa Bw Gachagua.

Wakili huyo alisema kuwa ili kesi hizo zisikizwe kwa rahisi na haki itolewe, kuna haja ya kuunganishwa pamoja badala ya kusikizwa moja baada ya nyingine.

“Amri kuhusu kuunganishwa kwa kesi hizo itazuia mahakama kuwa na vikao tofauti kusikiza kesi moja. Ikifanyika hivyo, korti inaweza kuafikia uamuzi ambao unagongana na kuaibisha mahakama,” akasema Karani wa Bunge la Kitaifa Samuel Njoroge.

Ombi la kuunganishwa kwa kesi hizo na kusikizwa kisha kuamuliwa pamoja pia lilikubaliwa na Seneti.

Katika kesi yake, Bw Malala anasema kuwa Bunge la Kitaifa jinsi lilivyo halitimizi vigezo vya kikatiba kutokana na kukosa kutimiza usawa wa jinsia.

Kando na Bw Malala, Naibu Rais mwenyewe amefika kortini kupinga kutimuliwa kwake akisema kuwa madai yanayotumiwa kumsulubisha hayana mashiko.

Pia Bw Gachagua amesema kuwa mikutano ya ushirikishaji wa umma ambayo ilifanyika wikendi haitoshi kubadilisha uamuzi wa raia ambao walimpigia kura pamoja na Rais William Ruto katika uchaguzi mkuu uliopita.

“Hoja ya kunitimua inalenga kubadilisha uamuzi wa Wakenya wengi ambao walinipigia kura kuwa Naibu Rais wa Kenya. Madai yaliyowekwa dhidi ya yangu ni ya uongo na hayana msingi hivyo basi hayatimizi vigezo vya kung’atuliwa kwangu,” akasema kwenye kesi yake.

Walimu watishia kususia usahihishaji wa mitihani

Katibu Mkuu wa Kuppet, Akello Misori. 

MUUNGANO wa Walimu wa Sekondari (KUPPET) umetishia kuwaongoza walimu kususia usahihishaji na usimamizi wa mitihani ya kitaifa kuhusiana na marupurupu duni.

Katibu Mkuu wa Kuppet Akelo Misori, alisema muungano huo unaitisha malipo ya hadi Sh4,000 kwa siku pamoja na malazi bora kwa walimu wanaosahihisha mitihani ya kitaifa.

Kwa sasa, Baraza la Kiaifa la Mitihani (KNEC) huwalipa watahini, waangalizi na wasimamizi wa vituo vya mitihani Sh400, Sh450 na Sh500, mtawalia kila siku. Muungano huo unasema wasahihishaji wa mitihani hulipwa hadi Sh150 na kupewa makazi duni.

“Hata vibarua katika vituo vya ujenzi wanalipwa malipo bora zaidi kuliko walimu wanaosimamia mitihani ya kitaifa yenye thamani kuu. Hii haikubaliki,” alisema Bw Misori.

Akizungumza wakati wa maadhimisho ya Sikukuu ya Walimu Duniani katika Kaunti ya Embu Jumamosi, Bw Misori alitaka marupurupu hayo yaongezwe kabla ya mitihani kuanza.

Haya yanajiri huku KNEC ikianzisha sheria kali za kuzuia udanganyifu kwenye mitihani ikiwemo kuwabadilisha wasimamizi na kupiga marufuku matumizi ya simu baina ya waangalizi.

Bw Misori ameonya ikiwa KNEC haitatoa jibu mwafaka, walimu watajiepusha na usimamizi wa mitihani.

KNEC inapaswa kujifahamisha kuhusu mikondo iliyopo sasa kiuchumi. “Walimu ni wataalam ilhali wanachukuliwa kama wafanyakazi wasio na ujuzi,” alisema.

Alisema, “Walimu wakuu ambao wana digrii huamka saa kumi unusu alfajiri kwenda kuchukua karatasi za mitihani na wanalipwa Sh500 kwa siku. Manaibu wao hata hawalipwi chochote. Hatutaruhusu hali hii kuendelea,” alisema. Bw Misori alisema Kuppet imepania kuhakikisha malipo bora kwa walimu wanaosimamia mitihani.

