Karibu katika Matangazo yetu ya jioni moja kwa moja kutoka Communication Center. Tumekuandalia mengi ikiwa ni pamoja
Radio Fortune Africa -Na Cantona Joseph
https://liveonlineradio.net/radio-fortune-africa
Muhtasari
- DR Congo: Makumi wafariki baada ya boti kuzama katika Ziwa Kivu
- Uingereza kuikabidhi Mauritius visiwa vya Chagos
- Israel yasema iliwaua viongozi watatu wakuu wa Hamas mjini Gaza
- Shambulio la Israel Gaza liliua watu 22 likilenga mwanachama mmoja wa Hamas
- CIA inawasaka wahudumu wapya Korea Kaskazini, Iran na China
- Mwanamuziki nguli wa nyimbo za Injili Afrika Kusini Solly Moholo afariki dunia
- Video: Tazama kupatwa kwa jua Amerika ya kusini
- Rwanda kuanza majaribio ya chanjo ya ugonjwa wa virusi vya Marburg
- Israel na Lebanon: Israel yafanya shambulio la kwanza katikati mwa mji mkuu Beirut
- Takriban watu sita wameuawa katika shambulizi la anga la Israel katikati mwa Beirut
- Mamlaka Tanzania zaifungia Mwananchi kuchapisha habari mtandaoni kwa ‘ukiukaji wa kanuni’
- Urusi yafanya mashambulizi ya mabomu ya Shahid na kamikaze katika maeneo tofauti ya Ukraine
- Biden: Marekani haiungi mkono shambulio la Israeli kwenye maeneo ya nyuklia ya Iran
Rais wa Sudan Kusini amfuta kazi mkuu wake wa ujasusi

Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir amemfuta kazi mkuu wake wa ujasusui wa muda mrefu Jenerali Akol Koor Kuc.
Alikua mkuu wa Huduma za Usalama wa Kitaifa (NSS) zilizoogopwa baada ya uhuru mnamo 2011 na akaendelea katika vita vikali vya wenyewe kwa wenyewe vilivyofuata.
Hakuna sababu iliyotolewa katika amri ya rais iliyotangaza kuondolewa kwake, ambayo ilisomwa kwenye runinga ya kitaifa Jumatano usiku – lakini amefanywa kuwa gavana wa jimbo la nyumbani la rais la Warrup, ambako ukosefu wa usalama umekithiri.
Wachambuzi wanasema huenda ikaashiria mzozo wa madaraka miongoni mwa wandani wa Kiir – huku baadhi ya watu wakiamini Jenerali Kuc anaandaliwa kuchukua madaraka kutoka kwa rais huyo mwenye umri wa miaka 73.
Haijulikani jasusi huyo wa zamani ana umri wa miaka mingapi – lakini anaaminika kuwa na umri wa kati ya miaka 50 au 60.
Mabadiliko katika idara ya ujasusu yanakuja wiki kadhaa baada ya uchaguzi uliotarajiwa kufanyika Desemba, kuahirishwa kwa miaka miwili.
Emirates yasitisha safari zake kuelekea Iran, Iraq na Jordan
Shirika la ndege la Emirates limetangaza kuahirisha safari zake kutoka Dubai hadi Iraq, Iran na Jordan kwa siku tatu kutokana na “machafuko ya kikanda”.
“Wateja wanaopitia Dubai kuelekea Iraq, Iran na Jordan hawatakubaliwa kusafiri katika maeneo yao ya asili hadi ilani nyingine itakapotolewa,” ilisema taarifa.
Wiki iliyopita Emirates iliahirisha safari za ndege kati ya Dubai na Beirut hadi tarehe 8 Oktoba.
DR Congo: Makumi wafariki baada ya boti kuzama katika Ziwa Kivu
Boti iliyokuwa ikisafirisha abiria katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo imepinduka mita mia chache kutoka bandari ya Kituku karibu na mji wa Goma mashariki mwa nchi hiyo.
Shughuli za uokoaji zinaendelea. Video zilizoshirikiwa kwenye mtandao wa X, zamani Twitter zinaonyesha chombo hicho kikigeuka upande mmoja na kupinduka.
Mwanaharakati wa eneo hilo Aaron Ashuza, aliambia BBC kuwa ameona miili ikiopolewa na baadhi ya majeruhi wakiokolewa na kupelekwa hospitali. Alisema boti hiyo ilikuwa ikisafiri kutoka Minova kwenda Goma.
Haijulikani ni watu wangapi walikuwa kwenye boti hiyo.
Tukio hilo bado halijathibitishwa rasmi na serikali ya DRC.

