Radio Fortune Africa -Na Cantona Joseph
https://zeno.fm/radio/radio-fortune-africa
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron anatazamiwa kukutana na viongozi wenzake wa Kongo na Rwanda wiki hii kwa nia ya kuwashinikiza kuhitimisha “makubaliano ya haraka iwezekanavyo” kumaliza ghasia mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), kulingana na chanzo katika Elysée.

Rais wa Ufaransa atampokea kwanza rais wa DRC Félix Tshisekedi siku ya Ijumaa huko Elysée, kabla ya kukutana na Rais wa Rwanda Paul Kagame siku ya Jumamosi kando ya mkutano wa 19 wa Francophonie, ambao utafanyika katika Grand Palais huko Paris. Emmanuel Macron “atahimiza pande hizo mbili kufikia makubaliano haraka iwezekanavyo ndani ya mfumo wa mchakato wa Luanda ili mapigano ya Kivu Kaskazini yafikie mwisho,” kimesema chanzo hiki.
Kundi la M23 (“March 23 Movement”), kundi lenye silaha lenye Watutsi wengi wanaoungwa mkono na Rwanda, limeteka maeneo makubwa tangu mwezi Novemba 2021 katika eneo hili la mashariki mwa DRC lenye utajiri wa madini na eneo linalokumbwa na vurugu tangu miaka 30 iliyopita. Kuibuka tena kwa uasi huu kumesababisha mzozo wa kibinadamu ambao haujawahi kushuhudiwa na karibu watu milioni 7 wakimbizi wa ndani.
Mwishoni mwa mwezi wa Julai, DRC na Rwanda zilitia saini makubaliano ya kusitisha mapigano, yaliyopatikana chini ya upatanishi wa Angola ilioteuliwa na Umoja wa Afrika. Nusu dazeni ya makubaliano ya kusitisha mapigano yalitangazwa, lakini hayajawahi kuheshimiwa kwa zaidi ya wiki chache.
Ikiwa ni sehemu ya mazungumzo ya awali ya kutiwa saini kwa mkataba wa amani, Kigali inaitaka serikali ya Kongo kuliangamiza kundi la waasi wa Rwanda wa FDLR lililoundwa na maafisa wakuu wa zamani wa Kihutu waliohusika mauaji ya kimbari ya Watutsi nchini Rwanda mwaka 1994, mshirika wa Kinshasa.
DRC, kwa upande wake, inadai “kuondoka mara moja na bila masharti kwa wanajeshi wa Rwanda” katika ardhi ya Kongo, kama Rais Félix Tshisekedi alivyothibitisha tena Septemba 25, wakati wa Mkutano Mkuu wa hadhara wa Umoja wa Mataifa, akitaka “vikwazo” dhidi ya Rwanda.
All Rights Reserved © Cantona Group PLC||2024
Discover more from cantonadigital
Subscribe to get the latest posts sent to your email.