Aidha, Bw Misori alielezea hofu yake kuhusu sera za serikali zinazodunisha maslahi na hadhi ya walimu katika jamii.

“Sera hizo duni zinajumuisha kupunguza bajeti za elimu zinazoathiri ajira ya walimu wapya, kuwapandisha vyeo walimu, na ustawishaji wa miundomsingi.”

Alilalamika kuwa ajira ya walimu inazidi kuingiliwa huku walimu wanaostahili wakifungiwa nje.

“Kupendelea jamaa wa familia na ubaguzi ni kawaida katika ajira ya walimu,” alisema.

DKT NCHIMBI AIPANGUA HOJA YA MPINA KUHUSU STAKABADHI GHALANI | “NI SERA YA CCM IKO KWENYE ILANI”

Ziara ya Katibu mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Balozi Dkt Emmanuel Nchimbi imeingia Siku yake ya Pili mkoani Simiyu, ambapo akizungumza na Wananchi katika Jimbo la Kisesa Wilayani Meatu, Baada ya Kuwasili ameahidi CCM itaendelea Kutatua Changamoto ambazo zinawakabili ikiwemo Suala la Uvamizi wa Tembo kwenye Makazi na Mashamba pamoja na kuhakikisha Wafugaji ambao wameshinda Kesi Wanarejeshewa Mifugo yao.

Akizungumza na Wananchi katika Kata ya Mwandoya Wilayani humo, Pia Dkt Nchimbi ametolea Ufafanuzi mfumo wa Stakabadhi Ghalani, Changamoto ambayo imewasilishwa na Mbunge wa Jimbo la Kisesa Luhaga Mpina.

“Habari ya Stakabadhi ni Sera ya CCM, hiyo ni Bada ya Utafiti wa Kina ambao Ulifanywa na Wataalamu, kwa hii huu mfumo ni Sera rasmi inayoeleweka kwa Sababu Wananchi ndio walioridhia kupitia Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM)” amesema Dkt Nchimbi.

TANZANIA YASHIRIKI MKUTANO WA MAENDELEO ENDELEVU WA HAMBURG UJERUMANI (HAMBURG SUSTAINABLY CONFERENCE)

Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso (Mb) amemwakilisha Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenye Mkutano wa Kimataifa wa Maendeleo Endelevu (Hamburg Sustainability Conference) unaofanyika Hamburg Ujerumani ambao umefunguliwa rasmi na Chancellor wa Ujerumani Olaf Scholz leo terehe 07 October 2024. Kwenye mkutano huo, Mhe. Aweso ameandamana na Mhe. Hassani Iddi Mwamweta, Balozi wa Tanzania nchini Ujerumani.

Mkutano huo umewakutanisha Marais, Mawaziri Wakuu, Rais wa Benki ya Dunia, Wakuu wa Taasisi za Kifedha kama IMF, Mawaziri, watu mashuhuri na Taasisi mbalimbali za maswala ya Maendeleo duniani.

Pamoja na mambo mengine. Mkutano huu unalenga kuwaleta pamoja wadau wote kutoka Sekta za Umma na binafsi kwa ajili ya kuunganisha nguvu ikiwemo upatikanaji wa Fedha ili kufikia Malengo ya Maendeleo Endevu (SDGs).

MAJALIWA: RAIS DKT. SAMIA ANAMATUMAINI MAKUBWA NA TAIFA STARS WAZIRI MKUU

Kassim Majaliwa ameitembelea Timu ya Taifa ya Tanzania ya Mpira wa Miguu (Taifa Stars) inayofanya mazoezi kwenye uwanja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) jijini Dar es Salaam na kusema kuwa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassaan anamatumaini makubwa kuwa timu hiyo itafanya vizuri kwenye michezo yote miwili.

Mheshimiwa Majaliwa ameyasema hayo leo (Jumatatu, Oktoba 07, 2024) alipozungumza na wachezaji, benchi la ufundi pamoja na viongozi wakiwa katika maandalizi ya michezo miwili ya kufuzu michuano ya AFCON 2025 dhidi ya Congo itakayochezwa Oktoba 10 na 15, 2024.