Mambo ya kufahamu kuelekea uchaguzi mkuu wa urais nchini Msumbiji
Raia wa Msumbiji wiki ijayo wanatarajiwa kuchagua rais na wabunge katika uchaguzi mkuu ambao huenda ukashuhudia chama tawala Frelimo kikiendelea kusalia madarakani huku masuala kadhaa yakitarajiwa kuwa ajenda kuu za wagombea.
Imechapishwa: 03/10/2024 – 06:49
Dakika 1
Cheza – 00:59
Ni uchaguzi ambao mgombea wa chama tawama Daniel Chapo, mtangazaji wa zamani na mhadhiri wa sheria, anatarajiwa kumrithi rais Filipe Jacinto Nyusi.
Hata hivyo masuala kadhaa yanatazamwa na wagombea ikiwemo vita dhidi ya makundi ya kijihadi kaskazini mwa nchi hiyo, ambapo maelfu ya raia wameuawa na wengine kukimbia makazi yao kwenye jimbo la cabo Delgado tangu mwaka 2017.
Aidha agenda ya kufufua uchumi kupitia miradi ya gezi ni suala jingine linalozungumzwa na raia, ambapo tangu kuzuka kwa uasi kaskazini mwa nchi hiyo, miradi yenye thamani ya karibu dola bilioni 50 ilisimama, kampuni ya kifaransa ya mafuta TotalErnergies ikilazimika kufunga kabisa opereshen zake nchini humo.
Kasha ya madeni na hasa sakata la kesi ya Tuna Bond, ambapo zaidi ya dola bilioni 1 na laki 5 fedha za mkopo zilizotolewa kwa serikali kwa ajili ya miradi ya uvuvi na benki ya Credit Suisse, zilitumika vibaya katika moja ya ubadhirifu mkubwa uliotia doa nchi hiyo.
Kadhalika suala la mabadiliko ya tabia nchi, ni moja ya jambo linaloangaziwa na wagombea, ambapo athari za mabadiliko ya hali ya hewa zimeathiri watu zaidi ya milioni 1 wanaoshuhudia ukame, hii ni kwa mujibu wa umoja wa Mataifa.
Suala jingine mtambuka ni kuhusu mkataba wa amani kati ya Frelimo na kundi la zamani la waasi lililogeuzwa kuwa chama cha siasa Renamo, ambao tangu maridhiano ya mwaka 1992, pande hizo zimekuwa zikivutana na wakati mmoja kutishia kuitumbukiza tena nchi hiyo kwenye machafuko na hasa wakati huu taifa hilo likijiandaa kwa uchaguzi mkuu.
Uingereza kuikabidhi Mauritius visiwa vya Chagos

Uingereza imetangaza mpango wa kuachia mamlaka ya kundi la visiwa muhimu vya kimkakati katika Bahari ya Hindi baada ya zaidi ya nusu karne.
Mpango huo – uliofikiwa baada ya mazungumzo ya miaka mingi – utashuhudia Uingereza ikikabidhi Visiwa vya Chagos kwa Mauritius katika hatua ya kihistoria.
Hii ni pamoja na eneo la kitropiki la Diego Garcia, linalotumiwa na serikali ya Marekani kama kituo cha kijeshi cha meli zake za jeshi la wanamaji na ndege za masafa marefu.
Tangazo hilo, lililotolewa katika taarifa ya pamoja ya Mawaziri Wakuu wa Uingereza na Mauritius siku ya Alhamisi, linahitimisha miongo kadhaa ya mazungumzo ya mara kwa mara kati ya nchi hizo mbili kuhusu visiwa hivyo.
Jeshi la Marekani na Uingereza litasalia Diego Garcia – jambo muhimu linalowezesha mpango huo kuendelea huku ushindani wa kijiografia katika eneo kati ya nchi za Magharibi, India na China ukiendelea.
Mkataba huo bado haujakamilishwa lakini pande zote mbili zimeapa kufikia hilo haraka iwezekanavyo.
Viongozi watatu wa Hamas waliuawa miezi kadhaa iliyopita – IDF

Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) limetangaza kwamba, miezi mitatu iliyopita, liliua viongozi watatu wakuu wa Hamas huko Gaza.
Miongoni mwao ni Rawhi Mushtaha, aliyetambuliwa na IDF kama mkuu wa serikali ya Hamas, pamoja na Sameh al-Siraj na Sami Oudeh, ambao walisimamia masuala ya usalama katika Hamas.
IDF inasema walikuwa wamejificha katika boma la chinichini kaskazini mwa Gaza na waliuawa kupitia mashambulizi ya angani.
Israel inasema Hamas haikutangaza vifo hivyo “ili kuzuia kupotea kwa ari na utendaji kazi wa mawakala wao wa ujasusi”.
Katika taarifa yake, IDF ilisema Rawhi Mushtaha alikuwa “mmoja wa watendaji wakuu wa Hamas na alikuwa na mamlaka ya za moja kwa moja katika uaamuzi unaohusiana utendakazi wa vikosi vya Hamas”.
Vifo vilivyotangazwa Alhamisi vinaongeza orodha ya viongozi mashuhuri wa Hamas waliouawa mwaka jana, tangu shambulio la Hamas dhidi ya Israel tarehe 7 Oktoba na vita vilivyofuata huko Gaza.
Mwezi Agosti, jeshi la Israel lilisema lilimpiga risasi kiongozi wa Hamas Wissam Khazem, wakati wa operesheni kubwa katika Ukingo wa Magharibi.
Macron atumai kuzishawishi DRC na Rwanda kutunza amani
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron anatazamiwa kukutana na viongozi wenzake wa Kongo na Rwanda wiki hii kwa nia ya kuwashinikiza kuhitimisha “makubaliano ya haraka iwezekanavyo” kumaliza ghasia mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), kulingana na chanzo katika Elysée.
Imechapishwa: 03/10/2024 – 17:21
Dakika 1

Rais wa Ufaransa atampokea kwanza rais wa DRC Félix Tshisekedi siku ya Ijumaa huko Elysée, kabla ya kukutana na Rais wa Rwanda Paul Kagame siku ya Jumamosi kando ya mkutano wa 19 wa Francophonie, ambao utafanyika katika Grand Palais huko Paris. Emmanuel Macron “atahimiza pande hizo mbili kufikia makubaliano haraka iwezekanavyo ndani ya mfumo wa mchakato wa Luanda ili mapigano ya Kivu Kaskazini yafikie mwisho,” kimesema chanzo hiki.
Kundi la M23 (“March 23 Movement”), kundi lenye silaha lenye Watutsi wengi wanaoungwa mkono na Rwanda, limeteka maeneo makubwa tangu mwezi Novemba 2021 katika eneo hili la mashariki mwa DRC lenye utajiri wa madini na eneo linalokumbwa na vurugu tangu miaka 30 iliyopita. Kuibuka tena kwa uasi huu kumesababisha mzozo wa kibinadamu ambao haujawahi kushuhudiwa na karibu watu milioni 7 wakimbizi wa ndani.
Mwishoni mwa mwezi wa Julai, DRC na Rwanda zilitia saini makubaliano ya kusitisha mapigano, yaliyopatikana chini ya upatanishi wa Angola ilioteuliwa na Umoja wa Afrika. Nusu dazeni ya makubaliano ya kusitisha mapigano yalitangazwa, lakini hayajawahi kuheshimiwa kwa zaidi ya wiki chache.
Ikiwa ni sehemu ya mazungumzo ya awali ya kutiwa saini kwa mkataba wa amani, Kigali inaitaka serikali ya Kongo kuliangamiza kundi la waasi wa Rwanda wa FDLR lililoundwa na maafisa wakuu wa zamani wa Kihutu waliohusika mauaji ya kimbari ya Watutsi nchini Rwanda mwaka 1994, mshirika wa Kinshasa.
DRC, kwa upande wake, inadai “kuondoka mara moja na bila masharti kwa wanajeshi wa Rwanda” katika ardhi ya Kongo, kama Rais Félix Tshisekedi alivyothibitisha tena Septemba 25, wakati wa Mkutano Mkuu wa hadhara wa Umoja wa Mataifa, akitaka “vikwazo” dhidi ya Rwanda.
Shambulio la Israel Gaza liliua watu 22 likilenga mwanachama mmoja wa Hamas-BBC yaambiwa

Onyo: Taarifa hii ina maelezo ambayo baadhi ya watu wanaweza kukasirishwa nayo
Shambulio la anga la Israel lililoua watoto wengi katika shule ya zamani siku kumi na mbili zilizopita lilikuwa likilenga mtu mmoja,mwanachama wa Hamas, BBC imeambiwa.
Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) lilisema “kituo cha udhibiti” cha Hamas kilikuwa kimepachikwa ndani ya boma katika mji wa Gaza, ambacho kililengwa katika “shambulio lenye usahihi” mnamo 21 Septemba.
Liliua watu 22, wakiwemo watoto 13 na wanawake sita, kulingana na wizara ya afya inayosimamiwa na Hamas.
Shule hiyo, iliyofungwa wakati wa vita, ilikuwa na makazi ya watu waliohamishwa, wizara ya afya ilisema.
Msichana mmoja mdogo, Amal, aliiambia BBC kuwa alikuwa ndani ya jengo la shule ilipogongwa na kuona miili “ikiwa imesambaratika”.
“Tumefanya nini kama watoto? Tunaamka na kwenda kulala kwa hofu,” alisema. “Angalau zilinde shule; hatuna shule wala nyumba – tunaenda wapi?”
Vyanzo vya habari vimeiambia BBC kwamba mmoja wa waliouawa ni mwanachama wa Hamas, ikimaanisha kuwa raia wengi walikufa kutokana na mtu mmoja kulengwa.
Huda Alhadad alipoteza watoto wawili – mtoto wa kiume Muhammad, 13, na binti Hanan, 12. “Nilikuwa nikitoka kwenye barabara wakati kombora lilipoanguka. Nilikuja na kumkuta mume wangu akipiga kelele akisema, ‘Watoto wangu, watoto wangu, watoto wangu,” aliambia BBC.
“Nikamuuliza, ‘Wako wapi?’ Niliwatafuta na kuwakuta chini ya vifusi.”
Katika siku kumi na mbili baada ya shambulio la anga, angalau mashambulio mengine manane mabaya yalifanyika huko Gaza kwenye majengo ya shule zinakoishi familia zilizohamishwa – shambulio la hivi karibuni zaidi katika safu ya mashambulio kwenye majengo kama hayo, ambayo yanatoa usalama mdogo.
Unicef imesema zaidi ya 50% ya shule zinazotumiwa kama makazi huko Gaza ziliathiriwa moja kwa moja wakati wa vita vya sasa, na “matokeo mabaya kwa watoto na familia”.
Katika kila shambulio la hivi punde, IDF ilitoa taarifa kwa umma ikisema shule za zamani zilikuwa na magaidi wa Hamas au vituo “chini ya udhibiti” wa Hamas.
CIA inataka kuwasajili wahudumu wapya Korea Kaskazini, Iran na China