“Kila mmoja aone ana jukumu kubwa, kwako wewe mwenyewe na kwa nchi yako, Mheshimiwa Rais Dkt. Samia anawatakia kila la kheri na alichofanya ametoa usafiri wa uhakika wa ndege itakayowapeleka nchini Congo kwa ajili ya mchezo wa Oktoba 10, 2024, hili ni jambo kubwa.”

Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa kwa jitihada za Rais Dkt. Samia amefanikiwa kushawishi mashirikisho ya mpira wa miguu ya Afrika na FIFA ili kuiona Tanzania ni nchi ambayo imeamua kuboresha viwango vya michezo ikiwemo mpira wa miguu.

“Tumeanza kuona heshima tunayoipata ya kuwa wenyeji wa baadhi ya mashindano ikiwemo CHAN.”

Kadhalika, Mheshimiwa Majaliwa amewataka wachezaji hao kushikamana, kuzungumza lugha moja na kutanguliza uzalendo. “Tumieni fursa ya imani ya Watanzania kwenu kuiwakilisha vyema Tanzania kwenye michezo iliyo mbele yenu.”

Kwa upande wake, Nahodha wa timu hiyo Mohammed Hussein “Tshabalala” amemshukuru Rais Dkt. Samia kwa kuwezesha kupatikana kwa usafiri wa ndege kwa ajili ya mchezo dhidi ya Congo. “Kwetu sisi hii ni motisha kuelekea michezo yetu miwili dhidi ya Congo, kwasababu itatusaidia kurejea haraka nyumbani kwa ajili ya maandalizi ya mchezo wa marudiano”

DG PSSSF ASEMA; WIKI YA HUDUMA KWA WATEJA INATUKUMBUSHA WAJIBU WA KUTOA HUDUMA BORA.

Wiki hii, makao makuu ya PSSSF yamezindua rasmi Wiki ya Huduma kwa Wateja, tukio ambalo linatarajiwa kuimarisha huduma zinazotolewa kwa wanachama na wadau wengine.

Akizungumza na watumishi wa makao makuu na kanda ya Dodoma, Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF, Bw. Abdul-Razaq Badru, alieleza kwamba wiki hii ni fursa ya kutafakari jinsi wanavyotoa huduma.

“Ukimhudumia mwanachama vizuri unakuwa uneenda above and beyond, na hii ndio theme inayotuongoza,” aliongeza.

Akisisitiza umuhimu wa wiki hii alisema, “Wiki hii ni muhimu sana kwani inatukumbusha kwa nini sisi watumishi tupo hapa. Wateja wetu ndio wanaotufanya sisi kuwa hapa kazini kwa lugha ya mjini wanasema ndio wanaotufanya tuwepo mjini.” Alisema.

Alisisitiza umuhimu wa kutoa huduma katika mazingira yote na kwa wateja wa aina zote. “Wiki hii inatukumbusha majukumu yetu kama mfuko, ambayo ni kuhakikisha kuwa fedha ya wanachama inakuwa salama na inapata thamani zaidi. Tunatarajia kwamba pale wanapolipwa fedha yao iwe na thamani,” alifafanua.

Badru alisisitiza kwamba PSSSF inatoa ahadi upya kwamba wana uwezo wa kutoa huduma bora na kuwafanya wateja wao kuwa na furaha na kuridhika. “Theme hii ya mwaka huu ni ‘Above and Beyond’ – Kutoa huduma kwa wateja wa aina zote, umri wote na jinsia zote, na kuwa na uwezo wa kuwaelewa na kuwasikiliza wateja wetu,” alisema.

Aliwashukuru watumishi wote kwa juhudi zao katika kutoa huduma bora na kutangaza kuwa wako tayari kutoa huduma kwa viwango vya juu zaidi na kutoa suluhisho kwa mahitaji na changamoto za wateja wao.

Alimalizia hotuba yake kwa kusema, “Katika kutoa huduma, ni lazima kutoa huduma kwa tabasamu, yaani ‘corporate smile’. Tabasamu ni ishara ya ukaribu na urafiki, na linachangia kwa kiasi kikubwa katika kuridhisha wateja wetu.”