Shirika la Ujasusi la Marekani limezindua mpango mpya wa kuwaajiri watoa habari nchini China, Iran na Korea Kaskazini.
Shirika hilo lilichapisha jumbe kwenye akaunti zake za mitandao ya kijamii katika lugha ya Mandarin, Farsi na Korea siku ya Jumatano, likiwaelekeza watumiaji jinsi ya kuwasiliana nalo kwa usalama.
Juhudi hizi za hivi punde zinafuatia kampeni ya kuwasajili Warusi kufuatia uvamizi wa Ukraine, ambao CIA inasema ulifanikiwa.
“Tunataka kuhakikisha watu binafsi katika tawala zingine za kimabavu wanajua kuwa tuko wazi kwa biashara,” msemaji wa CIA alisema katika taarifa.
Ujumbe wa ajira – ambao uliwekwa kwenye majukwaa kama vile X, Facebook, YouTube, Instagram, Telegram na LinkedIn- ziliomba majina ya watu binafsi, maeneo na maelezo kuhusu mawasiliano.
Maagizo ya kina yaliwashauri watumiaji kuwasiliana na CIA kupitia tovuti yake rasmi kwa kutumia Mitandao ya Kibinafsi (VPNs) inayoaminika au kivinjari kisichojulikana kinachojulikana kama mtandao wa Tor, ambao mara nyingi hutumiwa kufikia tovuti kisiri.
Mwanamuziki nguli wa nyimbo za Injili Afrika Kusini Solly Moholo afariki dunia

Msanii mkongwe wa nyimbo za Injili kutoka Afrika Kusini, Solomon Molokoane, almaarufu Solly Moholo, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 65, wasimamizi wake wametangaza.
Mwanamuziki huyo aliyeshinda tuzo alikuwa amelazwa hospitalini kwa wiki kadhaa baada ya kuugua akiwa katika ziara ya muziki nchini Botswana mwezi uliopita.
Alipata umaarufu mwanzoni mwa miaka ya 2000 na kuwa jina maarufu katika muziki wa injili wa kitamaduni wa Afrika Kusini.
Wasimamizi wake walisema atakumbukwa sana kwa “muziki wa uponyaji aliotupa kwa miaka mingi”.
Mwezi uliopita, timu ya Moholo ilisema alipatwa na kiharusi na kwamba viungo kadhaa mhuhimi wilini mwake vimeacha kufanya kazi.
Familia yake ilitoa ombi la umma la kuchangisha fedha za gharamia matibabu yake.
“Ni kwa masikitiko makubwa tunawataarifu kwa niaba ya familia ya Molokoane, kwamba gwiji wetu mpendwa ‘Solly Moholo’ amefariki dunia,” uongozi wake ulisema.
“Alifariki tarehe 2 Oktoba 2024 akiwa hospitalini.”
Rwanda kuanza majaribio ya chanjo ya ugonjwa wa virusi vya Marburg

Rwanda iko tayari kuanza majaribio ya chanjo na matibabu ya kutibu ugonjwa wa Marburg, Yvan Butera, waziri msaidizi wa afya alisema siku ya Alhamisi, huku taifa hilo la Afrika Mashariki likipambana na mlipuko wake wa kwanza wa homa hay ya virusi ambayo imewaua watu11.
Ugonjwa huo ulithibitishwa kwa mara ya kwanza mwishoni mwa Septemba, na watu 36 wameripotiwa kupata maradhi hayo hadi sasa, data ya wizara ya afya inaonyesha.
“Hii ni sehemu ya juhudi zetu za kusaidia watu kupona haraka kwa kutumia chanjo na dawa zilizotengenezwa mahsusi kupambana na mlipuko huu, kwa sasa katika awamu ya mwisho ya utafiti,” waziri, Sabin Nsanzimana, aliiambia Reuters.
“Tunashirikiana na makampuni ya dawa yaliyotengeneza dawa hizi, pamoja na Shirika la Afya Ulimwenguni ili kuharakisha mchakato huo kupitia ushirikiano wa kimataifa.”
Alisema serikali inazungumza na makampuni yaliyoko Marekani na Ulaya.
Wizara hiyo ilikuwa ikifuatilia watu 410 ambao walikuwa wamewasiliana na wale walioambukizwa, aliongeza, huku i wengine watano waliopimwa wakibainika kuwa hawana, lakini walisubiri matokeo ya vipimo zaidi.
Homa ya virusi Marburg hivyo husababisha kuvuja damu, na miongoni mwa dalili zake ni maumivu makali ya kichwa hadi kutapika, maumivu ya misuli na tumbo, na unaweza kuua baadhi ya wagonjwa, wizara imesema.
Israel na Lebanon: Israel yafanya shambulio la kwanza katikati mwa mji mkuu Beirut