Wiki ya Huduma kwa Wateja inatarajiwa kuendelea kutoa mwanga kuhusu majukumu ya kila mfanyakazi na kuimarisha uhusiano kati ya PSSSF na wanachama wake.

RAIS SAMIA ANATUPENDA SANA KIMARA, 2025 TUMPENI KURA ZOTE.

Akiwa kwenye mkutano wa viongozi na wanachama wa @ccmtanzania Kata ya Kimara, Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya CCM Wilaya ya Ubungo Ndugu Hamis Abeid Baruani @hamisabeid alisisitiza kuwa Kata ya Kimara ni moja ya Kata ambazo Rais @samia_suluhu_hassan anazipenda sana na anaziangalia kwa jicho la maendeleo.

Hayo yamesemwa baada ya kuelezwa miradi mingi ya maendeleo ambayo imeletwa Kata ya Kimara ikiwemo Miradi ya Elimu, Miradi ya Afya, Miradi ya Maji na Ujenzi wa Miundombinu ya barabara nyingi ambazo ziko chini ya DMDP, TANROADS, TARURA na Barabara ambazo ziko chini ya Halmashauri.

Aidha alisisitiza juu ya umuhimu na faida ya utanuzi wa Barabara ya Morogoro Road kuanzia Ubungo hadi Kimara Mwisho ambayo ni maelekezo ya Rais Samia ili wananchi wanaopita maeneo hayo wasipate usumbufu wa foleni na kuchochea shughuli za kiuchumi.

Vilevile aliongezea kuwa kwa sasa upinzani hauna nguvu tena na umekufa Kata ya Kimara maana hawana sera wala propaganda za kuwadanganyia tena wananchi.

AFANDE ANAUMWA HAJAFIKA MAHAKAMANI, WAKILI WAKE AFUNGUKA

kutoka mahakama ya Hakimu Mkazi (kituo Jumuishi Cha utoaji haki) Dodoma Kwa mara ya kwanza wakili mtetezi wa Afande Bi. Fatma Kigondo anayetuhumiwa kuratibu kundi la vijana wanne kumbaka na kumlawiti Binti wa Yombo amezungumza kuhusu mteja wake ambapo amesema kuwa Afande Fatma ameshindwa kufika mahakani hapo siku ya Leo Oct 7,2024 kutokana na changamoto ya kiafya

Wakili huyo aliyejitambulisha Kwa Jina la Cedric Mbunda amesema kuwa Kwa bahati mbaya mteja wake hakuweza kufika Mbele ya mahakama hiyo kutokana na changamoto ya kiafya.

Aidha Wakili Mbunda amesema kuwa anaamini tarehe ijayo iliyopangwa kwaajili ya shauri hilo Mteja wake atafika mahakamani

Kutokana na Afande Fatma Kigondo kutokufika mahakani hapo shauri hilo limeahirishwa mpaka Oktoba 15,2024

SEHEMU YA KUJISAFISHA AFANDE NI MAHAKAMANI – WAKILI MADELEKA

Kutoka mahakama ya Hakimu Mkazi(Kituo Jumuishi Cha utoaji haki) Dodoma Leo Oktoba 7,2024 wakili Peter Madeleka na mteja wake Paul kisabo wamefikia mahakamani hapo kwa ajili ya kusikiliza shauri lao walilomfungulia Afande Fatma Kigondo anayedaiwa kuwatuma vijana 4 ambao wameshahukumiwa Kifungo Cha maisha Kwa kosa la kumbaka na kumlawiti Binti wa yombo.