Mlipuko mkubwa ulisikika wakati Israel iliposhambulia Beirut usiku wa manane.
Jengo lililopigwa lilikuwa katika kitongoji cha Bachoura, karibu na bunge la Lebanon, likiwa ni shambulio la kwanza la anga la Israeli kupiga kitovu cha mji mkuu katika mzozo huu.
Picha za tukio hilo zilionyesha jengo la ghorofa lililoharibika sana, ghorofa ya kwanza ikiwa imeharibiwa kidogo.
Dahieh, ngome ya Hezbollah kusini mwa Beirut, pia ilishambuliwa. Jeshi la Israel lilitoa maagizo mapya kwa wakazi kuyahama maeneo kadhaa ya wilaya hiyo, likisema litalenga vituo na maslahi ya Hezbollah katika siku zijazo.
Kusini mwa nchi hiyo, kulikuwa na ishara kwamba Israel ilikuwa ikijiandaa kupanua uvamizi wake wa ardhini, huku wanajeshi zaidi wakitumwa kwenye mpaka hapo jana.
Takriban watu sita wameuawa katika shambulizi la anga la Israel katikati mwa Beirut

Maafisa wa Lebanon wamesema watu wasiopungua sita wameuawa huku Israel ikipanga kuendelea na mashambulizi yake ya anga.
Jeshi la Israel limekuwa likiwaonya wakazi wanaoishi kusini mwa Lebanon, karibu na mpaka wa Israel, wasirudi nyumbani.
Israel ilianza uvamizi wa ardhini wiki hii, na kutangaza kifo cha wanajeshi wanane wa Israel ndani ya Lebanon hapo jana.
Jana usiku waandishi wa BBC walisikia milipuko mikubwa mjini Beirut huku mashambulizi ya anga ya Israel dhidi ya mji huo yakiendelea. Milipuko pia ilisikika kupitia Dahieh, ngome ya Hezbollah katika vitongoji vya kusini.
Wakati hayo yakijiri sauti za ving’ora kaskazini mwa Israel zinasikika huku milio ya roketi ikiendelea kutoka Lebanon.
Zaidi ya makombora 240 yalirushwa kutoka kusini mwa Lebanon kuelekea kaskazini mwa Israeli siku nzima ya Jumatano, kulingana na Jeshi la Ulinzi la Israeli (IDF).
Na ufyatuaji wa roketi unaonekana kuendelea, huku ving’ora vya tahadhari katika angalau maeneo manne kaskazini mwa Israel vikisikika Alhamisi asubuhi, IDF imesema kwenye Telegram.
king’ora cha hivi punde zaidi kilikuwa Galilee Panhandle, karibu na mpaka wa Lebanon.
Mamlaka Tanzania zaifungia Mwananchi kuchapisha habari mtandaoni kwa ‘ukiukaji wa kanuni’