Akizungumza na Waandishi wa Habari nje ya Jengo la mahakama hiyo Wakili Madeleka amesema kuwa imechukua mwezi mmoja tangu shauri hilo kuahirishwa ili kurudi tena leo lakini Kwa taarifa za awali walizoambiwa kuwa mahakama bado haijampangia hakimu mwingine shauri hilo

Wakili Madeleka ameongeza Kwa amesema kuwa katika hali ya namna hiyo mahakama inahusika kuchelewesha shauri hilo

Aidha Wakili Madeleka amesema kuwa kama Afande Fatma Kigondo hajafanya hayo makosa anayotuhumiwa nayo sehemu sahihi ya kuja kujisafisha ni mahakamani lakini zinapofanyika hila asije mahakamani hapo basi hawamtakii mema

WANANCHI WAIBUA SHANGWE BAADA YA KUMKAMATA MAMBA MTATA

Wananchi wakazi wa kijiji cha Kahunda Halmashauri ya Buchosa Wilaya ya Sengerema Mkoani Mwanza wameibua shangwe mara baada ya maofisa wa TAWA kumnasa Mamba aliyekuwa akihatarisha usalama wa maisha yao katika ufukwe (mwalo) wa kijiji hicho.

Wakizungunza mara baada ya mamba huyo kuuliwa kwa kupigwa lisasi na askari wa TAWA wamesema kuwa Mamba huyo amekuwa akikamata kuku, bata na mbwa kijijini hapo huku wakijaribu kumuua bila mafanikio hadi walipotoa taarifa kwa maofisa wa TAWA ambao walikuja kumkamata kisha kumuua.

Akizungumza na wananchi hao ofisa habari wa mamlaka ya usimamizi wa wanyamapori Tanzania TAWA Beatus Magaja pamoja na maofisa wengine wamewapongeza wananchi hao kwa kutoa ushirikiano mzuri hadi kufanikisha kumkamata mamba huyo huku wakitumia fursa hiyo kutoa elimu ya kujilinda na wanyamapori wakali na waharibifu.

WANAWAKE MSIPOJIANDIKISHA MTAKOSA NAFASI YA KUWA VIONGOZI

Wakati Rais wa Tanzania Dkt Sania Suluhu Hassan akitarajiwa kujiandikisha kwenye daftari la kudumu la mpiga kura katika Jimbo la Chamwino jijini Dodoma Oktoba 11, 2024 ili kupata nafasi ya kushiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa Novemba 27 mwaka, huu na kuwahamasisha wananchi kujitokeza kujiandikisha nchi nzima.

Karika Halmashauri ya Meru Mkoani Arusha, Wanawake wametakiwa kutumia nafasi hiyo kujiandikisha katika daftari la mkazi ili waweze kuchagua na kuchaguliwa kwenye uchaguzi huo.

Msimamizi wa Uchaguzi halmashauri ya Meru Mwl Zainabu Makwinya ametoa rai hiyo wakati akiwahamasisha wanawake wa eneo hilo walipojitokeza kutazama fainali ya mpira wa miguu iliyozikutanisha timu maarufu kwenye eneo hilo.

Mwl Makwinya ametoanelimu kwa wakazi hao na kuwahimiza wanawake kugombea kwa kuwa wao wanauwezo mkubwa na sio kuwaachia wanaume tu kugombea nafasi za juu ikiwemo Mwenyekiti wa mtaa, Kijiji au Kitongoji.

Hata hivyo wanawake wa eneo hilo kutoka Jamii ya Wameru wameonyesha utayari wankuwania nafasi mbalimbali za kiungozi kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa.

BARABARA YA SONI- BUMBULI KM 22 ITAJENGWA KWA KIWANGO CHA LAMI

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Tanga Rajab Abdallah amewahakikishia wananchi wa Jimbo la Bumbuli kuanza kwa ujenzi wa Barabara ya Soni – Bumbuli ya Kilomita 22 kuanzia kwenye bajeti ya 2024-2025.

Rajab ameyasema hayo wakati akizungumza kwenye Mkutano wa Hadhara uliofanyika Kata ya Soni, Halmashauri ya Bumbuli wilayani Lushoto mkoani Tanga ambapo chama hicho kimeielekeza Serikali kukamilisha ujenzi huo kutokana na Upembuzi na Usanifu yakinifu kukamilika.

Amesema chama hicho kimeendelea kutekeleza ahadi zake kwa wananchi katika kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo ikiwemo Barabara, vituo vya afya, maji, Umeme, pamoja na kutatua Kero zinazowakabili Wananchi wake.

All Rights Reserved © Cantona Group PLC||2024


Discover more from cantonadigital

Subscribe to get the latest posts sent to your email.

Leave a comment