Mamlaka ya mawasiliano nchini Tanzania (TCRA) imesitisha kwa muda huduma za maudhui ya mtandaoni za Mwananchi Communication Limited (ML) kwa ‘ukiukaji wa kanuni’
Katika tangazo lake kwa umma TCRA imesema imesitisha leseni ya huduma za maudhui ya mtandaoni dhidi ya kampuni ya habari ya MCL nchini humo, kwa ukiukaji wa kanuni ya mwaka 2020.
TCRA imesema tarehe 01 Oktoba 2024, MCL ilichapisha maudhui mjongeo na sauti (audio-visual kwenye mitandao yake ya kijami, maudhui yaliyozuiwa kwa mujibu wa Kanuni ya 16 ya Kanuni za Maudhui Mtandaoni za mwaka 2020.
”Maudhui hayo yameleta tafsiri hasi kwa taifa, jambo ambalo linaathiri na kuharibu umoja, amani na mshikamano wa taifa’’, imeeleza taarifa ya TCRA , iliyotumwa kwenye mitandao yake ya kijamii:
”Umma unaarifiwa kuwa, kufuatia kuchapishwa kwa maudhui yaliyokatazwa na yanayopingana na sheria, TCRA imesitisha kwa muda leseni za huduma za maudhui mtandano za Mwananchi Communication Limited (The Citizen, Mwananchi Digital, Mwananchi na Mwanaspoti) tangu tarehe ya kutolewa taarifa hii, wakati masuala mengine ya kiusimamizi yanafanyiwa kazi,’’ limehitimisha tangazo hilo.
Mwananchi Communication Limited imesemaje?
Kufuatia kuondolewa kwa leseni hiyo, MCL imetangaza kuondoa maudhui yake ya michoro kwenye mitandao yake ya kijami.
Kupitia gazeti lake la lugha ta Kiingereza The Citizen, kampuni hiyo imesema: ‘’Tumeamua kuondoa michoro iliyoshirikishwa Oktoba 1, 2024 kwenye mitandao ya kijamii (X na Instagram), kwa kuwa ilionyesha matukio yaliyoibua hofu kuhusu usalama wa watu binafsi nchini Tanzania.’’
”Uamuzi wetu wa kuondoa katuni unatokana na kusababisha tafsiri mbaya ambayo ni kinyume na nia yetu’’, taarifa hiyo iliongeza.
Maudhui yaliyoiweka MCL lawamani ni ya katuni ambayo ilikuwa ikionesha raia wa nchi hiyo wakilalama kwenye runinga juu ya matukio ya watu kutekwa na kuuawa nchini humo. Katuni hiyo ilikuwa ikimuonesha mtu ambaye alikuwa akitizama runinga ambaye wengi wametafsiri kuwa ni Rais wa nchi hiyo Samia Suluhu Hassan.
Matukio ya watu kutekwa, kupotezwa na kuuawa katika mazingira ya kutatanisha yamezua gumzo katika miezi ya hivi karibuni nchini Tanzania.
Kenya : Wagonjwa wakabiliwa na changamoto chini ya mfumo mpya wa afya
Raia nchini Kenya na hasa wale wa kawaida wanaotegemea kupata matibabu katika hospitali za uma na zile za binafsi, wako katika sintofahamu, baadhi wakishindwa kuhudumiwa chini ya mfumo mpya wa bima ya afya kwa wote, SHIF.
Cheza – 01:11

Mfumo huu mpya ambao ulianza kutumiwa rasmi Octoba mosi, unachukua nafasi ya ule wa zamani uliokuwa unafahamika kama NHIF.
Hata hivyo, jana kwa siku ya pili mfululizo mtandao wa mfumo huo hasa wa kuhuisha takwimu za watumiaji, ulikuwa haufanyi kazi hali iliyowalazimu baadhi ya raia kutumia fedha zao binafsi kupata matibabu.
Ripoti zinaonesha kuwa baadhi ya hospitali binafsi zilikataa kuwahudumia raia waliojisajili chini ya mfumo mpya, kwa kile viongozi wao wanasema wana wasiwasi kuwa huenda madeni yao yaliokuwa chini ya NHIF yasilipwe kupitia mfumo mpya wa SHIF.
Athari za utoroshaji na utakatishaji fedha barani Afrika
Cheza – 09:58
Tatizo la fedha haramu barani Afrika linaligharibu bara hili kiasi cha dola za Marekani bilioni 50 na bilioni 80 kila mwaka, Asilimia 44 ya utajiri wa kifedha wa Afrika inadhaniwa kuwa nje ya nchi. Kwa mujibu wa Ripoti ya Maendeleo ya Uwazi wa Ushuru barani Afrika ya 2023, nchi za Afrika zimeokoa dola bilioni 2 kwa mwaka kutokana na watu kuweka wazi mapato yao, ubora wa kubadilishana taarifa na uchunguzi wa nje ya nchi.Tumezungumza na Ali Mkimo, mtaalamu na mchambuzi wa masuala ya uchumi na biashara akiwa Tanzania.

Urusi yafanya mashambulizi ya mabomu ya Shahid na kamikaze katika maeneo tofauti ya Ukraine

Jeshi la Urusi limetumia ndege zisizo na rubani za kamikaze na shahid katika maeneo ya kaskazini na kusini mwa Ukraine usiku kucha.
Jeshi la Anga la Ukraine linaripoti kuwa mabomu ya “shahid” yalirushwa katika maeneo tofauti juu ya mikoa ya Sumy, Poltava, Cherkasy, Kherson na Nikolaev.
Kituo cha ufuatiliaji wa vita nchini Ukraine kimeripoti kuwa kuwa tayari kuna ndege zisizokuwa na rubani hamsini zilizorushwa na jeshi la Urusi katika anga ya nchi hiyo.
Matangazo ya tahadhari ya mashambulizi ya angani yametangazwa karibu eneo lote la mashariki mwa Ukraine kufuatia mashambulizi hayo.
Mashambulizi ya mabomu katika mji wa KharkovWakati hayo yakijiri meya wa Kharkov na vyombo vya habari vya Ukraine wameripoti kuwa jeshi la Urusi limeupiga mji huo kwa mabomu ya glide
“Mlipuko ulitokea katika eneo hilo. Kharkov inashambuliwa na adui wa KABs. Uwe mwangalifu. Mashambulio ya mara kwa mara yanawezekana,” Meya wa Kharkov Igor Terekhov aliandika kwenye kituo chake cha Telegram.
Kwa mujibu wa Terekhov, shambulizi hilo lililenga wilaya za Shevchenkivsky na Kievsky za Kharkov, na habari kuhusu athari za mashambulizi hayo bado hazijatolewa.
Kituo cha Telegram cha mkuu wa utawala wa mkoa wa Kharkiv, Oleg Sinegubov, kimeandika kwamba, kulingana na data za awali, “kuna uharibifu wa miundombinu ya raia”
Vita vya Ukraine: Mengi zaidi
- YA MSINGI:Mzozo wa Ukraine: Kwanini Urusi inaivamia Ukraine na Putin anataka nini?
- UFAFANUZI:Mzozo wa Ukraine: Swift ni nini na kwa nini kuipiga marufuku Urusi ni muhimu sana?
- UCHAMBUZI:Mzozo wa Ukraine: Putin humsikiliza nani?
- KWENYE RAMANI:Uvamizi wa Ukraine: Shambulio la Urusi kwenye ramani
- ZELENSKY:Volodymyr Zelensky: Mfahamu rais wa Ukraine aliyeacha umaarufu wake wa TV na kuingia kwenye siasa
- PUTIN:Vladimir Putin: Rais wa Urusi aliyeagiza shambulio Ukraine
Biden: Marekani haiungi mkono shambulio la Israeli kwenye maeneo ya nyuklia ya Iran

Rais wa Marekani Joe Biden amesema kuwa haungi mkono shambulio katika maeneo ya nyuklia ya Iran kufuatia mashambulizi ya makombora ya masafa ya Iran dhidi ya Israel na kuitaka Israel kuchukua hatua ” sawia” dhidi ya adui yake mkuu wa kikanda.
Kauli za Biden siku ya Jumatano zilikuja siku moja baada ya Iran kurusha makombora zaidi ya 180 ya masafa marefu dhidi ya Israeli siku ya Jumanne, katika hatua ambayo Biden aliitaja kuwa “isiyofaa.”
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu aliapa kuwa Iran italipa gharama ya shambulio hilo.
Biden aliwaambia waandishi wa habari kabla ya kupanda ndege ya raias,b Air Force One, “Tutajadiliana na Waisraeli watafanya nini, lakini sisi sote (nchi za G7) tunakubali kwamba wana haki ya kujibu, lakini lazima iwe kwa uwiano.”
Katika miezi ya mwisho ya muhula wake, Biden anakabiliwa na ukosoaji mkali ndani na nje ya nchi kutokana na uungwaji mkono mkubwa wa kijeshi wa Marekani kwa Israel, ukosoaji uleule anaokabiliana nao naibu wake, Kamla Harris, mgombea urais wa Chama cha democrat.
All Rights Reserved © Cantona Group PLC||2024
Discover more from cantonadigital
Subscribe to get the latest posts sent to your email.